SI MZURI BINADAMU – SEHEMU YA 28. Nauhisi ubaridi kwenye uti wa - TopicsExpress



          

SI MZURI BINADAMU – SEHEMU YA 28. Nauhisi ubaridi kwenye uti wa mgongo. “Habari ndio hiyo, Hamisi. Ninakupa hadi mwisho wa wiki. Nitakupigia na kukuelekeza wapi tukutane na kunipa. Shilingi milioni ishirini keshi.” “Sina hiyo pesa. Mwisho wangu ni milioni tano.” Anajiinamia na kuchomoa sigara na kuiwasha. “Unapostarehe na mke wa mkubwa, lazima uwe na pesa ya kutosha kwa tahadhari. Jipigepige, bro. Mke wa bosi wako naye anaweza kuchangia. Hii ni kazi ya malipo ya mkupuo moja, sitarudi tena kukusumbua. Nikuachie uhuru wa kuchagua; kwenda jela, au uniandalie milioni ishirinui. Una siku sita. Nitakupigia Alhamisi unipe uamuzi wako.” Anasimama. “Nisamehe, nililazimika kukupiga, lakini hata hivyo, uliyataka mwenyewe haya. Tutaendelea kuwasiliana, na asante kwa kinywaji.” Namtazama akitoka kwa kutembea. Kichwa changu kinaanza kuuma tena na najisikia vibaya sana. Anatokomea na baada ya kitambo kidogo nasikia gari ikiwashwa na kuondolewa. Nasimama kwa tabu. Naenda bafuni na kulijaza beseni maji ya baridi. Nakitumbukiza kichwa changu majini. Narudi sebuleni nikiwa na nafuu. Ninakaa. Nalikodolea macho dari na kuwazua. Nimenasa, na wala si kidogo. Najiona sina ujanja. Nikienda kwa Gerson na kumueleza ukweli, kibarua sina. Nikitoka hapa na kwenda polisi kuwaambia, watamkamata Tina na bado kibaruani sitakuwa salama. Sasa nifanyeje? Kuna jambo moja tu la kufanya, najiambia. Unaenda kutoka mtegoni. Sio tu unaenda kutoka mtegoni bali pia unaenda kumpa kibano Abuu kabla ya kukupa wewe kibano. Hakuna namna nyingine. Ama zake ama zako. Angalau nina siku sita za neema. Jambo la kwanza kulifanya ni kuifanya mark II iwe salama. Sasa ni saa tatu unusu usiku. Naichukua simu yangu yamkononi na kumpigia Ismail, mwenye gereji, maeneo ya SIDO, ambayo huitumia kwa matengenezo ya gari yangu. “Ismail,” ninasema. “Ninasikitika kwa kukupigia mida hii lakini imebidi. Gari langu liliuparamia mti na limeharibika. Nataka litengenezwe haraka.” “Nina mafundi wawili hapa ambao hawana kazi ya kufanya wanaweza kuifanya kazi hiyo. Kama haijaharibika sana, Jumatano itakuwa tayari, lakini inanibidi nikione kiasi cha uharibifu kabla ya kuahidi chochote.” “Asante sana, Ismail,” ninasema. Ingawa kichwa changu kinanigonga kama nina kichaa, ninadhamiria kuiacha mark II mikononi mwa Ismail usiku huu. ITAENDELEA.
Posted on: Sun, 01 Sep 2013 06:28:30 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015