JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA FEDHA MAELEZO YA - TopicsExpress



          

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA FEDHA MAELEZO YA WAZIRI WA FEDHA KUHUSU MAJUKUMU YA WIZARA YA FEDHA KATIKA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI ULIOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA HABARI MAELEZO DAR ES SALAAM – JUMATATU, SEPTEMBA 23, 2013 WIZARA YA FEDHA P.O.BOX 9111 DAR ES SALAAM SEPTEMBA, 2013 1.0 UTANGULIZI Wizara ya Fedha imetoa mchango mkubwa katika kufikiwa kwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne katika kuendelea kutekeleza majukumu yake ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano na hivyo kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. 2.0 DIRA NA DHIMA YA WIZARA YA FEDHA Dira ya Wizara ya Fedha ni kuhakikisha kwamba uchumi unakua kwa kiwango cha juu na kupata matokeo yatakayonufaisha wananchi wote pamoja na kuhakikisha usimamizi thabiti wa fedha za umma na uwajibikaji. Aidha, Dhima ya Wizara ya Fedha ni kuhakikisha kunakuwepo ukuaji na utulivu wa uchumi mpana kwa kuandaa na kusimamia sera za fedha na uchumi. 3.0 MAJUKUMU YA WIZARA YA FEDHA Jukumu Kuu la Wizara ya Fedha ni kusimamia fedha za umma na uchumi. Hivyo, ni jukumu la Wizara ya Fedha kuhakikisha uwepo wa uchumi endelevu na tulivu, kuhakikisha utumiaji na mgawanyo wa rasilimali zilizopo kwenye sekta zenye matokeo ya haraka kwenye ukuaji wa uchumi na utoaji huduma kwa umma. Ili kufanikisha Dhima na Dira kama ilivyoelezwa hapo juu, Wizara ya Fedha inatekeleza majukumu yake kwa kutekeleza yafuatayo: i. Kuchambua na kubuni sera za uchumi jumla; ii. Kuratibu na kusimamia shughuli za kiuchumi pamoja na kuandaa miongozo ya uratibu na ufuatiliaji wa utekelezaji; iii. Kuandaa na kusimamia sera za mapato na matumizi ya Serikali; iv. Kuandaa na kusimamia sera za madeni na mkakati wa kuyadhibiti; v. Kuandaa na kusimamia sera za fedha na urari wa malipo na nchi za nje; vi. Kusimamia takwimu zote zinazohusu uchumi na Sekta ya Fedha; vii. Kusimamia Bajeti ya Serikali; viii. Kuratibu utekelezaji wa MKUKUTA; ix. Kusimamia matumizi ya fedha za Umma; na x. Kudhibiti fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi. 4.0 UTEKELEZAJI WA MALENGO YA SERIKALI Wizara ya Fedha katika kutekeleza majukumu yake inatekeleza malengo ya Serikali kwa ujumla. Hivyo basi, katika mwaka wa Fedha 2013/14, Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2013/14 na mfumo mpya wa utekelezaji wa vipaumbele vyenye Matokeo Makubwa na ya Haraka (Big Results Now-BRN); Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya Milenia 2015 (MDGs); Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010; na programu ya maboresho katika sekta ya umma. Lengo kuu ni kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Hivyo, Wizara ya Fedha inaendelea kutekeleza yafuatayo: Usimamizi wa Uchumi Jumla i. Ukuaji wa Uchumi Wizara imeendelea kusimamia ukuaji wa uchumi ambao umeonesha kuimarika na Pato la Taifa kuongezeka. Pato halisi la Taifa limekua kwa wastani wa asilimia 6.9 mwaka 2012 ikilinganishwa na 6.4 mwaka 2011. Katika robo ya kwanza inayoishia mwezi Machi, 2013 Pato halisi limekua kwa asilimia 7.5. Ili tuwe na uchumi endelevu utakaopunguza umaskini wa kipato, pamoja na mambo mengine ni muhimu uchumi ukue kwa asilimia 8 na zaidi kwa mwaka. Katika jitihada za kutathmini hali ya umaskini hapa nchini Wizara imefanikiwa kukamilisha zoezi la ukusanyaji wa takwimu za Utafiti wa Hali ya Mapato na Matumizi katika kaya binafsi ya mwaka 2012. Uchambuzi wa takwimu hizo unaendelea na unatarajia kukamilika kabla ya Desemba 2013. Sambamba na ukuaji wa Pato la Taifa, pato la kila mtanzania limeendelea kukua na kufikia pato la wastani la kila mtu shilingi 1,025,038 mwaka 2012 kutoka shilingi 770,464.3 mwaka 2010, sawa na ongezeko la asilimia 75. ii. Mfumuko wa Bei Lengo la Serikali ni kuthibiti kasi ya upandaji bei ili ibaki kwenye viwango vya tarakimu moja. Hata hivyo, kutokana na sababu kadhaa kama kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia, uhaba wa chakula nchini na nchi jirani mfumuko wa bei ulikuwa katika tarakimu mbili. Mwaka 2012 wastani wa mfumuko wa bei ulipanda na kufikia asilimia 16.0. Mwezi Desemba 2011, mfumuko wa bei ulifikia kilele cha asilimia 19.8. Hata hivyo, kutokana na juhudi zilizochukuliwa na Serikali mfumuko wa bei umeanza kurudi chini hadi kufikia asilimia 6.7 mwezi Agosti, 2013. Jitihada zilizochukuliwa ni pamoja na: a. Kuhakikisha kunakuwepo na chakula cha kutosha katika maeneo yenye upungufu; b. Kuongeza akiba ya chakula kwenye Wakala wa Taifa wa Chakula (NFRA); c. Kuhakikisha upatikanaji kwa wakati na matumizi ya pembejeo ikiwa ni pamoja na ruzuku ya mbolea, dawa na mbegu bora; d. Kutafutia ufumbuzi wa matatizo ya nishati ya umeme ili kuwa na umeme wa uhakika; e. Kupandisha kiwango riba kwenye amana za serikali kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40 kuanzia Desemba 24, 2012. iii. Mwenendo wa Biashara ya Nje Katika kipindi kilichoishia mwezi Julai 2013, mwenendo wa biashara ya nje ulikuwa mzuri ambapo thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje iliongezeka kwa asilimia 1.3 kutoka Dola za Kimarekani milioni 8,161.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2012 hadi kufikia Dola milioni 8,269.6. iv. Mapato ya Huduma Katika kipindi kilichoishia Julai 2013, mapato yatokanayo na huduma yaliongezeka kwa asilimia 13.9 hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 2,877.9. Hii ilitokana na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii na huduma ya usafirishaji ambayo kwa pamoja huchangia karibu asilimia 80 ya mapato yote yatokanayo na huduma. Mwenendo wa mauzo nje kwa baadhi ya bidhaa na huduma kwa kipindi kilichoishia Julai 2013 v. Bidhaa zilizoagizwa kutoka nje Thamani ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje katika kipindi kilichoishia mwezi Julai 2013 ilipungua kwa asilimia 0.7 kufikia Dola za Kimarekani milioni 12,877.6 ikilinganishwa na Dola za Kimarekani milioni 12,969.1 mwaka 2012. Upungufu katika uagizaji ulijitokeza zaidi katika malighafi za viwandani, mitambo, pamoja na bidhaa za matumizi ya kawaida. vi. Malipo ya Huduma Malipo ya huduma yaliongezeka kwa asilimia 2.1 kufikia dola za kimarekani milioni 2,391.8 katika kipindi kilichoishia Julai 2013. Hii ilitokana na kuongezeka kwa malipo ya huduma za usafirishaji wa mizigo kwenda na kutoka nchi za jirani. vii. Urari wa malipo ya kawaida (Current Accounts) Katika kipindi kilichoishia Julai 2013, urari wa malipo ya kawaida unaojumuisha urari wa biashara ya bidhaa, huduma, mapato ya vitega uchumi na uhamisho mali wa kawaida ulikuwa na nakisi ya dola milioni 4,234.8 ikilibganishwa na nakisi ya Dola za Kimarekani milioni 4,060.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. viii. Urari wa malipo yote na akiba ya fedha za kigeni Urari wa malipo yote umeendelea kuwa na ziada ambapo katika kipindi cha mapitio ulikuwa na ziada ya dola milioni 379.8 ikilinganishwa na dola milioni 331.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Kutokana na ziada hiyo, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola za Kimarekani milioni 4,353.4 (ukiondoa kiasi kinachotokana na uwekezaji wa mitaji ya kigeni ya moja kwa moja). Kiasi hiki cha akiba ya fedha za kigeni kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.3. ix. Kusimamia Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Fedha imeendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani. Mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani umeendelea kuwa mzuri kutokana na maboresho katika usimamizi wa kodi. Jumla ya mapato ya ndani (yakijumuisha mapato ya kodi, yasiyo ya kodi na vyanzo vya mapato ya Halmashauri) yameongezeka kwa asilimia 18.3 kutoka shilingi bilioni 7,221.4 mwaka 2011/12 hadi shilingi bilioni 8,542 mwaka 2012/13. Mapato ya kodi yanachangia wastani wa asilimia 90 ya makusanyo ya ndani. Kwa mwaka 2013/14, makusanyo ya kodi na yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 11,154.1. Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kuimarisha matumizi ya mashine za kielektroniki za kutoa risiti (Electronic Fiscal Devices-EFD) ambazo zimeunganishwa moja kwa moja na Mamlaka kwa mtandao wa kompyuta ili kuhakikisha Serikali inapata mapato yake stahiki. Kwa upande wa Matumizi, Wizara imeendelea kupanga matumizi kwa kuzipatia sekta muhimu zinazochochea ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma kama zilivyoainishwa katika vipaumbele vyenye matokeo makubwa na ya haraka (BRN) . Hayo yote yanafanyika kwa kuzingatia Sheria ye Fedha za Umma na Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 kama ilivyofanyiwa marekebisho Mwaka 2011. x. Usimamizi wa Deni la Taifa Wizara inasimamia deni la Taifa kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa Kusimamia Madeni na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 kama ilivyorekebishwa mwaka 2004. Kwa kuzingatia Sheria hiyo, mwaka 2012 Wizara ilifanya tathmini ya kuangalia uhimilivu wa Deni la Taifa na viashiria vyote vya kupima uhimilivu wa deni vilivyokubalika kimataifa vinaonesha kuwa, Deni la Taifa ni himilivu katika muda mfupi na muda wa kati. Mathalani, uwiano wa thamani ya sasa ya Deni la Taifa kwa Pato la Taifa ni asilimia 18.9 ikilinganishwa na ukomo wake wa asilimia 50. Matokeo ya Upimaji wa uhimilivu wa Deni la Taifa, Machi 2012 Kiashiria Matokeo (Asilimia) Ukomo (Asilimia) PV of Debt to GDP 18.9 50 PV of Debt to XGS 56.2 200 PV of Debt to Revenue 111.3 300 Debt Service to XGS 2.5 25 Debt Service to Domestic Revenue 5 35 Katika kuimarisha usimamizi wa Deni la Taifa, Wizara inakamilisha taratibu za kuanzishwa kwa Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa ndani ya Wizara ya Fedha. Aidha, Wizara inapitia upya Mkakati wa Kusimamia Deni la Taifa wa mwaka 2002 pamoja na kuifanyia marekebisho Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 iliyorekebishwa mwaka 2004. xi. Tathmini ya Uwezo wa Kukopa na Kulipa Madeni Serikali inaendelea na zoezi la nchi kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni (Sovereign Credit Rating). Kwa sasa, Serikali inajadiliana na makampuni yaliyoshinda zabuni ili kufanya tathmini kabla Serikali haijasaini mikataba na makampuni hayo ili yaanze tathmini. Kazi hii imepangwa kukamilika katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2013/14 ambapo itawezesha nchi kukopa kwa gharama nafuu katika masoko ya fedha ya kimataifa kwa ajili ya kugharamia miradi mikubwa ya miundombinu. Aidha, kampuni za Tanzania zitaweza kupata mitaji kwa urahisi zaidi kutoka kwenye masoko ya kimataifa. xii. Usimamizi wa Sekta ya Fedha Wizara iliendelea kutekeleza Sera ya Fedha yenye lengo la kupunguza ukwasi nchini ambapo Benki Kuu iliongeza mauzo ya fedha za kigeni katika soko la fedha za kigeni pamoja na mauzo ya dhamana za Serikali. Aidha, Benki Kuu ilipandisha kiwango cha chini cha fedha zinazotakiwa kuhifadhiwa Benki Kuu kwa ajili ya akiba ya amana za Serikali katika mabenki kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40, pamoja na kupunguza kiwango cha kuhodhi fedha za kigeni kulingana na mitaji yao kwa mabenki kutoka asilimia 10 hadi asilimia 7.5 kuanzia Desemba, 2012. Hatua hizo zilisaidia katika kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei usiojumuisha chakula na nishati (core inflation) kutoka asilimia 14.9 Agosti, 2012 hadi asilimia 6.9 Agosti, 2013. Vilevile, hatua hizi zilisaidia kuimarika kwa kiwango cha ubadilishanaji wa shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani. Thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani imeendelea kupangwa kwa kutegemea nguvu ya soko, ambapo Benki Kuu ya Tanzania hushiriki kwa dhumuni la kurekebisha ukwasi katika uchumi. Mwaka 2010, wastani wa thamani ya shilingi ya Tanzania ulikuwa sh. 1,395.7 kwa Dola moja ya Marekani ikilinganishwa na wastani wa sh. 1,571.7 kwa Dola moja ya Marekani mwaka 2012. Kutokana na jitihada za Benki Kuu za kuboresha ufanisi wa zana zake za kutekeleza Sera ya Fedha, ambapo kiwango cha kuhodhi fedha za kigeni kilipunguzwa kutoka ukomo wa asilimia 10.0 hadi asilimia 7.5 ya mtaji, kiliwezesha thamani ya shilingi kuserereka kwa kasi ndogo katika kipindi cha mwaka 2013. Hadi kufikia mwezi Agosti 2013, thamani ya shilingi ilikuwa wastani wa sh. 1,611.9 kwa dola ya Marekani. 5.0 ‘Big Results Now’ Kuhusu Mfumo Mpya wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo (Big Results Now – BRN), Serikali imedhamiria kwa dhati kutekeleza maeneo makuu sita yaliyobainishwa kama vipaumbele vya kitaifa katika kipindi cha muda wa kati. Maeneo hayo ni Maji, Nishati, Uchukuzi, Kilimo, Elimu na Utafutaji wa Mapato. Ili maeneo hayo yaweze kutekelezwa kwa ufanisi kunahitajika rasilimali fedha za kutosha. Hivyo, eneo la utafutaji wa mapato ni la muhimu katika kugharimia miradi mingine ya maendeleo toka katika maabara nyingine tano za mfumo wa BRN na hivyo kufanikisha upatikaji wa matokeo yaliyokusudiwa kwa kila sekta. Katika bajeti ya mwaka 2013/14, maeneo muhimu ya vipaumbele ambayo Serikali imeamua kwa makusudi kuyapatia rasilimali fedha za kutosha kupitia Bajeti ili kuleta matokeo makubwa na ya haraka ni pamoja sekta ya elimu iliyotengwa shilingi bilioni 3,127.9; Sekta ya Afya shilingi bilioni 1,497.8; sekta ya Kilimo shilingi bilioni 908.1; sekta ya Uchukuzi shilingi bilioni 2,177.3; Nishati na Madini shilingi bilioni 1,303.2; Muhimili wa Mahakama shilingi bilioni 273.1, Ardhi shilingi bilioni 108.3 pamoja na sekta ya maji shilingi bilioni 747.6. Maeneo haya yametengewa bajeti ya asilimia 68 ya bajeti ya Serikali ukiondoa Mfuko Mkuu wa Serikali (CFS). 6.0 Changamoto Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Wizara ya Fedha inakabiliwa na changamoto zifuatazo: i. Athari zilizojitokeza kwenye uchumi wa dunia (Mgogoro wa madeni katika nchi za Ulaya, upandaji wa bidhaa katika masoko ya dunia); ii. Athari kwenye hali ya hewa hasa ukame na kupelekea mahitaji makubwa ya ununuzi wa chakula cha akiba; iii. Kukosekana kwa umeme wa uhakika kunakotegemea vyanzo vya maji na uzalishaji wa kutumia mafuta pamoja na miundombinu chakavu ya kusafirisha umeme; iv. Uwezo mdogo wa mapato ya ndani kugharamia matumizi ya Serikali hasa miundombinu; na v. Kuongezeka kwa haraka kwa idadi ya watu kusikouwiana na ukuaji wa uchumi kunakopelekea mahitaji makubwa katika huduma za jamii. 7.0 Kukabiliana na Changamoto Katika kukabiliana na changamoto Serikali inafanya yafuatayo:- i. Kuhusu athari zilizojitokeza kwenye uchumi wa dunia kunakosababisha kupungua kwa misaada na mikopo nafuu kutoka nchi za Ulaya, Serikali inajitahidi kuboresha ukusanyaji wa mapato ili hatimaye ijitosheleze katika kugharamia ujenzi wa miundombinu pamoja na shughuli nyingine za Serikali. Aidha, Serikali inakamilisha kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni ili iweze kukopa kwa unafuu katika masoko ya fedha ya kimataifa; ii. Kuhusu athari kwenye hali ya hewa hasa ukame, Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji; kuongeza upatikanaji na utumiaji wa pembejeo za kilimo; kuimarisha huduma za ughani; na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya kilimo ili kuondokana na tishio la njaa; iii. Kuhusu kukosekana kwa umeme wa uhakika, Serikali inaendelea na mikakati ya kutumia gesi asilia kwa kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ili kuondokana na matumizi ya maji na mafuta katika kuzalisha umeme; iv. Kuhusu uwezo mdogo wa mapato ya ndani kugharamia matumizi ya Serikali hasa miundombinu, Serikali inaendelea kuimarisha matumizi ya mashine za kielektroniki za kutoa risiti (Electronic Fiscal Devices-EFD) pamoja na uanzishwaji wa maabara ya mapato unaosaidia kuibua vyanzo vipya vya mapato na usimamiaji mzuri wa maeneo yanayokusanya mapato; v. Kuhusu kuongezeka kwa haraka kwa idadi ya watu kusikouwiana na ukuaji wa uchumi, Serikali kupitia maeneo yaliainishwa kwenye “Big Results Now” yatachochea ukuaji wa uchumi kuwa mkubwa ikilinganishwa na ongezeko la idadi ya watu. 8.0 Hitimisho Kwa ujumla tungependa Taifa lifahamu kuwa utekelezaji wa malengo makuu ya Serikali unaendelea vizuri. Wizara inapenda kusisitiza kuwa changamoto zinazojitokeza hazitaathiri upatikanaji wa matokeo yaliyokusudiwa. Aidha, ieleweke kuwa changamoto kama hizi ni jambo la kawaida katika utekelezaji wa sera za uchumi na fedha mahali popote duniani na jambo kuu ni kubaini viashiria vyake mapema na kuvipatia ufumbuzi kabla ya madhara yake. Mwenendo wa Viashiria vya Ukuaji wa Uchumi, 2006 - 2012 2006 2007 2008 2009 2010 2011 2012 PATO LA TAIFA Ukuaji Halisi wa Pato la Taifa (mp) 6.7% 7.1% 7.4% 6.0% 7.0% 6.4% 6.9% Ukuaji Halisi wa Pato la Taifa (bp) 6.7% 7.2% 7.4% 6.0% 7.1% 6.4% 6.9% Ukuaji wa Pato la Taifa kwa bei za miaka husika (mp) 12.4% 16.8% 18.3% 13.8% 14.5% 16.2% 19.1% Ukuaji wa Pato la Taifa kwa bei za miaka husika (bp) 11.5% 16.7% 18.2% 13.6% 14.8% 16.3% 19.5% MWENENDO WA BEI Kasi ya upandaji bei (mwisho wa kipindi) 6.7% 6.4% 13.5% 12.2% 5.6% 19.8% 12.1% Kasi ya upandaji bei (Wastani wa mwaka) 7.3% 7.0% 10.3% 12.1% 7.6% 12.6% 16.0% GDP deflator inflation (fc) 4.5% 8.9% 10.1% 7.2% 7.3% 9.2% 11.7% GDP deflator inflation (mp) 5.3% 9.0% 10.1% 7.4% 6.9% 9.2% 11.4% UJAZI WA FEDHA Kiwango cha ukuaji wa M3 21.5% 20.5% 19.8% 17.7% 25.4% 18.2% 13.1% Kiwango cha ukuaji wa M2 16.7% 27.2% 24.4% 20.8% 21.8% 15.0% 16.0% Kiwango cha ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi 40.1% 43.1% 44.6% 9.6% 20.0% 27.2% 18.2% UWIANO WA MIZANIA YA MALIPO YA NJE NA PATO LA TAIFA Bidhaa zilizouzwa nje 13.4% 13.2% 17.3% 15.2% 18.8% 21.1% 21.0% Bidhaa na huduma zilizouzwa nje 24.1% 24.3% 26.9% 23.8% 27.6% 30.6% 30.2% Bidhaa zilizonunuliwa kutoka nje 27.1% 28.8% 33.8% 27.0% 31.0% 40.8% 36.2% Bidhaa na huduma zilizonunuliwa kutoka nje 35.8% 37.1% 41.9% 35.0% 39.1% 49.9% 44.5% Akiba ya fedha za kigeni (miezi) 5.0 4.8 4.3 5.7 5.4 3.7 3.8 UWIANO WA BAJETI YA SERIKALI NA PATO LA TAIFA Mwaka wa Fedha 2005/06 2006/07 2007/08 2008/09 2009/10 2010/11 2011/12 Mapato ya ndani 12.4% 14.1% 15.9% 16.2% 15.4% 16.3% 17.6% Matumizi 23.5% 23.0% 22.8% 25.7% 27.0% 26.6% 26.2% Matumizi ya Kawaida 15.7% 16.2% 14.9% 17.7% 18.3% 19.0% 17.0% Matumizi ya Maendeleo 7.7% 6.9% 7.9% 8.0% 8.6% 7.6% 9.2% Misaada 6.0% 5.0% 6.9% 4.7% 4.6% 4.7% 4.5% Nakisi (kabla ya misaada) -10.8% -9.9% -8.6% -9.3% -11.0% -11.6% -9.6% Nakisi (baada ya misaada) -4.8% -4.9% -1.7% -4.5% -6.4% -6.9% -5.0% Mikopo ya nje 3.3% 3.7% 3.2% 3.6% 4.6% 3.4% 4.2% Mikopo ya ndani (kutoka benki) 0.8% 0.1% -1.4% 0.8% 1.9% 2.6% 0.2%
Posted on: Mon, 23 Sep 2013 10:57:27 +0000

Recently Viewed Topics




© 2015