Tafakuri Jadidi Tunakimbiwa, Kikwete aachane na mradi wa bandari - TopicsExpress



          

Tafakuri Jadidi Tunakimbiwa, Kikwete aachane na mradi wa bandari Bagamoyo! Johnson Mbwambo Toleo la 318 2 Oct 2013 Ufukweni Bagamoyo itakapojengwa bandari Itakuwa ‘white elephant’ kama TAZARA HAKUNA shaka yoyote kwamba Uganda na Rwanda zimepania kujenga reli mpya itakayoungana na ile ya Kenya hadi bandari ya Mombasa itakayoziunganisha nchi hizo tatu – mradi ambao wakiukamilisha utakuwa ni pigo kubwa kwa bandari yetu ya Dar es Salaam hasa baada ya upanuzi wa hivi karibuni wa bandari ya Mombasa. Naweza kuthubutu kusema ya kwamba anayeupigia chapuo la nguvu mradi huo mkubwa ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye anaiona reli hiyo ya pamoja itaharakisha nchi hizo tatu kufikia shirikisho la kisiasa. Museveni ndiye anayelitamani zaidi shirikisho hilo kuliko viongozi wenzake wote katika Afrika Mashariki. Miaka miwili iliyopita alifanya ziara ya ghafla mjini Dar es salaam ambako alikutana na Rais Kikwete, na wawili hao, baada ya mkutano wao, wakatangaza mpango wa ujenzi wa reli mpya kutoka bandari yetu ya Tanga hadi Uganda. Waliachana kwa ahadi kwamba kila mmoja achacharike kutafuta wafadhili wa mradi huo. Sina hakika nini kilitokea hadi mradi huo ukaota ‘mbawa’, lakini nina hakika kwamba ni Museveni huyo huyo ndiye ‘aliyeuza’ kwa Rais Uhuru Kenyatta na Paul Kagame wazo la kujenga reli mpya itakayoziunganisha nchi hizo hadi bandari ya Mombasa. Hisia zangu ni kwamba Rais Museveni aliona ya kuwa Watanzania hatulichangamkii ipasavyo wazo lake la kujenga reli kutoka Tanga hadi Uganda kama ambavyo hatuchangamkii (atakavyo) wazo la kufikia haraka shirikisho la kisiasa, na ndiyo maana akahamishia wazo hilo kwa Kenya na Rwanda, na sasa reli hiyo itajengwa. Baada ya kikao cha marais hao cha Agosti kilichofanyika Mombasa, vimeshafanyika angalau vikao vingine viwili vya mawaziri husika kujadili mradi huo. Kwa kasi ya maandalizi wanayokwenda nayo, si miaka mingi ijayo twaweza kushuhudia reli hiyo ikikamilishwa. Wiki iliyopita Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Silas Rwekabamba, alinukuliwa na vyombo vya habari kwamba wameshaanza kufanya upembuzi yakinifu wa mradi huo. Ndugu zangu, nilieleza mwanzoni kwamba endapo, hatimaye, reli hiyo itakamilishwa kujengwa, itakuwa ni pigo kubwa kimapato kwa bandari yetu ya Dar es Salaam ambayo chini ya uongozi mpya wa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (THA), Mhandisi Madeni Juma Kipande, imekuwa ikijitahidi kuchuana na bandari ya Mombasa. Kwa mfano, TPA wamejitahidi, katika muda mfupi, kupunguza muda wa meli kukaa bandarini kupakua mizigo kutoka siku 21 hadi siku saba. Si hivyo tu; kwani bandari ya Dar es Salaam sasa imefikia kiwango cha kupakua magari 200 kwa saa ambacho ndicho wastani kimataifa. Ni matumaini yangu kwamba kwa kasi hiyo ya Waziri Mwakyembe na Mhandisi Kipande, bandari ya Dar es Salaam itaingia, hivi karibuni, katika orodha ya bandari 120 bora duniani au hata katika ‘tano bora’ za Afrika ambapo kwa sasa zimo bandari za Durban (Afrika Kusini), Mombasa (Kenya), Port Said na Alexandria za Misri na Tanger Med ya Morocco. Hata hivyo, inaweza kukatisha tamaa kwamba wakati ufanisi katika bandari yetu hiyo ya Dar es Salaam umeimarika maradufu katika kipindi kifupi tu, wenzetu Uganda, Rwanda na Kenya wamefikia makubaliano ya kujenga reli mpya itakayoziunganisha nchi hizo hadi bandari ya Mombasa. Ni dhahiri, kama nilivyoeleza mwanzo, kwamba reli hiyo mpya itakuwa pigo kubwa kiuchumi kwa bandari yetu ya Dar es Salaam kwa sababu tutapoteza wateja watatu wakubwa wa miaka mingi; yaani Rwanda, Uganda na Sudan Kusini. Kwa hakika, hata uteja wa Burundi nao utakuwa shakani. Nikumbushe tu hapa kwamba kwa miaka mingi nguvu ya kiuchumi ya bandari yetu ya Dar es salam ilitokana na kuhudumia nchi sita zisizo na bandari; yaani Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na DR Congo. Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba, hali kwa bandari yetu hiyo itakuwa mbaya kimapato kama Uganda na Rwanda zitakamilisha mradi huo wa ujenzi wa reli mpya inayounganisha nchi hizo na ile ya Kenya hadi bandari ya Mombasa. Hebu jiulize; kama bandari ya Mombasa inatupiku kimapato katika kipindi ambacho Dar es Salaam inahudumia mizigo ya Uganda, Burundi, Rwanda, DR Congo na hata Sudan Kusini, hali itakuaje siku reli hiyo mpya itakapokamilishwa kujengwa na nchi hizo, na hasa upanuzi wa bandari ya Mombasa utakapokamilika kabisa? Ni dhahiri kwamba upanuzi wa bandari ya Mombasa utakapokamilika kabisa na reli hiyo mpya na ya kisasa nayo ikakamilika kujengwa, Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na pengine Burundi zitasitisha kupitisha bidhaa zao kwenye bandari ya Dar es Salaam. Je, bandari yetu hiyo inaweza isitetereke kimapato hata kama itapoteza soko hilo kubwa la kuhudumia bidhaa za nchi hizo na hasa ikizingatiwa kwamba usafirishaji wetu bidhaa nje (export) kupitia bandari hiyo ni mdogo mno baada ya kuua kilimo na sekta ya viwanda? Hilo ni swali ambalo ukiwatupia watawala wetu watakupa majibu ya kisiasa zaidi badala ya kiuchumi. Tayari wameshaanza kutupa matumaini ya uongo kwamba eti hatutaathirika sana kiuchumi kama tutatupwa nje ya shirikisho jipya la kisiasa la Afrika Mashariki (na dalili tunaziona). Hoja yao ni kwamba hilo likitokea, tutaelekeza nguvu zetu kwenye ushirikiano na nchi za SADC! Mbali ya kauli hiyo tata, watawala wanatupa matumaini mengine dhaifu kwamba eti hata kama reli hiyo mpya inayounganisha Rwanda na Uganda na bandari ya Mombasa itajengwa, bado bandari yetu ya Dar es Salaam itaendelea kuimarika kimapato kwa kusafirisha mizigo ya nchi za DR Congo na Zambia. Lakini wengi wetu tunajua kuwa huo siyo ukweli wote; maana hata Zambia nayo imeshaanza mipango ya kuitosa bandari yetu ya Dar es salaam kwa kuanza kuwekeza vya kutosha katika miundombinu ya reli kuelekea Namibia na Afrika Kusini, na pia inakarabati barabara inayoelekea Beira, Msumbiji. Lengo likiwa ni kutumia njia hizo kusafirisha bidhaa zake, na hivyo kuachana na bandari yetu ya Dar – hatua ambayo pia itaidhoofisha TAZARA. Ni kwa kuzingatia yote hayo sioni mantiki ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kung’ang’ania kujenga bandari mpya ya Bagamoyo kwa mkopo kutoka China; hata kama tayari wameshatia saini mkataba (tata na siri) kwa ajili ya ujenzi huo. Ni busara akaachana na mpango huo kwa sasa. Kama upanuzi wa bandari ya Mombasa na ujenzi wa reli mpya itakayounganisha Rwanda, Uganda na Kenya tayari imeiweka bandari yetu ya Dar katika hatari kubwa na ya kweli ya kupoteza soko la nchi hizo nap engine Burundi na Sudan Kusini, kuna lojiki gani kwa sasa kuendelea na mpango wa kujenga bandari mpya ya Bagamoyo? Kama tayari Zambia nayo inaboresha miundombinu yake ili ipitishie bidhaa zake katika bandari za Beira (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini) na Walvis Bay (Namibia), kuna lojiki gani kwa Tanzania kujenga bandari mpya ya Bagamoyo karibu mno na bandari ya Dar ambayo inaboreshwa iwe ya kisasa zaidi? Bandari hiyo mpya ya Bagamoyo itahudumia mizigo ya nchi gani wakati tayari tunakimbiwa karibu na nchi zote za Afrika Mashariki, Kati na Kusini? Nauliza hivyo; maana lojiki ya mwanzo ya kujenga bandari mpya Bagamoyo ilikuwa ni kuipunguzia shinikizo bandari ya Dar es Salaam, lakini sasa shinikizo hilo halitakuwepo; kwa sababu wenzetu wameshachagua bandari nyingine za kupitishia mizigo yao. Nionavyo, serikali yetu inapaswa kuyasoma maandiko ukutani, na kuachana kwa sasa na mpango huo wa kujenga bandari mpya ya Bagamoyo ambayo itaishia tu kuwa ‘white elephant’ . Badala ya kujenga bandari mpya ya Bagamoyo, ni heri Serikali ya Kikwete ikatumia hizo dola za Kimarekani bilioni 10 za ujenzi huo, kuboresha bandari za Tanga na Mtwara kwa kiwango kikubwa zaidi, na pia kutumia sehemu nyingine ya fedha hizo kuboresha kwa kiwango kikubwa zaidi Reli ya Kati na ya TAZARA. Wanadai kuwa bandari hiyo ya Bagamoyo itakayojengwa na Wachina kwa mkopo itakuwa ndiyo bandari kubwa Afrika kuliko zote Kusini mwa Jangwa la Sahara, lakini nionavyo mimi, ukubwa wa eneo na aina ya vifaa vya kisasa vitakavyowekwa katika bandari hiyo, si hoja kuu. Hoja kuu ni wingi wa mizigo itakayohudumiwa na bandari hiyo au wingi wa nchi zitakazoitumia kupitisha mizigo yao. Unaweza ukawa na li-bandari likubwa lakini kwa wiki likapokea meli mbili tu! Kwa hiyo, saizi ni hoja lakini si hoja kuu. Hoja kuu ni wingi wa mizigo – wingi wa meli zitakazotia nanga bandarini hapo! Sasa, kama tayari tunaendelea kuboresha bandari ya Dar es Salaam, na huko tuendako tutakimbiwa na wateja wetu hao wa siku nyingi - Uganda, Rwanda, Zambia nk, hiyo bandari ya Bagamoyo itapata wapi mizigo mingi kuhalalisha hadhi yake hiyo kubwa ya kimataifa? Kwa maneno mengine, hofu yangu kubwa ni kwamba bandari hiyo itaishia tu kuwa ‘white elephant’ nyingine nchini kama ilivyo TAZARA hivi sasa. Tazara ni reli ndefu inayounganisha mataifa mawili na ilikuwa iwe mfano Afrika nzima, lakini kwa miaka mingi imebakia kuwa ‘white elephant’. Je, si kweli kwamba kung’ang’ania kujenga bandari hiyo mpya ya Bagamoyo ni sawa na kuongeza idadi ya miradi ambayo ni ‘white elephants’ katika nchi yetu? Ni kwa kuzingatia yote hayo, binafsi, naamini kuwa ni busara kwa serikali yetu kuingia katika mazungumzo mapya na Serikali ya China ili kukubaliana kuachana na mradi huo wa Bagamoyo, na badala yake mapesa ya mkopo huo yaelekezwe kwenye miradi mingine ya kuboresha miundombinu yetu mingine niliyoitaja; hususan uboreshaji zaidi wa bandari ya Dar na Reli ya Kati. Na kwa kasi inayoonyeshwa na majirani zetu hivi sasa, hilo la serikali kuisuka upya Reli ya Kati na kuzidi kuboresha huduma katika bandari ya Dar es Salaam, lazima lifanyike kwa haraka; vinginevyo tutakimbiwa pia na DR Congo ambayo haina sababu yoyote (hata ya kisiasa) kupitishia bidhaa zake Mombasa. Nihitimishe safu yangu kwa kusisitiza tena kwamba bandari yetu ya Dar es Salaam itapitia kipindi kigumu mno kimapato kutokana na ushindani itakaopata kutoka bandari za Mombasa na Malindi (Kenya), Beira (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini) na hata Walvis Bay ya Namibia. Ni dhahiri kwamba watawala wasipozinduka na kuongeza kasi ya kuiboresha zaidi bandari ya Dar, miaka si mingi ijayo inaweza ikapoteza asilimia 60 ya mapato yake, na hivyo kujisogeza katika hatari ya kupatwa na masahibu yaliyoikumba TAZARA ambayo baada ya kupigwa vita mno na matajiri nchini wenye malori makubwa yanayosafirisha mafuta na bidhaa nyingine kwenda Zambia na DR Congo, imebakia kuwa ‘white elephant’! Tafakari.
Posted on: Fri, 04 Oct 2013 06:31:21 +0000

Recently Viewed Topics




© 2015