NANI ANAJALI?: Vigogo wa CCM wakiwadhihaki wavuja jasho Charles - TopicsExpress



          

NANI ANAJALI?: Vigogo wa CCM wakiwadhihaki wavuja jasho Charles Misango KIPO kisa cha kusisimua nilichowahi kuhadithiwa zamani, kwamba katika himaya ya mfalme mmoja, kulizuka wasaidizi waliopewa nafasi ya kuongoza idara kadhaa za kifalme. Wasaidizi hao kwa mamlaka yao, wakapanga mipango mingi ya kuwanufaisha wao na jamaa zao. Wakawatumikisha wananchi kwa ujira mdogo, huku wao wenyewe wakijilipa ujira mkubwa kwa kazi isiyopaswa. Wasaidizi hao wakashiba, wakanawiri, wakawanda na wengine wakavimbiwa hata wakatapika juu ya meza za chakula. Katika shibe hiyo, wakasahau kama kuna watu wanaishi kwa dhiki, hawajui wale nini na wavae nini. Macho yao yakaingiwa na ukungu wa maisha ya anasa, kiasi kwamba baadhi yao wakadhani ni wateule na wanaostahili kuishi kuliko wengine. Ilifikia mahali, wenye mamlaka hao wakawa jeuri kiasi cha kupora wake na mabinti za watu kwa mabavu na jeuri ya fedha na vyeo. Kila msichana, mwanamke mzuri au mvulana mwenye sura jamali wakawa halali kwao. Aliyethubutu kupinga kutimiza matakwa yao alikiona kilichomfanya kanga asiote manyoya shingoni. Basi, tuseme kwa matanuzi hayo, ingeliwatosha wateuliwa hao ‘kuponda mali’ kimyakimya. Lakini starehe zikawapofusha na hivyo wakawa wakipita mitaani na kuwatwanga mishale masikini wote waliokutana nao. Kisa wanachafua heshima na hadhi ya mfalme. Kwamba wanatia doa kwa falme nyingine ikibainika kuwa katika himaya ile kuna watu wanaonuka kwa umasikini. Kauli za kuudhi, kejeli na zinazoashiria aina nyingine ya ulevi wa madaraka zilizotolewa kwa mara nyingine na mmoja wa viongozi wakubwa ndani ya taifa hili zimenifanya nikikumbuke kisa hiki. Juzi, Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesikika akidai kuwa mishahara ya wabunge ni midogo sana na hata posho ya sh laki tatu kukaa tu ndani ya Bunge, kusikiliza, kusinzia hadi kumwaga udenda, ama kuchangia hoja ya serikali mia kwa mia baada ya kufoka kidogo eti haitoshi! Mwanamama huyu aliyeingia katika rekodi ya kuwa spika aliyelalamikiwa mno kuliko wengine waliomtangulia kwa tuhuma za kuminya uhuru wa kujadiliana, hasa kwa wapinzani, akadai kuwa mshahara huo wa mamlioni ya fedha na posho hiyo, si lolote wala chochote kwa ‘wahishimiwi’ hao! Katika kuhalalisha madai yake, akatoa nyingine kali ya kufungia mwaka, kwamba kwa sababu fedha wanayopewa ni ‘cha mtoto’ ndiyo maana baadhi ya wanasiasa, hasa wale walioshindwa kutetea ubunge wao, wako ‘choka mbaya’ na wamefikia hatua ya kujipanga ofisini kwake, mithili ya akina ‘Matonya’, kwenda kuomba ngawira! Eti ili hayo yasitokee, ni vema wabunge hao wakaangaliwa zaidi kwa maslahi, maana kazi wanayofanya ni nzito! Tukumbuke tu kuwa wiki mbili zilizopita, mteule mwingine wa ufalme wa Rais Kikwete alikurupuka na kutoa ‘matusi’ kwa wanafunzi waliokuwa wakihangaika kupata mikopo, alipowaambia warudi makwao wakauze! Eti, kwa kuwa serikali haina uwezo wa kuwasomesha, basi kila mtu arudi kijijini akauze mashamba, nyumba ama mifugo ili apate fedha za kulipia elimu ya juu. Tushukuru kwamba aibu hii inajaribu kuondolewa na hatua ya serikali kuangalia namna watakavyoweza kuwasaidia wale waliokosa, ili waendelee na masomo yao. Lakini tayari mteule huyo aliweka mambo hadharani. Haya yanayozuka leo kwa wateule wetu, hata kama hatujasikia wakiwatwanga risasi masikini wa mitaani, hayana tofauti na kisa nilichokisimulia. Kama walivyokuwa wateule wa ufalme huo wa zamani, wateule wetu, nao wameelemewa na ulevi wa madaraka kiasi kwamba hawajali tena maisha ya wanyonge waliowafikisha hapo. Kama ilivyofanywa kwa wateule wa ufalme wa kisa hiki, kauli ya spika na ‘uduchu’ wa mishahara ya mamilioni inayosindikizwa na posho nono, iliyotanguliwa na ya Naibu Waziri, Philipo Mulugo, kuwataka waliokosa mikopo wakauze mali za nyumbani, hazina tofauti hata kidogo, na zote zinaashiria jambo moja tu. Kutojali kunakoweza kufanywa na mtendaji aliyelewa madaraka! Kauli ya spika kudai kuwa kipato cha sasa cha wabunge ni kidogo, ni sawa na kuwadhihaki mamilioni ya Watanzania wanaopata kipato cha chini. Kwanza wanachokipata wabunge ni kikubwa mara elfu ya anachopata mtumishi wa kawaida. Tunakumbuka namna wabunge wa zamani walivyokuwa wakilipwa. Hadi mwaka 2000, walikuwa wakipata mshahara wa sh 200,000 kabla ya makato. Walitumia magari ya kawaida, Landrover 109 au 110. Na wengine walilazimishwa kuwania ubunge kwa sababu ilikuwa kazi ya kujitolea. Wabunge walionyesha kujali maslahi ya watu na sio kama sasa ubunge umegeuzwa kazi ya kuwapatia ajira. Leo hii ubunge umekuwa kimbilio la baadhi ya watu wasio na kazi, wababaishaji na wengi wao (sio wote) wakiwa na tabia ya ulafi wa kutaka kupata fedha za mara moja. Makinda anatoa kauli ya dhihaka kwa wabunge makini waliolitumikia taifa kwa uzalendo mkubwa bila kutanguliza maslahi binafsi. Kwamba wabunge hao wastaafu wamekuwa ombaomba wa kutupwa kiasi cha kujipitisha katika ofisi za Bunge wakililia kusaidiwa posho. Nasita kuamini kwamba Makinda hakutafakari kwanza kabla ya kusema jambo hili. Nasita kuamini kuwa sasa tumefika mahali taifa linakuwa na wateule waliozama kuangalia maslahi yao tu na sio ya wanyonge wengi. Nasita kuamini kuwa tuna wateule ambao hawana muda, hawajali tena kile walichoapa ama kuahidi kuwatumikia watu kama wakati wakiomba kuchaguliwa. Nasita kuamini kuwa wanaotoa maneno ya aina hii, ni wale waliofaulu kushika nafasi walizonazo kwa hila, ujanja na rushwa. Nasita pia kuamini kuwa hata kama walichaguliwa kwa njia sahihi, basi wanafanana na wateule wa ufalme ule waliolewa madaraka kiasi cha kuona watu masikini kama takataka. Nasita kuamini kuwa kumbe hata tabia ya kuwakamata Watanzania ombaomba na kuwaondoa katikati ya Jiji la Dar es Salaam, pindi viongozi wa mataifa makubwa wanapofanya ziara, ni aina nyingine ya wateule kutojali wala kuumizwa na umasikini wa watu hawa. Naam wamekula, wameshiba, wamewanda na sasa wanaamini ni wao tu wenye haki ya kuishi hapa duniani na wengine wamekuja kwa bahati mbaya. Siwatukani, lakini sote tuwaulize watawala hawa, hivi kweli ni wabunge tu ndio wenye kazi nzito kuliko wengine? Inaingia kweli akilini kwa daktari anayeokoa maisha ya watu, nesi anayechezea usaha unaotoka katika madonda ya wagonjwa na mkunga anayemsaidia mama mjamzito kujifungua salama, kulipwa mshahara unaolingana na posho ya siku mbili ya mbunge anayelala usingizi bungeni? Ni haki gani hiyo? Ya utawala wa aina gani huo? Ni haki gani kwa mbunge kupata kiinua mgongo cha mamilioni ya fedha kwa miaka mitano tu ya kukaa bungeni na kufanya kazi ya kurusha vijembe, matusi, na michango ya mipasho ya ‘umebugi meen’ kama tulivyoshuhudia kwa baadhi yao zinazolingana na kiinua mgongo cha wafanyakazi 100? Ni aina ya wateule gani hawa tulionao wasioumizwa na hali mbaya ya ukosefu wa dawa katika hospitali na zahanati zetu? Ni aina gani ya wateule hawa wasioumizwa wala kujali kilio cha ukosefu wa mishahara kwa walimu wa shule za msingi na sekondari, kiasi kwamba huwezi kutofautisha kati ya mwalimu na mwanafunzi kwa kuwa wote wananuka kikwapa? Ni kina nani hawa wasiojali maisha magumu ya watoto wanaotembea kwa miguu umbali wa zaidi ya kilometa kumi kwa siku kwenda shule, au kina mama wanaotwangana makonde visimani wakigombea maji ya tope kwa ajili ya matumizi ya nyumbani? Naam, hawa ni wale wateule wasiojali shida za watu. Ni aina ya watawala ambao wamefura na kuruka hewani kwa hasira wanapoguswa na waandishi wa habari na wanasiasa makini. Ni aina ya watawala wasiopenda mambo yao yawe wazi wala kujali unyonge na maisha duni ya wengi. Sitashangaa kwa wateule hawa hawa kurudi tena kwa wale wale waliowaambia ‘wakauze’ wakiwachekea kinafiki wakitaka wachaguliwe. Na wala sitashikwa na bumbuazi, nikiona wale wale walioshindia uji na kufakamia maji ya tope wakipewa fulana na vikofia vya kufunika akili zao, wakipayuka na kumsifia mgombea wao kama mazuzu! Na wala haitanishangaza nikiona Watanzania ambao wenyewe walitupwa, wakatelekezwa, na kuachwa wakijifia kama kuku wa mdondo wakawachagua wateule hawa hawa kurudi tena bungeni kuomba ulaji tena. Nani anajali kwani?
Posted on: Sat, 26 Oct 2013 13:11:58 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015