RIWAYA: BONDIA MTUNZI: Hussein Tuwa SEHEMU YA - TopicsExpress



          

RIWAYA: BONDIA MTUNZI: Hussein Tuwa SEHEMU YA SABA.. “Kesho ndio mnaanza mechi za kugombea ubingwa wa wilaya, sio?” Hatimaye Roman aliuliza. “Yeah Roman. Naona vijana wako katika hali na ari nzuri, natumai tutashinda tu...” Kimya kilitawala tena. “Jina langu limo kwenye orodha ya mabondia waliosajiliwa kwenye timu yako?” Roman aliuliza tena. “Kama tulivyopanga Roman. Nilikusajili tangu wakati uko gerezani, na kama bado una nia ya kuendelea na azma uliyoweka, basi nawe utapanda ulingoni pindi ukiwa tayari...” “Azma iko pale pale Makongoro. Ila itabidi vijana wako wafanye kazi ya kuvuka katika ngazi hii ya wilaya, mimi nitaingia kwenye ngazi ya mkoa...nahitaji mazoezi zaidi...” Roman alimjibu, kisha akaendelea, “...unadhani wanaweza kutuvusha?” “Ninajua kuwa wanaweza kutuvusha...” Mark alijibu kwa kujiamini. **** Kwa wiki mbili mfululizo baada ya siku ile, Roman alijishughulisha katika mazoezi mazito sana ya ndondi. Akikimbia umbali mrefu kila alfajiri na kurudi kwenye ile klabu yao ya ndondi kwa ajili ya mazoezi zaidi ya viungo na ya ulingoni chini ya usimamizi makini wa kocha wake wa muda mrefu, Mark Tonto. Timu yao ya ndondi haikufanikiwa kuchukua ubingwa wa wilaya, lakini ilifanikiwa kusonga hadi ngazi ya mkoa kwa kutoka washindi wa pili katika ngazi ile ya wilaya. Na katika wiki mbili zile, pamoja na kuweka umakini wa hali ya juu kila alipokuwa, Roman hakuonana tena na Kate wala Inspekta Fatma. Mazoezi yaliendelea kwa nguvu, na kadiri alivyokuwa akiendelea na mazoezi, ndivyo alivyozidi kujihisi akirudia kwenye uwezo wake wa ngumi aliokuwa nao hapo awali...kabla hajapigwa marufuku kushiriki katika mchezo ule aliokuwa akiupenda sana, na kujikuta akikaa nje na ulingo kwa miaka mingi, miwili kati ya hiyo akiwa gerezani. Kadiri siku zilivyosogea, ndivyo alivyozidi kuhisi msisimko wa ajabu wakati utashi wa mchezo ule ukimtambaa ndani ya mishipa yake ya damu. Mchezo wa ngumi...ndondi...mchezo wa mabondia. Naye sasa alikuwa anajiandaa kuingia tena ulingoni kushiriki mchezo ule. Wengi walikuwa wakishiriki mchezo ule kwa ajili ya kutaka sifa na umaarufu, wakati wengine walikuwa wakishiriki kwa ajili ya pesa tu, ilhali wengine ilikuwa ni kwa ajili ya pesa na umaarufu na sifa. Na wachache miongoni mwa mabondia walikuwa wakishiriki mchezo ule kwa upenzi tu wa michezo kama ilivyokuwa kwake kabla hajapigwa marufuku... na kabla ya kifungo chake. Lakini safari hii Roman alikuwa anarudi ulingoni kwa ajili ya kutimiza azma. Azma ya hatari. Azma iliyokuwa ikifumfukuta moyoni kwa miaka miwili. Azma iliyogubikwa usiri mkubwa. *** Roman alikuwa akikimbia huku akitupa ngumi mbele yake na kuruka huku na huko kibondia kando ya barabara. Alikuwa amevaa suruali ya mazoezi na fulana nchinjo ya mazoezi ambayo ilikuwa na kofia iliyofunika kichwa chake. Usoni alikuwa amevaa miwani maalum ya kumkinga na upepo na vumbi. Mark Tonto alikuwa akimfuta nyuma taratibu akiwa kwenye baiskeli. Walikuwa kwenye mazoezi makali, ikiwa ni siku tatu tu kabla ya kuanza kwa mashindano ya ndondi za ridhaa kugombea ubingwa wa mkoa, safari hii Roman naye akiwa miongoni mwa mabondia wa Kawe Boxing Club watakaopanda ulingoni. Wakiwa katika harakati zao zile za mazoezi, hawakuitilia maanani kabisa Toyota Prado short chasis yenye rangi ya metallic iliyokuwa imeegeshwa kando ya barabara ile waliyozoea kuitumia kila asubuhi kwa ajili ya mazoezi yao makali. Ndani ya ile gari, Master D na Kate walikuwa wakiwatazama kwa utulivu wawili wale wakiendelea na mazoezi yao. Kate alimtazama yule jamaa aliyetoka gerezani siku kadhaa zilizopita jinsi akitupa masumbwi hewani namna ile huku akiranda kulia na kushoto kistadi wakati akikimbia kando ya ile barabara, na uso wake ukafanya tabasamu dogo. “Enhe? Nini kinafuata sasa Master D?” Alimuuliza yule mtu mzima aliyekuwa naye ndani ile gari huku bado akiwaangalia akina Roman. Ilikuwa ni zamu ya Dan kuachia tabasamu dogo, kisha akaliondoa gari kando ya barabara, akawapita akina Roman na kuondoka eneo lile. “Kinachofuata ni kukabiliana na Roman sasa...nadhani mambo yanaenda kama tutakavyo...” Master D alimjibu. “Okay...lini sasa?” Kate alihoji. “Soon...very soon...(muda mfupi sana ujao) mrembo wangu!” *** Mashindano ya ndondi kugombea ubingwa wa mkoa wa Dar es Salaam yalichukua muda wa wiki tatu. Katika wiki ya kwanza Kawe boxing club ilipandisha mabondia wanne ulingoni, watatu wakishinda na mmoja akipoteza pambano. Roman alikuwa miongoni mwa watatu walioshinda kwa kumuangusha mpinzani wake katika raundi pili tu ya pambano, na hapo hapo kujipatia mashabiki kwa jinsi alivyokuwa akipigana. Wakiwa mazoezini ndani ya ile klabu yao mwisho wa ile wiki ya kwanza,Roman alipata ugeni asioutarajia. Siku hiyo alikuwa ulingoni akipigana na bondia mwenzake ikiwa ni sehemu ya mazoezi, mkufunzi wao Mark Tonto akiwa kama muamuzi na wakati huo huo akitoa mafunzo. Mabondia wengine wa timu ile ya ndondi walikuwa nje ya ulingo wakifuatilia pambano lile la mazoezi kwa makini, wote sasa wakiwa wamemkubali Roman kama mwenzao na kama bondia mwenye uwezo mkubwa miongoni mwao. Yule bondia alikuwa akimjia kwa ngumi kali za mfululizo, na Roman alikuwa akiruka huku na kule, akitupatupa miguu yake mbele na nyuma kiufundi huku akimsogezea uso mpinzani wake na kuurudisha nyuma kila jamaa alipojaribu kumtupia konde, hoi hoi na vifijo vikirindima kutoka kwa mabondia wenzao waliokuwa nje ya ulingo. Jamaa alikuwa akimjia kwa kasi, Roman aliyumba kushoto na kubonyea kidogo huku akimsogelea, wakati jamaa alipotupa konde kali la kushoto lililopita hewani, na Roman aliibuka na upper cut iliyotua sawia kidevuni kwa mpinzani wake na kumpeleka chini kama mzigo. Shangwe ziliibuka kutoka kwa mabondia wenzao, wakati Roman akimsaidia bondia mwenzake kuinuka kutoka pale chini. “Pole partner...sikuipa nguvu zangu zote hata hivyo...kwa hiyo hutadhurika sana!” Alimwambia yule bondia huku akimsaidia kusimama. “Sasa huo ndio upiganaji Roman!” Mark alisema kwa hamasa huku akiwasogelea wale wapiganaji wake, na kumgeukia yule kijana aliyepelekwa chini kwa konde la Roman, “...na ule si upiganaji! We’ umenaswa kwenye mtego wa Roman, Chumbi... anakuchezeshea uso nawe unautamani uso, unasahau kujikinga...” Mark alikuwa akisema, lakini hapo macho yake yaliangukia nje ya ulingo, na kutulia huko kwa muda, sentensi yake ikibaki ikielea hewani. Alimtupia jicho la haraka Roman, na kuyarudisha tena macho yake kule nje ya ulingo. Roman aligeuka kufuata ulelekeo wa macho ya Mark, kama jinsi ambavyo na wale mabondia wengine walikuwepo pale walivyofanya. Inspekta Fatma alikuwa amesimama nyuma kabisa ya ule ukmbi wao wa mazoezi, akiwa amevaa mavazi yake ya kiaskari, kofia yake akiwa ameikumbatia chini ya kwapa lake la kushoto. Kwa mkono wake wa kulia alikuwa ameshika fimbo yake ya kiaskari ambayo alikuwa akiipiga-piga taratibu kwenye tumbo la kiganja chake cha kushoto. Uso wake uliokuwa umefunikwa kwa miwani myeusi ulikuwa ukimtazama Roman moja kwa moja kule ulingoni. “Sasa huyu anataka nini tena hapa?” Mark Tonto alisema kwa sauti ya chini huku akimtazama yule askari wa kike. Roman alimuacha Chumbi na kuusogelea ukingo wa ule ulingo na kusimama akiwa ameshika kamba ya ulingo ule huku akimtazama Inspekta Fatma. Walibaki wakitazamana kwa muda, kisha Inspekta Fatma aliweka kofia yake kichwani taratibu, na bila ya kusema neno lolote, aligeuka na kuondoka. Hivyo tu! Roman na Mark walitazamana, lakini hakuna yeyote kati yao aliyesema neno, kisha Mark akawageukia wale mabondia wake. “Alrigh, alright, alright, Hey! Haya tunaendelea, tumeshaona jinsi Roman na Chumbi walivyojifua...sasa nataka niwaone Dulla na Kibwe ulingoni...” Alisema huku akipiga makofi kuwahamasisha wachezaji wake. Roman aliteremka ulingoni, na taratibu aliondoka eneo lile kuelekea ofisini kwa Mark, ambako ndiko kilikuwa chumba chake cha kulala. Uso wake ulikuwa umekunjamana kwa tafakuri nzito. “Sasa ndio nini vile?” Mark Tonto alimuuliza Roman saa moja baadaye wakiwa wamekaa kwenye ile baa iliyokuwa nje ya klabu yao ya ndondi pale Kawe, kisha akaendelea, “...yule askari ana maana gani kuja hapa na kuondoka bila kusema neno?” Roman aliuma mdomo wake kwa hasira. “Alikuwa anajaribu kunipa ujumbe Mark...” “Ujumbe gani sasa?” “Kwamba bado ananifuatilia na kwamba nisisahau onyo alilonipa siku ile nilipotoka gerezani.” Mark alitikisa kichwa kwa mastaajabu. “Ama hakika huyu mwanamke majinuni...sasa tufanyaje Roman?” “Sisi tunaendelea na harakati zetu kama kawaida, hakuna kinachobadilika.Hii mikwara ya Inspekta Fatma hainitishi hata kidogo mimi.” Wiki ya pili ya mashindano ya ubingwa wa mkoa wa ndondi za ridhaa, Kawe boxing club ilipoteza bondia mmoja, na Roman na Chumbi wakasonga mbele kwenye fainali, safari hii Roman akimuangusha mpinzani wake katika dakika ya kwanza tu ya raundi ya nne na ya mwisho. Lilikuwa ni pambano lililojaa hoi hoi na nderemo kwa jinsi Roman alivyokuwa akimchezea yule mpinzani wake, na hatimaye kumuangusha kwenye ile raundi ya mwisho. Sasa Roman alikuwa ni miongoni mwa mabondia wenye mashabiki wengi kabisa katika mashindano yale. Jioni ile Mark aliandaa sherehe fupi pamoja na mabondia wake kuwapongeza Roman na Chumbi kwa kufikia fainali ambayo ingefanyika katika wiki ifuatayo. Wakiwa katikati ya sherehe zao pale kwenye ile baa iliyokuwa nje ya klabu yao, Mark alinunua gazeti la jioni lililokuwa likipitishwa na mchuuzi pale baa na kumuonesha Roman habari iliyokuwa kwenye ukurasa wa michezo wa gazeti lile. Deus wa mauaji kukabiliana na Mswazi. Kichwa cha habari ile kilinadi, na mara moja Roman akawa makini na habari ile, ambayo ilieleza kuwa bingwa wa dunia wa uzito wa Super Middle Deus “deadly” Macha alikuwa akitarajia kuzipiga na bondia kutoka Swaziland katika pambano la kimataifa kutetea ubingwa wake alioupata miezi sita iliyopita. Pambano lile lilipangwa kufanyika mwisho wa wiki ile, siku ya jumamosi katika ukumbi wa PTA jijini. Habari ile ilileta mjadala baina ya wale mabondia wa ile timu ya Kawe, baadhi ya wale mabondia wakimsifia Deus jinsi alivyo mahiri katika masumbwi, na jinsi alivyokuwa akiwaangusha wapinzani wake, wengine wakitamani siku moja kuwa kama yeye. Roman na Mark Tonto walitulia kimya akiwasikiliza wale vijana wakimjadili Deus. “Okay boys, mnaonaje sote tukienda kushuhudia pambano hilo jumamosi hii, eenh?” Hatimaye Mark aliuliza. Mayowe na shangwe vililipuka kutoka kwa vijana wale, wakiiafiki hoja ile ya Mark kwa mbinja na hoi hoi, wengine wakirukaruka huku wakitupa ngumi hewani na kucheza kibondia kufurahia swala lile. “Aaah, acheni fujo sasa, ebbo!” Mark aliwaasa wale vijana wake kwa ukali huku akiona wateja wengine pale baa wakionekana kuwashangaa na kukereka kwa mayowe yale. Roman aliinuka na kuondoka na lile gazeti kuelekea chumbani kwake bila ya kuaga. Mwili ulikuwa ukimtetemeka kwa mchanganyiko wa hamasa na jazba. *** Siku ya pambano ukumbi wa PTA ulifurika mashabiki wa kitaifa na kimataifa. Baada ya mapambano ya utangulizi hatimaye ulifika wakati ambao hasa watu wote waliofurika pale walikuwa wakiusubiri. Bondia kutoka Swaziland alipanda ulingoni akisindikizwa na kocha na wapambe wake wachache, shangwe kidogo zilisikika,lakini zaidi ilikuwa ni sauti za kuzomea kutoka kwa mashabiki wa Deus. Kisha akaingia Deus mwenyewe akiongozana na kocha na promota wake pamoja na msururu wa wapambe, muziki wa bongo flava maalum wa kumsindikiza ukirindima kutoka kwenye maspika makubwa yaliyotandazwa kila kona ya ukumbi ule, mayowe, vifijo na mbinja vilirindima kila upande, na kadiri zile shangwe zilivyozidi, ndivyo Roman, akiwa miongoni mwa watazamaji waliohudhuria pambano lile pamoja na mabondia wenzake wa Kawe Boxing Club na kocha wao Mark Tonto, alivyoweza kusikia muitiko wa pamoja kutoka pale ukumbini. “Deus...Deadly...Deus...Deadly...Deus...Deadly...!” Roman alitulia kimya akitazama kila tukio kwa makini, na kengele ya kuanza pambano ilipogongwa, alishuhudia jinsi Deus akimsulubu mpinzani wake kutoka uswazi kwa namna ambayo ilimfanya aelewe ni kwa nini alifikia hatua ya kuitwa “Deus wa mauaji”. Mswazi alienda chini mara mbili, kwenye raudi ya nne na ya tisa, na alipoenda chini kwa mara ya tatu kwenye raundi ya kumi hakuinuka tena. Kwisha kazi. Deus alikuwa amefanya “mauaji’ kwa mara nyingine. Ukumbi ulipagawa kwa vifijo. Mashabiki walijaribu kuvamia ulingo, kabla ya kutulizwa na Deus akatangazwa mshindi rasmi. Hapo ukumbi ulilipuka upya, Deus aliinuliwa juu huku akizungusha ngumi hewani kushangalia ushindi wake. Roman alisimama na kuanza kusogea karibu na ule ulingo, Mark Tonto akiwa sambamba naye. “Vipi Roman...” Mark aliuliza. “Nataka nimuone vizuri...” Roman alijibu huku akijisukuma mbele na kusimama hatua chache kando ya ule ulingo, akiwa amefumbata mikono kifuani kwake akimtazama yule bingwa wa dunia mtanzania akifurahia ushindi wake. Na ndipo ghafla, katika kuzunguka kwake huku na huko akishangilia ushindi wake ilhali uso wake ukiwa na tabasamu pana, macho ya “Deusdeadly” Macha yalipoangukia kwa Roman akiwa amesimama kando ya ule ulingo akimtazama. Walionana...uso kwa uso. Ghafla uso wa bingwa wa dunia Deus ulibadilika, na lile tabasamu likafutika, nafasi yake ikichukuliwa na mshangao, kisha kitu kama woga mkubwa, na haraka ule woga ukachukuliwa na ghadhabu. Alijikurupusha na kuteremka kutoka mabegani kwa yule shabiki aliyekuwa amembeba. Katika kufanya hivyo,aliinamisha kichwa chake kuangalia asianguke, na wakati alivyofanya vile, Roman aliweza kumuona Inspekta Fatma akiwa upande wa pili wa ule ulingo. Yule askari hakuwa akiangalia yale yaliyokuwa yakitendeka ndani ya ule ulingo, bali alikuwa akimtazama Roman kutokea kule alipokuwa amesimama! “Shit! Inspekta Fatma!” Roman alinong’ona kwa hasira na kujirudisha nyuma akijichanganya kwenye umati wa mashabiki waliokuwepo pale. “Wapi...wapi?” Mark Tonto alinong’ona kwa wahka, lakini Roman alimshika mkono na kumvutia kule alipokuwa akitowekea, akizidi kujichanganya katikati ya kundi la watu. “Deusdeadly” Macha, bingwa anayeendelea kutamba na mkanda wake wa dunia katika uzito wa Super Middle, alitoka mbio hadi kwenye ukingo wa ulingo katika ule upande ambao alimuona Roman akiwa amesimama hapo awali, na kuangaza macho yake yaliyojaa wahka eneo lile. Patupu! Roman hakuwepo! Badala yake aliona kundi la mashabiki tu wakimshagilia na kumpungia mikono huku nyuso zao zikiwa zimejawa tabasamu. Deus hakuwatilia maanani. Alikuwa akimtafuta Roman katika kundi lile lakini hakumuona tena. Aligeukia upande wa pili wa ulingo ule hali ikawa vilevile, aliranda huku na huko ndani ya ulingo ule akijaribu kumtafuta tena Roman, lakini Roman hakuonekana kabisa machoni mwake. Ilikuwa kama kwamba yule aliyemuona hakuwa Roman bali ni taswira tu iliyojijenga kichwani mwake! Kwenye kona moja ya ukumbi ule, Master D alimgeukia Kate na kumwambia huku akiinuka kutoka kwenye kiti chake. “Okay, tunaweza kwenda sasa mrembo wangu...tumeona mengi kwa leo au sivyo?” “Sana anko...sana tu. Si umeona jinsi uso wake ulivyohamanika alipomuaona Roman? E bwana we! Leo mbona tumeona mambo!” Kate alisema huku naye akiinuka. ITAENDELEA KESHO!!!
Posted on: Sat, 09 Nov 2013 03:51:11 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015