SURA YA KUMI NA NNE MASHARTI KUHUSU FEDHA ZA JAMHURI YA - TopicsExpress



          

SURA YA KUMI NA NNE MASHARTI KUHUSU FEDHA ZA JAMHURI YA MUUNGANO (a) Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano 206. Kutakuwa na Mfuko Mkuu wa Hazina wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano utakaoitwa “Mfuko Mkuu wa Hazina” ambamo fedha zote zitakazopatikana kwa njia mbalimbali zitawekwa, isipokuwa: (a) fedha ambazo zimetajwa katika Sheria kuwa zitumike kwa shughuli maalum au ziwekwe katika mfuko mwingine kwa ajili ya matumizi maalum; au (b)fedha ambazo kwa mujibu wa sheria, taasisi za Serikali zimeruhusiwa kukusanya na kubaki nazo kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa taasisi hizo. 207.-(1) Fedha zinaweza kutolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali kwa ajili ya matumizi kwa kuzingatia masharti yafuatayo: (a)fedha hizo ziwe kwa ajili ya matumizi ambayo yameidhinishwa kuwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali na idhini hiyo iwe imetolewa na Katiba hii au sheria nyingine yoyote; na (b)fedha hizo ziwe kwa ajili ya matumizi ambayo yameidhinishwa ama na Sheria ya Matumizi ya Serikali iliyotungwa mahsusi na Bunge au sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge. (2) Kwa kuzingatia masharti ya Ibara ndogo ya (1), fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali zitatolewa kutoka Mfuko huo kwa ajili ya matumizi kwa kuzingatia masharti kuwa matumizi hayo yawe yameidhinishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. (3) Fedha zilizomo katika mfuko Maalum wowote wa Serikali, isipokuwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, hazitatolewa kutoka mfuko huo kwa ajili ya matumizi isipokuwa kwa mujibu wa Sheria inayoidhinisha matumizi hayo. 208.-(1) Rais atatoa maagizo kwa watu wanaohusika kutayarishana kuwasilisha kwenye Bunge katika kila mwaka wa fedha wa Serikali makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kipindi cha mwaka wa fedha unaofuata. (2) Baada ya Bunge kuyakubali Makadirio ya Matumizi yaliyoainishwa katika Ibarandogo ya (1) kutawasilishwa kwenye Bunge Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali, kwa ajili ya kuidhinisha matumizi ya fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali zitakazogharamia shughuli mbalimbali za Serikali zinazohusu makadirio hayo. (3) ikiwa katika mwaka wa fedha wowote inaonekana kwamba: (a) fedha za matumizi zilizoidhinishwa na Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali kwa ajili ya kugharamia shughuli fulani hazitoshi; (b) imekuwa lazima kulipa gharama za shughuli ambayo haikupangiwa fedha za matumizi kwa mujibu wa Sheria; (c) kuna fedha ambazo zimetumiwa kwa ajili ya shughuli fulani kwa kiasi kinachozidi kiwango cha matumizi yaliyoidhinishwa na Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali kuhusu shughuli hiyo; (d) fedha zimetumiwa kulipia gharama za shughuli ambayo haikupangiwa fedha za matumizi kwa mujibu wa Sheria, kutawasilishwa kwenye Bunge makadirio ya matumizi ya nyongeza au, kadri itakavyokuwa, maelezo ya matumizi ya ziada, na baada ya Bunge kuyakubali hayo makadirio ya matumizi ya nyongeza au maelezo ya matumizi ya ziada, kutawasilishwa kwenye Bunge Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali kwa ajili ya kuidhinisha matumizi ya fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, na fedha hizo zitagharamia shughuli zinazohusika na hayo makadirio au maelezo. 209.-(1) Iwapo mwaka wa fedha wa Serikali umeanza na Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali inayohusika na mwaka huo haijaanza kutumika, Rais anaweza kuidhinisha fedha itolewe kutoka Mfuko Mkuu...
Posted on: Thu, 29 Aug 2013 09:36:52 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015