RAIS KAA IMARA! Nakualika Rais, katika hiki kikao, Kwa sababu - TopicsExpress



          

RAIS KAA IMARA! Nakualika Rais, katika hiki kikao, Kwa sababu ninahisi, una maswala kibao, Nuhu nina wasiwasi, wanakuhini wenzio, Uhuru kaa imara, Kenya isiyumbeyumbe! Kwanza ni hiyo gharama, ya bidhaa madukani, Wengi wetu tumehama, tunarudi mashambani, Bora tuende kulima, pametushinda mjini, Uhuru kaa imara, Kenya isiyumbeyumbe! Juzi juzi ulisema, wakati wa kampeni, Utapunguza gharama, kwa vitu vyote nchini, Sasa tunaona kama, umetubwagia zani, Uhuru kaa imara, Kenya isiyumbeyumbe! Kuna kitu nitasema, nisikilize ‘Rais ‘, Usiogope lawama, uvumi ama tetesi, Talaumiwa daima, na kuwekewa visasi, Uhuru kaa imara, Kenya isiyumbeyumbe! Kile ninachokuomba, hebu maliza migomo, Jifungue hii kamba, isikuvute kwa shimo, Kisha ujue ya kwamba, haifai mikingamo, Uhuru kaa imara, Kenya isiyumbeyumbe! Uhuru kuwa makini, katika utendakazi, Kwani huko mashinani, vijana hawana kazi, Wanajifunza uhuni, wengi wamekuwa wezi, Uhuru kaa imara, Kenya isiyumbeyumbe! Hebu kaa mbele mbele, usije kuhadaika, Walimu warudi shule, wakiwa wameridhika, Na wengine vile vile, walipe pesa haraka, Uhuru kaa imara, Kenya isiyumbeyumbe! Rais wetu Uhuru, tunakuombea mema, Mungu atakupa nuru, kidete utasimama, Ila punguza ushuru, hata sisi tule nyama, Uhuru kaa imara, Kenya isiyumbeyumbe! Hapa nafunga suhufa, naondoka kibosile, Naenda kuziba nyufa, katika mianya ile, Miye zee la kubofa, ninawaaga wavyele, Uhuru kaa imara, Kenya isiyumbeyumbe! Utunzi wa: Nuhu Zubeir Bakari ‘Al-Ustadh Pasua’ Shairi la Kipindi cha Kamusi ya Changamka katika QFM na QTV Huenda hewani kila Jumamosi asubuhi kuanzia saa 1 hadi saa 5.
Posted on: Mon, 05 Aug 2013 08:54:08 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015