Acheni kuonea watu, Rais awaagiza waendeshaji Operesheni - TopicsExpress



          

Acheni kuonea watu, Rais awaagiza waendeshaji Operesheni Tokomeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameagiza vyombo vya Serikali vinavyosimamia na kuendesha operesheni dhidi ya majangili wanaoua wanyamapori kutoonea wala kudhulumu watu wakati wanaendesha operesheni hiyo - Operesheni Tokomeza. Aidha, Rais Kikwete amesisitiza tena kuwa pamoja na matatizo yanayodaiwa kutokea wakati wa hatua ya mwanzo ya operesheni hiyo, bado Serikali itaendelea na operesheni hiyo yenye lengo la kukabiliana na majangili wanaua wanyama na hasa tembo na faru ili kupata pembe za wanyama hao. Rais Kikwete pia amewataka wananchi na hasa wafugaji kutokuingiza na kulisha ng’ombe katika hifadhi za taifa kwa sababu wanyama pekee wanaotakiwa kulishwa katika maeneo hayo ni wanyamapori tu. Rais Kikwete ameyasema hayo jioni ya jana, Alhamisi, Novemba 28, 2013, wakati alipohutubia maelfu ya wananchi kwenye Kituo cha Mabasi cha Meatu mjini Meatu akiwa kwenye siku ya tatu ya ziara yake ya tano katika Mkoa wa Simiyu. Baada ya kuwa amesikiliza malalamiko ya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kuwa baadhi ya maofisa wa Serikali wanaoendesha Operesheni hiyo wanaonea watu na kutaifisha mifugo yao, Rais Kikwete aliagiza: “Maagizo yangu siyo kuonea watu, siyo kudhulumu watu. Operesheni hii itaendelea lakini tusionee watu. Nataka kuona operesheni hii ikiendeshwa kwa madhumuni yake ambayo ni kupambana na majangili na wala siyo kuonea watu.” Rais amewataka wananchi wote ambao wanayo malalamiko ya kweli ya kukamatwa na kutaifishwa kwa mifugo yao, wawasilishe rasmi malalamiko yao Serikalini. “Kama kweli mtu ameonewa, ng’ombe wake wamekamatwa na kutaifishwa na maofisa wa Serikali atueleze kwa ndani malalamiko yake. Tajeni jina la mtu ambaye alidhulumu, tajeni idadi ya ng’ombe waliochukuliwa na eneo ambako walichukuliwa, mtu mwenye ukweli wa namna hiyo ana haki ya kudai na atalipwa.” Rais Kikwete leo, Ijumaa, Novemba 29, 2013, atakatisha ziara yake katika Mkoa wa Simiyu kwenda Kampala, Uganda ambako kesho atahudhuria mkutano wa mwaka huu wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, DAR ES SALAAM.
Posted on: Sun, 01 Dec 2013 09:17:24 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015