Mpenzi Msikilizaji wetu Habari za siku nyingi tum,erejea tena na - TopicsExpress



          

Mpenzi Msikilizaji wetu Habari za siku nyingi tum,erejea tena na sasa tunakukaribisha katika kipindi cha Global Planet ambacho kinaletwa kwako na sisi watanmgazaji wako Stephano Jonasi Simbeye na Bosco Nyambege katika yafuatayo tuliyokuandalia:- Gp Agost 7 SAIKOLOJIA NA MAISHA Kujiamini na kutojiamini Kujiamini: Kujiamini ni kuishi ukiwa kama wewe uliyekamilika, ukiwa huhitaji kitu kingine chochote ili kukukamilisha. Kutojiamini: Ni pale mtu anapojipa maoni ya chini kuhusu yeye na kujiona ni mtu ambaye thamani yake kama binadamu ina walakini, na kuhisi umepungukiwa vitu vingi ambavyo wengie wanavyo. Watu wasiojiamini huwa na uhusiano mbaya na wenzao. Hii inatokana na ukweli kwamba, ni pale tunapoamini katika sisi, ndipo tunapoweza kuamini katika wengine. SABABU ZA KUTOJIAMINI Sasa kama kila mmoja alizaliwa akiwa na thamani yake iliyokamilika, nini kimetokea hadi kufikia watu wengi wakaanza kuamini kwamba wana thamani ndogo au kubwa kuliko wengine? Misingi na ukweli wa imani hii unaanzia mbali kidogo. Kama tulivyokwisha kueleza katika mada zilizotangulia, kila mmoja wetu alisaidiwa na wazazi au walezi, mazingira, uzoefu wa kimaisha na jamii kwa ujumla, kujua yeye ni nani na kuyajua maisha kama anavyoyajua leo. Kila mmoja wetu aliambiwa yeye ni mtu wa namna gani, aliambiwa maana ya maisha kwa namna yake na akapangiwa hata thamani yake na kupangiwa pia ya wengine. Kuna sababu kuu tatu zinazosababisha kutojiamini kwa watu wengi. Sababu hizo ni kama ifuatavyo: 1. Wazazi na walezi Mara zote, mtoto huamini kwa asilimia mia moja kila kitu anachoambiwa na mzazi (baba au mama), kwa kuwa hao ndiyo mashujaa wake. Hata kama anachoambiwa na kuaminishwa siyo sahihi, kwa kuwa kimetoka kwa wazazi, mtoto hukichukua na kukiamini na anapokuwa mkubwa kuanza kukifanyia kazi kile alichoambiwa akiwa mdogo. Kwa bahati mbaya, wazazi wengi huwafundisha watoto wao mambo mabaya wakiamini kuwa kwa kuwa bado ni wadogo, hawaelewi chochote. Hili ni kosa kubwa ambalo ndiyo limekuwa chanzo cha kizazi hiki cha sasa kukosa muelekeo wa kimaisha. Kwa mfano mtoto anayegombezwa mara kwa mara, anayenyanyaswa na kuteswa, anayeoneshwa kuwa hapendwi, hathaminiwi wala hakuna anayemjali, unategemea aje kuwa mtu wa aina gani akiwa mtu mzima? Mtoto anayekulia katika dimbwi la umaskini, anayeshuhudia wazazi wakigombana kila kukicha, anayewaona wazazi wake wakitopea kwenye ulevi wa kupindukia na tabia nyingine hatarishi kama umalaya n.k, unategemea atakuja kuwa mtu wa namna gani? Wataalamu wa mambo ya mawazo ya kina na akili, wanaeleza kuwa kile ambacho mtoto anafanywa akiamini, ndicho atakachokitumikia akiwa mkubwa. Kama aliambiwa kizuri, atakitumikia jinsi kilivyo, kama aliambiwa kibaya atakitumikia pia bila kujali, kwa kuwa tu aliaminishwa na mashujaa wake, wazazi. 2. Mazingira Mazingira anayokulia mtu, huwa yana athari kubwa sana katika maisha yake ya baadaye. Tunaposema mazingira, tunamaanisha kila kitu kinachotuzunguka. Hii ni kuanzia watu wa nyumbani, shuleni, majirani, wapita njia, wafanyakazi wenzetu, wake au waume,wapenzi wetu n.k Wote hawa wana nafasi kubwa sana ya kutujenga au kutubomoa kutokana na maneno na vitendo vyao kwetu. Kama kwa wakati fulani walituambia kuwa sisi tuko hivi au vile, na tukawaamini, ni wazi sauti zao tunatembea nazo na zinatuamuru kuwa au kutokuwa namna fulani. Kwa bahati mbaya zaidi ni kwamba kimazoea hawa wote huwa wanatuambia na kutufanyia mambo mabaya, ambayo baadaye huwa tunayaamini kuwa yako sahihi na tunayahifadhi akilini mwetu tayari kwa matumizi tukiwa wakubwa. Hii huwa ni sababu kubwa sana ya watu wengi kushindwa kujiamini. Itaendelea wiki ijayo... HABARI MUHIMU MOMBA Madiwani wilayani Momba mkoani mbeya wametakiwa kusimamia ipasavyo fedha za serikali pamoja na zinazotolewa na wafadhili ili kufanya kazi iliyokusudiwa na kuleta maendeleo kwa wananchi. Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya hiyo Abiud Saidea wakati wa kikao cha baraza lamadiwani kilichofanyika Ukwile wilayani Mbozi. Amesema endapo halmashauri inapata hati chafu ina maana madiwani nao wamechangia kwani ni jukumu la jukumu lao kuhakikisha fedha hizo zinafanya kazi katika miradi iliyokusudiwa Ameongeza kuwa baadhi ya halmashauri huenda zikapata hati chafu kutokana na usimamiaji mbovu wa masuala ya fedha hizo. Aidha amesema endapo halmashauri ikipata hati chafu basi itakwamisha miradi yake kwani wafadhili hawatoi pesa kwa halmashauri ambayo zina hati chafu. Mbali na hilo amewasihi madiwani wilayani hapo kusimamia vizuri mapato ya wananchi kwani mavuno kwa mwaka huu inaonesha ni mengi lakini mapato ni kidogo. MBOZI Wananchi wa wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya wametakiwa kulinda na kutunza misitu kama rasilimali muhimu kwa matumizi ya sasa na kwa faida ya vizazi vijavyo. Akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake Afisa Mazingira Msaidizi wilaya ya Mbozi, Richard Mwailanga amesema jinsi siku zinavyozidi kwenda, wilaya inazidi kupoteza sifa ya kuwa na Misitu kutokana na shughuli za kila siku za binadamu kama kilimo cha kuhamahama, uchomaji mkaa, uchomaji moto pamoja na ufugaji holela. Amesema serikali imetenga maeneo ya Utambalila na Isenzanya ili yatumike kwa ajili ya shughuli za uchomaji wa mkaa kwa kibali maalumu kutoka katika halmashauli ya wilaya kwa kuwa mkaa umekuwa ni nishati muhimu kwa maisha ya watu . Aidha ameitaja baadhi ya misitu inayokabiliwa na tishio la kupotea kuwa ni pamoja na msitu wa Longisonte, Fonera na Ntanzu unaohalibiwa iliyopo katika tarafa ya Vwawa. Mwailanga amesema iwapo wananchi watakosa ushirikiano na serikali katika kutunza na kulinda misitu watajikuta wanakosa mahitaji muhimu yanayotokana na misitu. Amesema ,serikali imeandaa mkakati maalumu ili kubaini na kuwakamata wale wote wanaohusika na uharibifu wa mazingira maeneo ambayo hayajaruhusiwa Edward Kapinga ambaye ni mkazi wa Vwawa amekili kuwa yeye ni miongoni mwa watu wanaoharibu misitu kwa shughuli za mkaa na kusema kuwa tatizo kubwa ni kukithiri kwa wimbi la umasikini Kapinga amesema kitendo cha serikali kutenga maeneo mawili kwa ajili ya uchomaji mkaa, hakiwezi kusaidia chochote kwani maeneo hayo ni machache ukilinganisha na mahitaji ya watu wanaoishi maeneo hayo . MAUJI MBALALI Mkazi wa kijiji cha Ulambule wilayani Mbarali Juma Adamu (22) ameuwawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kundi la watu walioamua kujichukulia sheria mkononi baada ya kukutwa akiiba mpunga shambani kwa Emmanuel Erasto(24). Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kamishina msaidizi wa polisi Diwani Athumani amesema tukio hilo limetokea Agosti 5 mwaka huu saa 4 usiku Amesema Jeshi la Polisi linamshikiria mmiliki wa shamba hilo zinanywa ili afikishwe mahakamani. Mbeya. Imeelezwa kuwa Serikali inapoteza zaidi ya Shilingi 40 bilioni kila mwaka zinazotokana na uzalishaji wa zao la mpunga wilayani Mbarali kutokana na kukosa miundo mbinu ya barabara na nishati ya umeme maeneo yenye uzalishaji huo. Meneja wa Chama Cha Ushirika wa Kilimo na Masoko cha Madibira (Mamcos), kata ya Madibira Wilayani Mbarali, Charles Kadio amebainisha hilo wakati akizungumza na waandishi wa habarii kwenye banda la maonyesho ya wakulima nane nane katika viwanja vya John Mwakangale vilivyopo Jijiji Mbeya. Kata ya madibira ni miongoni mwa maeneo maarufu kwa kilimo na uzalishaji wa zao la Mpunga katika wilaya ya Mbarali ambapo ndani ya mradi wa shamba hilo kuna hekta 15,000 na nje ya mradi huo kuna zaidi ya hekta 15,000 na kwamba kila mwaka pato lake ni zaidi ya shilingi 40bilioni. Amesema changamoto ya barabara mbovu wilayani humo ni kikwazo kikubwa cha kuzorotesha uchumi kwani wakulima na wafanyabiashara wanashindwa kusafirisha mazao yao toka shambani kwenda Sokoni. Aidha Serikali iliwapelekea mashine kubwa ya kukoboa mpunga ambayo ilinunuliwa kwa shilingi 1.1 bilioni na kuifunga tayari kwa kuanza kufanya kazi lakini mashine hiyo haifanyi kazi kutokana na kukosa nishati ya umeme. Kadio amesema mashine zinazotumika kukobolea mpunga katika wilaya hiyo zinatumia diseli ambayo ni ghari hivyo kushindwa kumudu gharama za uendeshaji. Ameongeza kuwa bei ya kukoboa gunia moja la mpunga la kilo mia moja ni elfu 60,000 na bei ya mchele gunia moja la kilo mia moja ni shilingi 120,000 hivyo kuonyesha wazi kupotea kwa fedha nyingi . Mbeya. Wafanyakazi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (Nssf) Mkoa wa Mbeya, wametoa msaada wa vyakula kwa watoto yatima na waishio katika mazingira magumu eneo la Soko matola Jijini Mbeya ili waweze kusherekea sikukuu ya Iddi. Msaada huo uliotolewa na wafanyakazi hao ambao umegharimu kiasi cha shilingi laki sita ni Mchele kilogramu 160, mafuta ya kupikia plastiki moja, Chumvi katoni moja na Mbuzi wawili. Watoto hao wapatao 30 wamekusanywa na viongozi wa dini ya kiislamu katika madrasa ya Ittihal iliyopo eneo hilo. Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Meneja wa Nssf Mkoa wa Mbeya, Robert Kadege, amesema wafanyakazi wa shirika hilo maeneo mbalimbali wamekuwa na utamaduni wa kujichanga na kuisadia jamii isiyojiweza wakiwemo watoto waishio katika mazingira magumu. Amesema wamekuwa wakiguswa wanaposikia ama kuaona watoto yatima wakiwa wanaranda randa mitaani baada ya kuwakosa wazazi ama walezi. Aidha, Meneja huyo alisema jitihada zinazofanywa na viongozi wa madrasa hiyo katika kuwapatia watoto hao elimu ni jambo la msingi kwani lengo lake ni kuondokana na taifa lenye watu mbumbuu. Kwa upande wake Sheikh wa Madrasa hiyo, Sheikh Abbas Mshauri, amesema licha ya wao kuwafundisha masuala ya kidini lakini pia kimeamua kuwakusanya watoto wote bila kujali itikadi ya kidini lengo ni kuona wanapata msaada wa karibu kutoka kwa wadau. Amesema mara zote wao wamekuwa wakipita mitaani pia kuongea na viongozi wa Serikali za mitaa ili kuweza kuwapata watoto hao na kuwakusanya mahala pamoja na kuanza kuwahudumia. Mbeya. Taasisi za kifedha zimeshauriwa kuwa karibu na wakulima katika suala zima la kuwapatia mikopo ili waweze kujiinua kiuchumi badala ya kuwatenga na kuendelea kuwakopesha wafanyabiashara wakubwa. Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akiwa Jijini Mbeya mara baada ya kutembelea mabanda ya wakulima waliofika katika maonyesho ya wakulima ya nane nane ambayo kwa nyanda za juu kusini yanafanyika katika viwanja vya John mwakanagale Vilivyopo Uyole Jijini Mbeya. Mwambungu amesema kuwa baadhi ya taasisi za kifedha zimekuwa na kasumba mbaya kwa wakulima ambapo zimekuwa zikiwabagua wakulima hao pindi wanapofika kuomba msaada wa kukopeshwa. Aidha, Mwambungu amesema wafanyakazi wa mabenki na taasisi zingine za kifedha wanatakiwa kuwa karibu na wakulima hao pia watumie zaidi taaluma na uzoefu wao wa namna ya kuwasiadia wakulima hao ili waweze kujiinua kiuchumi. Amesema mabenki na taasisi za kifedha zinatakiwa kuondokana na kasumba kwamba kwa vile ni mkulima hivyo hana uwezo wa kurejesha mkopo na kuwathamini wafanyabiashara pekee wakati mkulima akipewa elimu juu ya matumizi sahihi ya fedha anazokupeshwa anakuwa na uwezo mzuri wa kurejesha mkopo huo. Ameongeza kuwa Mkulima bila ya kusaidiwa kwa vitendea kazi ataendelea kupiga hatua moja mbele na kurudi hatua tatu nyuma badala ya kusonga mbele na kwamba hata maonyehso hayo ya wakulima hayatakuwa na maana. SHINYANGA Imeelezwa kuwa Baadhi ya wazazi na walezi wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamekuwa wakiwazuia walimu kutoa elimu ya njia ya kujikinga na ukimwi kwa watoto wao wa shule za msingi ikiwemo matumizi sahihi ya condom. Hayo yamebainika leo katika semina iliyoandaliwa na shirika la UNESCO iliyojumisha wakuu wa shule za msingi na sekondari pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali iliyofanyika katika ukumbi wa Golden Valley Mjini Kahama. Akichangia hoja katika semina hiyo Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Korogwe Ashura Rugakingira amesema wamekutana na tatizo hilo toka kwa baadhi wazazi hao licha ya kuwa somo hilo lipo katika mtaala wa Serikali. Rugakingira amesema kuwa changamoto hiyo inawafanya walimu wengi kukata tamaa ya kutoa elimu hiyo ya kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa wanafunzi hao. Awali akifungua semina hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu Bi Isabela Chilumba amewataka walimu hao kuvunja ukimya na kuwa wawazi kuzungumza na wanafunzi wao kuhusu Maambukizi ya virusi vya ukimwi na UKIMWI. Sambamba na hayo Chilumba ametoa angalizo kwa wananchi kutodanganyika na takwimu za maandishi zinazotolewa na kwamba kila mtu awe mstari wa mbele kupima afya yake mwenyewe. Naye Msimamizi wa mradi huo wa Elimu ya Afya ya UKIMWI, uzazi na maadili kwa vijana kutoka UNESCO Mathius Herman amesema lengo la mradi huo ni kujenga mahusiano rasmi kati ya Mashirika yasiyo ya serikali na shule. DAR ES SALAAM UONGOZI wa Kiwanda cha Konyagi cha Tanzania Distileries Limited (TDL), umeiomba serikali kuondoa kodi inayotoza kiwanda hicho kutokana na ununuzi wa zao la zabibu kwa kuwa bado hakijajiimarisha kiuzarishaji. Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TDL, David Mgwassa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam ambapo alielezea wasiwasi wa zao kuja kudorora iwapo kodi hiyo itaendelea kutozwa. Amesema kutokana na uendeshaji wa kampuni kwa miaka sita tangu ifufue mashamba ya zabibu miaka saba iliyopita kwa kuagiza mbegu kutoka Afrika Kusini ni kipindi kifupi kuanza kukatwa kodi. Amesema TDL kwa mwaka huu imenunua lita milioni 1.720 za zabibu na kuwa lita milioni 1.1 ni kwa ajili ya kinywaji cha Valuer na 0.7 zilienda kwenye bidhaa nyingine. Mgwassa amesema kwa mwaka jana kampuni hiyo imetumia sh.bilioni 1.8 kwa ajili ya kununua zao hilo ambapo mwaka huu watatumia bilioni 2.3 na kuwa hali ya kilimo cha zao hilo ni nzuri pamoja na soko lake tofauti ni inavyodaiwa na baadhi ya watu. Ameongeza kuwa iwapo serikali itaendelea kotoza kodi hiyo upo uwezekano wa vinywaji vinavyozarishwa na kiwanda hicho bei yake kuwa juu kutokana na bei ya soko kulingana na ile ya vinywaji kutoka nje ya nchi. YALIYOJIRI MAGAZETINI NIPASHE Utoaji mimba kuna hatari kubwa kwa wanawake Utafiti mpya uliofanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii umeonyesha kuwa kutoboka kwa kibofu cha mkojo, kushamiri kwa kansa ya shingo ya uzazi, utasa na matatizo ya kisaikolojia kwa wanawake kunatokana na kasi kubwa ya utoaji mimba nchini. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Mtumwa Mwako, akizungumza mjini hapa jana, alisema ripoti ya utafiti huo inaonyesha kwamba, utoaji mimba ndiyo chanzo kikuu cha matatizo mengi kwa wanawake. Alisema licha ya mara nyingi utoaji mimba kufanywa na watu wenye utaalamu katika sekta ya afya wakiwamo wauguzi na waganga wanaokiuka maadili ya kazi zao, vitendo hivyo vinafanyika kwa usiri mkubwa. Alisema pia mtoaji mimba anaweza kushindwa kubeba mimba nyingine kutokana na mimba hizo kutunga nje ya kizazi na kuharibika muda mfupi baada ya kupata ujauzito. Aliwataka vujana wa kike kuacha tabia ya kutoa mimba kwani kunahatari kubwa kwa afya zao, huku akiisisitiza jamii kuwaelimisha vijana madhara ya utoaji mimba ili kukabiliana na tatizo hilo ambalo limeshamiri katika sehemu nyingi nchini hasa mijini. Wanafunzi Ilboru waendelea kugoma Mgomo wa wanafunzi wa Sekondari ya Ilboru, iliyopo wilayani Arumeru, kutoingia madarasani uliingia siku ya pili jana, wakishinikiza mwanafunzi mwenzao Ibrahim Kaebo wa kidato cha tatu ‘C’ aliyefukuzwa na bodi bila kupewa nafasi ya kujitetea, kurejeshwa shuleni. Akizungumza katika ofisi za NIPASHE mjini hapa, alisema yeye ni Makamu Mwenyekiti wa chakula na bwalo, hivyo akiwa kiongozi alikuwa anakabiliwa na changamoto za chakula kuwa kibovu na wenzake kugoma kula, hivyo kama wajibu wake aliandika taarifa, jambo lililomponza kuwa anajifanya mjuaji. Alisema alimsindikiza mwanafunzi mwenzao hospitalini, (hakumtaja jina), baada ya kuumizwa mkono kwa kuchapwa viboko na mwalimu, jambo lililopelekwa katika bodi kuwa alitaka mwalimu afukuzwe kazi. Makosa mengine aliyataja kuwa ni kuondoka shuleni bila ruhusa, kutofanya mitihani, kudharau walimu, kuwapiga wanafunzi na kuwajeruhi, kukataa kumeza dawa, jambo ambalo alieleza kuwa siyo la kweli. Kaebo alisema kinachomsikitisha zaidi ni kumfukuza shuleni hapo bila kumpa nafasi ya kujitetea na kwamba hajawahi kufanya kosa lolote lililosababisha apewe barua ya onyo. Alisema baada ya kutaka apewe barua yenye kueleza makosa aliyofanya hakupewa, badala yake alipata vitisho vya kutakiwa kuondoka shuleni hapo. Kaebo alisema wanafunzi wanagomea mambo mengi ikiwamo tabia ya kubadilishiwa mabweni na walimu bila kuhusisha uongozi wa shule kama mtaala unavyosema. Kasoro nyingine ni kubadilishiwa ratiba ya chakula na kulazimishwa kuchagua vyakula vya bei nafuu. Mmoja wa viongozi wa wanafunzi shuleni hapo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema alichotendewa mwanafunzi mwenzao siyo haki na makosa hayo siyo ya kweli, maana alikuwa mtetezi wao kama kiongozi. Alisema hata kama alikosa shule ingempa nafasi ya kujieleza, jambo ambalo hawakubaliani nalo na wataendelea kugoma. Wanafunzi hao wamegoma kwa kujikusanya kwenye mabweni, bila kuingia madarasani. Waandishi walikwenda shuleni hapo kutaka kumwona Mkuu wa shule lakini alikataa kuonana nao kwa kile kilichoelezwa kwamba akihitaji kuongea na waandishi atawaita. Malecela aipa somo Wizara ya Kilimo Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela, ameishauri Wizara ya Kilimo, Chakula na ushirika, kujipanga kukabiliana na tatizo la uzalishaji wa mbegu bora za kilimo ambalo kwa sasa halitoshelezi. Alitoa ushauri huo jana alipokuwa akitembelea banda la wizara hiyo katika Taasisi ya Kudhibiti ubora wa Mbegu Tanzania(TOSCI). Alisema ni vyema sasa Wizara ikatangaza kuwapata wazalishaji wengi wa mbegu nchini ili kutosheleza mahitaji na kuacha kuagiza nje ya nchi. Alisema kitendo cha kuzipa nafasi kampuni zinazozalisha mbegu zitangaze kuwapata wazalishaji wengi, itakuwa ni vigumu, hivyo kila mwaka kutakuwapo upungufu wa mbegu. Mkurugenzi wa Tosci, Tasiana Maingu, alisema uzalishaji wa mbegu hautoshelezi hapa nchini hivyo mbegu nyingine huagizwa kutoka nje ya nchi. Alisema kwa sasa kuna kampuni zaidi ya 60 za ndani na nje ya nchi zinazozalisha mbegu. Hata hivyo, alisema mahitaji ya mbegu ni makubwa ambapo kwa sasa ni tani 30,000 lakini kwa hapa nchini zinapatikana tani chache na hivyo kulazimika kuagiza nje. MWANANCHI Tendwa afunguka baada ya kustaafu Siku moja baada ya kutangazwa rasmi kwamba aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa amestaafu kwa mujibu wa sheria, amejitokeza na kueleza yaliyo moyoni mwake. Katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Harare jana, Tendwa alisema amepokea kwa mikono miwili kustaafu kutoka katika nafasi hiyo nyeti katika siasa za Tanzania, huku akisema anajiona mwenye bahati kufanya kazi na marais wawili katika nafasi yake. Tendwa amefanya kazi chini ya uongozi wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na baadaye Rais Jakaya Kikwete. Nafasi ya Tendwa, imechukuliwa na Jaji Francis Mutungi ambaye alikuwa jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma. Akizungumzia kuhusu viongozi wa vyama vya upinzani kupokea kwa nderemo kustaafu kwake, Tendwa alisema wala hashangai kuyasikia hayo kwani inaonyesha kwamba kazi yake alikuwa akiifanya vyema na mujibu wa sheria. Alisema kwamba, “Unajua kuvilea vyama ni kazi kubwa sana ndugu yangu, maana kuna wakati hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wanasema ninaegemea na kuvipendelea sana vyama vya upinzani. Leo nimestaafu nasikia vyama vya upinzani vinasema kwamba nilikuwa nawapendelea CCM, hiyo inaonyesha kwamba nilikuwa ninafanya kazi yangu sawa sawa.” Tunataka mambo matano yaondolewe katika Muungano Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, wametoa mapendekezo ya pamoja wakitaka mambo matano yaondolewe kwenye Muungano, yabaki kwenye Serikali washirika. Waliyopendekeza yaondolewe ni Mambo ya Nje, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki kuu, usajili wa vyama vya siasa pamoja na ushuru wa bidhaa wakisema kwamba kama yataendelea kuwepo kwenye Muungano kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba yatasababisha Serikali shirikishi kuwa dhaifu. Wakizungumza baada ya kuwasilishwa kwa kazi za makundi yaliyopewa jukumu la kujadili suala la mihimili, wajumbe hao walisema mambo hayo matano ndiyo yanayoweza kuzipa nguvu Serikali shirikishi ambazo zitakuwa Tanganyika na Zanzibar. Walitolea mfano wa mambo ya nje na kusema kuwa ikiwa Rais wa Serikali ya Tanganyika au Zanzibar ataondolewa jukumu la kuteua mabalozi na hata kuiwakilisha nchi nje ya nchi atakuwa ameondolewa meno. “Nchi washirika ziachiwe masuala ya mambo ya nje,”alisema Kassim Mohamed Kassi, mkazi wa Chimba akiwakilisha vijana. Kuhusu Sarafu na Benki Kuu, walisema sababu za kupendekeza iondolewe katika muungano ni kuwa itadhoofisha uchumi wa nchi washirika. Aidha kwa upande wa uraia na uhamiaji, walisisitiza kuwa kila nchi watu wake wana utamaduni usioingiliana na nchi nyingine washirika, hivyo kila upande uwe huru. Ushuru wa bidhaa, wajumbe hao walipendekeza ubaki kwenye nchi washirika na siyo Muungano kama inavyopendekezwa kwa sababu ikiwa itaachwa hivyo sehemu kubwa ya kodi na ushuru kutoka nchi washirika zitashindwa kuwanufaisha watu wake. Kuhusu usajili wa vyama vya kisiasa, wajumbe hao walisema hiyo ni moja ya kero za muungano iliyojitokeza baada ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi. Sheria ya chama ili kisajiliwe sharti kipate wanachama wa mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar. Walitaka mambo ya muungano yabaki mawili tu ambayo ni Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano Nape: Hatutawapuuza wanaodai Serikali Tatu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema chama chake hakitapuuzia maoni ya WanaCCM wanaopendekeza muundo wa Serikali tatu. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Nape alisema: “CCM tunapendekeza muundo wa Serikali mbili, lakini hii haitufanyi tuwapuuze au tugombane na wale wenye mawazo tofauti na yetu. Nape alisema kuwa CCM ilitangaza kujiunga kama Baraza la Katiba la kitaasisi, na kuwa baraza hili litaanzia kwenye ngazi ya tawi hadi taifa. Mpaka sasa ngazi ya matawi, wilaya na baadhi ya mikoa imeshakamilisha mchakato huo kwenye vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa vinavyotarajiwa kufanyika kati ya Agosti 20-25/08/2013 mjini Dodoma. Alisema vikao hivyo vya kitaifa vitapokea maoni na mawazo ya wanachama, kuyapitia, kuyaunganisha na kuyaweka tayari kwa ajili ya kuyawakilisha kwa tume na kwamba CCM imeridhishwa na jinsi mchakato wa mabaraza unavyoendelea licha ya kasoro zinazojitokeza. Nape alionya na kusema: “Hali inayojaribu kujengwa kwa nguvu si ya kweli. Tuache hoja zishindane kwa hoja na nguvu ya hoja ndiyo iwe msingi wa ushindani. Tushindanishe hoja bila kushutumiana na mwisho, mawazo ya wengi yasikilizwe na kuzingatiwa.” KURUNZI LANGU : Bodaboda ni janga, Serikali iamke Katika siku za hivi karibuni kumeibuka tabia ya waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda kujichukulia sheria mkononi pindi kunapotokea ajali zinazohusisha magari na pikipiki. Bila kujali ni nani mwenye makosa katika ajali hizi, waendesha pikipiki hao wameanzisha mtandao wa kuwashambulia madereva wa magari yanayohusika katika ajali hata kama wao ndio wenye makosa. Mara tu ajali inapotokea, huanza kupigiana simu na kuitana na baada ya dakika chache utakuta kundi kubwa la waendesha bodaboda hao wamezingira gari na kuanza kujichukulia sheria mkononi. Vijana hao badala ya kutoa taarifa polisi ili wafike na kufanya kazi yao, wao ndiyo hugeuka polisi na kuingia mitaani kumsaka aliyesababisha ajali iwapo anakuwa ametoweka kunusuru maisha yake. Wanapomkuta “mhalifu”, badala ya kumpeleka polisi wao wanaamua kumsulubu kana kwamba wao wako juu ya sheria. Kwenye gari lililohusika kwenye ajali, baadhi yao huvunja vioo, wengine hutembezea kipigo kwa dereva na hata abiria wasiohusika, kuiba mali za waliokuwepo kwenye gari husika na mara kadhaa imetokea hata kuchoma moto magari. Tabia hii ikiachwa izoeleke kwamba bodaboda wajichukulie sheria mkononi, hakika tutakuwa tunatengeneza bomu la hatari. Tayari kumeanza kujitokeza uhasama kati ya madereva wa magari na bodaboda kiasi kwamba wamiliki wa magari sasa hawataki kutoa msaada kwa waendesha bodaboda wanapopata ajali. Nimeshuhudia mmoja amegongwa na kila gari lililokuwa linapita eneo la ajali dereva akiombwa msaada, utasikia “hao wamezidi”. Asilimia 95 ya ajali zote zinazotokea nchini zikihusisha pikipiki, chanzo cha ajali hizo mara nyingi kinakuwa ni wenyewe waendesha pikipiki. Huu ndiyo ukweli, kwamba sasa hili ni janga la kitaifa. Ni jambo la kawaida mwendesha bodaboda kulipita gari kupitia upande wa kushoto na wakati mwingine dereva wa gari ameshaonyesha ishara kuwa anakata upande wa kushoto. Wakati mwingine pikipiki mbili hulipita gari kwa wakati mmoja, kila moja ikipita upande wake. Na si ajabu kukuta mwendesha bodaboda anawasha taa akionyesha ishara kuwa anakata kulia, lakini akakata kushoto au kinyume chake. HABARI LEO Mihadhara ya Ponda marufuku Zanzibar SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imempiga marufuku Katibu wa Jumuiya ya Taasisi ya Kiislamu, Shekhe Ponda Issa Ponda, kuendesha mihadhara ya kidini katika ardhi ya Zanzibar yenye mwelekeo wa kuleta mifarakano, chuki na uhasama. Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, alitangaza marufuku hiyo wakati akiahirisha jana Mkutano wa Bajeti wa Baraza la Wawakilishi kwa mwaka wa fedha 2013/2014. Alisema mahubiri ya sura ya uchochezi yenye lengo la kuiingiza nchi katika machafuko ya kidini, hayatavumiliwa kwa kuwa madhara yake ni makubwa. Kwa mfano, alisema Shekhe Ponda amekuwa akitumia wananchi wa Zanzibar kuendesha mihadhara yenye mwelekeo wa vurugu na chuki, hivyo wananchi wanatakiwa kutambua, kwamba vurugu zinapoibuka, waathirika ni Wazanzibari wakati Ponda akikimbilia Tanzania Bara. Balozi Seif alisema Wazanzibari wamechoka na mifarakano inayotokana na mivutano ya kisiasa, ambayo ilizuka tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992. Alikumbusha wajumbe kuwa juhudi za kuleta amani na utulivu zimechukua muda mrefu, huku zikiacha makovu kwa wananchi wa Zanzibar na hivyo wananchi wasikubali kurejea matukio hayo. Serikali isilaumiwe Balozi Seif alisema Serikali isilaumiwe kwa hatua itakazochukua kwa viongozi wa aina hiyo, na kutaka wananchi wasiunge mkono uchochezi kama huo. Balozi Seif alisema Zanzibar haina migongano ya kidini na waumini wake ambao wamekuwa wakishirikiana katika mambo mbalimbali na waumini wengine wa dini tofauti. Sensa CCM, CUF Balozi Seif pia alikemea vikundi vinavyopita Unguja na Pemba, kufanya sensa ya kutaka kubaini idadi ya wafuasi wa CCM na CUF. Alionya kuwa hakuna sensa ya aina hiyo na kutoa agizo kwa masheha kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi watakapokutana na watu wa aina hiyo. Mkutano wa Baraza la Wawakilishi ambao ulichukua takribani miezi miwili kujadili makadirio ya bajeti za Wizara kwa mwaka wa fedha 2013/2014, uliahirishwa hadi Oktoba 9. Moto mkubwa JKIA, uwanja wafungwa UWANJA wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta ( JKIA) uliopo Nairobi nchini Kenya umefungwa kwa muda usiojulikana baada ya moto mkubwa kuunguza eneo wanalotumia wageni wanaowasili uwanjani hapo. Inadaiwa kuwa, moto huo ulianza saa 11 alifajiri, vikosi vya zimamoto na uokoaji vya mamlaka mbalimbali vimefanikiwa kuuzima, lakini hakuna ndege zinazoruhusiwa kutua au kuruka uwanjani hapo. Ndege zilizotarajia kutua uwanjani jijini Nairobi zimeelekezwa zikatue katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi uliopo Mombasa, au Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu. Hadi sasa chanzo cha moto huo hakijajulikana, abiria, wafanyakazi wameondolewa uwanjani hapo na kwa mujibu wa maofisa katika uwanja huo, hakuna taarifa za kuwepo madhara kwa binadamu. Rais Uhuru Kenyatta alifika uwanjani hapo leo saa tatu asubuhi kujionea hali halisi ya madhara yaliyosabishwa na moto huo uliodumu kwa takribani saa tano. Mkuu wa Polisi nchini Kenya, Inspekta Generali wa Polisi (IGP), David Kimaiyo amesema, hakuna mtu aliyekufa, na kwamba, hadi ilipofika saa tatu asubuhi, sehemu kubwa ya moto huo ulikuwa umezimwa. Waziri wa Usafirishaji na Miundombinu wa Kenya, Michael Kamau ametangaza kuwa JKIA umefungwa kwa muda usiojulikana Mratibu wa masuala ya Taifa ya Kenya, Joseph Ole Lenku amesema, ulinzi umeimarishwa uwanjani hapo, na kwamba, juhudi zinaendelea kuhakikisha kwamba huduma katika uwanja huo zinaanza tena haraka kadri itakavyowezekana. Mkuu wa Ulinzi katika Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Kenya, Eric Kiraithe amesema, kwa viwango vya nchi hiyo, mpto huo ni mkubwa. Ofisa katika uwanja huo amekaririwa akisema kuwa, alifika uwanjani hapo saa 11 alfajiri na kukuta moshi ukitoka kwenye eneo wanalotumia abiria wanaowasili katika uwanja huo unaotumiwa na mashirika mengi ya ndani na nje ya Afrika wakiwemo abiria wanaokwenda Ulaya, Mashariki ya Kati na Asia. Shirika la Ndege la Kenya, Kenya Airways limetuma ujumbe kwa abiria wake wasiende katika uwanja huo, na kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, abiria wao wote waliokuwa wanaondoka au kwenda uwanjani hapo wapo salama. MAONI YA MHARIRI NIPASHE Wakulima tumieni vema maonyesho ya Nanenane Leo ni kilele cha Siku ya Wakulima maarufu kama Nanenane ambapo kitaifa inafanyika mkoani Dodoma. Tofauti na miaka mingine ilivyozoeleka ambapo kilele cha siku hiyo hufanyika Agosti 8 ya kila mwaka, mwaka huu inafanyika leo Agosti 7 kwa sababu ya matarajio ya sikukuu ya Iddi el Fitri iwapo mwezi utaandama leo. Hata hivyo, maonyesho hayo ya Nanenane yataendelea kama kawaida hata kama sikukuu ya Iddi el Fitri itaanza leo. Maonyesho ya Nanenane hutumika kwa wakulima kuonyesha uzalishaji wa mazao yao na vivyo hivyo, kubadilishana mawazo miongoni mwao kuhusu kilimo pamoja na kujifunza masuala mbalimbali ya kilimo bora. Ni maonyesho yenye umuhimu wa kipekee kwa wakulima wa Tanzania na kwa Taifa hasa kutokana na ukweli kwamba uchumi wa Taifa hili kwa asilimia kubwa hutegemea kilimo. Pia, takriban asilimia 80 ya wananchi wanaoishi vijijini, hutegemea kilimo. Ni kwa sababu hizo ndiyo maana serikali imekuwa ikitilia umuhimu katika kilimo. Lakini pamoja na msimamo huo wa serikali, ni vema basi nanyi wakulima mkayachukulia maonyesho hayo kama fursa ya kujifunza ili kilimo chenu kiwe chenye tija. Kilimo kisichozingatia utaalamu, hakika hakitawakomboa wakulima na pia hakitalikomboa Taifa kiuchumi. Tunajua wakulima mnakabiliwa na changamoto nyingi katika kilimo chenu ikiwamo zana duni kama jembe la mkono, ukosefu wa mitaji, uwezo wa kununua pembejeo za kilimo kama mbolea na mbegu, ukosefu wa masoko ya uhakika, kuporomoka kwa bei ya mazao, kuzitaja baadhi, ni muhimu mkazingatia ushauri wa watalaamu kwa kila zao mnalolima. Lakini wakati wakulima mnatakiwa kuzingatia hayo, serikali nayo kwa upande wake inatakiwa kuwawekea mazingira bora ya kilimo. Baadhi ya mazingira mazuri kwa wakulima ni pamoja na kuwahakikishia kuwa kila mkulima anapatiwa ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo kwani wapo wengine ambao licha ya kuwa nia ya kulima, lakini hawana ardhi ya kutosha na hivyo kulazimika kukodi. Sisi tunasema ni muhimu basi mamlaka zinazohusika kuhakikisha kwamba zinawagawia ardhi wakulima wadogo vijijini ili waachane na utaratibu wa kukodi maeneo ya kilimo kila msimu. Hata sera ya Kilimo Kwanza itapata mafanikio makubwa zaidi kwa kumuinua mkulima wa chini. Vilevile, serikali ina wajibu mkubwa wa kumhakikishia mkulima soko la uhakikia la mazao yake ili isimkatishe tamaa. Haipendezi mkulima alime mazao yake halafu akose mahali pa kuuza hadi yanaharibika. Hali kadhalika, kumekuwapo na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wakulima kutokana na utaratibu wa kuwatumia mawakala katika kusambaza mbolea na mbegu kwenda kwa wakulima. Katika hili, tungeishauri serikali ijaribu kuliangalia upya suala hilo kwani uzoefu unaonyesha kuwa utaratibu wa sasa hauwanufaishi wakulima kama ilivyotarajiwa. Ni ukweli ulio wazi kwamba mawakala walioteuliwa na serikali kusambaza mbolea na mbegu kwa wakulima, baadhi yao siyo waaminifu na wamegeuza miradi yao na kusahau kumtumikia mkulima. Hivi sasa msimu wa kilimo unapowadia, ni kawaida kusikia kelele kutoka karibu kila kona ya nchi wakilalamikia utaratibu mbovu wanaoutumia mawakala hao. Tungeiomba serikali ibuni utaratibu mpya wa kumsaidia mkulima afikie malengo yake. Aidha, ni vema pia serikali ikawaelekeza wakulima kulima kile kinachohitajika katika soko kwa wakati husika. Hii itapunguza malalamiko ya wakulima ya mazao yao kukosa soko. Tunasema kama kweli serikali imedhamiria kuendelea na msimamo wake kuwa kilimo ni uti wa mgongo, basi hapana budi itekeleze hayo tuliyoyasema kwa upande wake na vivyo hivyo wakulima nao kwa upande wao watekeleze ushauri wetu huu. MAKALA MAALUM Rungwe inavyojitahidi kumilikisha ardhi wakulima WILAYA ya Rungwe imepata fursa ya ufadhili katika kutekeleza sheria namba tano ya ardhi ya vijiji kwa vipindi vitatu tofauti. Utekelezaji wa sheria hii umekuja kupitia mradi wa uwezeshaji wananchi kumiliki ardhi kisheria. Awamu ya kwanza ilifadhiliwa na Shirika la Abbot Axio mwaka 2004/2005, lengo likiwa ni kuwasaidia wajane na watoto yatima wa Kata ya Kinyala kumiliki ardhi. Mradi huo ulitekelezwa katika vijiji tisa ambapo pia zilitolewa nakala za sheria na kanuni za ardhi vijijini kwa wananchi. Awamu ya pili ilitekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ufadhili wa Muungano wa Ulaya (EU) mwaka 2007, 2008. Mradi huu ulitekelezwa katika vijiji 16 ambapo vinane kati ya hivyo viko Rungwe Mashariki na vilivyosalia Rungwe Magharibi. Vijiji hivi vilikuwa vya mfano kwa lengo la kupima mashamba yote bila kuzingatia aina ya mazao. Pia mradi uliwezesha ujenzi wa masijala ya ardhi ya Kijiji cha Ikama na masijala ya wilaya ambapo pia wafadhili walitoa samani za ofisi zote mbili. Wakulima wa chai Katika awamu ya tatu ya upimaji wa ardhi ambayo ndio makala haya yanaiangalia kwa kina, wilaya imefadhiliwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge nchini (Mkurabita) kwa kushirikiana na Bodi ya Chai Tanzania na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima wadogo wa chai, lengo likiwa ni kupima mashamba ya chai. Awamu hii iliyoanza Novemba 19 mwaka 2012 na kukamilika Juni 15 mwaka huu ilijikita katika kuwawezesha wakulima wa chai wa skimu ya Segera inayojumuisha vijiji 19 vya Masukulu, Kyambambembe, Segera, Mpombo, Ijigha, Ntandabala na Matwebe. Vijiji vingine vilivyo katika skimu hiyo ni Busisya, Bulongwe, Mpumbuli, Nsongola, Nsyasya, Bujela, Njugilo, Lufumbi, Kasyeto, Igembe, Kiloba na Ngaseke. Mratibu wa mradi wa uwezeshaji wakulima wa chai wa skimu ya Segera, Gwabo Mwansasu, anasema tangu kuanza hadi kukamilika kwake, mradi kwa awamu hii ya tatu umegharimu Sh 64,078,440 zikiwa ni fedha kutoka kwa wadhamini waliotajwa hapo juu. “Mradi ulitarajia kupima mashamba ya wakulima 2440 yenye jumla ya hekta 606.10. Lakini tumefanikiwa kupima mashamba ya wakulima 1,891 yenye ukubwa wa jumla ya hekta 485.12 na kufanya upungufu wa mashamba ya wakulima 549 yanayokadiriwa kuwa na ukubwa wa jumla ya hekta 120.98,” anasema Mwansasu. Kukataa kupimiwa mashamba Kwa mujibu wa Mwansasu, uwepo wa mitazamo tofauti kwa wakulima hasa wanaouza chai yao kwa Kampuni ya Mohamed Enterprise (MeTL) kuhusiana na shughuli hii, kulipelekea baadhi yao kuwazuia maofisa na wapimaji wasaidizi kupima mashamba yao na kwamba hiyo ni changamoto iliyosababisha kukwama kufikiwa kwa malengo. “Mitazamo tofauti ya wakulima kuhusiana na zoezi hili imesababishwa na sababu kadhaa kama vile kushawishiwa na viongozi waliopewa dhamana ya kuwaongoza kwa kuwakataza wasiruhusu mashamba yao kupimwa kwa hofu ya kupoteza umaarufu wa misimamo na itikadi zao mbalimbali. “Ndani ya wakulima wenyewe kuna wabishi kupita kiasi na wengine wana hofu ya kunyang’anywa mashamba yao kwa kukosa kuiamini Serikali kama ni kweli inaweza kuwasaidia kupimiwa mashamba yao bila ya kuwatoza gharama. Hii ni changamoto kubwa,” anasema. Mwansasu anasema walijitahidi kuwaelimisha umuhimu wa zoezi hilo wakiamini watabadili misimamo yao lakini mpaka zoezi linaelekea ukingoni wapo walioendelea ‘kukomaa’ na misimamo yao batili. “Mwisho wa siku waliokataa tuliwaacha na tukaendelea na wale tu walioturuhusu kuwahudumia. Lakini wamekosa kitu muhimu sana na kuna siku watajutia bahati hii,” anafafanua. Hati miliki kumaliza migogoro Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispin Meela, anasema upimaji wa ardhi na kutoa hati miliki za kimila ni miongoni mwa njia sahihi za kuwezesha wakulima kujitenga na tatizo la migogoro ya ardhi. Meela aliyasema hayo kwenye hafla ya kukabidhi hati miliki za kimila 400 kwa wakulima wadogo wa zao la chai waliokubali kupima mashamba yao iliyofanyika katika kijijini Ntandabala. Meela anasema kumekuwepo na migogoro mingi baina ya wakulima wilayani humo ikihusu kugombea ardhi, hali inayotokana na kutokuwepo kwa nyaraka zenye kumtambulisha kisheria mmiliki rasmi. “Mingi kati ya migogoro hiyo ni ile inayohusisha wajane na watoto kudhulumiwa adhi mara baada ya baba wa familia kufariki dunia na ndugu walio na tamaa kutaka kuitumia fursa hiyo kujinufaisha. “Njia pekee itakayowezesha kuondokana na migogoro hiyo na yatima na wajane kupata haki zao ni wamiliki wa ardhi kuwa na hati miliki. Ndiyo sababu tunalalamikia uwepo wa kikundi cha watu kilichokwamisha upimaji ardhi kwenye eneo hili kupitia mradi huu na kusababisha tusifikie malengo,” anasema Meela. Wakwamishaji washughulikiwe Akikabidhi hati kwa wakulima 400, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro anasema watu wanaokwamisha shughuli ya upimaji ardhi kwa kuwadanganya wananchi juu ya malengo ya Serikali wanapaswa kushughulikiwa kwani wanakwamisha maendeleo na kupindisha lengo zuri la Serikali kwa wananchi wake. “Watu wote wanaoeneza chokochoko na kusababisha wananchi kuichukia Serikali yao wanapaswa washughulikiwe. Hatuwezi kuendelea kuwavumilia watu wachache wanaokwamisha maendeleo ya wengi. Angalia sasa wakulima waliokataa kupima mashamba yao hii leo wanawatamani wenzao wanavyokabidhiwa hati zao,” anasema. Kandoro pia anawataka wakulima waliokabidhiwa hati hizo kuzitunza kwa uangalifu mkubwa huku wakiwaepuka matapeli wanaoweza kuziiba ama kuwadanganya na kuwapa hasara. Hata hivyo, anawataka wadau kutoishia kupima ardhi ya wakulima na kuwakabidhi hati miliki hizo, bali ni wakati mwafaka kwao, hususani Mkurabita na taasisi za kifedha kurudi kwa wakulima hao na kuwapa elimu ya ujasiriamali ili waweze kunufaika nazo kwa kuchukua mikopo yenye kulenga kukuza kipato chao.
Posted on: Wed, 07 Aug 2013 13:23:57 +0000

Recently Viewed Topics




© 2015