A DAY TOO LONG Sehemu ya - TopicsExpress



          

A DAY TOO LONG Sehemu ya 4 Ilipoishia … uwezo wake ulikuwa mkubwa ambao ungemfanya kuwa katika shule yenye watoto wenye vipaji, uwezo ambao ungewafanya wanafunzi wote kushangaa japokuwa alikuwa mlemavu wa mguu mmoja. Songa nayo… Maisha ya shule yalikuwa yakiendelea zaidi na zaidi. Hali ambayo ilikuwa ikitokea shuleni ilionekana kuwa kama changamoto katika maisha yake. Idadi kubwa ya wanafunzi walikuwa wamemtenga Abuu, ni idadi ndogo kabisa ya wanafunzi ndio ambao walikuwa wakionyesha upendo kwa Abuu. Hali ile ilionekana kumuumiza kupita kawaida, muda mwingi alikuwa akionekana kuwa na mawazo. Katika maisha yake alikuwa akitamani sana kuingia shuleni na kisha kuanza masomo jambo ambalo aliamini lingempa furaha zaidi lakini katika kipindi hiki hali ikaonekana kuwa tofauti na matarajio yake. Furaha yote ambayo alikuwa ameitarajia kuipata shuleni pale ilikuwa imepotea kabisa. Kutengwa na baadhi ya wanafunzi ikaonekana kutokumpa furaha kabisa. Ulemavu ambao alikuwa nao ndio ambao ulikuwa umemfanya kuwa katika hali ile. Ingawa wanafunzi wengi walikuwa wamemtenga huku wengine wakionekana kuwa karibu nae, ni mvulana John tu ndiye ambaye alionekana kuwa karibu nae sana. John ndiye mwanafunzi ambaye alikuwa karibu nae sana, mara kwa mara walikuwa pamoja huku wakipiga stori pamoja. Ukaribu wao haukuwa nje ya darasa tu bali hata darasani walikuwa wakikaa karibu karibu sana. Urafiki ule ukaonekana kudumu zaidi na zaidi, John akaonekana kuwa mtu muhimu sana katika maisha ya Abuu shuleni pale. John hakuwa ametoka katika familia ya kimasikini kama ilivyokuwa kwa Abuu, yeye alitoka katika familia ambayo ilikuwa na uwezo fulani kifedha. Fedha ambazo alikuwa akipewa kwa ajili ya matumizi ya shuleni, siku zote alikuwa akitumia pamoja na Abuu ambaye alikuwa hapewi fedha yoyote ya matumizi zaidi ya fedha ambayo alitakiwa kuitumia kama nauli mara aendapo na arudipo shuleni. Urafiki wao ulikuwa mkubwa kiasi ambacho kiliufanya shule nzima kuuona urafiki ambao ulikuwa wa ajabu sana. Ulemavu ambao aliendelea kuwa nao Abuu ulionekana kuwa kama kero kwa wanafunzi wengine. Maneno mengi yalikuwa yakiongelewa lakini kwa Abuu hakuonekana kujali kitu chochote kile. “Mmmh! Maisha haya yananifanya hata shule nimalize mapema niondoke” Abuu alimwambia John katika kipindi ambacho walikuwa wakinywa chai muda wa mapumziko. “Kwa nini?” John aliuliza. “Angalia watu wanavyoniangalia kwa jicho la chuki. Yaani kwa hali hii mpaka naichukia shule” Abuu alimwambia John. “Usijali. Utamaliza shule tu na kuondoka mahali hapa” John alimwambia Abuu. “Nitashukuru Mungu” Abuu alimwambia John. Maisha ya shule yaliendelea zaidi na zaidi mpaka katika kipindi cha majaribio mbalimbali ya mitihani yalipoanza shuleni hapo. Majaribio yale yakafanyika na Abuu kuongoza kwa kiasi kikuba sana. Kila mwanafunzi alionekana kushtuka, hawakuamini kama Abuu angeweza kuongoza kwa kiasi kile na wakati alikuwa amechelewa kufika shuleni hapo. Fitina zikaanza mahali hapo, wanafunzi wengi wakaanza kuwaambia walimu kwamba Abuu alikuwa akiingia katika chumba cha mtihani huku akiwa ameandika majibu ya mtihani katika gongo lake ambalo alikuwa akilitumia kutembelea. Maneno yale yakaonekana kumuumiza sana Abuu, mara kwa mara alikuwa akiitwa ofisini na kuulizwa na walimu juu ya zile tetesi. “Sijawahi kufanya kitu kama hicho” Abuu alimwambia mwalimu Mshana. “Sasa mbona kila mwanafunzi anasema hivyo?” “Sijui kwa nini mwalimu. Sijawahi kudanganya katika chumba cha mitihani” Abuu alijitetea. Mwalimu Mshana akachukua gongo ambalo alikuwa akilitumia Abuu kutembelea na kisha kuanza kuliangalia. Alichukua muda mrefu kidogo kuliangalia lile gongo kwa umakini, alipomaliza akamrudishia. “Umekwishayafuta majibu ya mtihani ambayo uliyaandika?” Mwalimu Mshana alimwambia Abuu. “Hapana mwalimu. Sijawahi kudanganya kwenye mtihani” Abuu aliendelea kujitetea. “Sawa. Nenda. Mwisho wa siku tutakuja kujua ukweli. Na kama tukifahamu kwamba unadanganya kwenye mitihani, tutakufukuza shule” Mwalimu Mshana alimwambia Abuu. Abuu akaondoka ndani ya ofisi hiyo, machozi yalikuwa yakimlengalenga, na alipofika nje ya ofisi hiyo tu, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake. Moyo wake ulimuuma sana, hakuamini kama jitihada ambazo alikuwa akizifanya kusoma ndizo ambazo ziliwafanya wanafunzi kuhisi kwamba alikuwa akidanganya katika mitihani ya shuleni pale. **** Baadhi ya wanafunzi wakabaki wakimwangalia Abuu ambaye alikuwa akitoka ndani ya ofisi ile ya walimu huku akilia. Wengi hawakujua ni sababu gani ambayo ilikuwa ikimliza Abuu katika kipindi kile japokuwa wengi wao walikuwa wakifurahia kuyaona machozi yake ambayo yalikuwa yakitiririka mashavuni mwake. Abuu alitembea kwa mwendo wa taratibu huku akitumia gongo lake mpaka kuingia darasani. Akatulia kitini huku akiwa ameinamisha kichwa chake juu ya meza na kuendelea kulia. Maneno ambayo aliongea mwalimu Mshana yalionekana kumchoma kupita kawaida, kitendo cha kusingiziwa kudanganya katika chumba cha mitihani kilionekana kumuumiza sana moyoni mwake. Kwa wanafunzi ambao walikuwa wakimchukia sana Abuu walionekana kuwa na furaha kupita kawaida, muda wote ambao walikuwa wakimuona Abuu akilia walionekana kuwa na furaha kupita kawaida. Abuu aliendelea kuwa katika hali ile mpaka pale rafiki yake, John alipokuja mahali hapo na kuanza kumfariji. Maneno ya faraja ambayo alikuwa akiyaongea John ndio ambayo yalionekana kumuumiza sana Abuu, alimfanya kuendelea kulia zaidi na zaidi mahali pale. John hakuacha kumfariji rafiki yake, alijua fika kwamba alikuwa katika kipindi kigumu shuleni hapo, kwa hiyo ukaribu wake pamoja na faraja yake ni vitu ambavyo vingemfanya kumtia moyo katika kila hatua ambayo alikuwa akipitia shuleni pale. Abuu hakutaka kuwa kimya, mara baada ya kufika nyumbani akaanza kumhadithia mama yake, Jamala juu ya kile ambacho kilikuwa kimeendelea shuleni kule. Jamala alionekana kuumia sana, maneno mbalimbali ambayo alikuwa akiambiwa mtoto wake yalikuwa yakimuumiza kupita kawaida. “Mungu atakuwa pamoja nawe” Jamala alimwambia Abuu. Siku zikaendelea kukatika, mitihani mingine ikazidi kufanyika shuleni pale. Hali haikuonekana kubadilika kabisa, bado Abuu alionekana kuwa juu kuliko wanafunzi wote wa kidato cha kwanza. Hali hiyo ndio ambayo iliwafanya walimu kuanza kumwangalia kwa mtazamo wa tofauti kabisa. Halikuwa jambo la kawaida kwa mwanafunzi yeyote shuleni pale kupata alama zote mia moja katika masomo yote saba. Abuu akaitwa tena katika ofisi ya walimu, katika kipindi hali ilikuwa ni tofauti kabisa, hakuitwa kwa sababu kulikuwa na tetesi za kudanganya kwenye chumba cha mtihani bali walimu walikuwa wakitaka kufahamu mengi kutoka kwake na kumpongeza katika kile ambacho alikuwa amekifanya shuleni pale katika mitihani ile. “Hongera sana” Mwalimu mkuu wa shule ile, Mkwasa alimwambia Abuu. “Asante” Abuu alijibu. Abuu akaonekana kuanza kuonyesha kile ambacho kilikuwa kichwani mwake katika kipindi hicho. Hakutaka kubaki nyuma katika masomo, alionekana kuwa mwanafunzi wa ajabu sana. Hakuwa akisoma sana kama wanafunzi wengine lakini kile ambacho alikuwa akikisoma au kufundishwa darasani kilikuwa akitoki kichwani mwake. Uwezo wake wa kukumbuka na kuelewa ulikuwa ni wa hali ya juu sana jambo ambalo hata wanafunzi wengine wakapigwa na mshangao kupita kawaida shuleni pale. Huyu Abuu ambaye alikuwa mlemavu, huyu Abuu ambaye alikuwa akitengwa na wanafunzi wengi shuleni pale ndiye ambaye akawa lulu katika kipindi hicho. Wanafunzi wengi wakahitaji msaada wake, walimu wengi ambao walikuwa wakiingia darasani na kufundisha, walikuwa wakimpa Abuu nafasi ya kuweza kuwafundisha wanafunzi wenzake pale ambapo hawakuwa wamepaelewa. Chuki ambazo zilikuwepo ndani ya mioyo mingine ya wanafunzi zikaanza kupotea, tayari Abuu akaonekana kuwa mtu muhimu sana katika masomo ya kila mwanafunzi. Miezi ikaendelea kukatika mpaka mitihani ya mwisho wa mwaka kuingia. Kama kawaida yake, Abuu alikuwa amefanya vizuri kwa asilimia mia moja jambo ambalo lilionekana kuwashangaza sana walimu. Tayari Abuu akaonekana kuwa mtu muhimu ambaye hakutakiwa kupotezwa shuleni hapo, walimu wakahitajika kuwa karibu na Abuu. “Huu mtihani hadi aibu” Mwalimu wa hesabu, Kenani aliwaambia walimu wenzake. “Vipi tena?” Mwalimu Lucy aliuliza. “Huyu Abuu Selemani amepata hesabu zote. Yaani nilijaribu kutoa hesabu ngumu lakini amepata zote” Mwalimu Kenani aliwaambia walimu wenzake. Hali hiyo haikuwa kwa mwalimu wa hesabu tu bali hata walimu wengine walikuwa wakizungumzia kitu hicho hicho. Mwisho wa mwaka huo Abuu alionyesha makali yake katika masomo yote shuleni. Hali ya kuwa na uwezo darasani haikuishia hapo, ilizidi kuendelea zaidi na zaidi mpaka pale walipoingia kidato cha pili na cha tatu. Katika miaka yote hiyo mitatu bado Abuu alikuwa akiendelea kuongoza kama kawaida yake. Wanafunzi wengi ambao walikuwa wakimtenga kutokana na ulemavu wake kwa wakati huu asilimia kubwa walikuwa marafiki zake ambao alikuwa akiwasaidia kila siku katika masomo. Kila mwanafunzi alikuwa na hamu ya kuwa karibu na Abuu ambaye alionekana kuwa na akili za kuzaliwa. Abuu hakutaka kuwa mbinafsi, bado alikuwa akiendelea kuwafundisha wanafunzi wenzake pale ambapo palikuwa pakihitajika msaada wake. Wasichana wengi wakatokea kuvutiwa na Abuu ambaye alionekana kuwa lulu shuleni hapo na hata katika shule za jirani ambazo huko napo alikuwa akiwaongozea katika kila mitihani ya wilaya ambayo ilikuwa ikifanyika mara kwa mara. Japokuwa alikuwa na uwezo mkubwa darasani na kumfanya kufaulu vizuri lakini moyo wake ulikuwa kama binadamu wengine. Kama walivyo binadamu wengine, Abuu nae akatokea kumpenda msichana mmoja ambaye alitokea kuvutiwa nae kupita kawaida. Msichana huyu alikuwa Jasmin Hamisi. Moyo wa Abuu ulikuwa kwenye mapenzi kwa asilimia mia moja kwa msichana Jasmin ambaye alikuwa hafahamu kama mvulana ambaye alikuwa akiongoza sana shuleni hapo tayari alikuwa ameangukia katika mapenzi yake. Kutokana na kutokuwa mtu wa wasichana kama vijana wengine, Abuu alikuwa akimuogopa sana Jasmin ambaye alikuwa na mvuto mkubwa machoni mwake. Kila siku Abuu alikuwa akijifanya kuwafundisha wanafunzi wengine lakini huku lengo lake likiwa moja tu, kuongea na Jasmin ambaye alionekana mkimya kupita kawaida. Moyo wake ulikuwa na hofu sana, hakujua kama ingetokea siku ambayo angeweza kusimama mbele ya Jasmin na kumwambia kwamba alikuwa akimpenda sana. Ni mara nyingi alikuwa akimuona Jasmin akiwa amekaa peke yake huku akiwa amezungukwa na viti vilivyokuwa wazi lakini Abuu hakuwa na uwezo wa kumfuata Jasmin na kumwambia ukweli juu ya jinsi alivyokuwa akijisikia moyoni mwake kwa wakati huo. Jasmin ndiye ambaye alikuwa moyoni mwake, kila alipokuwa akilala kitandani, mawazo yake yalikuwa yakimfikiria Jasmin tu. Kila siku usiku alikuwa akikata shauri kwamba siku inayofuatia ilikuwa ni lazima amfuate Jasmin na kumwambia ukweli juu ya jinsi alivyojisikia, lakini alipofika shule na kumuona Jasmin, woga ulirudi na hivyo kutokumfuata. “Mbona unamuangalia sana Jasmin?” John alimuuliza Abuu ambaye muda mwingi alikuwa akimkodolea macho Jasmin. “Ninampenda sana” Abuu alijibu kwa sauti ya chini. “Kama unampenda mfuate tu umwambie ukweli” John alimwambia. “Unafikiri ni kazi rahisi? Ni bora nipewe hesabu za kidato cha sita nizifanye nitaweza kuliko kumfuata Jasmin na kumwambia kuhusu hisia nilizo nazo moyoni mwangu juu yake” Abuu alimwambia John. “Kwa hiyo utateseka mpaka lini juu yake?” “Nafikiri mpaka pale nitakapoamua kumwambia ukweli” “Lini sasa?” “Sijui” Abuu alijibu kinyonge. Hiyo ndio ilikuwa hali ambayo ilizidi kuendelea zaidi na zaidi moyoni mwa Abuu. Jasmin, kwake alionekana kuwa kama malaika ambaye alishushwa duniani kwa makusudi ya kumjaribu yeye. Urembo wa Jasmin ulikuwa ukizidi kuuteka moyo wake kila siku. Kumfuata na kumwambia ukweli lilionekana kuwa jambo gumu sana kufanyika. “Au nimwandikie barua?” Abuu alimuuliza John. “Mmmh! Usifanye hivyo. Ushahidi huo” John alimwambia Abuu. “Ushahidi! Kivipi?” “Akikukataa na kuamua kuipeleka kwa walimu. Hauoni ni tatizo hilo” John alimwambia Abuu. “Kwa hiyo nifanye nini sasa?” “Mfuate na kumwambia ukweli” John alimwambia Abuu. “Haiwezekani hata kidogo. Hilo ni jambo gumu sana kufanyika kwani kama nikifanya hivyo halafu akinikataa, vile vile anaweza kwenda kuwaambia walimu” Abuu alimwambia John. “Afadhari iwe hivyo, hapo unaweza kujitetea kwamba haukumwambia maneno kama hayo” John alimwambia. “Unafikiri walimu wataniamini?” “Kwa nini wasikuamini?” “Kwa sababu Jasmin si kichaa mpaka aseme hivyo” “Kwa hiyo unaona uamuzi wa kuandika barua ndio mzuri?” “Ndio. Kwani naamini siwezi kuionea aibu karatasi wala kalamu” “Acha hizo Abuu. Hilo litakuwa tatizo kubwa. Kama ukishindwa kuongea nae, achana nae kuliko kuamua kumwandikia barua” John alimwambia Abuu. “Kwa hiyo unashauri kumwambia mdomo kwa mdomo ndio uamuzi sahihi?” “Ndio maana yake” “Basi ngoja nijaribu. Mmmh! Ila naogopa sana mpaka nashangaa wale wanaweza huwa wanakuwa na moyo gani” Abuu alimwambia John na kisha kuchukua gongo lake na kuanza kutoka nje huku akijipitisha karibu na kiti alichokuwa amekalia Jasmin. Mateso yakaongezeka zaidi moyoni mwake, kuumia kwake kukaongezeka zaidi na zaidi. Wivu wa mapenzi ukazidi kumkamata kila alipokuwa akimuona Jasmin akiongea na wavulana wengine iwe wa mule darasani au wavulana wengine wa vidato vingine. Bado alikuwa akitamani sana kumfuata na kumwambia ukweli lakini tatizo lilikuwa moja tu, uoga. Ingawa alikuwa kidato cha tatu lakini uoga juu ya wasichana ulikuwa mkubwa moyoni mwake, kila alipokuwa akimuona Jasmin machoni mwake, alikuwa akitetemeka huku mapigo ya moyo wake yakidunda kwa kasi sana. Mzunguko wake wa damu ulikuwa mkubwa kupita kawaida, Jasmin alionekana kuwa mtu wa tofauti moyoni mwake. Siku ziliendelea kukatika mpaka walipomaliza kidato cha tatu na kisha kuingia kidato cha nne. Bado hali iliendelea kuwa vile vile. Shuleni alikuwa akiendelea kuwaongoza lakini na moyo wake uliendelea kuumia zaidi na zaidi. Miezi ikakatika mpaka kufikia siku ambayo aliamua kumwambia Jasmin ukweli. Hakujali ni kitu gani kingetokea au angeonekana vipi mbele ya macho ya msichana huyo, kitu ambacho alikuwa akikitaka kwa wakati huo ni kuushusha mzigo mzito ambao ulikuwa moyoni mwake kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu. “Naweza kuongea nawe?” Lilikuwa swali ambalo Abuu alimuuliza Jasmin ambaye alionyesha tabasamu pana. “Yeah! Unaweza. Kuna nini?” Jasmin alimuuliza Abuu huku akitoa tabasamu pana ambalo lilimchanganya sana Abuu. “Ningependa kuongea nawe kipindi hiki” Abuu alimwambia Jasmin. “Kuongea na mimi! Kuhusu nini?” Jasmin alimuuliza Abuu. “Mahusiano” Abuu alijibu huku kwa mbali kijasho chembamba cha uoga kikianza kuonekana usoni mwake. “Mahusiano gani?” Jasmin aliuliza. Abuu akakaa kimya kwa muda, swali ambalo alikuwa ameulizwa mahali hapo lilikuwa jepesi sana kujibika lakini kulitoa jibu lake lilihitaji ujasiri wa hali ya juu. Hali ya uoga ikazidi kumuingia zaidi Abuu, mapigo yake ya moyo yakazidi kudunda zaidi, ujasiri wote ambao alikuja nao ukaanza kupotea. Katika kipindi hicho aliombea kitu chochote kitokee darasani hapo ambacho kingemfanya kuondoka mbele ya uwepo wa Jasmin. “Abuu” Jasmin alimuita. “Naam” “Mbona hauongei tena?” Jasmin alimuuliza. “Najaribu kukufikira kidogo” Abuu alimjibu. “Kunifikiria?” “Ndio” “Kunifikiria kuhusu nini?” “Uwezo wako wa kusoma hisia, yaani saikolojia ya mtu” Abuu alijibu. “Mmmh! Mbona unanichanganya?” “Usichanganyikiwe. Jaribu kusoma saikolojia ya mtu Jasmin” Abuu alimwambia Jasmin na kisha kuchukua gongo lake na kuondoka mahali hapo. Jasmin alibaki kimya huku akimwangalia Abuu ambaye alikuwa akiondoka taratibu kukifuata kiti chake. Maneno ya mwisho ambayo alikuwa ameyaongea yalionekana kuanza kujenga mambo fulani moyoni na akilini mwa Jasmin. Aliyafikira maneno yale kwa muda wa zaidi ya dakika moja, moyo wake ukaanza kupata hisia fulani juu ya maneno ambayo aliongea Abuu. “Ananipenda.” Jasmin alijisemea huku uso wake ukionyesha kuwa na tabasamu. Abuu alipokifikia kiti chake, akakikalia huku John akiwa pembeni yake akicheka kisirisiri. Abuu alionekana kutokuwa katika hali ya kawaida kabisa, alionekana dhahiri kuwa na hofu kubwa moyoni mwake. Akajiona kuutua mzigo mkubwa ambao ulikuwa umemuelemea moyoni mwake. “Vipi?” John alimuuliza Abuu. “Mmmh! Moyo unavyodunda……..naweza kufa muda wowote ule” Abuu alijibu na wote kuanza kucheka kisiri. ******************************* ****** Je nini kitaendelea? ***** ******Je Abuu ataweza kumpata Jasmin? ******Je ndoto alizokuwa nazo Abuu zitaweza kukamilika maishani mwake? ITAENDELEA.................
Posted on: Fri, 16 Aug 2013 04:59:22 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015