USALAMA: UJAMAA NDIYO MWOKOZI WETU?/Wanderi wa - TopicsExpress



          

USALAMA: UJAMAA NDIYO MWOKOZI WETU?/Wanderi wa Kamau ALIKASHIFIWA na kukosolewa. Alibandikwa ‘mwaasisi wa falsafa dhoofu na hafidhina ya ujamaa’ ambayo iliimaskinisha Tanzania badala ya kuistawisha kiuchumi. Licha ya hayo, marehemu Mwalimu Julius Nyerere alishikilia msimamo wake. Na dondandugu la ongezeko la uhuni linapotukosesha usingizi, tunakimbilia ‘kuiba’ kanuni za kijamaa kama mwokozi wetu. Si tulikataa utabiri wa marehemu Jaramogi Oginga Odinga? Narejelea pendekezo la Waziri wa Ndani na Uratibu wa Serikali Kuu Joseph Ole Lenku la mkakati wa ‘Nyumba Kumi’ kama mujarabu wa kukabiliana na ongezeko la uhalifu. Katika mkakati huu, kila nyumba kumi huwa na kiongozi maalum ambaye huhakikisha kuwa majirani wanaoishi katika nyumba hizo wanafahamiana na kusaidiana kwa lolote linalojiri. Kwa kifupi, ni mkakati ambao huhakikisha uwepo wa undugu miongoni mwa majirani wanaoishi pamoja. Haya ni maono waliokuwa nayo waanzilishi wa mataifa ya Kiafrika, hasa baada ya kuhudhuria makongamano yaliyolenga kulikomboa bara la Afrika kutokana na minyororo ya wakoloni katika miaka ya hamsini; ndoto ya mshikamano. Uanaharakati wa viongozi wa Muungamo wa Watu Weusi (Pan Africanists) kama marehemu Booker T Washington, WEB du Bois, Marcus Garvey na wengineo ulilenga kujenga ujamaa endelevu barani humu, uliokusudiwa kuleta moyo wa kujaliana na kusaidiana. Hivyo ndivyo Mwalimu Nyerere na Mzee Jomo Kenyatta (Kenya), Dkt Hastings Kamunzu Banda (Malawi), Leopold Senghor (Senegal) kati ya wengine walivyopata misukumo ya kuendeleza sera za ujamaa katika mataifa yao, ili kuziunganisha jamii zao kuzipa nguvu harakati za kupambana wakoloni katika nchi hizo. Hata hivyo, mkosi mkuu ulitokea kuwa hata baada ya mataifa hayo kujinyakulia uhuru na kubuni sera za kuyaunganisha, sera hizo zilibaki tu katika karatasi zilimoandikwa- bila utekelezaji wowote. Hiyo ndiyo ilikuwa chemichemi ya mafarakano na machafuko isiyoisha katika bara hili. Kivuli cha ubepari kikajenga wivu na ubinafsi katika kizazi kilichofuata. Kama mataifa mengine, Mzee Kenyatta alibuni falsasa ya Ujamaa wa Kiafrika (African Socialism), ambayo haikutekelezwa kamwe. Nchi ikasambaratika kwa misingi ya kikabila na kitabaka; pengo la matajiri na wachochole likaongezeka- nao roho wa uhalifu ukasheheni. Naamini kuwa Ujamaa ndiyo mwokozi wetu. Ndiyo njia pekee ya kuponya roho wa uhayawani na kutojali miongoni mwetu. Kwa waziri Lenku, huenda hii ni hatua ya kwanza ya kuhakikisha kuwa Wakenya wanakombolewa kutokana na athari za kutozingatiwa kwa ndoto za waasisi wetu. Uponyaji wa changamoto ya ukosefu wa usalama hauhitaji bunduki, twahitaji suluhu letu wenyewe.
Posted on: Sun, 20 Oct 2013 13:19:16 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015