UCHAWI WA KURITHI 28: Sura ya Nyuta ikabadilika na akaanza - TopicsExpress



          

UCHAWI WA KURITHI 28: Sura ya Nyuta ikabadilika na akaanza kukoroma. Pendo alikuwa pembeni yake akimuangalia tu na kikubwa ni kuwa alikuwa akimngoja atapike kile alicholishwa utotoni. Ila alimuona Nyuta akikaa vizuri huku akiweka mikono yake shingoni na kuanza kutapatapa kama mtu anayetaka kutapika. Ila hakutapika, kitendo hicho kilimshangaza Pendo kwani alingoja na kungoja ila Nyuta hakutapika. Ndipo Pendo akaamua kurudi jikoni na kwenda kuzungumza na yule mmama. Pendo akaamua kumweleza ukweli halisi na kwanini ameamua kufanya ayafanyayo. PENDO: Nia yangu atapike kile alicholishwa utotoni. MMAMA: Ila dawa si umeshampa? PENDO: Ndio, nilimpa pamoja na ule uji ila nashangaa hadi sasa hatapiki. Kwani unaweza kutambua ni nini tatizo? MMAMA: Tatizo ni kuwa, kitu alicholishwa Nyuta ni cha kurithi. Sasa inatakiwa apatikane mtu wa kukirithi. PENDO: Itakuwaje sasa? MMAMA: Unatakiwa wewe ukubali kukirithi. PENDO: kwani hakina madhara? MMAMA: Hakina madhara ila humfanya mtu ateseke sana pale muda wake wa kufa unapofika. PENDO: Bibi hapana mimi sitaki kurithi hicho kitu. MMAMA: Asante kwa kunipa heshima ya ubibi Pendo. PENDO: Usijari wewe ni kama bibi yangu, nakuomba tutafute njia nyingine ila sio ya mimi kurithi. Sitaki matatizo zaidi maishani. MMAMA: Njia nyingine ni kuwa tumbebe Nyuta hadi mtoni ili akatapikie huko kwani kile kitu huwa kinataka kikitoka kiweze kutembea na kwenda kwingine. PENDO: Tufanye hivyo basi ili tuwahi. Basi Pendo na yule mmama wakaamua kufanya mpango wa kumbeba Nyuta ili kumpeleka huko mtoni. Wakaingia chumbani kwa Nyuta, na Nyuta alipomuona yule mmama alichukia sana alitamani kusema kitu ila alishindwa sababu ya kile kitu kilichomkaba kooni. Yule mmama ndiye aliyeamua kumbeba Nyuta mgongoni, na kumwambia Pendo aibebe ile fimbo ili waende nayo pamoja. Pendo alipoibeba ile fimbo ikageuka kuwa nyoka yani ikafanya kama ilivyofanya wakati wapo kule kwa bibi wa Nyuta, kwakweli kwa mtu asiye na ujasiri hawezi kuibeba ile fimbo kama Pendo afanyavyo. Pendo alikuwa ni mtu jasiri sana kwani aliweza kufanya mambo mengi kwa ujasiri alionao. Safari ya kuelekea mtoni ikaanza na Pendo akijihesabia ushindi moyoni kwani hapo atakuwa amekamilisha lile lililompeleka pale nyumbani kwa Nyuta. Walipofika mtoni, wakaingia katikati ya maji na kumshusha Nyuta, yule mmama akamwambia Pendo kuwa amchape Nyuta na ile fimbo mgongoni ili awe kama anamshtua. Na kweli baada ya kufanya hivyo Nyuta alishtuka na kuanza kutapika. Akatapika kitu kisicho na rangi yani kipo kama maji ila ni cha mviringo na kinalepweta. Kikaangukia kwenye maji na kuondoka kikifata uelekeo wa maji yale. Pendo na yule mmama wakamchukua Nyuta na kutoka ndani ya yale maji. PENDO: Kwahiyo kile kitu ndio kimeondoka? Yule mmama akamzuia Pendo kama ishara kuwa hawatakiwi kuongea chochote mahali hapo. Pendo akawa anamshangaa kwani hakujua masharti hayo kabla. Tangu Nyuta atapike kile kitu akawa amezimia kwa muda na hakuona chochote kilichoendelea mahali pale. Wakati wanataka kuondoka, mara kikatokea kitu na kuanguka mbele yao. Ilikuwa ni sanamu ila yenye umbo la mnyama. Sanamu ile ikaanza kuwafata, Pendo na yule mmama wakawa wanaogopa. Pendo akataka tena kusema kitu ila yule mmama akamzuia Pendo kusema kwa kidole bali alimuonyesha ishara kuwa anyanyue ile fimbo na kuielekeza kwa sanamu yule, naye Pendo akafanya kama alivyoamriwa na hapo hapo ile sanamu ikatoweka. Yule mama hakutaka wajadili jambo lolote mahali hapo bali waanze safari ya kurudi na wakafanya kama walivyokwenda yule mmama akambeba Nyuta na Pendo nae akaishika ile fimbo vilevile hadi wakafika tena nyumbani kwa Nyuta. Wakiwa nyumbani kwa Nyuta wakampeleka Nyuta chumbani kwake na kumlaza. Pendo akaamua kuhoji kwanini alikuwa anazuiliwa kuongea. PENDO: Mbona ulikuwa unanikataza kuzungumza? MMAMA: Hairuhusiwi kabisa kuongea, unaona ukataka kuzua tatizo lingine! PENDO: Kwahiyo lile sanamu lingetudhuru? MMAMA: Ndio lingetudhuru. PENDO: Asante bibi kwa kunisaidia mambo haya. Pendo akaenda kumuonyesha yule mmama wale watoto mapacha walioonekana kulegea sana. Ikabidi wawape ule uji uliobaki ili kuwatia nguvu. MMAMA: Usijari kuhusu hawa watoto, kumtoa mtoto uchawi si kazi ngumu kama ilivyo kwa mtu mzima. PENDO: Tena mtu mzima mwenye moyo kama wa Nyuta. MMAMA: Ni kweli, si rahisi kwa mtu kama Nyuta kuacha uchawi. Pendo akaendelea kuwaza namna ya kumteketeza Nyuta kwani kila kitu kilikamilika kilichobaki ilikuwa mauti ya Nyuta pekee. Pendo na yule mmama wakiwa kwenye chumba cha Nyuta. NYUTA: Pendo umeamua kunimaliza mimi ila tambua kwamba kuna watu kama mimi wengi sana. PENDO: Ila wewe ni zaidi kwani umetutesa sana. Pendo aliongea kwa ujasiri mkubwa sasa. NYUTA: Na wewe Maria hata sijui na nani aliyekutoa. MMAMA: Umenichukia bila sababu ya msingi Nyuta. NYUTA: Yupo Maria mwenzako kwenye jeneza, ni miaka na miaka sasa. Pendo akashtuka sana na kugundua kuwa mtu aliyemuona kwenye jeneza kuwa nae ni Maria. PENDO: Bibi kwanini unawachukia? NYUTA: Maria alipendwa na Yusuphu sitaacha kumchukia Maria kwani alifanya Yusuphu asinipende mimi kabisa. PENDO: Hata kama bibi, ila Maria aliyekuchukiza ni mmoja iweje sasa uwachukie wote wakina Maria? Nakumbuka hata rafiki yangu aliyeitwa Maria ni wewe uliyemuua bibi, kwanini ufanye hivyo? NYUTA: Maria alifanya nisipendwe, na kama angekuwa anaitwa Pendo basi ningewachukia Pendo wote duniani. Ni hapo ambapo Pendo akagundua kuwa bibi yake anakisasi cha kudumu moyoni mwake. Ni hapo akauliza kwa yule mmama. PENDO: Na mbona bado inakuwa ngumu kummaliza Nyuta. MMAMA: Kumbuka Nyuta ni mchawi wa muda mrefu tena uchawi wake ni wa kurithi inatakiwa kuwa makini sana katika kumuangamiza. PENDO: Tutafanyaje sasa? MMAMA: Nadhani hilo jeneza lenye mtu ni kiashirio tosha cha mauti ya Nyuta. Yule mmama na Pendo wakapanga mkakati wa kumuokoa Maria aliyewekwa kwenye jeneza kwani uzima wa Maria huyo ndio itakuwa mauti ya Nyuta. Wakajiandaa kutoka ili kwenda kutimiza mipango yao. Wakati wanatoka nje wakakutana na bonge la joka lenye asili ya chatu yani ni lile joka lililomviringa Pendo akiwa kwa bibi wa Nyuta. Sasa Pendo alihisi mpambano mkali kwani lile joka lilikuwa ni kiashirio kikubwa cha yule bibi. Itaendelea kesho...!!! Kama umeipenda like. Kumradhi kwa kutokuwa na muda muafaka wa kupost.
Posted on: Sun, 28 Jul 2013 21:33:26 +0000

Recently Viewed Topics




© 2015