Hatima ya dhamana ya Sheikh Ponda Leo Morogoro. Uamuzi wa dhamana - TopicsExpress



          

Hatima ya dhamana ya Sheikh Ponda Leo Morogoro. Uamuzi wa dhamana ya mshtakiwa Sheikh Ponda Issa Ponda anayekabiliwa na mashtaka matatu unatarajia kutolewa Septemba 17 (leo) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, baada ya Mahakama hiyo kupitia vifungu vya sheria kutokana na upande wa utetezi kuwasilisha ombi la dhamana wakati upande wa mashtaka ukipinga dhamana ya kiongozi huyo. Ombi la dhamana ya Sheikh Ponda liliwasilishwa mahakamani hapo Agosti 28 na wakili wake, Juma Nasoro mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Richard Kabate baada ya wakili huyo kuiomba Mahakama kumpatia dhamana kiongozi huyo kwa madai kuwa kutokana na mashtaka hayo, mteja wake kisheria anayo haki ya kupatiwa dhamana. Pamoja na kuomba mteja wake kupatiwa dhamana, pia Wakili Nassoro aliwasilisha ombi la kupatiwa hati yenye maelezo ya mlalamikaji wa kesi hiyo ambaye ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani alidai kuwa anahitaji maelezo hayo kwa ajili ya kuandaa utetezi. Licha ya kuwasilishwa maombi hayo mahakamani hapo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Bernad Kongola ulipinga dhamana ya mshtakiwa huyo kwa madai kuwa ombi hilo halina msingi wowote na kwamba kutokana na cheti kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini DPP, kimepinga dhamana ya mshtakiwa huyo kwa maslahi ya usalama wa nchi. Kutokana na mvutano kati ya pande hizo mbili, Hakimu Kabate aliahirisha kesi ili aweze kupata nafasi ya kupitia vifungu mbalimbali vya sheria, ambapo leo atatoa uamuzi wa kumpa ama kutompa dhamana mshtakiwa huyo ambaye anakabiwa na shtaka la uchochezi, kuharibu imani za dini za watu wengine na kushawishi kutenda kosa ambayo aliyatenda Agosti 10 mwaka huu eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro. Pamoja na kutoa uamuzi wa dhamana, pia kesi hiyo itasomwa na kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa, kwani upande wa mashtaka ulidai kuwa umekamilisha upelelezi ambapo wanatarajia kupeleka mashahidi 15 na vielelezo zikiwamo DVD mbili na kibali cha kongamano la Eid lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri Mkoani Morogoro ambalo mshtakiwa alitenda makosa hayo akiwa katika kongamano hilo.
Posted on: Tue, 17 Sep 2013 05:07:08 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015