ULINIUA GLORIA 21 Peter akawa mpole, akatulia benchini pale - TopicsExpress



          

ULINIUA GLORIA 21 Peter akawa mpole, akatulia benchini pale alipokuwa. Vijana wale wakamsogelea na kisha kukaa karibu yake huku wakiwa wamemuweka mtu kati. Peter hakujua wale vijana walikuwa ni wakina nani na walitoka mahali gani, kila alipokuwa akiwaangalia alikuwa akishikwa na wasiwasi, moyo wake ulimwambia kwamba vijana wale hawakuwa vijana wa amani maishani mwake. “Unajua kwamba unamiliki milioni kumi?” Kijana mmoja alimwambia peter. “Kivipi?” Peter aliuliza huku akitetemeka. “Yeyote atakayefanikish a kukamatwa kwako, milioni kumi ndio zawadi yake” Kijana huyo alimwambia Peter. “Naombeni mnisamehe. Gloria ndiye ambaye amesababisha haya yote, naombeni mnisamehe niondoke zangu kuelekea tanzania” Peter aliwaambia vijana wale. “Hatuna lengo la kukukamata” kijana mmoja alimwambia Peter. “Lengo letu kubwa ni kuondoka nawe” Kijana mwingine aliingilia. “Kuondoka na mie? Kwenda wapi?” Peter aliuliza huku akionekana kushtuka. “Usijali. Sehemu salama” “Naombeni mnisamehe” “Usijali. Huyo Gloria yupo wapi?” “Sijui. Sijui yupo wapi” “Ok! Hilo si tatizo. Ungependa kumfanya nini pindi utakapokutana nae?” Kijana mmoja alimuuliza peter. “Kumuua. Nisipomuua ataniua yeye” “Hilo si tatizo. Tutakusaidia endapo utatusaiidia kitu kimoja” Kijana mmoja alimwambia Peter. “Kuwasaidia nini?” Peter aliuliza swali ambalo liliwafanya vijana wale kuangaliana, wakatoa tabasamu pana ambayo yalimfanya Peter kuchanganyikiwa . **** Mzee Mbwana alionekana kuchanganyikiwa mara baada ya kupokea simu kutoka kwa vijana wake ambao walimpa taarifa kwamba hawakufanikiwa kumpata Peter ambaye alitoroka ndani ya nyumba ile ya wageni. Uso wake ukatawaliwa na ndita, kile ambacho alikuwa akikisikia mahali hapo kikaonekana kumharibia siku. Akaanza kuuma meno yake kwa hasira. “Mmeleta uzembe” Mzee Mbwana alisema huku hasira kali zikiendelea kumakata. “Hapana bosi. Alitoroka hata kabla hatujaingia ndani ya nyumba ile ya wageni” Sauti ya kijana mmoja ilisikika. “Sasa alijuaje kama nyie mlikuwa ndani ya nyumba hiyo?” “Bosi si ulituambia tuue kila tutakayemkuta! Tulianza kwa kuwaua polisi” Kijana yule alisikika akisema. “Ila pamoja na hayo, mmeleta uzembe mkubwa sana. Kitu ninachokitaka ni kuona huyo mjinga anapatikana haraka iwezekanavyo” Mzee Mbwana alisema huku akiwa na hasira, hakutaka kuendelea kuongea zaidi, alichokifanya ni kukata simu. Moyo wake ulikuwa kwenye hasira kali kupita kawaida, kitendo cha vijana wake kumkosa Peter kilionekana kumuumiza kupita kawaida, kitu ambacho alikuwa akikitaka sana kwa wakati huo ni kuona Peter anauawa hata kabla hajatiwa mikononi mwa polisi ambao nao walikuwa mstari wa mbele kumtafuta. Mara baada ya simu kukatwa, mzee Mbwana akatulia katika kochi lake, macho yake yalikuwa yakiangalia darini huku akiendelea kuwa na hasira sana. Kila kitu ambacho alikuwa akikitaka kitokee kwa wakati huo aliona kikiwa kimekwenda ndivyo sivyo. Peter, alikuwa mtu pekee ambaye alimhitaji sana lakini kijana huyo alionekana kuwa na uwezo mkubwa sana wa kuweza kuwakimbia polisi na watu wengine. “Nitampata tu” Mzee Mbwana alisema na kisha kuinuka mahali hapo. Kitu cha kwanza alichokifanya ni kuelekea chumbani kwake ambapo huko akachukua simu yake na kisha kumpigia Bwana Stewart na kisha kuanza kuongea nae. Maneno ya Bwana Stewart ndio ambayo yalikuwa yakimtia hasira zaidi za kutaka kumpata Peter popote pale alipokuwa kwa wakati huo. “Vijana wako wazembe sana. Hivi hawajui kama kadri wanavyozidi kumkosa huyu mpumbavu na ndivyo ambavyo nae atapata nguvu ya kukutafuta na kukuua?” Bwana Stewart alimuuliza mzee Mbwana ambaye akaonekana kuuona umuhimu wa kumpata Peter haraka zaidi. “Yaani hapo ndio ninaposhangaa kabisa. Mtu yupo ndani ya nyumba ya wageni, sijui wamemkosa vipi” Mzee Mbwana alisema huku akionekana kuwa na hasira sana. “Kwa hiyo umeamuaje? Kumtafuta na kumuua au kukutafuta wewe na kukuua?” Bwana Stewart alimuuliza mzee Mbwana. “Kumtafuta na kumuua” “Kama ni hivyo yakupasa kumtafuta kwa haraka sana. Nimepata tetesi kwamba Peter yupo katika kundi la waasi la ZSAG (Zambia Sldiers Against Government). Na walikuwa wamemtuma kwa ajili ya kumuua mtoto wako na kisha baadae kukua wewe mwenyewe” Bwana Stewart alimwambia mzee Mbwana. “Unasemaje?” “Nimekumegea siri. Ni lazima uchunguze na ujue kabisa kwamba unazidi kumkosa huyu kijana, kuna siku atakuja kukuua wewe” Bwana Stewart alimwambia mzee Mbwana maneno ambayo yalionekana kumchanganya kupita kawaida. “Nitamtafuta” “Lini sasa?” “Vijana wangu ndio wanaoniangusha kwa sasa. Ila nitamtafuta tu” Mzee Mbwana alimwambia Bwana Stewart. “Sawa. Ila kumbuka, unavyochelewa nawe unakarinbia kuuawa” Bwana Stewart alimwambia mzee Mbwana. “Nitawaharakish a vijana wamuwahi mapema” “Sawa” Maneno ya Bwana Stewart yakaonekana kuingia ndani ya kichwa chake, yakaanza kumuogopesha na kumuona Peter ni mtu mbaya ambaye kama asingefanya jambo fulani basi angeweza kuuawa yeye. Alilifahamu kundi la kijeshi la waasi la ZSGA ambalo kila siku lilikuwa na kiu ya kutaka kuuchukua uongozi wa nchi ya Zambia pamoja na kuua matajiri waliokuwa ndani ya nchi hiyo, aliposikia kwamba Peter alikuwa ametumiwa na kundi la waasi la ZSGA akaonekana kutetemeka sana. Alijua fika kwamba watanzania wengi walikuwa ni watu wa kuongea sana, watu ambao walikuwa wakikubalika katika nchi nyingi za Afrika, watu ambao hawakutakiwa kupewa nafasi hata mara moja katika suala zima la kuongea. Aliwaona watanzania kuwa watu wajanja wajanja ambao walikuwa na ujanja wa kufanya mambo mengi katika maisha yao, alijua fika kwamba kama Peter alikuwa akifanya kazi na ZSGA basi watu hao walikuwa serious katika kumteketeza yeye pamoja na familia yake. Simu ile ndio ambayo ilionekana kumshtua zaidi jambo ambalo lilimfanya kuwapitgia simu vijana wake kwa kutaka kujua wamefikia wapi katika suala zima la kumtafuta Peter. Japokuwa dakika kadhaa zilizopita alikuwa ameongea nao na kumwambia kwamba wangehakikisha kwamba mtu huyo anapatikana lakini kutokana na maneno ya Bwana Stewart, akaamua kuwapigia simu tena. “Vipi?” “Kuhusu nini bosi” “Kuhusu Peter” “Si tumekwishakwamb ia Bossi kwamba kila kitu kitafanyika kama tulivyopanga” Sauti ya kijana wake ilisikika upande mwingine. “Hapana. Nataka mfanye kazi leo leo, nataka mhakikishe kwamba huyu mtu anauawa leo hii hii, nisipomuua mimi ataniua yeye” Mzee Mbwana aliwaambia huku akionekana kuwa na wasiwasi. “Hakuna tatizo bosi” “Unajua mnaniletea utani. Hivi mnajua kwamba Peter anahusika na kundi la ZSGA?” Mzee Mbwana aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa . “Hapana” “Peter anahusika nao, na wana lengo la kutaka kunimaliza mimi mwenyewe” Mzee Mbwana alimwambia kijana wake ambaye akaonekana kutokuelewa vizuri. “Inakuwaje hapa bosi?” “Ndio hivyo. Peter anahusika na kundi hilo kwa ajili ya kuniteketeza” Mzee Mbwana alimwambia kijana wake. “Sidhani. Sidhani kama Peter anaweza kuungana na kundi hilo. Hivi kweli unalifahamu kundi hilo bosi?” Kijana yule aliuliza. “Sikiliza Bosco. Sitaki maneno maneno. Ninachokitaka ni kuona Peter anakamatwa na kuuawa tu. Basi...hayo mengine yatajulikana akishakuwa kaburini” Mzee Mbwana alimwambia Bosco. “Sawa bosi” Bosco aliitikia na kisha simu kukatwa. **** Serikali ya Zambia ilikuwa imechanganyikiw a, mauaji ya polisi ambayo yalitokea katika nyumba ya wageni ya Sasara yalionekana kuichanganya serikali kupita kawaida. Kila mtu mitaani alikuwa akiongea lake jambo ambalo lilionyesha ni kwa jinsi gani suala lile lilikuwa limemshangaza kila mtu nchini Zambia. Hiyo ndio ilikuwa ni mara ya kwanza nchini Zambia kwa polisi kuuawa kwa wingi katika mashambulizi. Kila mtu ambaye alikuwa amelishuhudia tukio lile alikuwa akiongea lake. Vikao vya dharura vikaitwa na moja kwa moja kumuingiza Peter katika tukio lile kwamba yeye ndiye ambaye alikuwa amehusika katika kila kitu pamoja na kuchonga mchongo mzima wa polisi wengine kuuawa. Peter akaonekana kama gaidi nchini Zambia, Peter akaonekana mtu wa kutisha ambaye hakutakiwa kusogelewa hata mara moja. Kila mtu ambaye angeweza kumuona Peter alitakiwa kuwasiliana na kituo chochote cha polisi kwani tayari thamani yake ilikuwa imekwishaongeze ka na alikwishaandali wa kesi ya kujibu, kesi ya ugaidi ambayo ilikuwa ikimkabili kwa wakati huo. Hayo pamoja na mambo mengine ndio ambayo yalikuwa yamejadiliwa katika vikao vya polisi ambavyo vilikuwa vimefanyika katika makao makuu ya polisi, Peter alitakiwa kutafutwa popote pale alipo kwa ajili ya kufikishwa mahakamani na kutakiwa kujibu kesi ya ugaidi ambayo ilikuwa ikimkabili kwa wakati huo. Taarifa hiyo ikapelekwa mpaka nchini tanzania, watanzania wakatakiwa kufahamu kwamba kulikuwa na mtanzania nchini Zambia ambaye alikuwa amehusika katika ugaidi nchini Zambia. Kila mtanzania ambaye aliisikia habari ile akaonekana kushtuka, haikuwa kutokea kwa mtanzania kuhusika kakatika mambo ya ugaidi kama vile ambavyo Peter alikuwa amehusishwa. “Hivi huyu Peter ni nani? Mambo yake yananifanya nimkumbuke Savimbi” Jamaa mmoja wa alimwambia mwenzake. “Hata mimi mwenyewe nashangaa. Mtanzania kuhusishwa na ugaidi! Ni jambo geni sana masikioni mwangu” Jamaa mwingine alimwambia mwenzake. “Sasa inakuwaje kwa huyu Peter?” “Hata mimi nashangaa. Nahisi kuna kitu, nahisi kuna watu wapo nyuma yake” Jamaa mwingine alisema. Kwa kila mtanzania ambaye alikuwa amesikia taarifa ya kijana wa kitanzania, peter kuhusishwa katika ugaidi alionekana kushangaa, lilikuwa jambo gumu kwa Tanzania, nchi ambayo ilikuwa ikisifika kwa amani raia wake kuhusishwa katika ugaidi sehemu yoyote ile. Kamanda wa jeshi la polisi nchini Tanzania akawaita watu mbalimbali katika jeshi lake na kisha kuweka kikao juu ya namna ya kumpata huyo mtanzania ambaye alikuwa amekwenda kuichafua nchi ya Tanzania nchini Zambia. “Tunatuma wapelelezi wetu kwenda huko haraka iwezekanavyo. Hivi ninavyoongea ninataka wapelelezi wawili wakubwa waelekee huko” Kamanda mkuu wa jeshi la polisi aliwaambia polisi wenzake katika kikao hicho cha dharura. Hakukuwa na kilichoendelea zaidi, kilichofanyika ni wapelelezi watatu kuandaliwa na kisha kutakiwa kuelekea nchini Zambia kwa ajili ya kupeleleza ili kujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea nchini Zambia pamoja na kumtafuta Peter ambaye alionekana kama gaidi katika kipindi hicho. “Mtakapompata, breki ya kwanza hapa nyumbani. Kwanza tunataka kuonana na mtu wetu, inawezekana kuna jambo limejificha nyuma ya pazia” Kamanda mkuu wa jeshi la polisi nchini Tanzania, Bwana Kimario aliwaambia wapelelezi wa kitanzania ambao walikuwa wakijiandaa kuelekea nchini Zambia. “Hakuna tatizo mkuu. Tutafanya hivyo” Mpelelezi Michael alimwambia kamanda mkuu. Je nini kitaendelea?
Posted on: Sat, 31 Aug 2013 19:28:35 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015