Thailand tunaambiwa, China, Marekani siri Na Edson Victoria - TopicsExpress



          

Thailand tunaambiwa, China, Marekani siri Na Edson Victoria KamukaraKWA bahati mbaya sana Watanzania tumekuwa watu wa kuridhika na hali ya mambo ilivyo. Hatua hii ni mbaya na imetuharibu kwa kudhani kila kitu kiko hivyo na hakiwezi kubadilika. Watanzania wakati wote ni watu wa furaha, tunacheza ngoma kwa madoido makubwa hata kama tunakuwa tumekasirika, tuna furaha msibani, harusini hata tunapoibiwa. Kwa ujinga wetu tumefikia hatua ya kutothamini uhai wetu, hivyo kuridhika na mabavu ya watawala ndiyo maana hata kwenye maandamano ya amani, watu wanauawa halafu inakuwa kawaida tu. Haishangazi kusikia wakisema kuwa: “Watu wanne tu wamekufa kwenye maandamano ya amani.” Lakini hakuna anayejali kwa vile tumeridhika kwamba mambo ndivyo yalivyo. Hili ni tatizo la kutofikiri badala yake tunapayuka tu pasipo kutuliza akili yetu kwenye chumba cha fikra na kutafakari mambo kwa busara kuhoji ni kwa nini iwe hivyo? Wiki hii tumetembelewa na Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra. Kama kawaida yetu tulifurahi na kumchezea ngoma, tukaburudika kila eneo alilofanya zira na kisha tukasaini naye mikataba minne. Tofauti na wageni wengine waliotutembelea halafu tukawachezea ngoma lakini hatukuambiwa tumesainiana nao mikataba gani, viongozi wetu hapa wamekuwa wepesi wa kueleza tulichokubaliana na Thailand. Nadhani hii ni kutokana na mikataba hiyo kutokuwa na ulaji ndani yake ndiyo maana viongozi wetu wakawa wepesi kwa kutoifanya ya giza kama ile tuliyosaini na China na Marekani inayogusa gesi na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo. Kwamba tumekubaliana na Thailand kuhamasisha na kulinda uwekezaji, kubadilishana wafungwa na kutekeleza sheria ya vifungo, ushirikiano wa kiufundi pamoja na ushirikiano baina ya Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi ya Gem and Jouely ya nchi hiyo. Taifa la watu wenye furaha wakati wote, wala hatukuhoji ni kwanini iwe mikataba ya Thailand pekee ndiyo inawekwa wazi wala si ile ya China na Marekani. Jibu nimeishalitoa hapo juu kuwa ni kutokana na kutokuwa na masilahi ya ulaji ndani yake. Ukitazama kwa undani utaona ni njia ya kulenga kuwanusuru watu fulani. Swali la kujuliza hapa ni kwamba tumesaini kubadilishana wafungwa. Ni Watanzania wangapi wamefungwa Thailand na walifanya makosa gani? Je, ni watoto wa kina nani? Walikamatwa na pembe za ndovu au kitu kingine? Sheria za kule zikoje hadi tuharakishe wafungwa wetu warudishwe? Hivi Thailand ina wafungwa wangapi Tanzania? Walifanya nini na kwa nini warudishwe kufungwa huko? Majibu ya maswali hayo utatafuta mwenyewe, leo nataka tujitafakarishe zaidi. Nasisitiza tena kuwa haifai kuwa watu wa kufurahi na kucheza wakati nchi yetu ikiuzwa. Lazima tujifunze kufikiri kwa kina na kuhoji. Kwa nini tuwe taifa la kutembelewa na kusaidiwa na kila mtu? Ni kweli sisi tunahitaji misaada au kufanya biashara huru ya haki ili kujikwamua? Nani anatusaidia na lengo lake baadaye ni nini? Kwa nini watawala wetu wanafanya siri kwenye mikataba wanayoisaini kwa niaba yetu? Miezi michache iliyopita alikuwapo Rais wa China hapa nchini, Xi Jinping. Tulishangilia ujio wake tukacheza ngoma na kujisifu kuwa ni ziara ya kihistoria nchini, alikuja kufanya nini? Majibu hakuna. Ukijidai kuhoji ziara hiyo, wenye majibu yao yaliyotayarishwa watasema wamesaini naye mikataba 17 ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya serikali yetu na nchi yake. Uliza kwa Rais Jakaya Kikwete, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, jibu lake utaambiwa mikataba hiyo ni siri, kwamba haiwezi kuwekwa wazi kwa kila mtu. Hapo lazima utagundua kuwa Tanzania si ya Watanzania bali ina wenyewe, ambao wanachagua bandari mpya ijengwe Bagamoyo na si kupanua na kuzifufua zile za Mtwara, Tanga, Dar es Salaam na nyingine ili zitoe huduma bora. Watakwambia kuwa wameamua kwa matashi yao bila idhini ya wananchi wa Mtwara na Lindi, gesi itoke kwao ipitie Bagamoyo na kuja hadi Dar es Salaam ili wawekezaji wasisumbuke kwenda maporini kuifuata. Ukibahatika sana baada ya kuhoji, utapigwa changa la macho kuwa baadhi ya mikataba hiyo 17 ilihusiana na uboreshaji wa sekta ya viwanda, kilimo hasa cha tumbaku ikiwemo kuwatafutia soko wakulima kutoka mikoa ya Tabora na Ruvuma ili waweze kuuza zao hilo katika soko la China. Niliwahi kuandika huko nyuma nikieleza kuwa marais wa mataifa makubwa kiuchumi tunaowashangilia na kudeki barabara ili wapitishe magari yao, kamwe hawaji huku kutalii na kushangaa kama sisi tunavyofanya tukienda kwao. Wamarekani wana usemi kuwa: ‘Hakuna chakula cha bure Marekani.’ Halafu wanasisitiza kuwa hawana rafiki wala adui wa kudumu. Hii ina maanisha kuwa Mmarekani akitaka kitu kwako atakihangaikia kwa gharama yoyote na akishafanikiwa wewe huna maana kwake. Tulicheza ngoma na kufurahi alipokuja Rais Barack Obama wa Marekani. Tulizuzuka na kusafisha kila mahala jijini Dar es Salaam hadi kupulizia dawa za mbu mitaani, kwa fikra duni kuwa amekuja kutazama hayo. Alipotua akiahidi vijisenti vya kusambaza umeme, sisi hao tukaonesha meno yote kwa kuamini tunapendwa zaidi ya nchi ya baba yake Kenya. Wala hatufikiri kwa nini alikuja kwetu akaacha kufika kwao. Tumesaini mikataba ya siri na Marekani kama tulivyofanya kwa China, rasilimali zinazofichwa ni za Watanzania lakini hawapaswi kujua zikiuzwa watanufaikaje. Kwa nini tuambiwe mikataba ya Thailand pekee na ile ya wakubwa inakuwa siri? Tafakari!
Posted on: Mon, 05 Aug 2013 08:50:19 +0000

Recently Viewed Topics




© 2015