ALI KIBA:MSANII AMBAYE HATAISAHAU SINDERELA MAISHANI MWAKE Na - TopicsExpress



          

ALI KIBA:MSANII AMBAYE HATAISAHAU SINDERELA MAISHANI MWAKE Na Taji Hamza MUZIKI wa bongo flavor ni muziki ambao umetoa ajira kwa vijana wengi nchini,miongoni mwa vijana hao ambao wamepata ajira na kunufaika na muziki huo ni pamoja na Ali Salehe Kiba au maarufu kwa jina la Ali Kiba ambaye ni msanii hodari ambaye anatamba na nyimbo mbalimbali na ni nyota ambaye tangu nyota yake ing’are haijawahi kushuka. Unapozungumzia wasanii wenye mafanikio basi hauwezi kumuacha Ali Kiba,ambaye kupitia muziki ameweza kujiajiri na kupata mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi,kujulikana sehemu mbalimbali duniani na kubwa ni kukutana na kufanya nyimbo na mfalme wa R&B duniani Robert Kelly”R Kelly”. Ali Kiba anasema alianza muziki rasmi mnamo 1998 ambapo alikuwa anapenda sana kuimba nyimbo za mastaa mbalimbali wa kipindi hicho kama Joseph Mbilinyi”Mr 11”na wengine wengi,alikuwa anatamani siku moja na yeye aje kuwa kama wao,anasema alikuwa ana tabia ya kujifungua ndani na kuimba nyimbo za wasanii na hata pale alipokuwa njiani akielekea dukani alikuwa anafanya hivyo. . Ali Kiba ambaye alizaliwa mwaka 1986 jijini Dar es salaam,anasema kwa mara ya kwanza kusikika redioni ilikuwa ni mwaka 2002 akiwa ameshirikishwa katika nyimbo ya Ab Skilz iitwayo Maria yeye akiwa amepewa aimbe ubeti wa tatu. ”Nilijisikia raha sana kwa mara ya kwanza kuanza kusikika redioni,niliamini sasa ndoto zangu zinaweza kutimia kwani baada ya kushirikishwa katika nyimbo ile niliona milango ya heri ikianza kufunguka”. Mnamo Mwaka 2003 Ali Kiba alifanikiwa kupata rebo katika studio ya G records chini ya prodyuza ambaye kwa sasa ni marehemu G lover,kisha ndipo alianza kurekodi nyimbo,na nyimbo yake ya kwanza ilikuwa Sikuoni ambayo alikuwa amemshirikisha msanii mwenzake anayeitwa Zaharani . “Sikuoni,ilifanikiwa kunitangaza japo si sana,kidogo nilianza kupata matumaini na kuna baadhi ya watu walinifata na kuniambia waziwazi kuwa nina kipaji na kama nikiendelea hivi nitafika mbali”baada ya sikuoni ninilitoa nyimbo ya Njiwa ambayo kwa kweli ilinitangaza kwa kiasi kikubwa na nilianza kupata maonyesho mbalimbali. Ali Kiba alifunga kazi mara baada ya kutoa nyimbo ya Sinderela ambayo ilikubalika na watu wa aina zote”yaani kaka katika maisha yangu,sitakuja kusahau nyimbo ya Sinderela ni nyimbo ambayo imenipa mafanikio makubwa na ndio ilionitangaza hadi nje ya nchi,na albamu yake niliuza sana,naamini imenifanya niwe hapa nilipo”alisema. Sinderela ni nyimbo iliyompa umaarufu ndani na nje ya Tanzania.Baada ya Sinderela alitoa Nakshi nakshi Mrembo,Nichumu,Sabrina,Shamba,Najui ni kipi,ambayo amemshirikisha mdogo wake Abdu Kiba na Shababi ambayo aliwashirikisha Marlow na Mabovu. Mnamo mwaka 2008 ndipo alifanikiwa kutoa albamu ya kwanza iitwayo Sinderela na baada ya hapo ilifatia albamu ya pili Mali yangu,ambayo ilikuwa na nyimbo kama,Hadithi,Far away,Yaa karim,na nyingine nyingi,ila kwa sasa anakamilisha albamu ya tatu ambayo itakuwa inaitwa”Single Boy” Ali Kiba amepata tuzo mbalimbali za Kili Music Awards,mnamo mwaka 2009 Sinderela ilipata tuzo ya wimbo bora wa mwaka,na tuzo ya msanii bora wa kiume mwaka huohuo. Mwaka 2010 alitwaa tuzo ya mtungaji bora mashairi wa mwaka,na mwaka huu wimbo wake wa Dushelele umechaguliwa kuwa wimbo bora wa Zouk. Mbali na muziki pia Ali Kiba ni muigizaji ambaye pindi anapoigiza huipendezesha filamu,filamu ambazo ameshapata kuigiza ni Mrembo Kikojozi,na Mama”unajua mimi nina kipaji,siwezi kushindwa kuigiza ninaigiza pindi ninapopata nafasi,tatizo muda huwa unanibana sana,nakuwa ninakosa kufanya mazoezi na filamu husika ila ambao wameona baadhi ya filamu ambazo nimeigiza wanajua ninafanya nini” Ali Kiba ambaye ni mtoto wa kwanza kwa mama yake ana wadogo zake watatu ambao ni Abdul Salehe Kiba,Zabibu Salehe Kiba,na wa mwisho ni Abuu Kiba. Ali Kiba ana watoto wawili wa kwanza wa kike na wa pili wa kiume ambaye anaitwa Sam mwenye umri wa miaka mitatu,alisema kwa hapa nchini anawakubali na kuwapenda wasanii wote ila kwa kuwa alipewa nafasi chache,aliwataja baadhi ambao ni mdogo wake Abdul Salehe Kiba”Abdu Kiba”wa pili ni Dully sykes,wa tatu ni Chidi benzi pamoja na Waziri. Alipoulizwa kuhusu mahusiano alisema kuwa hivi karibuni anataraji kufunga ndoa na msichana ambaye bado hajamuweka wazi”ha ha ha kaka kwa sasa nipo single ila muda si mrefu nataraji kuingia katika maisha ya ndoa,muda ukifika nitakwambia ila kwa sasa sitaweza kukutajia hata jina,wewe kuwa na subira,kuna mambo yangu kidogo namalizia kasha nitakutaarifu rasmi nawe uje katika harusi”alimalizia. Akielezea mafanikio aliyoyapata kupitia muziki cha kwanza amefanikiwa kujenga nyumba tatu za Kifahari,Tabata amejenga mbili na Mbagala amejenga moja,ana shamba hekari tano lililopo Kiliuvya Madukani Mkoani Pwani,pia kafungua duka la Spea za magari lililopo Ilala Dar es salaam,anamiliki magari matatu,moja aina ya Honda,Mark 11,na Herrier.Ana Tax nne kwa ajili ya biashara ambazo humuongezea kipato. Akizungumzia malengo yake ya baadae ni kujitangaza zaidi nje ya nchi,pia kufungua kampuni yake ambayo itakuwa inajihusisha na masuala ya kuinua vipaji vya wasanii wachanga,pia amefanikiwa kufanya nyimbo na mfalme wa R&B kutoka Marekani R Kelly. “Kwa sasa nipo katika hatua ya kujitangaza zaidi,kufanya nyimbo na msanii mkubwa ni moja kati ya njia za kujitangaza,kutoka sehemu moja na kuelekea sehemu nyingine,kwangu mimi nimeona nimepiga hatua japo bado nina mipango mingi mbele ya kuwashirikisha wasanii wengine zaidi”alisema. Ali Kiba ameongea na mwandishi wa makala hii kwa njia ya simu akiwa nchini Marekani,akimaliza maonyesho nchini humo,ataenda Uingereza kisha atamalizia Uholanzi,anasema atarudi nchini Agosti 20 mwaka huu”kwa sasa hivi,mara nyingi nimekuwa nikipata maonyesho ya nje,yaani hauwezi kuamini huwa simalizi miezi mitatu,lazima niitwe huku” Aliongeza pia anamshukuru sana mama yake kwani ndiye anayesimamia kila kitu chake,anampa ushauri nini afanye na pindi anapokosea mama yake amekuwa mstari wa mbele kumuongoza”namshukuru sana mama yangu,yeye ndie kila kitu kwangu,amekuwa ananishauri mambo mema daima,pindi ninapokosea hunirekebisha kwa kweli najivunia na najidai sana pindi napokuwa na mama,naye haishi kunibariki kila mara” Pia aliomba mashabiki wake kusubiri albamu yake mpya ambayo ataitoa hivi karibuni itakayokuwa inaitwa Single boy kwani ndani yake kutakuwa na nyimbo nyingi kali ambazo amefanya ndani na nje ya nchi na amewashirikisha wasanii wa aina mbalimbali kama Waziri,D sample(ambao wapo chini ya rebo yake),Lady Jay Dee,na wengine wengi.
Posted on: Thu, 26 Sep 2013 15:54:32 +0000

Trending Topics




© 2015