RIWAYA: MTAFITI MTUNZI: HUSSEIN TUWA SEHEMU YA ISHIRINI NA - TopicsExpress



          

RIWAYA: MTAFITI MTUNZI: HUSSEIN TUWA SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA Zay alikuwa amechanganyikiwa vibaya sana wakati akitoka nje ya jengo lilenakukatisha barabara. Alianza kukata mitaa bila ya kujua ni wapi hasa alikuwa anaelekea… ____________ Mara walipoona kuwa Zay amefanikiwa kuzusha tafrani pake ofisini na amewatoka, Bilanga na Chabbi waligeuza haraka, kila mmoja akichukua uelekeo tofauti bila hata ya kuambizana. Bilanga alijitoma ndani ya ile lifti na kushuka nayo chini, wakati Chabbi akirudi mbio kwenda kule ofisini kwake. “Pumbavu! Hakuna moto bwanaaaa!” Alimaka huku akihangaika kupitisha ufunguo kwenye mlango wa ofisi yao, ambamo Bilanga alikuwa amemfungia mama Mwamtumu muda wote, akiwa amemtuliza kuwa alikuwa anaenda kumuitia mtu ambaye angemueleza kwa kituo juu ya habari za mwanaye Mwamtumu, baada ya kuona mabishano kati ya Zay na yule dada wa mapokezi kupitia kwenye runinga iliyokuwa mle ofisini kwake, kama jinsi ilivyokuwa ofisini kwa Chabbi. Muda Chabbi alipoufungua tu ule mlango wa ofisi yao, ambapo alitakiwa aipite ofisi ya Bilanga kwanza ndio aifikie ile ya kwake, alikumbana na mwanamke aliyetoka mbio mle ofisini huku akiwa amehamanika vibaya sana na akipiga mayowe. “HEEEEEY, NANI WEW…?” Chabbi alipayuka kwa hamaniko huku akisukumwa pembeni bila hadhari, kwani hakujua kabisa kama mle ndani kulikuwa kuna mtu na hakuwa amepata nafasi ya kuongea na Bilanga juu ya hilo mara alipofika pale mapokezi kutokana na ile tafrani ya Zay. Mama Mwamtumu alimpita ubavuni kwa kasi na kutoka nje ya ofisi ile na kuwahi kule kwenye ngazi, ambako bado kulikuwa kuna wafanyakazi wachache wakimalizikia kukimbia hatari ile ya moto usiokuwepo. “SHIIIIT! AKH!!” Chabbi alilaani kwa hasira, lakini hakumfuata. Alipitiliza moja kwa moja hadi ofisini kwake na kunyakua kipaza sauti cha kurushia matangazo mle ofisini. Akaanza kunadi kuwa wafanyakazi watulie na warudi kuendelea na kazi, kwani hatari ya moto ilikuwa imeshadhibitiwa. Alilirudia lile tangazo kama mara tatu, kisha akazima kile kisemeo na kuketi kitini kwake pale ofisini, akitafakari jinsi mambo yalivyokwenda kwa kasi ya ajabu ndani ya muda mfupi sana. Yule Zay keshafika hadi hapa? Alikuwa anataka nini? Na Yule mama aliyekuwa amefungiwa na Bilanga humu ofisini…ni nani? Mwili ulimsisimka Chabbi Cheka, kama jinsi ambavyo huwa unamsisimka akabiliwapo na changamoto kama zile. Yeye siku zote huwa anajihesabu kuwa ni mtu wa sekeseke, na sekeseke zikiwa zinamtokea kama hivi ndio hujiona kuwa hakika yuko duniani. Luis Kambesera alifika pale mlangoni kwake kama mzimu na kumtumbulia macho. “Kumbe uko jengoni muda wote na hukuja kuniona? Si nilikwambia…” Luis alianza kumlaumu kwa jazba, na Chabbi akamkatisha. “Mi ndo nimeingia hapa muda huu huu… na kukutana na zahma hii!” “Ni nini kinatokea lakini Chabbi? Mambo yanazidi kutuandama tu namna hii? Hii kengele ya moto imetokana na nini tena?” Luis alimaka. “Sit down Luis…we need to talk!” Chabbi alimwambia huku akionekana kuwa mchovu sana, akimaanisha kuwa Luis akae wafanye maongezi. “Tutaongelea ofisini kwangu!” Luis alijibu kwa kiburi na kugeuka kurudi ofsini kwake. Chabbi alibenyua midomo kwa aidha kukereka au kudharau kitendo kile au kwa kuwa hakuwa na kingine cha kufanya wakati ule, mwenyewe ndio alikuwa anajua, na kupandisha miguu yake juu ya meza. Alitoa simu yake na kumpigia Bilanga, lakini ile simu ilikuwa ikiita tu bila majibu. Maumivu makali yalimchoma kwenye lile jeraha aliloachiwa na Mwamtumu begani kwake, naye akafinya uso na kuuma midomo kwa maumivu yale. “Pumbavu sana Mwamtumu! Pumbavu sana!” Alinong’ona kwa hasira, na kubaki akiwa ameketi pale ofisini namna ile kwa muda mrefu. Kisha alisonya na kuinuka. Akaliendea jokofu dogo lililokuwa mle ofisini kwake na kutoa chupa ndogo ya pombe kali. Akaifungua, na akiwa amesimama pale pale mbele ya lile jokofu akapiga funda moja kubwa, kisha akaunguruma kwa faraja ya mshuko wa kinywaji kile kooni kwake. Akamung’unya midomo huku akilifunga lile jokofu, halafu akatoka na kinywaji chake mkononi hadi ofisni kwa Luis. ____________ Wakati yale ya kule Liquid Diamond Incorporated yakiendelea, Inspekta Kwakwa na Sajenti Pojo walikuwa kwenye mtanziko mzito. Walikuwa ofisini kwa Inspekta Kwakwa pale kituo cha polisi cha kati, au “central” kama kilivyozoeleka kwa wengi jijini Dar. “Kwa hiyo unadhani kifo cha yule dereva wa bajaji si cha bahati mbaya?” Kwakwa aliuliza tena, na Pojo akaafiki kwa kichwa. “Kabisa afande…yaani kwanza jamaa aliyemkodi yule kijana amemchukua muda ule ule ambao mimi ndio nilikuwa nimefika pale…halafu wakati alipokuwa anataka kuniambia jambo muhimu kuhusu mtu aliyekuwa na Mwamtum siku ile hapo hapo ajali ikamkuta!” “Ah! Sasa hiyo we’ inakwambia nini?” “Inaniambia kuwa bila shaka huyo jamaa alikuwa naye kwenye bajaji muda huo!” “Huoni kuwa kama hivyo ndivyo, na yeye pia basi atakuwa ameumia ajalini?” Kwakwa alisaili, na Pojo akatikisa tena kichwa kuafikiana na hoja ile. “Inawezekana…” “Lakini umeniambia kuwa askari waliofika pale eneo la tukio hawakuona maiti nyingine au majeruhi atokanaye na ajali ile zaidi ya huyo kijana…” Kwakwa alizidi kumtahini Yule sajenti mtu mzima. “Na ndio la kutia mashaka zaidi hilo afande…! Kwa nini mtu apate ajali kama ile akiwa na abiria, halafu abiria asionekane? Ina maana hata kama kaumia, muhusika aliona ni muhimu sana yeye kutoonekana eneo lile kuliko kusubiri kupatiwa msaada na wasamaria!” Pojo alisisitiza. Kwakwa alimtazama kwa muda akiwa amekunja uso. “Hoja yako inaleta maana sana Sajenti…” “Of course inaleta maana afande! Sasa swala ni wapi tutampata huyo jamaa…?” “Nadhani haitatuchukua muda mrefu tutamjua tu…” Kwakwa alisema, na hapo simu yake ikaita… ___________ Bilanga aliwahi kufika chini kabla ya wote waliokuwa wakishuka kutoka kule ghorofani kwa kutumia ngazi za miguu kwa kufuata ule utaratibu wa kutotumia lifti wakati wa hatari ya moto jengoni. Kwa kuwa yeye alijua kuwa hakukuwa na moto, alitumia lifti kushuka kule chini bila ya shaka yoyote. Akiwa upande wa pili wa barabara nje ya jengo lile, alimuona Zay akitoka nje ya lile jengo kwa wahka mkubwa, naye akaanza kumfuatilia kwa mbali, akiwa makini kulivua lile koti lake la jeans na kubaki na fulana nyekundu aliyoluwa ameivaa chini ya koti lile ambalo alibaki akiwa amelishika mkononi. Alimfuata Zay wakati akikata mitaa kadhaa mjini na akaona moja kwa moja kuwa yule binti alikuwa amechanganyikiwa na hakuwa na uelekeo maalumu. Simu yake ikaanza kuita, lakini hakuipokea, kwani hakutaka kupoteza umakini. Yeyote awaye, atampigia baadaye. Baada ya mizunguko kadhaa mjini hatimaye yule binti akaingia kwenye mgahawa fulani, naye akabaki akiwa amesimama nje, ubavuni mwa mgahawa ule huku akili ikimzunguka. Hakujua iwapo ule mgahawa ulikuwa na mlango wa nyuma au la, na wakati huo huo alihofia kuzunguka huko nyuma kuthibitisha hilo kwa mashaka kuwa wakati akiwa huko nyuma yule binti atatoka huku mbele na kumpotea. Afanyaje sasa? Hakusubiri sana kupata jibu. Yule binti alitoka nje ya ule mgahawa na kuendelea na safari yake, wazi kuwa hata alipoingia mle mgahawani hakujua alienda kufanya nini, hivyo akaamua kutoka. Ila sasa mwendo wake ulimwambia kuwa yule binti alikuwa ameshapitisha uamuzi juu ya mahala alipokuwa anataka kwenda, kwani alionekana akitembea kwa lengo na uelekeo maalum. Zay alirudi hadi pale alipoegesha gari lake na kujifungia ndani yake. Alikuwa akitetemeka mwili mzima. Hakuamini kuwa amewachoropoka wale watu kule kwenye ile ofisi ya kifo. Sasa alikuwa na uhakika kabisa kuwa wale ndio jamaa waliomteka Mwamtumu, kwani aliikumbuka vizuri sana sauti ya yule jamaa aliyetoka kwenye lifti na kumwita kwa jina lake. Ilikuwa ni ile ile sauti aliyoisikia kwenye simu siku ile alipopigiwa na kudaiwa awape chao ile wamrejeshee Mwamtumu, na akamsikia Mwamtumu akimpigia kelele. Baridi ilimtambaa mwilini, na akakumbuka jinsi Sajenti Pojo alivomuasa kuhusu kuionesha sura yake kwenye ile ofisi, na alivyomtahadharisha kuhusu uhatari wa wale watu. Naam, sasa alijihakikishia kuwa wale jamaa walikuwa ni hatari kweli kweli. Lakini sasa ningefanyaje? Mama Mwamtumu alikuwa ameshaingia mle ndani…ningemuacha? Mama Mwamtumu! Oh, My God…mama Mwamtumu! Watamuua wale watu jamani! Alikurupuka na kuikusanya simu yake iliyosambaratika kutoka kwenye begi lake na kuiweka sawa, kisha hapo hapo akaiwasha. Na meseji ikaingia kabla hata hajapiga simu aliyotaka kupiga. UKO WAPI WEWE? NIPIGIE HARAKA SANA! Ulikuwa ni ujumbe kutoka kwa Inspekta Kwakwa. “Oh, laiti ungejua na mi’ ndo nataka kukupigia!” Alisema peke yake na kumpigia yule askari makini. “Ah, Zay…! Vipi wewe, mbona…?” Inspekta Kwakwa aliongea simuni na Zay akamkatisha. “Mama Mwamtumu yuko hatarini afande, please nenda kamuokoe…watamuua!” Alipayuka, na upande wa pili Kwakwa akamakinika, akimtupia Pojo jicho la pembeni. “Yuko matatani kivipi? Yuko wapi?” Alihoji. “Kule kwenye ile kampuni! Kaenda na nadhani jamaa wamemteka…!” “Sasa kaenda au katekwa…?” “…mi nimechomoka kimajaaliwa tu afande!” Zay alizidi kuwahkika simuni, na Kwakwa akazidi kujazbika. “What do you mean umechomoka kimajaaliwa, ulienda liquid Diamond wewe?” “Ah! Huyu demu sasa anataka kutuchanganyia habari, kaenda kutafuta nini huko sasa?” Pojo alilalamika peke yake huku akimtazama Kwakwa. “Like sikuwa na namna afande! Mama wa watu atakufa huko please nenda ukamsaidie!” Zay alipayuka, huku akisikia simu nyingine inataka kuingia. “Mahabusu inakuhusu Zay! Tena nakutia ndani mimi mwenyewe! Wewe ushakuwa hatari kwa maisha yako, bloody shit!” Kwakwa alimfokea simuni na kukata simu. “Twen’zetu!” Alimwambia Pojo huku akiongoza njia kutoka nje ya ofisi yake. Bila kubisha Pojo aliinuka kumfuata, naye akiwa ameghadhibika vibaya sana. Kule garini Zay alikata simu na hapo simu nyingine ikaingia. Alikuwa mama Mwamtumu. Heh! “Mama! Uko wapi? Um…umetokaje kule…?” “Oh, Zay mwanangu ni balaa kubwa! Wale si watu wazuri wale…mwanangu wanaye wale…wanaye, wanaye tena wanaye! Kwa nini lakini?” Mama Mwamtumu alilalama simuni huku akidhihirika wazi kuwa alikuwa akilia. “Hebu ngoja kwanza. Umetoka kwenye ile ofisi?” Zay aliulza, akili ikimuwanga. “Nimechomoka kama ulivyochoka wewe mawanangu!” Khah! “Unamaanisha nin…anyway, hapo ulipo chukua bajaji upesi elekea kituo cha polisi cha kati mama…tukutane central polisi. Mi’ naelekea huko!” Zay alisema kwa wahka, na kukata simu. Akampigia Kwakwa. “Mama Mwamtumu katoroka kule! Nimemwambia aje central polisi!” Alimwambia. “Ama!” Kwakwa alistaajabu. “Na mi’ nakuja huko, so nadhani na we nisubiri hapo hapo tu afande, na usiniletee habari ya eti kuniweka ndani mimi!” Zay alimkoromea kisha akakata simu. Alitia gari lake moto na kuliondoa kwa kasi kutoka eneo lile. Harakati zake zote za ndani ya gari zilikuwa zimeonwa na Bilanga aliyekuwa amesimama mbele ya meza ya muuza magazeti akijitia kuperuzi vichwa vya habari magazetini. Aliitazama ile Vitz ya Zay ikiondoka eneo lile akiwa tayari ameshaikariri namba zake za usajili. “Nimeshakujua sasa we’ malaya…kukupata haitakuwa taabu tena kwangu!” Alijisemea huku akirudi taratibu kule ofisini kwao… ___________ “WHAAT?” Luis Kambesera alibwata kwa hamaniko huku akimsukumizia Chabbi uso wake kutokana na yale maelezo aliyopewa na Chabbi, mtu wake muhimu sana katika maswala yake yote ya haramu, ambayo yalikuwa mengi. Chabbi alibaki akimtazama huku amejibweteka pale kwenye kochi mororo. “Yaani pamoja na yote hayo bado makabrasha ya Grayson hujayapata Chabbi?” Luis aliuliza tena baada ya kuona kuwa Chabbi amepiga kimya. “Ndio boss…hali ndio iko hivyo mpaka sasa. Lakini sio mbaya kihivyo, hali inadhibitika!” Chabbi alisema na kupiga funda jingine kutoka kwenye ile chupa ndogo ya pombe kali. “Sio mbaya kihivyo? Hali ni mbaya sana Chabbi, na sasa ndio imekuwa muhimu zaidi kuyapata hayo makbrasha ya Grayson kuliko wakati wowote mwingine! Una hakika nyumbani kwa Grayson mlipekua vizuri kweli?” Luis alisema na kuuliza. “Huko tulishamaliza kupekua tangu Grayson hajawa marehemu na sote tukakijiridhisha kuwa hakuna kilichobakia kule…” Chabbi alimjibu “Still…panahitaji kutazamwa tena…!” “Hizo karatasi najua aliye nazo Luis. Yaani we’ amini kuwa nitazipata tu!” Chabbi alimwambia, na Luis alipomtolea macho ya kuuliza, akamweleza kuhusu Zay, na kituko chote kilichosababisha zile kengele za moto kulia mle mjengoni mchana ule. Luis alikuwa juu vibaya sana. “Unaona? Yaani sasa hata watoto hao wanadiriki kuja hapa ofisini kwetu?” “Yule mpumbavu alikuwa anakuja kuulizia habari za rafikiye tu…kila kitu kitakuwa sawa Luis. Zay anayo makbarasha yale, na mi’ ntayapata tu!” Chabbi alimwambia. “Hujui usemalo Chabbi. Hebu sikia hii…” Luis alimwambia, na hapo akamweleza kinaga ubaga kile kilichopitikana pale ofisini baina yao na Inspekta Kwakwa. “Sasa unahitajika kuripoti kituoni na kujisalimisha kwa Inspekta Kwakwa, Chabbi. Ndani ya saa ishirini na nne!” Luis alimalizia, na Chabbi akamkazia macho. “Nadhani ulisema tunatakiwa tuamue ni nani aende selo kati yangu na nyinyi wakurugenzi…sasa vipi we’ unaamua moja kwa moja kuwa mimi ndiye niende?” Chabbi alimuuliza, na Luis akagwaya. “Ah, Chabbi…si unajua madhara kwa kampuni yatakavyokuwa ikiwa…” “Achana na hilo. Naelewa…mimi natakiwa niende kujisalimisha kutokana na tuhuma za kutoweka kwa Mwamtumu…” Chabbi alisema, na kubaki akiwa ameuma midomo kwa tafakuri. “Of Course wakili wetu atakuja kukutolea dhamana fasta tu utatoka, lakini cha msingi ni kwamba hakutakuwa na lolote la kukuonaisha na huyo binti. Na kwa maelezo yako ni kwamba hakuna. Vyovyote iwavyo, kusiwe na chochote cha kukuhusisha naye!” Luis alisema. “Si nimekwambia kuwa hilo nimelimaliza mchana huu Luis? Hakuna lolote la kuniungaisha na kupotea kwa yule binti sasa!” “Yah…safi sana! Limebakia hilo la wewe kwenda kwa Inspekta Kwakwa tu…” Luis alisema. Chabbi alipiga kimya kwa muda mrefu. Kisha akashusha pumzi ndefu, akapiga funda jingine la ile pombe yake, na kuinuka, “Sio taabu. Najua cha kufanya. Kisha nitaenda mwenywe kwa huyo Inspekta!” Alisema huku akitoka nje ya ofisi ile, akimwacha Luis akimtazama kwa mashaka. Nje ya ofisi ya Luis, Chabbi alimpigia tena Bilanga. “Yes Chabbi…nilikuwa nataka kukupgia sasa hivi. Kuna mengi ya kuongea…” Bilanga alimwambia. “Hakuna muda. Tunaelekea Mbagala sasa hivi!” Chabbi alimwambia, na Bilanga akapiga kimya kidogo. “Oh!” Hatimaye alisema. “Ndio. Tuna kazi ya kufanya kule!” Chabbi alithibitisha, na kukata simu. **** Nini kitatokea Mbagala? “NJOO TUTAFITI KESHO SAA MOJA ASUBUHI PANAPO MAJAALIWA…
Posted on: Fri, 27 Sep 2013 03:50:01 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015