Rebecca (16) Ilipoishia Ijumaa iliyopita... Kadhalika hakuwa na - TopicsExpress



          

Rebecca (16) Ilipoishia Ijumaa iliyopita... Kadhalika hakuwa na uhakika kama katika siku zile mbili ambazo aliwahi kuwa na John dereva aliweza kuwaona na kumtia akilini. Na ukizingatia hakuwa na picha ya huyo mtu ambayo ingalimsaidia dereva kumsaka atakavyoweza. Akaamua kuifanya kazi hiyo yeye mwenyewe na endapo atashindwa ndipo atajaribu kuomba msaada siyo wa dereva tu, hata mama yake ambaye alikuwa karibu naye ikibidi. Endelea... Juhudi za Rebecca katika kumtafuta John, hazikuonesha kuzaa matunda. Mwaka wa kwanza wa masomo ukapukutika kama mchezo bila dalili wala fununu za kupatikana John. Hakukata tama, akaongeza juhudi na kuzidisha mitego karidi alivyoona inafaa huku akiwatumia baadhi ya marafiki zake aliosoma nao pale Jangwani ambao walikuwa wametawanyika katika Vyuo Vikuu mbalimbali nchini kumpatia taarifa kuhusu mtu huyo aliyemsaka. Mwaka wa pili nao ukafutika kama kimbunga kiwezavyo kufuta uso wa dunia bila kizuizi. Jambo lilikuwa lile lile, hakuna habari za John. Mwaka wa tatu wa masomo ndiyo huo umeanza, lakini tangu umeanza haujonesha dalili zozote za kumsaidia kumpata John. Wakati huu ndiyo moyo wake ukaonesha kukata tama. Akajilaumu kwa kukataa kwenda Uingereza kwa kutaka kufanya jambo asilofanikiwa. Jambo aliloweka juhudi kubwa, lakini hakuna mafanikio hata ukufi. Aliona bora angalikwenda huko kusoma kuliko kuutesa moyo wake kwa jambo lisilowezekana. Kutokana na kujawa na mawzo mengi kichwani, ikapelekea kuwaza kuwa huenda hata John mwenyewe hayupo tena katika uso wa dunia. “Pengine hata amekufa kutokana na msongo wa mawazo ya kuondokewa na wazazi wake kwa mpigo.” Alipohisi kutawaliwa na mawazo haya, akajilaani kwa kumuombea mambo mabaya kiumbe cha watu, akajihadhari nayo na yalipomtoka, yakamjia mawazo kuwa huenda ameamua kurudi kwao Mtwara baada ya maisha ya hapa mjini kumshinda. Ama kweli mfa maji haishi kutapatapa, akapanga kwenda kumtafuta huko. Lakini akajiona mjinga aotaye ndoto za mchana. Kama ameshindwa kumpata hapa jijini ambako ana uzoefu napo, ataweza huko ambako zaidi ya kusoma katika magazeti, vitabu na wakati mwingine kuona katika luninga, hajawahi hata kuwaza kwenda. Siku moja wakati Rebecca anatoka darasani, alikutana na mtu mmoja ambaye hisia zake hazikumdanganya kuwa alikuwa ni mmoja wa marafiki wakubwa wa John kipindi kile wako tuition miaka mitano iliyopita na aliwahi kuwaona wako pamoja mara kadha. Moyo wake ukafurahi sana akijua kuwa atapata fununu fulani kuhusu John. Akasogea alipokuwa huyo mtu na kumsalimu bila kumtaja jina kwani hakulifahamu na kama alilifahamu, basi amelisahau, “Mambo!” “Ah! Rebecca?!” Akashangaa yule jamaa na kuendelea, “Mambo vipi Rebecca, habari za siku nyingi?” “Salama kabisa, hujambo wewe?” Akaitikia Rebecca. “Mi niko poa sana. Vipi shemeji hajambo?” Akatania yule jamaa huku akimaanisha kile alichokisema. Rebecca akakerwa na swali lile ila hakutaka kuonesha chuki ya wazi wazi, hivyo alijibu kwa mzaha pia akimaanisha. “Kuolewa wapi ndugu yangu. Siku hizi waoaji wenyewe hawaonekani kabisa. Vipi wewe umeshavuta jiko?” “We mwanamwali una makusudi wewe! Yaani kunona kote huko halafu usiolewe, au bado hujaacha yale mambo yako ya shule?” Akaendeleza yule jamaa. Hapa Rebecca ndiyo akachafuka kabisa, kidogo amjibu vibaya lakini alijizuia kufanya hivy kwa kuchelea kukosa alichokikusudia, hivyo akatabasamu. Japo tabasamu lile lilikuwa la bandia, lakini lilionesha kila dalili ya urimbwende alojaaliwa na Maulana. “Wacha utani wako bwana. Enhe, niambie, umepata kumwona bingwa wa mathematics enzi zile. Hivi anasoma wapi sasa hivi au yuko na mambo gani?” Akauliza Rebecca kwa lengo la kumpoteza maboya yule jamaa asielewe lengo lake. “Nani, John! Duh, kwa kweli hakuna mtu ninayemtafuta kama rafiki yangu John. Sijamuona muda sasa. Nakumbuka mara ya mwisho kuonana naye ni baada ya kumaliza kidato cha sita ambapo tulikutana Ubungo siku aliyotoka Tanga na kuniambia kuwa anakwenda kusubiri majibu nyumbani kwao Mtwara. Tangu hapo sijamuona wala kupata habari zake zozote. John, sijui bado atakuwa Mtwara?” Naye bila kujua, akajibu kwa masikitiko makubwa. “Hakukupa namba ya simu?” Akauliza Rebecca. “Alinipa, lakini niliifuta kwa sababu tangu anipe, sikuwahi kumpata hewani hata mara moja.” Akajibu yule jamaa. Moyo wa Rebecca ukaugulia kwa maumivu kwa habari hizi ambazo hakuzitarajia kuzisikia. Yeye alitarajia kusikia kuwa John yuko mahala fulani la sivyo, apate habari nyingine nzuri zitakazomsaidia kumpata John. Akataka kumuuliza yule jamaa kwa nini alifuta namba ya simu ya John. Pengine wakati huu angalikuwa anapatikana. Akajizuia. “Kwani we hujapata habari zake?” Akauliza yule jamaa aliyeoneka kuzama katika mawazo. “Hapana, mimi mwenyewe namtafuta sana tena kwa muda mrefu, lakini sijabahatika.” “Mh! Any way, tufanye hivi…” Akasema yule jamaa na kuendelea, “…tumtafute kwa pamoja na kila hatua itakayofikiwa na mmoja wetu, basi tupeane taarifa. Namhitaji sana rafiki yangu John.” “Sawa haina shida.” Akaafiki Rebecca. “Chukua basi namba yangu ya simu na wewe nipe ya kwako ili turahisishe mawasiliano, au vipi?” Akashauri yule jamaa. Rebecca hakuwa tayari kutoa namba ya simu kwa kuogopa kusumbuliwa, lakini baada ya kutafakari sana akakubali. Wakabadilishana. “Nisave jina gani?” Akauliza Rebecca. “Muntari.” Akajibu yule jamaa. “Ah, we vipi, mi nataka jina lako bwana, Muntari ndiyo nini?” Akafoka Rebecca. ************** John! John! Oooh! John! Unatafutwa na akupendaye kwa dhati ya moyo...uko wapi John?. Juhudi za Rebecca kumtafuta John zinashika hatamu ingawa hazioneshi dalili ya mafanikio lakini hakati tamaa. Sasa ameongezeka mtu mwingine wa kumsaka John kwa udi na uvumba. Je, watafanikiwa kumpata ama kujua aliko? Andika ubashiri wako hapo chini!. Tunawatakia siku njema___
Posted on: Mon, 09 Sep 2013 02:41:39 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015