RIWAYA: HATIA MTUNZI: George Iron Mosenya . . SEHEMU YA - TopicsExpress



          

RIWAYA: HATIA MTUNZI: George Iron Mosenya . . SEHEMU YA THELETHINI . . “Weka pembeni naomba niendeshe!!!” alizungumza kwa amri. Dereva akatii. . . Defao akakikalia kiti akajifunga mkanda, akachukua marashi aliyotembea nayo akajipulizia akawasha gari na kuiondoa taratibu huku akipiga simu ikapokelewa. . . “Nambie!!” aliunguruma. . . “Kama hujavuka bado mi nipo hapa Buzuluga simama twende wote Igoma si upo na gari lako” . . “Ndio nipo nalo aaahh!! Hebu ngoja nakupigia.” Akasita kumalizia akakata simu. . . “Buzulula ndo wapi??” alikosea kutaja jina hilo. . . “Buzuluga?? Buzulula” dereva alimrekebisha. Defao hakujibu kitu. Dereva akajiongeza!! . . “Ni vituo viwili nyuma hapo!!” alielekeza. . . Defao akasimamisha gari kituo cha Mecco, kabla ya kushuka akapiga simu. . . “Nimepapita kidogo narudi sasa hivi!!” alisisitiza kwenye simu. Wakati anakata simu, simu yake ikaita, hakutaka kupokea akakata halafu akapiga. . . “Nipo hapa kituoni mama yangu hii gari Spacio ya rangi ya maziwa!!!” alitoa maelekezo huku akijitanua kwenye usukani. . . Laiti kama angeujua ugeni huo ni bora angeanza na ugeni wa hapo Buzuluga alipopapita. . . Mwanamke wa makamo alilifikia gari hilo aliloelekezwa na Defao ama Gervas Kilinde. Defao alishuka haraka haraka akampokea kwa kumkumbatia. . . “Mh!! Gere huyooooo!!!! Marashi yako mazuri mwanangu” . . Sifa ya kwanza!!!! . . “Aah!! Kawaida mamangu!!! Kawaida sana” alizuga huku akitikisa funguo za gari. . . “Na gari lako Gervas mwanangu!!” . . Sifa ya pili!!! . . “Ndio la muda tu mbona!!!” alidanganya . . “Hongera mwanaweeee umenenepa jamani!!!” . . Sifa nyingine tena!!!! Defao akauona ufahari. . . “Karibu ndani ya gari tuzungumze kidogo basi walau unikumbushe sasa!!” aliomba Defao. Yule mama hakupinga akaingia ndani ya gari. Dereva alikuwa kimya akisikiliza mziki katika simu yake. . . Dakika mbili za maongezo zilikuwa zimetosha sana kumweka Defao matatani, kiumbe asiyekuwa na huruma alifika eneo lile, aliufungua mlango wa kushoto kwa dereva na kumsihi yule mama ashuke mara moja, yule mama akiwa anatetemeka akajitetemesha hadi mkoba ukabaki ndani ya gari. Aliyekuwa siti za nyuma akaamuliwa kukaa siti ya mbele, halafu nyuma akaingia mwenyewe kiumbe huyu matata sana. Haya yote yalifanyika kimya kimya kwani mdomo wa bunduki ulikuwa umeangaza tayari bila wananchi wengine kushuhudia. Ile hali ya wawili hawa kutetemeka ikampa picha kuwa hawakuwa wamejiandaa kwa shambulizi hili la ghafla sana. John Mapulu akajitangazia ushindi mapema alikuwa amemuingiza adui kwenye mkenge kwa njia nyepesi sana. . . “Nyasaka!!!” aliamrisha John, Defao hakuelewa kitu, akashtushwa kwenzi kubwa kichogoni pake!! Akataka kujikuna akasita. . . “Endesha kwenda Nyasaka!!” alitoa karipio huku safari hii akimpiga kwenzi yule dereva bila sababu. . . “Mimi sipajui huyu ndiye dereva!!!” . . “Haya haraka kwenye usukani.” Haraka haraka huku akitetemeka alitua katika usukani, hakuuliza maswali yake yale ya awali yaliyomkera Defao safari hii aliendesha moja kwa moja kuelekea Nyasaka. . . . . ***** . . Matha alisubiri sana baada ya kuwa amempigia simu mtu aliyekuwa amejitambulisha kwake kama Nakayange Mutukula. Alikuwa makini sana akiangaza huku na huko ili awe wa kwanza kumtambua huyo mtu kabla yeye hajatambulika. Wazo la kumpigia simu Nakayange na kumtaarifu kuwa yupo hapo Buzuluga lilikuwa ni kwenda kumteketeza moja kwa moja. Matha aliona kama maadui wamekuwa wengi sana upande wake, haki aliyoona inawafaa kabisa ilikuwa ni kifo. Siku hiyo pia alikuwa amejiandaa kwa ajili ya kuua akiwa amevaa baibui ndani yake alikuwa amehifadhi kisu kikali kilichotandazwa sumu ya kuua upesi sana. Matha alikuwa katika kusubiri kwa mategemeo ya kumuona adui yake lakini haikutokea hivyo, wasiwasi ukaanza kumwingia akahisi kuna mtego anapangiwa ajiingize kichwa kichwa. Akaamua kupiga simu lakini wakati huu Nakayange Mutukula ambaye ndiye Defao hakuwa akipatikana kwenye namba yake. . . Simu ilikuwa imezimwa!!! . . Ni wakati huu ambao tayari alikuwa mikononi mwa John Mapulu. . . Defao hakuwa na ujanja wowote, na ilikuwa afadhali yake kwenda kwa John Mapulu kuliko Matha maana Matha alikuwa amepanga kummaliza wakiwa kwenye gari. Harufu ya kifo ikatawala pande zote. . . Matha alivyoona Nakayange hapatikani akachukua tahadhari akaondoka eneo lile, hakurudi kwake akaenda saluni kupiga stori hadi jioni bado Nakayange alikuwa hapatikani. . . Kengere za hatari zikamchangamsha kichwa chake akafikiria mengi sana kisha akawaza juu ya hatari kubwa iliyopo mbele yake. Hatari ya kuuwawa kwa mkono wenye nguvu, mkono wa John Mapulu. . . Alipotoka saluni alienda moja kwa moja Mecco nyumbani kwa John, akamkuta Michael Msombe. Kwa sauti isiyokuwa na raha akamwita katika chumba walichokuwa wanafanyia mazoezi ya kutumia bunduki. . . Michael alifika na kumshika Matha bega, Matha naye akaushika kwa juu mkono wa Michael, wakawa wamebadilishana joto la miili yao. Michael akakaa pembeni ya Matha, Matha akajilaza katika bega la Michael, Michael akaanza kumchezea chezea nywele zake, Matha akasikika akihema kwa shida, Michael hakushtuka alijua ni tatizo alilokuwanalo Matha akiguswa nywele zake. Akaacha!!!! . . Matha akarejea katika hali ya kawaida baada ya dakika kadhaa akaweza kuzungumza. . . “Maik nadhani ni wakati wa kusahau mambo mengi na kufanya maamuzi!!” . . “Maamuzi yapi mpenzi!!!” . . “Kuondoka kabisa eneo hili halitufai tena, tutauawa maadui wamekuwa wengi na mimba hii imekua” neno mimba lilimshtua sana Michael alikuwa hajalisikia siku nyingi sana. Akakaa vizuri uso wake uliokuwa na tabasamu muda mwingi likapotea taratibu. . . “Nahisi siri hii inaelekea kufichuka!” aliendelea Matha, . . “Nimejaribu kupambana sana Maik wangu, nimepigana sana juu ya amani yetu lakini nahisi sasa nimezidiwa naamini pona pona yangu na wewe ni kukimbia….nisamehe sana Maik nimekutia hatiani..nisamehe..” Alianza kulia Matha huku akimkumbatia Michael kwa nguvu sana. . . Joto la Matha likapenya katika mwili wa Michael, matiti yake ambayo bado yalikuwa na nguvu za kusimama peke yake yakamchoma choma Michael katika hali ya kuburudisha, kucha zenye urefu wa wastani zikatambaa na kumfinya finya maeneo ya uti wa mgongo na mbavuni, uso wa Matha ukawa unatiririsha machozi, Michael akajaribu kumbusu shavuni akakutana na ladha ya chumvi chumvi ya asili. Uvumilivu ukamshinda, ujasiri ukapungua akayaruhusu machozi na yeye yammwagike, hawakuwa na wasiwasi kwani chumba kilikuwa kimefungwa. Michael akauhisi kwa kasi kubwa upendo wa mama ambao ameukosa kwa siku nyingi sana. Upendo wa dhati aliuhisi katika lile kumbatizi alilofanyiwa na Matha. . . Matha alikuwa anampenda Michael!!!!! . . Michael akakubaliana na wazo la Matha, wazo la kutoroka, upendo wa ajabu ukajengeka juu ya mtoto aliye katika tumbo la Matha, Michael akaamini kuwa alitakiwa kucheza nafasi yake kama baba. Ghafla akaondoa hofu yake juu ya John, akaona alikuwa na kila haki juu ya Matha. . . Mipango ya haraka ikatakiwa kusukwa. . . Michael na Matha wakiwa wameungana kwa nia moja. . . . . ****** . . John Mapulu aliwaongoza, Defao na yule dereva hadi katika nyumba yake maeneo ya Nyasaka, moja kwa moja waliingizwa katika vyumba viwili tofauti. Milango ikafungwa, vyumba vilikuwa vina mvuto sana japo hakuna sauti iliyoweza kupenya nje, Defao alikuwa amejikojolea tayari, hofu ilikuwa imemtawala sana hakuamini kama alikuwa katika hali ya kutekwa na hakuwa akimtambua huyu mtu aliyemteka ni nani. Mwili ulikuwa unakumbwa na baridi kila mara alipofikiria juu ya hatma ya kutoka mahali pale. . . Dalili za kifo zikaanza kujionyesha bila kificho, hakika alikuwa na ulazima wa kuwazia kifo maana alionyeshwa bunduki kabla ya kufikishwa hapo bila shaka mtu aliyewateka hakuwa mtu mzuri. . . Chakula kizuri kililetwa, Defao akafanya mgomo wa kula, akiamini kuwa amewekewa sumu, aliamini kwa kugoma kula chakula anaweza kuachiwa huru na kukikwepa kifo, mawazo hafifu kabisa!!!! . . Hakubembelezwa na mtu yeyote kula chakula kile, aliachwa akiwa anashangaa chakula kikachukuliwa. . . Giza lilipoingia hakuwa na mgomo juu ya kipigo baada ya kudai kuwa hamjui hata kidogo mtu aliyehusika na mauaji ya Joram. . . “Unamfahamu Adrian!!” lilikuwa swali jingine, Defao akasema hamjui. . . “Nani alikutuma kwa Joram??” . . “Simjui huyo mtu” alikataa Defao, ghafla mbavu zake ziliamishwa kidogo kutoka mahali pake, lilikuwa teke lenye nguvu sana, alitoa ukelele mkubwa sana huku akijaribu kupambana na maumivu yale. Kabla hajakaa sawa kiatu kigumu kiliukanyaga uso wake akajisikia ganzi halafu chumvi chumvi ikawa inapenya mdomoni mwake, akili ikiwa haiko sawa bado akakutana na vitu kama nyanya ya kopo vikimiminika katika vigaye vilivyokuwa hapo ndani, alianza kujiuliza vimetokea wapi kabla ya kugundua kuwa ni mdomoni mwake. Na ile chumvi chumvi ilikuwa damu yake. . . “Ulikuwa na dili gani na Joram??” . . “Baba mimi huyo simjui” alizidi kupinga Defao huku akilia kama mtoto na kitambi chake. . . “Umetokea wapi hadi kufika hapa??.” . . “Hapa Igoma.? Alijichanganya Defao, na kweli hakuwa akiujua mji. . . Majibu ya Defao hayakumshawishi kabisa John akaamini kuwa Defao alikuwa mtu jasiri sana ambaye anaweza kuficha siri za kambi yake, watu kama hawa John aliwatambua kwani naye alikuwa mmoja wao kati ya wanaume wanaovumilia suluba kama hizo katika kazi yake haramu ya ujambazi. . . Mjeledi!!! Akawa amefikiria juu ya adhabu nyingine kwa huyu bwana ambaye hata alikuwa hajamtambua jina. Laiti kama angejua jinsi Defao asivyoyajua yale yeye anayoyafikiria nadhani asingeumiza kichwa chake. Defao alikuwa ni bwege tu!!! . . Mijeledi mitatu ya nguvu iliichana chana ngozi ya Defao, alilia kama mtoto akiwa ameuma meno kwa nguvu sana. Macho yake yalilegea akatoa kilio kingine cha uchungu mkali akapoteza fahamu. John Mapulu akamwacha hapo akaelekea katika chumba cha dereva. . . Dereva akasema hamjui huyo abiria wake. . . “Hata jina humjui??” . . “Simjui bosi wangu.” . . “Gari ya nani hiyo??.” . . “Pale Kirumba wanapokodisha kaka.” Alijibu katika njia ya kuijitoa hatiani. . . “Kwa hiyo mmetokea wapi kuja kule Mecco??.” . . “Kirumba huko huko.” . . Jibu hilo likamtibua John akili yake akawa kama kichaa tena, huyu anasema Igoma huyu anasema Kirumba. . . Wananidanganya!!!! Aliwaza John huku akiiuma uma midomo yake moja kwa moja akawa amemtia hatiani yule dereva. Ngumi nzito ya kushtukiza kutoka katika mkono wa kuume wa John ilitua katika kinywa cha yule dereva akatema jino moja na supu ya damu. . . John alipotulia kwa muda alishangaa kumwona yule dereva akimfuata kumkabili akiwa na bisibisi mkononi, hakushangazwa na uwepo wa ile bisibisi ndani kwani hakuwa amewakagua mateka wake. . . Aliitazama ile bisibisi kama kimswaki wanachotumia watoto. Dereva akakurupuka mzimamzima na kumrukia John Mapulu, mkono wake ukadakwa juu kwa juu akarushwa mzobemzobe, kabla ya kutua chini vizuri mfupa wa mkono ukalia ‘ko!’ . . “Mamaa mkono wangu!!” akapiga kelele. . . Alipotua chini akiwa bado analalamika juu ya mkono wake, John alifanya shambulizi jingine la ghafla aliunyanyua mguu wake sole ya kiatu ikagandamizwa kwa nguvu katika mguu wa dereva mfupa mwingine ukalia ‘ka!’, maumivu ya mkono yakawa afadhali kuliko ya lile pigo la mguuni. Akapiga mayowe mengine. . . “Bado unayo mifupa mingine mingi, ukitaka kuondoka nayo utanieleza yule jamaa ni nani na nani amewatuma” alisema John, huku akitaka kuondoka, yule dereva akamtukana mama yake John, John akacheka kwa kejeli kisha akawa kama anataka kuendelea mbele. . . Hivi kanitukania mama yangu!! Alipata kumbukumbu, akarudi mbio mbio akaruka teke moja katika staili ya tik-tak likaufikia uso barabara, nguvu zikauzidi uso mwili ukafuata, dereva akajibamiza ukutani, akaanza kukoroma huku bisibisi ikiwa pembeni yake. . . John akatoka nje!!! **** **DEFAO mikononi mwa John Mapulu.... hatimaye mbio za sakafuni zimeishia ukingoni BOFYA LIKE KAMA TUPO SAMBAMBA.... NA USIACHE KUTOA MAONI YAKO.....KILA NENO LAKO UNALOANDIKA LINASOMWA NA KUFANYIWA KAZI
Posted on: Sat, 31 Aug 2013 09:00:00 +0000

Recently Viewed Topics




© 2015