YANGA SC imepunguza pengo la pointi dhidi ya watani wao wa jadi, - TopicsExpress



          

YANGA SC imepunguza pengo la pointi dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hadi kubaki tatu kufuatia ushindi wa mabao 2-0 jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga sasa inatimiza pointi 12 na kupanda hadi nafasi ya pili, wakati Simba SC inaendelea kuishi kileleni kwa pointi 15, baada ya timu zote kucheza mechi saba. Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Isihaka Shirikisho, aliyesaidiwa na Mohamed Mkono na Kudra Omary wote wa Tanga, hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao hayo 2-0. 3PILLARSNAYANGA3 Pasi ndefu ya Athumani Iddi ‘Chuji’ ilimilikiwa vyema na Mrisho Khalfan Ngassa, akamzidi maarifa beki Salvatory Ntebe kabla ya kufumua shuti kumtungua kipa Hussein Sharrif ‘Casillas’ dakika ya sita. Baada ya kufunga bao hilo, Ngassa aliwaelelekea mashabiki wa Simba SC na kuanza kuwatambia kwa ishara kwamba yeye anajua na anatumia akili. Mrisho Ngassa tena alimtoka vyema beki wa pembeni wa Mtibwa, Paul Ngalema na kutia krosi maridadi iliyounganishwa nyavuni na Didier Kavumbangu dakika ya 24. Kwa ujumla Yanga SC ilicheza vyema kipindi cha kwanza na kutawala mchezo na Mtibwa Sugar pamoja na kufanya mashambulizi kadhaa, lakini hawakuweza kuipenya ngome ya wana Jangwani. Kocha Mecky Mexime wa Mtibwa alimtoa beki Salvatory Ntebe kipindi ha kwanza na kumuingiza Dickson Daud, ambaye hata hivyo mwanzoni mwa mchezo alionekana kufanya makosa mengi kabla ya kuimarika. Kipindi cha pili, Mtibwa walirudi wakiwa imara zaidi na kuonyesha upinzani kwa Yanga, wakijitahidi kuwadhibiti vizuri washambuliaji wa timu hiyo na pia kushambulia. Hata hivyo, uimara wa safu ya ulinzi ya Yanga iliyoongozwa na mchezaji bora Tanzania, Kevin Yondan uliinyima Mtibwa japo bao la kufutia machozi. Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite/Juma Abdul dk77, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar Khalfan dk59, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza/Said Bahanuzi dk80. Mtibwa Sugar; Hussein Sharif, Hassan Ramadhan, Paul Ngalema, Salvatory Ntebe/Dickson Daud dk33, Salim Abdallah, Shaaban Nditi, Ally Shomary, Awadh Juma, Mussa Mgosi/Juma Luizio dk66, Shaaban Kisiga na Vincent Barnabas/Masoud Mohamed dk37. Katika mchezo mwingine, Mgambo JKT imefungwa nyumbani 1-0 na Prisons Uwanja wa Mkwakwani, Tanga bao pekee la Peter Michael dakika ya 62.
Posted on: Sun, 06 Oct 2013 16:36:31 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015