MTUME MUHAMMAD (swallallahu alaihi - TopicsExpress



          

MTUME MUHAMMAD (swallallahu alaihi wasallam) ..SUNNA-SIYRAH.....RAHMA KWA WALIMWENGU SEHEMU YA TANO Utawala Wa Makka Nabii Ismaa’iyl (‘Alayhis Salaam) aliishi miaka 137, na muda wote huo yeye ndiye aliyekuwa mkuu wa mji wa Makkah, na baada ya kufa kwake walitawala wanawe wawili Nabit kisha Qaydaar, na riwaya nyingine zinasema kinyume cha hivyo, yaani kwanza Qaydaar kisha Nabit, kisha akatawala ...babu yao Mudhaadh Al-Jurhumiy, na kutoka hapo utawala wa Makkah ukaingia mikononi mwa watu wa kabila la Jurhum. Watoto wa Nabii Ismaa’iyl waliendelea kuwa na heshima kubwa sana hapo Makkah, lakini mambo yote ya kuhukumu nchi yalikuwa mikononi mwa Jurhum, walioendela kutawala miaka mingi huku wakitumia vibaya mali iliyokuwa ikipatikana kutokana na Al-Ka’abah, jambo lililojenga chuki kubwa baina yao na baina ya ‘‘Adnaaniyiin walioamua kushirikiana na watu wa kabila la Khuzaa na kulipiga vita kabila la Jurhum. Jurhum walishindwa na kutolewa nje ya Makkah, na hatimaye wakarudi Yemen. Walipokuwa wakihama, watu wa Jurhum walikifukia kisima cha maji ya Zamzam kisiweze kujulikana tena, wakaondoa alama zote za karibu yake ili kuwanyima watu wa Khuzaa heshima ya kukimiliki kisima hicho, na wakazika ndani yake jiwe jeusi pamoja na panga na dhahabu nyingi. Anasema Al-Mubaarakpuri katika ‘Ar-Rahiyq Al-Makhtuum’; “Inakadiriwa kuwa zama za Nabii Ismaa’iyl ni karne ishirini kabla ya kuzaliwa kwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) na kwa ajili hiyo inakisiwa kuwa Jurhum waliishi Makkah muda wa karibu karne ishirini na moja na walitawala muda wa karibu karne ishirini, kisha utawala ukashikwa na watu wa kabila la Khuzaa.” Yemen Watu wa kabila la Saba-a wanajulikana kuwa ni katika makabila ya zamani sana waliotawala nchi ya Yemen tokea mwaka 650 kabla ya kuzaliwa kwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam), isipokuwa katika mwaka wa 115 kabla ya kuzaliwa kwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) hadi mwaka 300 baada ya Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) kulitokea mapambano mengi ya wenyewe kwa wenyewe na mapinduzi mengi katika nchi ya Yemen, na utawala ukawa unabadilika mara kwa mara ukitoka mikononi mwa watu wa kabila la Hamyar na kurudi tena katika mikono ya Saba-a nk. jambo lililowafanya wawe chambo chepesi kwa Mataifa mengine, yaani vita vya panzi neema ya kunguru. Katika mwaka 340 baada ya Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) Wahabashi wakaitumia fursa hiyo ya kupigana watu wa Yemen wenyewe kwa wenyewe kwa kuivamia kwa mara ya mwanzo nchi ya Yemen baada ya kusaidiwa na Warumi waliotangulia kuuteka mji wa Aden. Wahabashi wakaendelea kuitawala nchi ya Yemen mpaka mwaka 378 baada ya Nabii ‘Iysa walipopata uhuru wao Katika mwaka wa 523 baada ya Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) Myahudi mmoja aitwae Nuwaas aliwapiga vita watu wa Najran[5] na kuwalazimisha kuiacha Dini waliyokuwa wakiifuata ya Nabii ‘Iysa na kuingia Dini ya Kiyahudi, na walipokataa akachimba mahandaki makubwa na kuwasha moto ndani yake kisha akawa anawatupa ndani ya moto huo kila aliyekataa kufuata Dini yake, na hii ndiyo tafsiri ya kauli ya Allaah Aliposema: “Wameangamizwa watu waliowaadhibu Waislamu katika mahandaki. Yenye moto wenye kuni (nyingi).” Suratul Buruuj – 4-5 Kutoka siku hizo Warumi walianzisha kampeni kubwa ya kuziteka nchi za Kiarabu huku wakiwasaidia Wahabashi katika kutayarisha jeshi kubwa, wakawasaidia pia kuunda merikebu za vita, na katika mwaka wa 525 baada ya Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) Wahabashi wakafanikiwa kuiteka nchi ya Yemen kwa mara ya pili chini ya uongozi wa Irbat, na mfalme wa Uhabashi akampa Irbat ugavana wa Yemen na akatawala mpaka alipouliwa na Abraha Mhabashi aliyekuwa mmoja katika majemadari wa jeshi la Uhabashi, na Abraha huyu ndiye aliyepeleka jeshi lake Makkah likiongozwa na tembo kwa nia ya kuibomoa Al-Ka’abah, waliokuja kujulikana kwa jina la ‘Asw-haabul Fiyl’. Baada Wahabashi kujaribu kuibomoa Al-Ka’abah, watu wa Yemen walighadhibika sana, kwa sababu waarabu wote walikuwa wakiiheshimu sana nyumba hiyo ya Allaah, na kwa ajili hiyo wakaomba msaada kutoka nchi ya Faris (Uajemi), na kwa pamoja wakafanikiwa kuwashinda Wahabashi na kuwatoa nje ya Yemen, wakawa huru chini ya uongozi wa Muad bin Yukrab bin Sayf bin Dhiy Yazin Al Hamyariy aliyejitangazia ufalme wa nchi hiyo, huku wakiwa chini ya himaya ya Waajemi mpaka nchi ya Yemen yote ilipoingia katika Uislamu mwaka 638 baada ya Nabii ‘Iysa. Shaam na Iraq Utawala katika nchi za Sham na Iraq ulikuwa ukiogelea ndani ya mkondo ule ule waliokuwa wakiogelea ndani yake watu wa Yemen na watu wote wa zama hizo katika kupigana vita, mara wenyewe kwa wenyewe na mara nyingine wakipigana dhidi ya Waajemi na mara nyingine wakipigna na Waroma. Utawala wa nchi hizo ulikuwa ukibadilika mara kwa mara ukitegemea nguvu za mtawala. Mara ulikuwa chini ya ufalme wa Waajemi na mara nyingine chini ya makabila ya Kiarabu, na mara nyingine chini ya Waroma, isipokuwa nchi ya Hijaazi ilikuwa na shani kubwa mbele ya waarabu waliokuwa wakiitukuza sana na kuiheshimu kwa sababu ya kuwepo kwa nyumba ya Allaah ‘Al-Ka’abah’ katika ardhi yake, lakini watawala wa nchi hiyo hawakuwa na uwezo wa kupambana na majeshi makubwa kama ilivyokuwa pale Abraha alipokuja na jeshi lake kutaka kuibomoa Al-Ka’abah. ITAENDELEA....
Posted on: Thu, 12 Sep 2013 11:52:35 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015