RIWAYA; LOVE STORY, Tanganyika na Unguja. MTUNZI; AMRI - TopicsExpress



          

RIWAYA; LOVE STORY, Tanganyika na Unguja. MTUNZI; AMRI BAWG. SEHEMU YA KUMI. Omar alianza kuingiwa na wasiwasi hapo alipokuwa amekaa peke yake juu ya kochi la saruji. Lakini mara alipotupa jicho alimuona Leila kwa mbali anakuja. Moja kwa moja alifika na kukaa upande wa kulia wa Omar. “Nilikwishaanza kutia wasiwasi, ungechelewa kidogo tu ninge..... ‘ “Ungefanza nini Omar?!” “Ningekuja nyumbani kwenu kwanza, kuhakikisha kama umetoka au vipi?” “Inaonyesha huogopi kuja nyumbani kwetu Omar.” “Niogope kitu gani? Siji kwa uovu wala uadui, naja kwa amani na mapenzi, halafu si ulikwisha nikaribisha mwenyewe nyumbani kwenu?” “Tuyaache haya, hebu nipe habari za huko.” “Habari za huko, hivi sasa nilikuwa na mchumba wangu, na hata nyumbani wanajua saa hizi nipo sinema na huyo mchumba.” Omar alimkodolea macho Leila na kumuangalia vizuri bila kusema neno. Ndipo Leila alipoanza kumuhadithia matukio yote ya mchana ule toka walipoachana mpaka wakati huu wanakutana. Omar alisikiliza kwa makini na kujaribu kuhifadhi kila neno lililotamkwa na Leila. Baada ya kusikia habari nzima, alirudisha pumzi kwa nguvu na kusema. “Sasa Leila unaifikiriaje hali kama hii?” “Kwa kuwa na yeye Vuai yupo katika hali kama yetu nitamsikiliza atasemaje, au wazee watasemaje, lakini lelote liwalo, kama watasisitiza mambo yende kama wanavyotaka wao. Mimi nisubiri Dar es Salaam, nitatoroka, hivyo tafuta pa kuniweka kabisa.” “Kesho, mimi inanibidi nirudi Dar es Salaam, lakini nitakuachia namba ya simu, ikiwa jambo lolote litakuletea taabu, nipigie simu nikuachie pesa.” “Pesa sina tatizo nazo, ninazo za kunitosha kunifikisha karibu na wewe, nipe namba ya simu, basi.” Waliagana. Leila akarudi alipomuacha Vuai, na Omar akarudi hatelini. Vuai aliporudi nyumbani kwao usiku ule hakuwa na raha kabisa. Alimuendea kaka ake Zahran na kumwambia; “Tafadhali Zahran, ninakuomha uniambie habari za Eda.” “Ewe, weye vipi yakhee,” bado unauliza habari za Eda tu, wakati unarejea toka matembezini na Leila!” “ Zahran, nakuomba tafadhali nieleze habari za Eda.” Vuai alionekana amebadilika na kujaribu kujizuia asihamaki zaidi. “Sawa, iwapo unalazimisha kuzijua habari za Eda, ni kuwa tulikutana naye, lakini la kusikitisha zaidi baada ya kuhojiana naye, alikiri kuwa alikupenda kwa kujua, kuwa wewe unazo pesa. Na zaidi ya yote, baba alimpa pesa na kumwambia aachane na wewe, naye Eda alizichukua pesa hizo bila ya aibu. Na akasema atatumia mbinu za kukujulisha kuwa hana haja na wewe tena. Lakini itakuchukua muda.... Na tulipomueleza kuwa unaye mchumba, alituambia ni afadhali tusipoteze wakati tukuoze haraka iwezekanavyo. Kwa kweli jinsi ulivyomuelezea na namna tulivyomuona na kumsikiliza ni tofauti. Na ndio maana tuliporudi tu, tuliona ni afadhali tuwakutanishe na mchumba wako Leila.” Vuai alimtazama kaka yake machoni na kumwambia; “Hivi kweli wewe kaka yangu unaweza kuwa katili wa nafsi yangu namna hii? Siamini unayoyasema. Ninamuelewa Eda zaidi kiasi cha kujua kuwa hawezi kufanya hivyo usemavyo,” “Nenda kamuulize baba.” “Simuulizi mtu yeyote, baba, mama wala nani, ninyi fanyeni mpendavyo, nami nitafanya nitakavyo.” Vuai aliondoka kwa hasira na kumuacha kaka yake katulia. Usiku ule hakuweza kula na usingizi ulikuwa shida. Asubuhi kulipokucha, aliamua aende Dar es Salaam kuonana na Eda. * **** Eda, baada ya kukutana na baba yake na kaka yake Vuai na kukataa kishawishi chao cha fedha walizotaka kumpa ili amuache Vuai, alirudi nyumbani kachanganyikiwa. Siku iliyofuata alipokwenda kazini, alijaza fomu za likizo upya, ili achukue likizo nzima ya mwaka badala ya wiki mbili kama alivyodhamiria hapo mwanzo. Bahati nzuri likizo ilipitishwa na kuambiwa angoje juma linalofuata aanze likizo hiyo. Alipokuwa yupo nyumbani siku hiyo, jioni yake walikuja mjomba wake, na mke wa mjomba wake, baba na mama yake Omar Kondo. Walikaa sebuleni wakazungumza na mama yake Eda kwa muda mrefu, halafu walimuita Eda, alipofika, Mzee Kondo alimtamkia. “Mwanaeda, hebu kaa hapo, tuna mazungumzo na wewe. Eda alikaa juu ya kiti kilichokuwepo kando kidogo na wazee walipokuwa wamekaa. Mzee Kondo alianza; “Mwanangu, tumekwita mama ili tukueleze ushauri wetu tuliokuwa tukishauriana hapa. Sisi wazazi wenu tumeona ni bora wewe tukuoze Omar, binamu yako. Kwani yeye ameshafikia umri wa kuoa, hali kadhalika na wewe pia upo tayari kabisa katika umri mzuri wa kuolewa, isitoshe nyote mpo katika taaluma moja, nafikiri itakuwa ni vizuri sana nyinyi mkaoana, unasemaje Eda?” “Mimi sina la kusema kwa sasa hivi mjomba, isipokuwa naomba nipewe muda wa kufikiri, pia naomba kuuliza.” “Uliza mama, uliza.” “Je, kaka Omar amekwishaambiwa suala hili? Na amejibu nini?” “Omar nimemwambia, naye pia nimempa muda wa kufikiri kwani kasema mambo mengi tu yasiyo na maana na hayupo amekwenda Unguja, lakini kesho atarudi.” Mzee Kondo alijibu kwa kubabaisha. Eda aliomba aruhusiwe aondoke. “Sawa mama, ondoka, lakini nakuomba ufikiri sana suala hili. Na nitumaini langu kuwa utakubaliana na sisi.” Eda alikuwa katika mtihani wa maisha, alichokuwa na hamu nacho kikubwa ni kukutana na Vuai na sasa pia kukutana na Omar na siku ifike ya kuanza likizo aende zake Tanga akapumzike. Aliona dunia haimwendei vizuri. Wakati yuko kazini siku iliyofuata, aliitwa na kuambiwa kuna simu yake, aliwaza... “Ni nani tena huyo Yaillahi, kichwa changu kimejaa matatizo ya dunia.” Alinyanyua chombo cha simu kwa unyonge na kuitikia; “Halloo, Eda anazungumza hapa nani mwenzangu?” “ Hallo hapa ni Vuai, habari za siku Eda?” “Nzuri tu Vuai, lakini ni kweli wewe ni Vuai?” “Kwa nini uulize hivyo Eda?” “Sababu mara ya mwisho nilipopokea simu, mtu alijitambulisha kuwa yeye ni Vuai na kumbe alikuwa sio wewe.” “Ni mimi ninahitaji kofi shavu la pili dokta wangu, ni nani aliyekupigia akasema ni mimi?” “Alikuwa ni kaka yako Zahran, na niliamini, sababu sauti zenu zinafanana.” “Ni kweli sasa Eda, mimi nimeingia muda huu huu tukutane saa ngapi na wapi? Tuna mengi ya kuzungumza au wewe huna?” “Maradufu ya uliyonayo wewe.” “Ok, sasa wapi?” “Wewe sema wapi mimi nitafika, kwanza leo nimekuja na nguo za nyumbani, popote ninaweza kuingia.” “Ingawa njaa inaniuma lakini siwezi kula kabla ya kukuona wewe, unajua labda ni wapi tutapata chakula kizuri na cha moto wakati wewe ukitoka kazini?” “Chef’s Pride............CP.” “Ni wapi hapo?” “Chagga street, kitaa kidogo kati ya mitaa ya Libya na Jamhuri, eneo la Kisutu.” “Nimepapata, nilikwishawahi kwenda pale ni kweli chakula chake kizuri, kwa hiyo saa ngapi?” “Tisa kamili nitakuwa pale, nikukute unanisubiri.” “Sawa, saa hiyo basi, kwa heri.” “Kwa heri.” “Ngoja kidogo, wait” “Nini tena?” “I Love you.” “Me too.” Eda aliweka chombo cha sirnu chini akarudi wadini, huku akijihisi damu inamsisimka, aliwaza, “Ni kweli ninampenda Vuai.” Saa tisa kamili Eda alitoka kazini, akakodi taksi, akaelekea hoteli waliyoagana na Vuai kupata chakula cha mchana, Chef’s Pride. Kweli alipofika hapo alimkuta tayari Vuai anamsubiri yeye. Waliingia ndani ya hoteli wakatafuta meza wakakaa. “Enhee habari za siku Eda.” “Nzuri tu, sijui zako wewe.” “Kwanza utakula nini Eda.” Utakacho kula wewe Vuai nami niagizie hichohicho” “Waliagiza chakula, wakaletewa. Wakati wanakula Vuai alianza tena kuzungumza; “Hewaa, mimi sijambo, haya nipe habari mwenzangu Eda vipi?” “Vipi katika yapi?” “Ulikutana na baba na kaka yangu Zahran?” “Pamoja na mhasibu wenu Haji.” “Enhee, ilikuwaje? Walikuambia nini?” Eda alimuelezea Vuai toka mwanzo alivyopigiwa simu za Zahran na mpaka mwisho aliposhawishiwa kwa kupewa pesa chungu nzima lakini kwa sharti kuwa aachane na yeye Vuai na jinsi alivyozikataa na kuchana cheki. “Ina maana hukuchukua hata pesa moja?” “Ungekuwa wewe ungechukua?” “Hapana sina maana mbaya kukuuliza hivyo Eda, maana yangu ni kuwa nimeambiwa, umechukua pesa na ukakiri kuwa unanipenda kwa ajili ya pesa.” “Umeambiwa na nani maneno hayo.” “Na kaka yangu Zahran.” Na wewe uliamini kuwa nimechukua pesa au nilikupenda kwa ajili ya pesa.” Kama ningeliamini nisingekuwepo hapa sasa hivi, ninakuuliza ili kupata uhakika tu. Lakini nilijua kuwa sio kweli.” “Nashukuru kwa irnani yako juu yangu Vuai.” “Nami pia nashukuru kwa pendo lako juu yangu Eda, nami pia nakuhakikishia ninakupenda. Na leo ninakupenda zaidi kuliko jana, na nina hakika kesho nitakupenda zaidi kuliko leo. Pendo langu kila siku linazidi kuota juu yako.” Walimaliza kula, Vuai akalipa na wakatoka nje ya hoteli. “Sijui ulikuwa na mpango gani kwa siku ya leo baada ya kutoka kazini, kabla sijakupigia simu mimi Eda.” “Nilikuwa nikitoka kazini niende nikamuone kaka Omar, binamu yangu ambaye ninatakiwa anioe.” “Eda unasema nini?” Vuai alimuuliza kwa taratibu kisha akamvuta mkono na kurudisha hotelini CP sehemu ya nje, akamkalisha kwenye kiti cha meza ya mwisho pembeni. “Hebu rudia tena usemi wako.” “Ndio hivyo, kuna uchumba umezuka nyumbani kwetu, natakiwa niolewe na binamu yangu Omar.” “Na wewe umewajibu nini?” “Sijawajibu lolote, na ndio maana nimekwambia tuna mengi ya kuzungumza. Ninataka nikutane na Omar kwanza. Nisikilize kauli yake na maoni yake juu ya huo uamuzi wa wazee, kabla sijatoa uamuzi wangu. Pia nimekwishaomba likizo ya siku ishirini na nane, ya mwaka. Nitaanza wiki ijayo. Ninataka kwenda kupumzisha akili yangu kwa shangazi Tanga.” “Kwanza niambie Eda umewajibu nini hao wanaotaka uolewe na binamu yako?” “Nakuambia sijawajibu chochote, kwanza nataka kuonana na kaka Omar.” “Umuone afanyeje? Akiwa anawaunga mkono hao wazazi utafanyaje.” “Akiwaunga mkono au asiwaunge mkono, awaunge mguu, mimi siolewi na Omar lakini kwa nini unauliza jibu Vuai? Kwani una wasi wasi na mimi?” “Hapana, isipokuwa saa zote nataka unihakikishe kuwa ni mimi tu, hakuna mwingine. Halafu sijakuambia kitu kimoja Eda.” “Kitu gani hicho?” “Ya kuwa hata huyo mchurnba niliyepewa huko Unguja naye pia ana mpenzi wake, naye pia hataki kuolewa na mimi kama vile mimi nisivyotaka kumuoa yeye, au kama vile wewe usivyotaka kuolewa na Ornar, sijui Omar naye atasernaje.” “Sijui, ngoja nikutane naye tutafahamu.” Waliagana wakutane siku inayofuata baada ya Eda kuzungumza na Omar. ITAENDELEA KESHO!!!
Posted on: Sat, 07 Sep 2013 16:38:56 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015