Riwaya: ONLY GOD CAN FORGIVE ME Sehemu: 04 Ilipoishia marafiki - TopicsExpress



          

Riwaya: ONLY GOD CAN FORGIVE ME Sehemu: 04 Ilipoishia marafiki zake wakubwa sana, wa kwanza alikuwa Brian Ruttaba ambaye alikuwa ametoka nchini Tanzania na wa pili alikuwa Antonio Sanchez, kijana kutoka nchini Mexico, nae maisha yake yalikuwa kama ya Alan, japokuwa baba yake alikuwa tajiri mkubwa nchini Mexico lakini Antonio hakutaka kuishi maisha ya kifahari kabisa. Songa nayo... Alan akajitahidi kujivika ujasiri moyoni mwake. Hakuonekana kuwa na amani kabisa, alionekana kuwa na wasiwasi mwingi kupita kawaida. Hakuamini kama kitendo cha kuwa mahali hapo kwa ajili ya kumuona Albertina na kuongea nae ndicho ambacho kilikuwa kimeanza kumpa hofu kiasi hicho. Mwili wake ukaanza kutetemeka, amani ikatoweka moyoni mwake kiasi ambacho wakati mwingine akaonekana kujuta kwa kuamua kutaka kufanya kile alichikuwa akitaka kukifanya mahali pale. Wakaingia ndani na kisha kukaa kochini. Kila wakati Alan akawa mtu wa kujiangalia kama alikuwa sawa au la. Muda wote huo Brian alikuwa akimwangalia tu, Alan alionekana kutokujiamini kabisa, uso wake ulionekana kuwa na hofu kubwa kupita kawaida. Alichokifanya Brian ni kuondoka sebuleni hapo, aliporudi baada ya dakika moja, alirudi akiwa na Albertina kitu ambacho kilimfanya Alan kuusikia moyo wake ukipata mshtuko mmoja mkubwa, mzunguko wa damu mwilini mwake ukaongezeka zaidi. Kwa siku hiyo, Albertina alionekana kuwa mrembo zaidi usoni mwa Alan, alibaki akimwangalia Albertina usoni, bado hakuonekana kuamini kama msichana aliyekuwa na urembo mkubwa namna ile angekuwa barani Afrika tena katika nchi kama Tanzania. Albertina akamsalimia Alan huku akiachia tabasamu pana usoni mwake, tabasamu ambalo lilionekana kumchanganya zaidi Alan. Kama walichokipanga ndicho ambacho kilitakiwa kufanyika mahali hapo. Alichokifanya Brian ni kuaga kwamba alikuwa akielekea katika kituo cha mafuta kwa ajili ya kununua mafuta ya gari na angeweza kurudi baada ya dakika kadhaa huku akimtaka Albertina kubaki na Alan ili asijisikie upweke mahali hapo. Hiyo ndio ilionekana kuwa njia nyepesi lakini kwa Alan ukaonekana kuwa mtihani mkubwa sana katika kufanikisha kile alichokuwa akitaka kukifanikisha kwa wakati huo. Msichana ambaye alikuwa akimtaka sana kwa wakati huo alikuwa mbele yake tena huku wakiwa wawili tu pale sebuleni. Alan akabaki akimwangalia Albertina huku kila wakati akimeza fundo la mate. Kwa muonekano ambao alikuwa nao mahali hapo alionekana kutokufahamu ni mahali gani ambapo alitakiwa kuanzia ili apate kueleweka moyoni mwa Albertina. “Unaonekana tofauti sana” Alan alimwambia Albertina, kwa sababu hakujua aanzie wapi, yeye akaanza kuyatamka maneno ambayo yalimjia mdomoni wakati huo. “Kivipi?” “Unaonekana mnyonge sana, mwenye mawazo mengi na wakati uso wako unaonyesha kwamba hautakiwi kuwa katika hali hiyo” Alan alimwambia Albertina ambaye akaanza kumtilia umakini Alna. “Uso wangu unatakiwa kuonekana vipi?” Albertina alimuuliza Alan. “Unatakiwa kuonekana kuwa na furaha. Tabasamu ndicho kitu pekee ambacho ninaamini kinaweza kuupendezesha zaidi uso wako” Alan alimwambia Albertina. “Huwa ninatabasamu kila siku na kila wakati” “Labda katika kipindi ambacho sipo mahali hapa” “Kila wakati ninatabasamu Alan” “Hivi ni muda gani ambao nilikuwa ndani ya nyumba hii na ukatabasamu?” Alan alimuuliza Albertina. “Muda wote” “Unanidanganya. Ninatamani sana kukuona ukitabasamu. Hata kama una shida, wakati mwingine yakupasa kusahau shida zako” Alan alimwambia Albertina. “Najua na ndio maana najitahidi kutabasamu kila wakati” Albertina alimwambia Alan. Huo ndio ukaonekana kuwa mwanzo wa Alan kuanza kuongea na Albertina. Alijua fika kwamba moyoni alikuwa akihofia sana na hivyo alitakiwa kwanza kumzoea Albertina hata kabla hajamwambia jinsi alivyokuwa akijihisi ndani ya moyo wake juu yake. Muda ukazidi kusonga mbele, dakika zikazidi kukatika huku mazungumzo ya hapa na pale yakizidi kuongezeka zaidi na zaidi mpaka kufikia kipindi ambacho Alan akaonekana kumzoea Albertina. “Kuna mengi ninatamani sana kukwambia, ila nadhani moja ni la umuhimu kuliko yote” Alan alimwambia Albertina ambaye kwa mbali akaonyesha mshtuko. “Kama lipi?” “Kuhusu uzuri wako, mvuto wako na mengine mengi yanayokuhusu wewe” Alan alimwambia Albertina ambaye akaanza kujiangalia. “Kati ya wazuri mimi ni mzuri?” “Unajionaje?” “Wa kawaida sana” “Hapana. U mzuri sana. Nimekuwa nikiutafakari uzuri wako katika usiku mzima uliopita. Taswira ya sura yako imekuwa ikinijia kila wakati mawazoni mwangu Albertina” Alan alimwambia Albertina. “Umekuwa ukinifikira?” Albertina alimuuliza Alan huku akionekana kushtuka. “Huo ndio ukweli. Nimekuwa nikikufikiria sana. Nadhani ni kwa sababu ya jinsi ulivyo, nina uhakika” Alan alimwambia Albertina ambaye akabaki kimya, ukimya ambao ukampa ujasiri Alan na kuendelea kuongea. “Nimesafiri umbali mrefu sana kuja kumtembelea Brian, katika safari yangu hii nadhani Mungu alikuwa ameniandalia kitu kwa ajili ya maisha yangu. Katika kipindi ambacho ninaianza safari sikuwa nikifahamu ni kitu gani ambacho Mungu alikuwa ameniandalia ila kwa sasa nimeanza kugundua, safari yangu haikuwa ya bure, baada ya kukaa kwa kipindi kirefu, nadhani Mungu amejibu maombi yangu, ameyajibu kupitia safari yangu” Alan alimwambia Albertina ambaye alikuwa kimya, alionekana kufahamu Alan alimaanisha nini. “Najua unataka kuniambia nini. Tafadhali, naomba usiniambie unachotaka kuniambia” Albertina alimwambia Alan huku akionekana kuanza kubadilika. “Kwa nini nisikwambie? Kuna ubaya kama nikikwambia wewe ni msichana mzuri ambaye umetokea kuuteka moyo wangu na kukuhitaji katika maisha yangu? Kuna ubaya kama nitasema kwamba baada ya kukuona wewe moyo wangu umekuwa radhi kukupenda kwa moyo mmoja? Sidhani kama kuna ubaya Albertina” Alan alimwambia Albertina. Maneno ya mbalimbali yakaonekana kutokuwa na uwezekano wa kuubadilisha msimamo wa Albertina, alichokifanya ni kumsogelea na kukaa karibu yake. “Albertina….!” Alan alimuita Albertina ambaye alikuwa ameuinamisha uso wake chini, alipouinua, machozi yalikuwa yakimtoka. “Kuna nini tena? Mbona unalia?” Alan alimuuliza Albertina. “Naomba usiendelee zaidi” Albertina alimwambia Alan. “Kuna tatizo Albertina?” “Nakuomba usiendelee” “Najua nimekukumbusha mbali na kukuumiza, najua una maumivu makubwa moyoni mwako, naomba unipe nafasi moyoni mwako, si nafasi ya kukuumiza zaidi, ninahitaji nafasi ya kuyaondoa maumivu ambayo umekuwa nayo moyoni. Ninaomba unipe nafasi hiyo Albertina, ninakuahidi kukutunza na kukupenda kwa mapenzi ya dhati, zaidi ya hayo, ninakuahidi kukuoa, uwe mke wangu wa ndoa” Alan alimwambia Albertina. Maneno mengi ambayo alikuwa akiyaongea Alan ndio ambayo yalikuwa yakimfanya Albertina kuanza kumfikiria Kelvin. Kila neno ambalo lilikuwa likimtoka Alan yaliyafanya mawazo juu ya Kelvin kichwani mwa Albertina kujirudia zaidi na zaidi. Kama ni kidonda kilichokuwa kikitaka kupona, Alan alikuwa amekitonesha na kukifanya kuwa kibichi tena moyoni mwa Albertina. Maisha yamapenzi ambayo alikuwa ameyapitia yalionekana kumuumiza kupita kawaida, hakujiona kuwa na uhitaji wa kuwa na mwanaume yeyote katika maisha yake, mapenzi yalikuwa yamemuumiza, mwanaume mmoja ndiye ambaye alimfanya kuyachukia mapenzi na kuchukia kila kitu ambacho kilikuwa kikihusu mapenzi. Ni miezi sita tayari ilikuwa umepita tangu Albertina aachane na Kelvin ambaye alimsababishia maumivu makali moyoni mwake. Leo hii mbele yake kulikuwa na mwanaume mwingine ambaye alikuwa akiongea maneno mengi ambayo yalikuwa yakifanana na maneno yale aliyoyaongea Kelvin katika kipindi cha nyuma. Maneno yale hayakuonekana kubadilisha kitu chochote kile moyoni mwa Albertina, hata Alan nae alionekana kufanana na Kelvin, ili kuyaepuka maumivu mengine moyoni mwake, njia nyepesi ambayo alikuwa akiiona ni kutojihusisha na mapenzi katika maisha yake. “Albertina….” Alan alimuita Albertina huku akimshika mkono kitu ambacho kilimshtua Albertina na kumletea msisimko mkubwa mwilini mwake. “Nakuomba Alan. Unaniumizaaaaa…..!!” “Najua. Nahitaji nafasi moyoni mwako. Nahitaji kuwa nawe, ninahitaji uwe mke wangu wa ndoa. Nadhani Mungu kanileta Afrika kwa ajili yako. Nakuomba uwe mke wangu wa ndoa” Alan alimwambia Albertina ambaye alibaki kimya. Kila ukimya ambao ulikuwa ukitokea mahali hapo ukaonekana kuwa kusudi la kumtaka kufanya jambo jingine zaidi, jambo la maendeleo ambalo lingemfanya kumuweka Albertina katika hali ya tofauti kabisa. Alichokifanya Alan ni kumsogelea zaidi Albertina na kisha kuupitisha mkono wake mabegani mwa Albertina na kisha kumwangalia usoni. Machozi yalikuwa yakitiririka mashavuni mwa Albertina jambo ambalo lilimpelekea Alan kutoa kitambaa chake kilichokuwa mfukoni na kuanza kumfuta machozi Albertina. “Ninahitaji nafasi kutoka kwako. Ninaomba unifanye nijione kuwa mwanaume mwenye bahati katika maisha yangu” Alan alimwambia Albertina ambaye alibaki kimya, Alan hakunyamaza, akaendelea kutoa maneno mazito ya mapenzi. “Ninachokihitaji kutoka kwako ni kuweka uaminifu wako juu yangu, sitaki kuonekana mtu nisiyekuwa na msimamo kwa kila ahadi ninayokupa katika kipindi hiki, ninahitaji kusimama imara katika kila ahadi ambayo nimekwambia siku ya leo. Ninachokihitaji ni kuwa nawe tu, ninachokihitaji ni kukuoa tu, sipendi kukuona uso wako ukiwa kwenye maumivu makali, sipendi kuyaona machozi ya uchungu yakitiririka mashavuni mwako, ninachokihitaji ni kukuona ukiwa na furaha, ukitabasamu na kukufanya uvutie zaidi” Alan alimwambia Albertina ambaye alibaki kimya, maneno ya Alan bado yalikuwa yakiendelea kumuingia na kumkaa moyoni mwake. “Ninakuhitaji. Popote utakapokwenda jua kwamba ninakuhitaji, utakapokuwa ukitembea, ukilala, ukikaa au hata ukipika jua kwamba ninakuhitaji, jua kwamba kuna mwanaume anakuhitaji sana katika maisha yake, jua kwamba kuna mwanaume ambaye yupo tayari kujitolea maisha yake kwa ajili yako, jua kwamba kuna mwanaume ambaye yupo radhi kukuoa na kuwa mke wake wa ndoa” Alan alimwambia Albertina ambaye akasimama na kisha kuanza kuelekea chumbani kwake. Alan hakusema kitu kingine, hakumzuia Albertina, akamuacha aondoke mahali hapo. Albertina akaanza kulia tena kwa kwikwi, Alan akabaki kochini akimwangalia Albertina ambaye akapotea machoni mwake. Alan akajiona kuutua mzigo mkubwa ambao ulikuwa ndani ya moyo wake, hakuamini kama alikuwa amefanikisha kumwambia Albertina jinsi alivyokuwa akijisikia moyoni mwake. Ingawa alikuwa ameongea maneno mengi ya mapenzi lakini hakuwa na uhakika kama Albertina angeweza kumkubalia au la. “Akinikataa itakuwaje?” Alan alijiuliza lakini akakosa jibu kabisa. ***** Alan hakutaka kuchoka, alijua fika kwamba kulikuwa na kazi kubwa mbele yake ambayo alitakiwa kuifanya kwa mikono yake, alijua fika kwamba Albertina alikuwa ametoka katika maumivu makali ya mapenzi, maumivu ambayo yalimfanya kutokuyatamani tena mapenzi. Alan hakujiona kuwa na ulazima wa kufanya haraka, aliona kwamba kwa jinsi hali ilivyokuwa ilikuwa ni lazima afanye mambo kwa taratibu tena hatua kwa hatua. Hakuishi hapo, siku iliyofuata kama kawaida akaelekea nyumbani hapo na kuendelea kupigilia misumali ya moto moyoni mwa Albertina ambaye muda mwingi alikuwa akibaki kimya tu. Maneno mengi matamu ambayo alikuwa akiyaongea Alan yakaonekana kuingia moyoni mwa Albertina na kueleweka zaidi na zaidi lakini maneno hayo hayakumfanya Albertina kuwa mwepesi, bado aliendelea na msimamo wake kwamba hakutaka kujiingiza tena katika mahusian ya kimapenzi. Alan hakukoma, leo aliishia hapa na kesho kuendelea kwa kuamini kwamba kungetokea siku ambayo Albertina angeweza kukubaliana nae na hatimae kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na hatimae kumuoa lakini hali ikaonekana kuwa tofauti kabisa, Albertina alionekana kuwa mgumu sana. “What should I do Brian? (Natakiwa kufanya nini Brian)” Alan alimuuliza Brian mara baada ya kuona kwamba kila maneno matamu ambayo aliyaongea kwa Albertina hayakuwa yakieleweka. “Just keep going Alan (Endelea Alan)” Brian alimwambia Alan. “We always fight Brian and sometime we have to give up, maybe God prepares someone for me (Mara kwa mara tunapigana Brian na wakati mwingine yatupasa kusalimu amri, inawezekana Mungu kaandaa mtu mwingine kwa ajili yangu)” Alan alimwambia Brian huku akionekana kukata tamaa. “Do you real want to marry Alby? (Ni kweli unataka kumuoa Alby?)” Brian alimuuliza Aan. “I do….I always do (Ninataka…kila wakati ninataka)” “Then ask her for dinner (Muombe uende nae kula chakula cha jioni)” Brian alimwambia Alan. Brian shauku yake ilikuwa ni kuona Alan akimchukua Albertina na kisha kumuoa. Alijua fika kwamba Albertina hakuwa katika hali nzuri hata kidogo, muda mwingi alikuwa akionekana kuwa katika mawazo, hakupenda kumuona katika hali ile, kila siku alitamani kumuona dada yake akitabasamu tena na kuwa na furaha kama zamani na hiyo ndio ilikuwa sababu pekee ambayo ilimfanya kufanya kila kilichowezekana kuhakikisha kwamba Alan anakuwa na Albertina. Kitu alichokisema Brian kikaonekana kuwa na msingi sana, alichokifanya Alan ni kumuomba Albertina kwenda nae kula chakula cha usiku. Albertina hakukataa, kwa sababu Alan alionekana kuwa muelewa, akakubaliana nae. Mpaka kufikia hatua hiyo Alan akaona kwamba alikuwa anakwenda kufanikiwa kwa kile kitu ambacho kila wakati alikuwa akikihitaji kutoka kwa Albertina, kwa sababu hakuwa akizifahamu sehemu nyingi ndani ya jiji la Dar Es Salaam, akamchukua Albertina na kwenda nae katika hoteli ya Kilimanjrao ambapo hapo wakaanza kula chakula cha usiku. Kidogo mtoko ule ukaonekana kuanza kumbadilisha Albertina, tabasamu lake likaanza kuonekana mara kwa mara usoni mwake, alionekana kufurahia kwa kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea lakini bado msimamo wake ulikuwa ni ule ule kwamba hakutaka kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na Alan. Huo ukaonekana kuwa mwanzo tu, katika kipindi cha siku tano zilizokuwa zimebakia kabla ya kurudi Marekani Alan alitaka kuhakikisha kwamba msichana Albertina anakuwa wake na mwisho wa siku kumuoa na kuwa mke wake wa ndoa. Hakunyamaza, kila siku alikuwa akimwambia Albertina kuhusiana na jinsi alivyokuwa akiendelea kujisikia moyoni mwake. Tabasamu pamoja na muonekano wake wa tofauti usoni mwake ukaonekana kama kuulegeza msimamo wake lakini kila alipokuwa akiulizwa kama alikuwa tayari, jibu lake lilikuwa lile lile, hakuwa tayari. Kikafika kipindi ambacho Alan alionekana dhahiri kukata tamaa, kama ni maneno matamu alijiona kumaliza kila neno ambalo alitakiwa kulizungumza mbele ya msichana huyo lakini katika kila neno bado Albertina alionekana kuwa mgumu kumuelewa, yaani alionekana kuwa kama kiziwi. Siku hazikumsubiri, bado ziliendelea kukatika mpaka kufikia siku moja kabla ya kuanza safari ya kurudi nchini Marekani. Katika siku hiyo alishinda siku nzima nyumbani kwa mzee Ruttaba huku akiongea na Albertina tu. Alan alijitahidi kumfurahisha na kumuonyeshea mapenzi ya dhati lakini kwa Albertina alionekana kama kutokuyaona matendo ya kimapenzi ambayo alikuwa akimuonyeshea. Tayari Alan alijiona kuwa na mkosi, alijona kutokuweza kukamilisha kile ambacho alikuwa akitaka kukikamilisha kwa wakati huo, aliona kila dalili kwamba alikuwa akitakiwa kurudi nchini Marekani huku akiwa hajakamilisha kitu chochote kile kwa Albertina. Katika kipindi ambacho alikuwa akiendelea kuongea na Albertina hapo ndipo jina la msichana mwingine likaanza kujirudia kichwani mwake. Stacie, lilikuwa jina la mtu pekee ambaye alionekana kuwa na pingamizi kubwa la yeye kuwa na Albertina. Historia ya kimapenzi ambayo alikuwa nayo pamoja na Stacie ikaonekana kuanza kumchanganya kabisa kichwa chake. Wazazi wake walikuwa wakimfahamu sana Stacie na kila siku walikuwa wakitamani sana mtoto wao, Alan awe pamoja na msichana Stacie lakini kwa Alan katika kipindi hicho hakuonekana kuwa tayari kuwa na Stacie. Ni kweli alimchukulia Stacie kuwa kama mpenzi wake, walikuwa wakifanya mengi isipokuwa mapenzi tu. Stacie akawa amekufa na kuoza kwa Alan lakini kwa Alan mambo yalionekana kuwa tofauti kabisa. Alimpenda Stacie lakini hakuwa akimpenda kama vile alivyotakiwa kumpenda. Hakutaka kuwaambia wazazi wake kwamba Stacie hakuwa chaguo lake kwa sababu tu katika kipindi kile hakukutana na msichana ambaye alitokea kumpenda zaidi ya Stacie. Barani Afrika ndani ya nchi ya Tanzania katika jiji la Dar es Salaam ndipo ambapo Alan alikuwa amekutana na msichana ambaye alikuwa ametokea kumpenda kuliko msicha ayeyote yule, msichana huyu alikuwa Albertina. Albertina ndiye alionekana kuwa msichana wake sahihi ambaye alikuwa amezaliwa kwa ajili yake na si Stacie kama wazazi wake walivyokuwa wakifikiria. Alikuwa tayari kufanya lolote juu ya Albertina, hakutaka kumkosa msichana huyo, hata kama wazazi wake walikuwa wakitaka amuoe Stacie, kwake kitu hicho kisingeweza kukubalika kabisa, yeye alikuwa akimtaka Albertina tu. “Why are you doing this to me? (Kwa nini unajifanyia hivi?)” Alan alimuuliza Albertina. “How am I suppose to love you, Alan? I know that you real love me, but I can’t go back ( Natakiwa kukupenda vipi Alan? Najua kwamba unanipenda lakini siwezi kurudi nyuma)” Albertina alimwambia Alan. “Pleaseee (Tafadhaliiii)” “I CAN’T (SIWEZI)” Albertina alimwambia Alan na kisha kusimama na kuondoka mahali hapo. Huo kama ukaonekana kuwa msimamo wake wa mwisho ambao alikuwa amejiwekea, akaelekea chumbani kwake na kujilaza kitandani. Kila wakati Alan alipokuwa akiongea maneno ya kimapenzi yalimfanya kumkumbuka Kelvin. Hakujiona kama aliruhusiwa kupenda ndani ya dunia hii, kwa jinsi alivyokuwa amempenda Kelvin hakuamini kama ingetokea siku ambayo mwanaume huyo angeweza kumkataa kwa sababu ya mama yake. “Wanaume wote hawafanani Albertina. Inawezekana ulikuwa ukiyalazimisha mapenzi kwa Kelvin na wakati hakuwa mwanaume sahihi katika maisha yako. Kwa jinsi ulivyonielezea, nadhani Alan ni mwanaume sahihi katika maisha yako” Bi Janeth alimwambia Albertina. “Mama! Wanaume wanafanana mama” Albertina alimwambia mama yake. “ Sidhani kama Alan yupo hivyo. Amekuja kwako moja kwa moja na kukwambia kwamba anataka kukuoa, kwa nini usimpe nafasi ya kumsikiliza na kukubaliana nae? Hii inaweza kuwa nafasi yako Albertina, nafasi hii inaweza isijirudie tena katika maisha yako, inawezekana kamwe usimpate mwanaume mwenye mapenzi ya dhati kwako endapo utamuacha Alan aondoke bila kukubaliana nawe” Bi Janeth alimwambia Albertina. ***** Kila kitu alichokuwa amejaribu kukifanya kikaonekana kuwa si kitu chochote kwani bado Albertina alikuwa akiendelea kukataa kuwa nae. Alan akaonekana kuwa mnyonge, moyo wake ukakosa amani mpaka kufikia kipindi ambacho akaanza kujuta. Alijuta sababu iliyomfanya kuja nchini Tanzania ambapo ndipo alipokutana na Albertina na kujikuta akiingia katika mzigo mzito wa mapenzi huku msichana huyo akionekana kutokujali kitu chochote kile. Hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kuishi mara atakaporudi nchini Marekani siku inayofuatia. Hakupenda kurudi nchini Marekani huku moyo wake ukiwa katika mzigo mzito wa mapenzi juu ya msichana ambaye hakuwa akimhitaji, alikuwa akitamani sana kukamilisha kila kitu lakini tatizo lilikuwa lile lile kwamba Albertina alikuwa amemkataa. Usiku hakulala, alikesha huku akimfikiria Albertina, alishindwa kabisa kumtoa moyoni msichana huyo, alipogeuka huku, alikuwa akimfikiria Albertina na hata alipogeukia upande mwingine bado alikuwa akimfikiria Albertina tu. Alan alijua kwamba nchini Marekani kulikuwa na msichana aliyeitwa Stacie, msichana ambaye wazazi wake walikuwa wakimtaka kuwa nae kwa sababu nae alikuwa mtoto wa tajiri lakini Alan hakuonekana kuwa na muda wa kumfikiria Stacie tena. Moyo wake ukazama kwa msichana wa kitanzania, msichana ambaye alikuwa na kila sifa ya kuitwa mrembo mbele ya macho yake. Kitendo cha kumkosa Albertina kikaonekana kumuumiza sana, hakutarajia kama ingetokea siku ambayo angekuja kukataliwa na msichana ambaye alitokea kumpenda kwa mapenzi yote moyoni mwake, kwake aliamini kwamba kama Mungu alikuwa amempangia msichana fulani basi ilikuwa ni lazima ampate. “Au kuna jambo Mungu anajaribu kuniepushia?” Alan alijiuliza. “Inawezekana” Alijijibu. Siku ya safari ya kurudi nchini Marekani ikaingia, kwa sababu siku hiyo ndege ya shirika la American Airlines ilikuwa ikiondoka saa tano asubuhi tofauti na siku nyingine ambapo huwa inaondoka usiku wa manane, saa mbili asubuhi Alan tayari alikuwa amekwishajiandaa na ni Brian ndiye ambaye alikuwa akimsikilizia kwa ajili ya kuondoka hotelini hapo na kuelekea uwanja wa ndege. Saa tatu kasoro asubuhi Brian akaingia ndani ya eneo la hoteli hiyo huku akiwa ndani ya gari lake, akamtaka Alan kuingia garini kwa ajili ya kuondoka mahali hapo. Alan hakuonekana kuwa na furaha, bado alionekana kuwa mnyonge kupita kawaida, alipoingia ndani ya gari na macho yake kukutana na macho ya Albertina ambaye alikaa kiti cha nyuma, Alan akaonekana kushtuka. “Karibu” Albertina alimkaribisha Alan huku uso wake ukiwa na tabasamu pana. Alan hakuonekana kuamini, wakati mwingine alijiona kama alikuwa katika usingizi mzito ambapo baada ya muda fulani angeshtuka na kujikuta akiwa kitandani. Hakuamini kama Brian alikuwa amekuja pamoja na Albertina kwa ajili ya kumsindikiza kuelekea uwanja wa ndege. Albertina alikuwa katika kiti cha nyuma huku Brian na Alan wakiwa katika viti vya mbele, muda wote Alan alionekana kuwa na furaha tele, uwepo wa Albertina ndani ya gari lile ukaonekana kumpa furaha kupita kawaida. Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamekwishafika uwanja wa ndege. Alichokifanya Brian ni kuteremka kutoka garini na kuwaacha wawili hao ndani ya gari. Alan akaonekana kutokuridhika, akatoka pale katika kiti cha mbele na kuelekea katika kiti cha nyuma, wakabaki wakiangaliana tu. “Ujio wako unamaanisha nini?” Alan alimuuliza Albertina huku akionekana kutabasamu. “Unahisi unamaanisha nini?” Albertina nae akauliza. “Umeniacha njia panda” Alan alimwambia Albertina. Alichokifanya Albertina ni kumsogelea, akahakikisha kwamba uso wake upo karibu na uso wa Alan na kisha kumbusu shavuni. Alan akashtuka, kila kilichokuwa kikiendelea mahali hapo kilionekana kama ndoto moja nzuri ambayo alikuwa akiitamani katika maisha yake yote. Albertina hakuishia hapo, akaupeleka mkdomo wake katika mdomo wa Alan na kisha kuanza kubadilishana mate. Kwa kile kitendo kilichokuwa kimetokea, tayari kilionyesha kwamba ukurasa wa mapenzi kati ya watu hao wawili ulikuwa umekwishafunguliwa. “Umekuwa wangu hatimae” Alan alimwambia Albertina. “Naomba usiniumize” Albertina alimwambia Alan huku akiwa amekiinamisha kichwa chake kifuani mwa Alan. “Nakuahidi kutokukuumiza” Alan alimwambia Albertina. Hilo ndio lilionekana kuwa tukio la kwanza la furaha ambalo lilikuwa limetokea katika maisha yake yote. Moyo wake ukalipuka kwa furaha, hakuamini kwamba msichana ambaye alikuwa akimhitaji siku zote hatimae alikuwa amekuwa mpenzi wake na alionekana kuwa tayari kufunga nae ndoa. Alan akateremka kutoka garini, akamsogelea Brian na kisha kumkumbatia huku wote wawili wakionekana kuwa na furaha. “Nashukuru kwa kila kitu. Nakuahidi kutokumuumiza Albertina” Alan alimwambia Brian. “Hakikisha unafanya hivyo. Nakuamini” Brian alimwambia Alan. Wakaagana mahali hapo na kisha Alan kuanza kupiga hatua kuufuata mlango wa kuingilia ndani ya jengo la uwanja wa ndege. Majonzi aliyokuwa nayo, mawazo ya maumivu aliyokuwa nayo katika kipindi hicho kila kitu kikaonekana kubadilika kabisa. Majonzi yakawa furaha huku maumivu yale ya moyo yakiwa yamebadilika na kuwa faraja yake. “STACIE…!” Lilikuwa ni jina ambalo lilijirudia kichwani mwa Alan, tayari akaona kulikuwa na kitu kikubwa kingetokea endapo angewaambia wazazi wake kwamba alikuwa amempata msichana ambaye aliamini kwamba aliletwa duniani kwa ajili yake, ila pamoja na hayo, hakujua Stacie angelichukuliaje suala hilo. Je nini kitaendelea? Je mahusiano kati ya Alan na Albertina yataweza kudumu zaidi na zaidi? Je msichana Tracie ataweza kuwa kizuizi cha mahusiano haya? Haya na mengine mengi, tuonane kesho mahali hapa.
Posted on: Sat, 05 Oct 2013 12:11:19 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015