A DAY TOO LONG SEHEMU YA 25 Ilipoishia.. “Kwa hiyo ratiba - TopicsExpress



          

A DAY TOO LONG SEHEMU YA 25 Ilipoishia.. “Kwa hiyo ratiba yako ipo vipi?” Bwana Mhina aliuliza. “Kesho nitakwenda katika chuo cha Uuguzi cha Muhimbili kuonana na rafiki yangu na kisha kuondoka wiki ijayo mara baada ya kuwaona wagonjwa wa magonjwa ya kansa ambao wanateseka hospitalini hapo” Abuu alimwambia Bwana Mhina. Songa nayo sasa…. “Wewe mtu unatisha sana, sikutegemea kama mambo yangekuwa namna hii kwa muda mchache” John alimwambia Abuu katika kipindi ambacho alikwenda kumsalimia katika chuo cha Uuguzi cha Muhimbili. “Kila kitu kilikuwa katika mipango ya Mungu. Mungu ameniumba hapa duniani ili watu wengine wapate nafasi ya kuishi kupitia mimi. Namshukuru sana mungu kwa hili” Abuu alimwambia John. Mara baada ya wanachuo kugundua kwamba mtu ambaye alikuwa pamoja na John kwa wakati huo alikuwa Abuu, mtu pekee duniani ambaye alikuwa akitengeneza dawa ya magonjwa ya kansa, wakaanza kumzunguka. Kila mmoja alikuwa haamini kama yule ambaye alikuwa akimwangalia ndiye alikuwa Abuu mwenyewe ambaye alikuwa amesababisha vita kati ya Marekani na nchi ya Afghanistan pamoja na kuleta uhasama mkubwa ambao bado ulikuwa ukizidi kuendelea kati ya nchi ya Marekani na india. Abuu alionekana kuwa kijana mdogo sana ambaye wala hakutakiwa kuwa kama vile ambavyo alikuwa katika kipindi hicho. Wanachuo zaidi ya mia saba wakamzunguka na kisha kuanza kuongea nae huku wakimuuliza maswali kadhaa ambayo yalikuwa yakihusiana na ugonjwa wa kansa pamoja na historia yake. Kwa wanafunzi ambao walikuwa na simu pamoja na kamera, wakaanza kumpiga picha Abuu pamoja na kupiga picha nae. Kwao, kwa wakati huo Abuu alionekana kuwa mtu wa tofauti kabisa, kila mtu alikuwa akimuona mtu huyo kuwa na mvuto mkubwa katika macho yake. Watu wakapigiana simu juu ya uwepo wa Abuu chuoni hapo jambo ambalo baada ya nusu saa tu, idadi kubwa ya watu wakaanza kumiminika katika eneo la chuo hicho hali iliyopelekea walinzi wa chuo hicho kufunga geti huku zaidi ya watu elfu tatu wakitaka kuingia ndani ya eneo la chuo hicho kwa lengo la kumuona Abuu na kuona anafanana vipi japokuwa walikuwa wakimuona sana katika vyombo vya habari Siku hiyo, Abuu aliitumia kuwa chuoni hapo. Uwepo wake mahali hapo ukaharibu ratiba nzima ya masomo, kila mmoja alikuwa akitaka kuongea na Abuu ambaye kwao alionekana kuwa mtu muhimu sana. Waandishi wa habari wala hawakukosa, nao walipopata taarifa, wakafika ndani ya eneo la chuo hicho kwa ajili ya kupiga picha kadhaa na kisha kuziweka katika magazeti yao katika siku inayofuatia. Abuu alipata nafasi ya kuwaelezea historia ya maisha yake. Historia yake ilionekana kumgusa kila mtu, hakukuwa na mtu aliyeamini kama Abuu alikuwa amepitia maisha yale ambayo alikuwa amepitia mpaka katika kipindi hicho. Kila mmoja alimuona Abuu kuwa mpiganaji hasa katika maisha yake, katika kila hatua ya maisha ambayo alikuwa akipitia, alikuwa akiishi kwa malengo makubwa. Saa kumi na moja Abuu akaondoka katika maeneo ya chuo hicho na kuahidi kuelekea katika hospitali ya Muhimbili siku inayofuatia. Kitendo cha watu kusikia kwamba Abuu angekuwepo katika hospitali hiyo kuanzia saa nne asubuhi, saa moja asubuhi siku iliyofuata zaidi ya watu elfu kumi na mbili walikuwa wamekusanyika katika hospitali hiyo. Kila mmoja alikuwa na shauku ya kumuona Abuu, kila mmoja alitaka kuhakikisha kwa macho yake kwamba Abuu alikuwa kijana mdogo kama magazeti yalivyokuwa yakisema au la. Hata picha zake ambazo zilikuwa zimetolewa katika vituo mbalimbali vya televisheni watu hawakuonekana kuziamini, walitaka kumuona kwa macho yao wenyewe. Saa nne, gari aina ya Benzi ya Mjerumani ikaanza kuingia katika eneo la hospitali ya taifa ya Muhimbili. Kila mmoja alikuwa na shauku ya kutaka kumuona Abuu, hata wale watu ambao walikuwa wamefika hospitalini hapo kwa ajili ya matatibabu, wakasahau maumivu yao, nao wakataka kumuona Abuu. Abuu alionekana kuwa na thamani katika kipindi hicho, alikuwa akionekana kama lulu katika maisha ya WaTanzania wengi. Fujo zikaonekana kutaka kutokea hospitalini hapo kiasi ambacho kikawafanya askari kuongezeka mahali kwa ajili ya kutuliza ghasia ambazo muda wowote ule zingewea kutokea kutokana na kila mtu kutaka kumuona Abuu. Ikaanza kuonekana fimbo yake ya kutembelea na hatimae Abuu kuteremka. Japokuwa moja ya sheria za hospitalini ni kutopiga kelele, watu wote wakajikuta wakipiga kelele za shangwe, kitendo cha kumtia Abuu machoni mwao kilionekana kuwa kama muujiza. Abuu akatembea kwa hatua chache na kisha kuanza kuwapungia watu mikono huku pembeni yake akiwepo Jasmin ambaye alikuwa amemshika mtoto wake, Zubeda Manesi na madaktari nao wakashindwa kuvumilia kabisa. Kila mmoja akaiona hiyo ndio kuwa nafasi pekee ya kumuona Abuu katika maisha yake, nao walikuwa wamesimama pembeni mwa watu waliokuwa mahali hapo wakimwangalia Abuu. Watu walikuwa wakimpiga picha Abuu ambaye alikuwa akitembea kwa hatua za taratibu. Msafara huo, hakuwa Abuu peke yake bali hata Makamu wa raisi, Bwana Adrian Mhina alikuwa pamoja nae. Abuu alitembea mpaka katika sehemu alipokuwa dokta mkuu wa Hospitali hiyo, Dokta Mwamboka na kisha kumsalimia. “Karibu sana Abuu” Dokta Mwamboka alimkaribisha Abuu. “Asante sana” Abuu aliitikia na kisha wote kuanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo. “Kwa siku, ni zaidi ya wagonjwa saba wanakuja hapa wakiwa na magonjwa mbalimbali ya kansa. Magonjwa haya yamekuwa yakiwatesa sana watu, kama tulivyokuwa na vyumba maalumu vya watu ambao wamevunjika viungo vya mwili kutokana na ajali mbalimbali hasa za pikipiki basi napo tuna chumba maalumu, chumba kikubwa ambacho humu kuna wagonjwa mbalimbali ambao wanaugua kansa katika miili yao” Dokta Mwamboka alimwambia Abuu. “Siupendi ugonjwa huu. Nitauchukia mpaka kifo changu” Abuu alimwambia dokta Mwamboka. “Huu ni ugonjwa unaotisha sana. Unawasumbua sana wanawake kutokana na matiti yao kuharibiwa sana na ugonjwa huu. Japokuwa dawa zako zimeanza kusambazwa lakini zimekuwa ngumu sana kupatikana katika bara la Afrika na ndio maana watu wanazidi kuteswa na magonjwa hayo” Dokta Mwamboka alimwambia Abuu ambaye alikuwa akilengwa na machozi. Bado walikuwa wakitembea tu. Katika kila hatua ambazo walikuwa wakipiga, waandishi wa habari walikuwa wakiendelea na kazi zao za kuwapiga picha kama kawaida yao. Safari ile ikaishia katika chumba kimoja kikubwa sana ambacho kilikuwa kimejaa vitanda ambavyo vilikuwa na wagonjwa kadhaa wa kansa. Abuu alipowaangalia watu wale tu, machozi yakaanza kumtoka. Kwa sababu muda huo ulikuwa ni muda wa kuwaangalia wagonjwa, watu ambao walikuwa wamekuja kuwaangalia wagonjwa ndani ya hospitali ile walikuwepo pamoja na wagonjwa wao huku wakiwa wamewaletea vyakula mbalimbali. “Kuna wanawake ambao wanasumbuliwa sana na kansa ya matiti. Asilimia tisini na nane ya wagonjwa wa kansa kwa wanawake wanasumbuliwa na kansa ya matiti ndani ya chumba hiki. Kwa wanaume, wengi wanasumbuliwa na magonjwa ya kansa ya vifua kama huyo mzee na vijana wale kule” Dokta Mwamboka alimwambia Abuu huku akimnyooshea kidole mzee mmoja aliyelala kitandani ambaye alikuwa na mwanamke mmoja aliyeonekana kuwa na majonzi. “Shikamoo” Abuu alimsalimia mzee yule mara baada ya kumfikia. “Marahaba” Mzee huyo aliyekuwa amelala aliitikia salamu ile kwa tabu huku akimwangalia Abuu. “Shikamoo mama” Abuu alimsalimia mwanamke ambaye alikuwa amekuja kumuona mzee huyo. “Marahaba kijana wangu” Mwanamke yule aliitikia. “Mzee anaumwa nini tena?” Abuu aliuliza huku akijifanya hajui. “Anaumwa kifua. Sijui ni kifua kikuu au sijui ni kifua cha kawaida, wala sijui” Mwanamke yule aliyejitambulisha kwa jina la Siwema alijibu. “Poleni sana. Ila dokta hajawaambia anasumbuliwa na nini?” Abuu aliuliza. “Kuna nesi alituambia kwamba ana kansa ya kifua” Bi Siwema alimwambia Abuu. “Ilianza vipi hiyo kansa?” Abuu aliuliza. “Alikuwa akivuta sana sigara hata kabla sijakutana nae alipotoka Afrika Kusini” Bi Siwema alijibu. “Baada ya hapo mlikwenda katika hospitali yoyote ile kuangalia afya yake?” Abuu aliuliza. “Hakuna. Hatukwenda. Kutokana na fedha ambazo alikuwa nazo katika kipindi hicho alikuwa akitumia dawa tu” Bi Siwema alimwambia Abuu. “Na wewe ulikutana nae kwa muda gani mpaka sasa?” Abuu aliuliza. “Ni muda mrefu sana. Si chini ya miaka ishirini iliyopita. Ni kipindi kirefu sana mpaka sasa hivi tuna watoto ambao wamemaliza kidato cha nne” Bi Siwema alimwambia Abuu. “Pole sana mgonjwa na pole sana mama kwa kuwa mvumilivu kumuuguza mzee” Abuu alimwambia Bi Siwema. “Asante sana” Bi Siwema alimwambia Abuu. “Ugonjwa wake umenigusa sana, sikutarajia kama ningekutana na mtu mwenye kansa ya kifua. Mama yangu alifariki kwa kansa ya matiti lakini nayo ilienea mpaka kifuani. Nilivyosikia ni kansa ya kifua ndio inamuweka hapa tena imetokana na uvutaji mkubwa wa sigara, imeniuma sana. Sijui unaniruhusu nipige nae picha japo ya ukumbusho?” Abuu alimuomba Bi Siwema. “Usijali baba yangu. Unaweza kupiga nae tu” Bi Siwema alijibu na kisha Abuu kupiga picha na mzee yule ambaye alionekana kuwa hoi kitandani pale. “Nashukuru sana mama kwa ruhusa yako. Ugua pole mzee wangu” Abuu alimwambia mzee yule. “Asante sana kijana wangu” “Usijali mzee wangu. Mimi ninaitwa Abuu, sijui wewe unaitwa nani?” Abuu alimuuliza. “Naitwa Selemani. Selemani Ramadhani” Mzee yule alijibu. “Jina lako ni kama la marehemu baba yangu. Ugua pole sana mzee wangu” Abuu alimwambia mzee Selemani. “Asante sana” Mzee Selemani alijibu na kisha Abuu kuondoka mahali hapo kwenda kuwatazama wagonjwa wengine ambapo napo huko aliendelea kuwafariji. ***** Tandi na Selemani walionekana kutokuwa na furaha kabisa, tukio la harusi ambalo lilikuwepo mbele yao lilionekana kuwahuzunisha kupita kiasi. Kila mmoja alikuwa akimpenda sana mwenzake katika kipindi hicho na ndio maana walijisikia vibaya sana endapo tukio lile lingekaminilika. Wakati mwingine Selemani alikuwa akijuta, alijuta sababu ambayo ilimfanya kuchelewa kuingia nchini Afrika kusini mpaka kukuta Tandi akiwa tayari ana mtu wake. Kuolewa kwa Tandi kulimaanisha kuwa mwisho wa kila kitu katika maisha yao ya uhusiano, hiyo ilimaanisha kwamba wasingeweza kulala pamoja wala kuishi pamoja. Tandi ndiye ambaye alikuwa akiumia zaidi, mapenzi, matunzo na moyo wenye kujali ambao alikuwa akionyeshewa na Selemani ndio ambao ulikuwa ukimfanya kujisikia vibaya zaidi. Alijua fika kwamba kwa Pokwane, asingeweza kuyapata yale ambayo alikuwa akiyapata kutoka kwa Selemani, yale ambayo Selemani alikuwa akimpa yalikuwa yakipatikana kwa wanaume wa KiTanzania peke yao katika bara hili la Afrika. Siku ziliendelea kukatika kama kawaida, alichokifanya Selemani kwa wakati huo ni kuanza kumchuna hasa Tandi. Kila siku alikuwa akimtumia kuchukua fedha kwa Pokwane jambo ambalo lilimpatia kiasi kikubwa cha fedha katika hazina yake. Zaidi ya randi milioni kumi zilikuwa kwenye hazina yake ambayo wala hakutaka ionekane na Tandi. Bado maisha yalikuwa yakiendelea, Tandi alijua fika kwamba angeweza hata kukataa kuolewa na Pokwane lakini kwa kufanya hivyo alikuwa akihofia juu ya maisha ya Selemani. Alijua fika kwamba kama angesema akatae na hatimae kuanza kuendelea kuishi na Selemani ambaye ni Mtanzania, basi kijana huyo angeuawa kutokana na chuki ambayo angekuwa nayo Pokwane. Alikuwa akikubali kuolewa na Pokwane kwa sababu tu alihitaji Selemani aendelee kuishi na ndio maana kila kitu ambacho alikuwa akikihitaji Selemani alikuwa akimpatia bila kuuliza swali lolote lile. Majonzi hayakuisha, kila siku walikuwa wakiendelea kuhuzunika kupita kiasi, harusi ile bado ilikuwa ikiwaondolea furaha kupita kawaida. “Kwa hiyo itakuwaje?” Nyerere aliuliza. “Bado sijajua itakuwaje” Selemani alijibu. “Ila ulifanya kama ulivyopanga?” “Kufanya nini?” “Kuchukua chapaa” “Hiyo kama kawa. Toka lini umeona watoto wa Kibongo tukichelewa kufanya maamuzi katika mambo ya fedha?” “Hahaha! Mimi nakukubali hapo tu, hurembi hata kidogo” Nyerere alimsifia Selemani huku wakigonganishiana mikono. “Ila tuache utani. Hivi nishauri nifanye nini juu ya huyu mwanamke” Pokwane alimuuliza Nyerere. “Kama vipi mtoroshe” “Nimtoroshe?” “Ndio. Sasa wewe unaogopa nini hapo? Mwanamke si unampenda na hutaki kumuona akiolewa na mtu mwingine. Mtoroshe tu” Nyerere alimwambia Selemani. “Kwa hiyo unamaanisha niende nae nchini Tanzania?” “Hiyo ndio maana yangu halisi” Nyerere alimwambia Selemani. “Ila si unajua sina vibali?” “Yeah! Ila njia za panya si zipo kwa ajili ya wasiokuwa na vibali? Tena kwako itakuwa rahisi kwa sababu unarudi nchini kwako” “Poa. Ngoja nijaribu kuchonga nae, mambo yakiwa mwake, nitatoroka nae” Selemani alimwambia Nyerere. Hilo ndilo wazo ambalo alikuwa ameambiwa na bila shaka aliliona kuwa la muhimu sana kuliko wazo jingine. Alichokifanya Selemani ni kumfikishia Tandi wazo lile ili aone ingekuwaje. Kwa Tandi, wazo lile likaonekana kufaa kupita kawaida, aliliunga mkono kwa asilimia mia moja. Wangeanzia wapi? Wangetoroka vipi? Hayo ndio maswali ambayo yalionekana kuwatatiza kwa wakati huo. Kutokuwa na vibali vya kusafiria kulionekana kuwa tatizo kubwa sana kwa Selemani, kama angekuwa na vibali hivyo, kuondoka nchini Afrika Kusini lisingekuwa jambo gumu, kingekuwa ni kitendo cha kupanda ndege na hatimae kuelekea nchini Tanzania tu bila kipingamizi chochote kile. “Nina wazo” Tandi alimwambia Selemani. “Wazo gani?” “Ngoja niwatafute wajanja watutengenezee vibali. Hawawezi kushindwa” Tandi alimwambia Selemani. Hilo ndilo lilikuwa wazo jingine ambalo liliafikiwa na lilitakiwa kufanywa kwa haraka sana. Alichokifanya Tandi ni kuwatafuta wajanja wa mjini na kisha kuomba kutengenezewa passport kubwa ambayo ingeonyesha kwamba Selemani alikuwa Mtanzania ambaye alikuwa amekuja hapo nchini Afrika Kusini mara moja. Kwa wajanja wa mjini, hilo halikuonekana kuwa tatizo, walichokihitaji ni randi elfu kumi na kisha kuanza kuangaikia ishu ambayo walikuwa wamepewa na Tandi huku tayari wakiwa wamepewa picha za passport saizi ambazo alikuwa amepiga Selemani. Ndani ya siku mbili tu, kila kitu kilikuwa tayari, passpoti ilikuwa imekwishaandaliwa na ilionyesha kwamba Selemani alikuwa Mtanzania ambaye alikuwa amefika tu nchini Afrika Kusini mara moja. Kila kitu kilichokuwa kimefanyika katika pasipoti ile kilionekana kuwa sawasawa na pasipoti yenyewe. Hazikuonekana kutofautiana hata mara moja jambo ambalo lilionyesha kwamba wajanja hao wa mjini walikuwa na watu katika kila sekta nchini hapo. Hawakuishia hapo, bado waliendelea kumtafutia vibali vingine mpaka vilipokamilika. Mpaka kufikia hatua hiyo, kila kitu kikaonekana kuwa tayari na ni safari ya kuelekea nchini Tanzania ndio ambayo ingeanza, wasingeweza kutumia ndege kwani walionekana kutokujiamini, usafiri ambao waliuona kufaa ni kutumia basi ambalo lilikuwa linapitia Mozambique, Malawi na hatimae kuingia nchini Tanzania. ******************************************** ***** Je nini kitaendelea..?? ITAENDELEA KESHO.....................
Posted on: Tue, 20 Aug 2013 14:28:50 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015