MWAKYEMBE AIPUUZA RWANDA *Apanga kukutana na waziri - TopicsExpress



          

MWAKYEMBE AIPUUZA RWANDA *Apanga kukutana na waziri mwenzake *Asema nchi haitayumba, Lipumba aonya WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amepuuza madai ya Serikali ya Rwanda kwamba itaacha kutumia Bandari ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kusafirisha mizigo yake. Kutokana na hali hiyo, Dk. Mwakyembe amesema Tanzania haiwezi kuyumbishwa, badala yake inajikita zaidi kuimarisha sekta ya uchukuzi. Akifungua semina ya wadau wa sekta ya Usafirishaji mjini Dar es Salaam jana, Dk. Mwakyembe alisema haamini kama Rwanda wanaweza kujitoa kupitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa sababu wamekuwa na unafuu wa kufupisha safari zao. Dk. Mwakyembe, alitoa kauli hiyo, ikiwa ni siku moja tu baada ya Rwanda kutangaza kutotumia Bandari ya Dar es Salaam, kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu kupitisha mizigo ya wafanyabiashara wake. Uamuzi huo, ulibainika baada ya Umoja wa Wasafirishaji wa Mizigo kwa njia ya Barabara Tanzania (TATOA), kuieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti nia ya nchi hiyo ikishirikiana na Uganda zilivyokusudia kuachana na mipango yao ya kupitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam. Alisema, ni mwendawazimu pekee ambaye anaweza kupitisha mizigo Bandari ya Mombasa kwenda Kigali Rwanda kutokana na umbali uliopo, kwani kutoka Dar es Salaam kwenda Rwanda ni karibu zaidi. Mwendo wa barabara kutoka Kigali kwenda Mombasa kupitia Uganda ni kilometa 1,704 na hutumia saa 25, tofauti na Bandari ya Dar es Salaam ambayo hutumia kilometa 1,460 na hutumia saa 18 tu kufika Kigali. Alisema anatarajia hata wakijitoa au wasijitoe, Tanzania itaendelea na juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya uchukuzi kwa lengo la kukuza uchumi ikiwemo ya reli, bandari na kuondoa vizuizi 56 vilivyopo na kubakiwa na vitatu. “Hayo maneno ni ya kwenye magazeti, siamini kama Rwanda wanaweza kuamua kutumia Bandari ya Mombasa ambako pana mwendo mrefu sana tofauti na Dar es Salaam ambako ni karibu na wanatumia saa chache. Tunachofanya sasa ni kuhakikisha tunaondoa vikwazo ikiwemo vizuizi vingi ambavyo ni kikwazo kwa kasi ya uchumi tuitakayo sasa, lakini pia natarajia kukutana na waziri mwenye dhamana wa Rwanda. “Ni mwendawazimu pekee anayeweza kufikiria kuacha kutumia bandari yetu na kuamua kutumia ile ya Mombasa ambayo ina umbali mrefu zaidi,” alisema Dk. Mwakyembe Kuhusu sekta ya Uchukuzi, waziri huyo alionya watendaji watakaoshindwa kutekeleza mpango wa Serikali wa kupata matokeo makubwa kwa haraka (BRN), kwamba wajiandae kufukuzwa kazi kwani hakuna mtumishi ambaye ana ajira ya kudumu ambayo haiwezi kuguswa. Mbali na hilo, ameonya watendaji wa Mamlaka ya Bandari (TPA), watakaoshindwa kutekeleza Mpango wa Serikali ujulikanao kama Tekeleza sasa kwa matokeo makubwa (Big Result Now-BRN), na kusema hakuna mwenye ajira ya kudumu ambayo atashindikana kufukuzwa. Alisema watendaji wa sekta ya uchukuzi ambao watashindwa kufanyakazi kwa kufuata uhiari wa BRN, basi ajiondoe mwenyewe na akatafute biashara ya chips kwani ndiyo inayomfaa. Alisema lengo na mpango wa Serikali kwa sasa ni kufufua reli ili kuondokana na usafirishaji wa mizigo mizito kwa njia ya barabara, ambazo ni hatari kwa barabara pamoja na hali ya sasa ya kusafirisha tani 200,000 tu kwa mwaka, ili ifikie tani milioni tatu. Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Rais ya Kufuatilia Matokeo ya Mpango wa BRN, Omary Issa alisema tayari wamekwishaanza ufuatiliaji ambapo kila Jumatatu ya kila wiki wizara zilizopo kwenye mpango huo, zinalazimika kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yao kwao. LIPUMBA Wakati huo huo, Mtaalamu nguli wa uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba, ameonya pato la uchumi wa Tanzania litaathirika iwapo wafanyabiashara wa nchi za Rwanda na Uganda, wataendelea na msimamo wao wa kutopitisha mizigo yao kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Akizungumzia hatua hiyo, Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), alionya kuwa jambo hilo lisichukuliwe kisiasa na badala yake aliutaka uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), kuongeza ufanisi wa kazi kwenye Bandari ya Dar es Salaam. “Tatizo hapa la msingi ni ushindani wa kibiashara katika bandari ya Dar es Salaam, inawachukua muda mrefu kushusha mizigo kwa siku 28, wakati bandari ya Mombasa inawachukua siku nne tu…..Lakini pia tozo kubwa, gharama za usafirishaji na rushwa iliyokithiri barabarani. “Makampuni ya mafuta na mizigo yataathirika, kuna ajira katika sekta hiyo pia itaathirika, hii siyo siasa, tuweke ushindani zaidi, tutaathirika na tunahitaji kuongeza biashara. “Changamoto yetu kubwa ni kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kuondoa tatizo la rushwa katika traffick,” alisema Profesa Lipumba. Kwa mujibu wa Prof. Lipumba Uganda ina asilimia kumi ya biashara inayopitia Bandari ya Dar es Salaam, huku Rwanda ikiwa na theluthi moja ya biashara inayopitia Bandari ya Dar es Salaam. Inaaminika Rwanda wanatumia zaidi Bandari ya Mombasa. MFANYABIASHARA Katika hatua nyingine, mmoja wa wafanyabiashara wakubwa mkoani Iringa, ameonya vikali hatua hiyo na kusema kama hatua hazitachukuliwa wafanyabiashara wajiandae kufilisika. CHANZO: Mtanzania
Posted on: Fri, 23 Aug 2013 07:36:14 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015