Ni Rwanda dhidi ya JK au Tanzania? KAMA yanayoandikwa magazetini - TopicsExpress



          

Ni Rwanda dhidi ya JK au Tanzania? KAMA yanayoandikwa magazetini na kwenye mitandao ya habari, ingekuwa ni risasi, basi vita ya tatu ya dunia ingekuwa imeanza kati ya Rwanda na Tanzania. Vyombo vya habari vya Rwanda na Uganda vimechukulia matatizo ya kidiplomasia yaliyopo kati ya Rwanda na Tanzania kuwa uhasama wa kusababisha vita. Mitandao kama Chimpreports na News of Rwanda, imeandika mambo mazito yakimlenga Rais Kikwete binafsi na uongozi wake, kwa madai kwamba kuwafukuza wahamiaji haramu, wakiwamo Wanyarwanda ni matayarisho ya vita dhidi ya Rwanda. Madai haya ni mazito na yametolewa na mitando ambayo pengine imeamua kujiingiza kwenye kueneza propaganda hatari za kutangaza hali ya vita ambayo Tanzania haina habari nayo. Katika habari ambazo zimetolewa na baadhi ya magazeti ya Rwanda, Rais Kikwete na Mke wake, Salma, wameshambuliwa kama watu wenye undugu na Rais Juvenali Habyarimana, aliyeuawa kwa bomu lililoipiga ndege yake alipokuwa anarejea kutoka Tanzania katika mkutano wa usuluhishi. Jitihada za kujaribu kumhusisha Rais Kikwete na mauaji ya kimbari hazitofanikiwa kama zile za kumpa mbwa wa jirani jina baya kuwa anaugua ‘kichaa cha mbwa’, ili aangamizwe. Tanzania ina kila sababu ya kujivunia huduma na hifadhi ambazo imetoa kwa wakimbizi kutoka kwa nchi za jirani ambazo zilikumbwa na migogoro ya kisiasa, vita ya wenyewe kwa wenyewe na pia ukatili wa tawala za kidikteta. Wakimbizi kutoka DRC, Rwanda, Burundi, Uganda, Msumbiji, Zimbabwe, Afrika Kusini, Namibia na Angola, wameishi Tanzania. Baadhi yao wamepata uraia hapa nchini na wengine waliamua kurudi kwao, hasa baada ya ukombozi au hali ya amani na usalama kurejea. Tangu Rais Kikwete alipoingia madarakani, mwaka 2005, wakimbizi wapatao 160,000 kutoka nchi za jirani walipewa uraia. Mamia ya maelfu ya wakimbizi, wakiwamo wa Rwanda, walirejea kwao baada ya amani kurejea. Haiingii akilini kwamba Tanzania kupitia ardhi yake inaweza ikawa chanzo cha kuleta uvunjifu wa amani kutokana na matakwa binafsi ya Rais na familia yake. Wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia Afrika Mashariki na ulimwenguni kote, wanajua jitihada na diplomasia ya Tanzania ya kutaka eneo la Maziwa Makuu kuwa la amani kwa madhumuni ya kuleta maendeleo kwa watu wa nchi zote za jirani. Tanzania ina mipaka na nchi jirani zote za Afrika Mashariki, Kusini na Maziwa Makuu. Tanzania inapakana na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia, Malawi, Msumbiji, Comoro na Sychelles. Kibiashara na kiuchumi, Tanzania iko kwenye nafasi nzuri ya kukua na kupata maendeleo yenye ulinganifu na nchi za jirani. Katika dunia ya leo, diplomasia ya uchumi ni njia kuu katika sera za nje na nchi yoyote. Hivyo vita ni kitu cha kuepukwa na siyo cha kukaribisha. Tanzania inajua fika kwamba kukosekana amani na kuwepo vita ni adui wa maendeleo ya nchi husika na mahusiano ya kiuchumi kati ya nchi na nchi, hasa zile ambazo ni majirani na zote ni wanachama wa jumuiya moja kama Rwanda na Tanzania zilivyo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Madola na Ushirikiano wa Nchi za Maziwa Makuu. Kama tulivyoandika huko nyuma, baadhi ya wakimbizi walikubali kurudi kwao na wengine walipewa uraia wa Tanzania. Baadhi walikataa kuchukua uraia wa Tanzania na pia kurudi kwao. Hao waliokataa kurudi kwao na wengine waliokataa kuchukua uraia wa Tanzania ndio wanaoleta matatizo ya kukaa katika nchi ya watu bila kibali chao. Lakini si hao tu wenye kuleta matatizo. Kuna waliokuwa wakimbizi wakarudi kwao na baadaye wakatafuta njia za panya wakarejea Tanzania kwenye sehemu walizozikana toka mwanzo. Kwa nini baadhi ya wakimbizi wanapenda kurejea Tanzania? Hapa Tanzania kuna amani na utawala wa sheria na siyo wa kijeshi. Vile vile Tanzania inayo ardhi kubwa tofauti na ilivyo Rwanda na Burundi. Kama ni suala la vita, Rwanda ingeshaingilia sehemu ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania kama inavyoingilia DRC kila kukicha. Sehemu za mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita ni sehemu ambazo uhalifu, unyang’anyi na ujambazi umekithiri. Silaha ndogo ndogo zimesambaa. Lakini mazingira ya Tanzania, licha ya matatizo ya ujambazi na silaha ndogo ndogo, ni tofauti na DRC. Tanzania kumetulia. Rwanda haiwezi kuingilia kijeshi kwa madai ya kutaka kupambana na Interahamwe! Sasa nani anataka vita, Rais Kikwete ambaye anataka kuondosha ujambazi katika mikoa ya Kagera na Kigoma na kuitaka Rwanda iache kuingilia DRC, au Kagame anayetangaza ubabe dhidi ya Rais Kikwete na Tanzania?
Posted on: Sun, 25 Aug 2013 04:51:31 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015