ZBC MJUE KUBWA LISHAPITA MSIPALILIE FITINA TENA Na Salim Said - TopicsExpress



          

ZBC MJUE KUBWA LISHAPITA MSIPALILIE FITINA TENA Na Salim Said Salim KWA mara nyengine pamesikika malalamiko mengi ndani ya Baraza la Wawakilishi juu ya namna kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kinavyofanya kazi. Huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa Wawakilishi kulalamika kwamba kituo hiki kinajihusisha zaidi na kile kilichodaiwa kama uchochezi na kampeni ya kuwagawa watu wa Unguja na Pemba. Mwakilishi mmoja alisema utendaji kazi wa ZBC Televisheni kama wanavoita wenyewe, hautofautiani na wa Radio ya Interahamwe ya Rwanda ambayo ilichochea kufanyika mauaji ya halaiki nchini humo mwaka 1994. Siku hizi yaliyofanywa na Radio Interhamwe miaka 10 iliyopita hutolewa kama mfano wa namna chombo cha habari kinavyoweza kutumika vibaya na kusababisha balaa na maafa katika jamii ndani au nje ya nchi. Miaka michache kabla ya kuzuka mauaji yale ya kinyama Rwanda, viongozi wa serikali ya Rwanda na wa kituo cha radio hicho walionywa kuhusu hatari ya matangazo yao ya kusambaza habari za upande mmoja, siasaza chuki, uhasama, unafiki na uzandiki. Onyo hilo lilipuuzwa kwa vile viongozi hao walikuwa wamelewa madaraka na kuamini walikuwa na haki ya kufanya uchochezi na hakuna aliyekuwa na uwezo wa kuwawajibisha kisheria. Masikini roho zao kwani walijidanganya na kupuuza kwamba katika dunia mipaka ya nchi au kisingizio cha watawala kutaka wasiingiliwe katika mambo ya ndani ya nchi yao. Baada ya kutokea mauaji yanayotajwa kuchangiwa sana na matangazo ya Radio Interahamwe, ndio wahusika walionekana kujiulaumu kwa kufumbia macho uchochezi uliokuwa ukifanyika na wao kufurahia. Baadhi yao siku hizi utawaona wanyonge, kama vile ni wanaostahiki kuitwa binaadamu,kesi zao zinaposikilizwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita iliyoko Arusha (ICTR). Wapo wanaotoa visingizio kuwa hawakujua kutozuwia matanagazo yale kungesababisha wawe katika shutuma za kuleta mauaji hayo. Wengi tulitarajia mauaji ya halaiki ya Rwanda yangelitoa somo kwa nchi zilizo jirani na Rwanda, hasa za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini mambo bado ni tofauti, kama vile yaliyofanyika Rwanda ni madogo na “kubwa lijalo”. Yote haya yanatokana na watu kupenda ukubwa na ulwa, hata ikilazimika kutumia hila, hadaa, udanganyifu na kuuwa watu. Hapa nataka kuelezea jinsi madaraka yanavyomlewesha mtu kwa kukumbusha kauli ya Rais mstaafu wa Zanzibar, Komandoo Dk. Salmin Amour Juma, ambaye alisema ‘kiti cha Ikulu ni kitamu na si vibaya hata kidogo kuuwa hata watu 10 ili ubaki madarakani’ (aliyasema katika mkutano wa hadhara wa Kisonge, mjini Unguja). Masikini Komandoo, naye alijisahau, lakini labda leo anakumbuka na huenda ikawa anasikitikia kauli yake ile na kama hapendi irejewe, basi asingeitamka. Baada ya mauaji ya halaiki ya Rwanda tulishuhudia mauaji ya mamia ya watu baada ya uchaguzi wa mwisho wa Desemba 2007 nchini Kenya. Katika machafuko yale, kituo kimoja cha radiokilihusishwa na uchochezi na mmoja wa watangazaji na wapanga vipindi wake sasa Joshua Arap Sang, anakabiliwa na tuhuma za kuhusika na mauaji yale katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC, The Hague)pamoja na baadhi ya viongozi wakuu wa kisiasa wa Kenya. Haya ni matokeo ambayo Zanzibar inafaa kuyatumia kama mafunzo, lakini inaonekana wapo watu wasiotaka kabisa kujifunza. Inawezekana madai ya Wawakilishi yamekuzwa, lakini ukweli ni kwamba mwenendo wa ZBC Televisheni umekuwa ukitoa taswira inayoonyesha kama ipo ajenda maalum ya kupaka matope baadhi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kwani panaonekana hutafutwa kila mwanya kuwaonyesha kuwa si waadilifu. Habari zinazotolewa huwa zaidi ni za maoni na ni za upande mmoja na kwa kiasi kikubwa, kwa wale wanaojali misingi ya taaluma ya habari, huwa hazizingatii maadili na uwajibikaji. Baadhi ya vipindi, kama vya kujadili rasimu yakatiba, huwa zaidi vya maoni ya watu maalum, kama ni wao tu ndio wenye haki ya kusikika na misimamo yao ndio sahihi na wenye mitazamo tofauti ni wanafiki na wasaliti. Mwenendo huu si wa haki hata kidogo. Kituo cha habari cha umma hakipaswi kutumika kufanikisha kampeni au propaganda zinazolenga maslahi ya watu binafsi au kikundi cha watu hao. Watu wa Zanzibar wametoa maoni yao juu yaKatiba mpya wanayoitaka na kupendekeza mfumo wa serikali wanayotaka. Lakini kituo hiki kimeng’ang’ania kutoa nafasiya kusikika wale wanaotaka serikali mbili tu kama vile watu wa kundi hilo ndio wanaomiliki kituo chenyewe. Hapo wahusika wajuwe wanakiuka misingi ya haki na ile ya taaluma ya habari – uadilifu. Kinachosikitisha ni kwamba viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanajidai hawaoni ubaya huu, lakini waelewe kuwa moto huanza na cheche na cheche zinazowashwa na kituo hiki huenda zikazusha balaa Zanzibar. Ni vizuri kwa wahusika kutafakari haya na kuchukua tahadhari badala ya kungojea kuzuka balaa.
Posted on: Sat, 03 Aug 2013 22:28:58 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015