WAKATI UKITAFAKARI UJIO WA OBAMA...SOMA UTAFITI WANGU HUU KUHUSU - TopicsExpress



          

WAKATI UKITAFAKARI UJIO WA OBAMA...SOMA UTAFITI WANGU HUU KUHUSU MASUALA USIYOYAJUA KUHUSU OBAMA. Pembetatu ya Kisumu, Zanzibar, Hawaii Agosti 28, 1963 siku Dkt. Martin Luther King alipotoa utabiri wake juu ya nafasi ya mtu mweusi nchini Marekani hakuna Mmarekani mweusi au mzungu aliyemtilia sana maanani-Dkt. King alionekana kuota ndoto, ndoto ya kisiasa, ndoto ya kusadikika, ndoto ambayo kila mmoja katika taifa hilo aliiona kuwa ni ndoto kweli kutokana na siasa za wakati huo. Wakati Dkt. King ‘akiota’ ndoto hiyo, siku hiyo hiyo mtoto aliyejulikana kwa jina la Barack Obama, nyanya zake wa kizungu wakimuita ‘Barry’ alikuwa ndio kwanza ametimiza siku ya 24 tangu alipofikisha miaka miwili ya kuzaliwa. Kadiri ndoto hiyo ilivyokuwa ikionekana kuwa ndoto, hakuna aliyefahamu kuwa masuala kadhaa yaliyotokea katika miji ya Kisumu, Kenya; Zanzibar, Tanzania na Hawaii, Marekani ndiyo ambayo kwa muunganiko wa aina yake, yangekuja kuitimiza ndoto hiyo takribani miongo minne baadaye. Kisumu, Kenya Ukoo wa Wajaluo wenye jina la Obama, ni miongoni mwa koo katika kabila hilo zinazotambuliwa kwa ujasiri wao wa kuthubutu, kutoa vijana wasomi na wenye kufanikisha kile wanachokuwa wanakitaka. Utafiti wa makala haya umebaini kuwa ukoo huo una asili za aina mbili. Kwanza Tanzania hususani katika mkoa wa Mara na pia Kisumu Kenya katika kijiji cha Kagero. Kwa mujibu wa Mbunge wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jimbo la Rorya lililoko mpakani mwa Tanzania na Kenya, Bw. Phillemon Sarungi, ukoo huo wa Obama una asili mkoani humo na katika ushuhuda wake kwa wanahabari alitaja baadhi ya wanaukoo wa ukoo huo kuwa bado wako mkoani Mara. Iwe ukoo huo una asili Kenya na kwamba umekuwa ukiingia Tanzania kwa sababu mbalimbali za kiujirani mwema, au asili yao ya awali ni Tanzania kabla ya baadaye kuhamia Kenya, ni suala la utafiti zaidi, lakini kilichodhahiri tu ni kwamba asili ya Rais Barack Obama ni ya pande nyingi inayomfanya kuwa Rais wa Kimataifa zaidi. Pamoja na kuwa na ndugu pande nyingi, sehemu rasmi inayokubalika na wanahistoria wengi kwa sasa kuwa ‘nyumbani’ kwa Rais huyo (kwa upande wa ukoo wa baba yake) ni katika kijiji cha Kagero, Kisumu-mahali lilipo kaburi la baba yake mzazi na babu yake mzaa baba. Kabla hata Dkt. King hajaoteshwa ndoto yake na wakati taifa la Marekani likizidi kuwa katika vuguvugu la harakati za kudai uhuru hasa kwa watu weusi, Wakenya nao hasa Wajaluo, kabila la ukoo wa Obama, nao walikuwa katika kipindi kigumu, kipindi cha kupigania uhuru wao. Kama ilivyokuwa katika mataifa mengi ya Afrika na hata Marekani kwenyewe, pamoja na kukandamizwa na kubanwa haki zao, bado kulipotokea matatizo makubwa ya kuhitaji nguvukazi, watu weupe walikimbilia kwa watu weusi. Ni katika mfumo huu wa utawala wa ‘watenge lakini wategemee,’ ndipo kuibuka kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, kulipoandika historia nyingine katika maisha ya Rais Barack Obama-uhusiano wake tena na Tanzania na zaidi mwanzo wa jambo lililokuja kutishia zaidi mbio zake za Urais-dini ya kiislamu. Mzee Onyango Obama, babu yake Rais Obama, alikuwa mmoja wa Wakenya waliochukuliwa kwenda vitani, akiwa mpishi katika jeshi la Kiingereza. Vita hiyo ya dunia ilimfikisha Mzee Onyango Obama visiwani Zanzibar na hapo historia nyingine ikaandikwa. Zanzibar, Tanzania Mzee Onyango Obama ambaye baadaye akiwa Zanzibar alifahamika kwa jina la umaarufu zaidi la Mzee Onyango, aliingia visiwani humo katika kipindi ambacho kama ilivyokuwa Kenya, harakati za watu weusi zilikwishashika kasi katika kudai uhuru wao. Kama ilivyokuwa Kenya kwa akina Mzee Jomo Kenyatta baadaye kuongoza harakati za uhuru, Zanzibar nako vuguvugu lilipokolea baadaye akina Mzee Abeid Aman Karume na wanasiasa wengine waliibuka na kuongoza mapambano. Mzee Onyango aliingia Zanzibar akiwa ametokea vitani na kupendezwa zaidi na hali ya hewa na utamaduni wa visiwa hivyo kiasi cha kuamua si tu kuweka makazi yake bali pia kuathiriwa na utamaduni wa visiwa hivyo. Ni visiwano humo ambako uhusiano wa kwanza wa Rais Barack Obama na uislamu ulipanza kufuatia Mzee Onyango kuamua kusilimu na kuwa muislamu. Haijafahamika iwapo uamuzi wake wa kubadili dini ulitokana na kuvutiwa na utamaduni wa dini hiyo au ulitokana na shauku ya kijamii hasa haja ya kuoa. Kwani baada ya kubadili dini, Mzee Onyango aliitwa Hussein, jina lake kamili likawa Hussein Onyango Obama, na kisha akamuoa binti wa kiislamu, Halima (baadhi ya fasihi zikimtaja kwa jina la Helima) ambaye kwa historia hii, damu ya Rais Obama inazidi kuwa na muungano na Tanzania. Lakini wakati Mzee Onyango ambaye ni mtoto wa pili katika familia ya watoto nane ya Mzee Onyango Apiya, akioa Zanzibar alishakuwa na mke aliyekuwa amemwacha nchini Kenya aliyekuwa amemuoa kimila aliyeitwa Akumu Nyanjoga (baadaye aliitwa Habiba) Ni kupitia mke huyu ndipo baadaye alipozaliwa kijana aliyekuwa na afya njema lakini ambaye kwa usomi wake aliokuja kuupata baadaye, alitofautiana vitu vingi na mzazi wake ikiwemo kutoiridhi dini ya kiislamu, huyu si mwningine bali ‘mzaa chema’ Barack Obama Sr., (ambaye kwa muktadha wa kitabu hiki tutakuwa tukimtaja kwa jina la Obama mkubwa). Ingawa Obama mkubwa (Baba yake Rais Obama) hakuiridhi dini ya kiislamu na katika utoto wake akielezwa kuwa alikuwa mtu asiyekuwa mfuasi wa masuala ya dini, lakini utamaduni wa kiislamu ambao mzazi wake alikuwa ameuchukua (na ambao ndugu wengi wa ukoo wao waliathiriwa nao pia ndio maana kuna majina kama Said Obama, Omar Obama, Maliki Obama, Zeituni Obama, Sarah Obama) haukumpita mbali ndio maana hata asili ya jina la mwanaye aliyekuja kuzaliwa Marekani aliitwa Barack (likiwa na maana ya baraka au neema, katika lugha ya kiarabu) inatokana na mizizi ya dini hiyo. Mzee Onyango baada ya kuishi Zanzibar baadaye alirejea kwao Kenya ambapo anaelezwa kuwa alirejea huko akiwa mtu tofauti-alikuwa muislamu asiyetaka mchezo na imani yake na pia akiwa mtu aliyeshiriki vita ya dunia, hakuwa mtu rahisi kutii amri za machifu wake wa jadi. “"Alirejea akiwa mtu tofauti, uzoefu wake katika vita ulimfanya awe mtu asiyekubaliana kirahisi na amri za machifu wa Kijaluo. Kutokuelewana kwake na chifu wa kijaluo aliyekuwa akiheshimika sana na ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kijaluo, Paul Mbuya Akoko kuliwafanya ndugu zake kumshauri ahame na kwenda kuishi kijijini Kagelo ambako ardhi ilikuwa nyingi na nzuri na ndiko ilikokuwa asili ya wazee wake,” anasema Hezron Ogembo, aliyekua pamoja na Mzee Onyango. Akiwa pia amerejea Kenya, haifahamiki kama alimchukua mkewe Halima na kama kupitia ndoa hiyo waifanikiwa kuwa na watoto au la, lakini kufuatia kifo cha mkewe Anjumu, Mzee Onyango alioa mke wa tatu, Sarah Ogwel, ambaye ndiye nyanya wa rais Obama ambaye amekuwa akifahamika sana kwa sasa akiishi hapo hapo kijijini Kagelo. Ingawa Sarah hana ufahamu wa kutosha wa kuzungumza lugha ya Kiingereza huku akizungumza Kiswahili pia kwa uchache, akiwa mweledi zaidi katika lugha ya kijaluo, ndiye amekuwa karibu sana na Rais Obama, mara nyingi akilazimika kutumia mkalimani wakati wa mzungumzo yao iwe kwa simu au hata ana kwa ana wakati Obama alipotembelea Kenya.akiwa Seneta Bibi huyu ndiye aliyemsaidia Obama kuijua historia ya babu na baba yake na kuyaweka masimulizi hayo katika “Dreams From My Father.” Ni kwa historia hii pia ndio maana wakati Obama akiwania Urais, katika mji wa Stone Town, Zanzibar, ambako Mzee Onyango alikuwa maarufu, vijana kadhaa waliojitambulisha kuwa wafuasi wa Obama waliweka makao makuu ya kile walichokiita ‘Zanzibar for Obama.’ Kwa hiyo unapozungumzia “uislamu” wa Rais Barack Obama, Zanzibar ndiko chimbuko la jina lake hilo ingawa hakuna ubishi kuwa Obama mwenyewe kama yeye hajawahi kuwa muislamu...ni mkristo safi. *MAKALA NA UTAFITI HUU NILIUFANYA NA KUANDIKA KATIKA GAZETI LA MAJIRA JUMAPILI MWAKA 2008 NIKIWA MASOMONI KWENYE CHUO KIKUU CHA MAINE, MAREKANI. UNAWEZA KUONGEZA KILE UNACHOKIJUA NA WEWE LAKINI MENGI YA HAYA OBAMA MWENYEWE PIA AMEYAGUSIA KATIKA KITABU CHAKE CHA "DREAMS FROM MY FATHER."
Posted on: Mon, 01 Jul 2013 08:58:34 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015