Simulizi za Kalibonge Niliacha shule ili niwe mganga - TopicsExpress



          

Simulizi za Kalibonge Niliacha shule ili niwe mganga (34) Ilipoishia jana... Alikuwa anakaa mtaa wa Forest ambako alikuwa amepanga chumba na ukumbi. Ndani mwake mulikuwa safi na kulikuwa na kila kitu kizuri kinachostahili kukaa ndani mwa mwanamke wa namna yake. “Karibu sana.” “Asante.” Tuliingia pale sebuleni na nikataka kukaa kwenye sofa akanikataza. “Haujafika unakoenda, haya ingia huku.” Akaniambia huku akiniongoza kuingia chumbani, sikubisha. Endelea... Huko chumbani hamukua na vitu vingi; kitanda, kabati la nguo, dressing table na kistuli chake na kulikuwa na meza ndogo na sofa moja. Nilipoingia nikaenda kujilaza kitandani. Hilda akarudi sebuleni na baada ya dakika chache akaingia chumbani. Akanishika mkono hadi pale sebuleni ambako alinielekeza moja kwa moja mezani. Tukaa huku tukielekeana na kuanza kula taratibu. Alikuwa amepika wali na njegere na alitayarisha sharubati ya parachichi. Tulipomaliza kula, tukarudi tena chumbani na kujitupa kitandani. Hapo Hilda akataka kujua matatizo niliyiyapa, nami nikafunguka; nikamuhadithia mwanzo mpaka mwisho na namna nilivyotaabika porini hata kule kijijini. Alisikitika sana na kunihurumia. “Dunia hii ina mambo mengi, lakini jamno la muhimu ni uzima wako. Madhari umepona, hapo mengine yanatafutwa yakapatikana ila uhai ukikutoka, ndiyo basi tena.” Akaniambia kwa kunihurumia. “Namshukuru Mwenyezimungu nimesalimika na hayo mengine kama usemayo, yatapatikana kwa uwezo wake.” Baada ya habari hizi zilizonipata, tuliongea mambo mengine kwa muda mrefu hata nikachoka. “Hilda nimechoka sana, labda mengine tutazungumza wakati mwingine.” “Wakati mwingine upi? Hapa huendi Tanga hata wiki moja imepita.” Akaniambia ambapo mara ya kwanza nilidhani ni utani, kumbe alidhamiria. “Sawa umeshinda.” Nilipomwambia hivi akainuka pale kitandani hadi kwenye kabati la nguo, akavua zile alizokuwa amezivaa na kuvaa nguo za usiku kisha akazima taa na kuja kitandani. Aliponifikia, akanikumbatia nami nikamkumbatia, tukakumbatiana. Hakika Hilda alikuwa ni namna ya mwanamke niliyemuhitaji katika maisha yangu na nilikuwa tayari kuingia katika maisha mapya na mwanamke huyu aliyenivutia kwa kila kitu; upole, ukarimu, hekima, busara na huruma. Pia alikuwa na mapenzi ya dhati na mwenye heshima. Kwa kipindi cha wiki moja niliyokuwa naye, sikuhisi tena maumivu ya kupotewa na mtaji wangu. Hilda alikuwa nami kila nilipokumbuka madhila yaangu, akanifariji na kunitia moyo hata nikawa na matumaini mapya katika maisha. Katika siku hizo nilizokuwa naye, sikuwahi hata siku moja kutoa hela yangu mfukoni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani pale. Nilikula, kunywa, kulala na zaidi alinifanyia manunuzi ya nguo hata nikaonekana kijana wa kisasa kabisa. Kwa hivi nikawa na wazo moja tu; malo ni kufunga ndoa na Hilda na nilipanga nikifika Tanga, jambo hili litakuwa la mwanzo kuwahafamisha wazee wangu halafu hayo mengine yatakuwa ya ziada. “Hilda!” “Bee!” “Nitakukumbuka sana nikifika Tanga.” “Usijali Bilal kila kitu kitakuwa sawa na ukifika fanya kama tulivyozungumza. Mimi tayari nimeongea na mama na ameahidi kuzungumza na baba.” “Sawa hakuna shida ila wewe ni mwanamke niliyekuwa namuhitaji.” “Hata wewe ni mwanaume niliyekuwa namuomba Mwenyezimungu anitunuku. Kesho utaondoka saa ngapi?” “Kwani hiyo tikiti inaonesha saa ngapi?” “Ah! Hata sikuangalia mimi nimeinunua tu na kuiweka kwenye mkoba. Hebu niangalie.” Akainuka kutoka kitandani na kwenda sehemu anapoweka mikoba yake na kuuchukua mkoba ambao alikuwa nao mchana ule kisha akaingiza mkono na kutoa karatasi ndogo hivi. “Ni saa kumi na mbili na nusu asubuhi.” Akasema huku akikirudisha kile kikaratasi mkobani halafu akarudi tena pale kitandani. Siku iliyofuata, Hilda aliamka mapema sana na kunitayarisha kwa ajili safari ya kurudi nyumbani. Baada ya matayarisho kukamilika, tulitoka huku tukishikana mikono na kuongozana hadi Msamvu ambako nilipanda garini tayari kwa safari na baada ya muda mchache basi liliondoka na Hilda akarudi kwake. ******************** Njia nzima nilikuwa na Hilda; alijaa mawazoni mwangu hata sikumbuki kama niliwahi kukumbuka madhila yaliyonikuta. Hilda alinijaa kichwani na kila sehemu ya mwili wangu, nilimpenda sana Hilda na nilikuwa tayari hata kuhama Tanga kwenda popote alipohitaji kwenda nami. Nilifika Tanga saa kumi alasiri na moja kwa moja nikaenda nyumbani kupumzika. Nilikaa nyumbani mpaka ilipotimia majira ya saa tatu usiku nikaenda kwa baba mkubwa ambako nilipofika alishangaa kwa kukaa muda mrefu bila kumtembelea. Nikajitetea kwa kumwambia matatizo yaliyonikuta, akasikitika sana na kunipa pole. Pia nilimwambia nia yangu ya kuoa naye akafurahi sana. Tuliongea sana hata ilipotimia saa tano usiku, nilirejea kwangu kupumzika huku nikipanga kesho niende Handeni kwa wazazi wangu. Palipokucha, niliamka mapema sana kana kwamba nilikuwa na safari ya mbali sana. Nikajiandaa na ilipotimia majira ya saa mbili unusu asubuhi nilikuwa kwenye gari safari ya Handeni. Nilipofika huko, mazungumzo mengi yalihusu jambo langu la kuoa, licha ya kuwahadithia juu ya mkasa wangu wa kusikitisha, lakini msisitizo mkubwa ulikuwa katika kuoa. Walinipa pole kutokana na matatizo hayo na zaidi walisema nimshukuru Mwenyezimungu kwa kuniepusha na kifo kibaya na kunitumuku uhai huku wakisema kuwa pumzi ndiyo jambo la muhimu na hayo mengine hutafutwa tu hapa ulimwenguni. Hakika nilifarijika kuwa na wazazi wangu ambao wakati wote walikuwa nami katika matatizo yote. Walikuwa bega kwa bega katika jambo langu hili huku wakifanya juhudi za kupeleka posa nyumbani kwa Hilda pale Tanga mjini ambako aliishi shangazi yake. Nilitaka jambo hili liende haraka sana kwani dhamira ya kuwa na familia yangu ilikuwa juu, pia nilikusudia kufanya hivi ili kulinda heshima ya wazazi wangu ambao wamenilea katika misingi ya maadili mema. Na kuonesha dhamiri yangu katika hili, nilimsisitizia baba juu ya kuandika barua ya posa na kuipeleka kwa shangazi yake Hilda pale Tanga mjini. Baba hakuwa na kipingamizi, hivyo tulipanga baada ya siku tatu hivi atakuja Muheza kwa baba mkubwa halafu utaratibu mwingine utafuata. Nyumbani kwa wazazi wangu, nilikaa siku moja na siku ya pili nikarejea Muheza ambako niliendelea na na shughuli zangu pale mashine. Kilikuwa ni kipindi kigumu sana. Watu walishangaa nimerudi mikono mitupu pale mashine bila mzigo kama nivyoahidi kabla ya kuondoka. Nikawasimulia kilichonikuta na wengi walisikitika ingawa wapo walioniona muongo. Waliniona muongo kwa sababu waliamini kuwa kama mtu anapata ajali katika eneo nililopata mimi ajali, yaani mlima Kitonga, basi haponi. Hivyo walishangaa mimi kupona kwenye ajali na kupona kuliwa na wanyama pori. Hawa sikutaka kutumia nguvu nyingi kubishana nao, zaidi niliwaeleza wale walioniamini ambao walinipa pole huku wakisema kuwa ilikuwa ni mitihani ya dunia. Nikaungana nao tena katika biashara, ingawa sikuwa na mtaji mkubwa zaidi ya ule mzigo mdogo niliouacha kabla ya kusafiri kwenda Mbeya. Siyo kama sikuwa na akiba benki, la! Akiba ilikuwepo lakini haikuwa kubwa kwani fedha nyingi niliwekeza katika mpunga nilioupoteza kule Kitonga, hivyo hapa nilikuwa nauza mzigo huu ambao haukuwa mkubwa, halafu kulikuwa na watu ambao nilikuwa nawadai na nilitegemea kulipwa wakati wowote. Mawasiliano yangu na Hilda yalizidi kila leo. Kila tulipoongea basi msisitizo ulikuwa katika kujenga familia bora, hivyo kila mtu alimtaka mwenzie kujiandaa katika hilo. Kama vile tulivyoongea na baba, ingawa alichelewa kuja kwa baba mkubwa, lakini alifika na tukafanya kile tulichopanga kukifanya. Barua iliandikwa na safari ya Tanga mjini ikafanywa nami na baba mkubwa. Kwangu ilikuwa ni hatua muhimu sana katika maisha. Tulipofika Tanga mjini, hatukupata shida sana kupajua nyumbani kwa shangazi yake Hilda kwani alinielekeza vizuri na hata baba mkubwa alikuwa mzoefu sana. Nilipomtajia tu Ngamiani, haikuwa kazi kubwa. Tulikaribishwa vizuri sana hata nikashangaa namna ya mapokezi tuliyopewa. Nikajiuliza pengine Hilda alishatoa taarifa kwa shangazi yake kuwa kuna watu fulani watafika. ********** Mapenzi ya Bilal na Hilda yamechipua na sasa yamestawi vizuri. Bilal anawashauri wazazi wake juu y akuoa na wanamruhusu. Sasa wako Tanga mjini kupeleka posa kwa shangazi yake Hilda. Je, ndoa hiyo itafanyika? Unafikiri nini? Andika ubashiri wako hapo chini na itaendelea Jumatatu!. Ijumaa njema__
Posted on: Fri, 28 Jun 2013 03:21:51 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015