.RIWAYA: JERAHA LA HISIA MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU YA - TopicsExpress



          

.RIWAYA: JERAHA LA HISIA MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA “Lilian..unataka kuniua..unataka kuniua baada ya kunigombanisha na Naomi wangu..unataka kuniua baada ya kunilaghai nikafanya mapenzi na wewe wakati nina mke wa ndoa Lilian….sasa unataka kuniua, visu vya nini humu ndani Lilian…kumbe wewe ni muuaji…wewe ni mmoja wa wachuna ngozi Lilian…..Lili..Lili kweli ni wewe Lili…haya niue sasa….si ulinidanganya unatoka kidogo kumbe umeharibu umeridhika na sasa unatabasamu tu…muuaji mkubwa wewe…ulidhani ule ujumbe wa Naomi sitauona eeh..” Walter alikomea pale, alikuwa anatetemeka sana hisia zote za usaliti ziliishi naye na kujikuta katika wakati ule mgumu. Lilian alikuwa anaduwazwa na maneno ya Walter. Alijaribu kuisoma akili yake lakini alimuona kama aliyechanganyikiwa na ambaye hayupo tayari kubadilishwa kwa lolote lile katika mawazo yake. Lilian akajiuliza ni kipi cha kuanza nacho ili kuijenga akili ya Walter upya. Lilian akaingiza mikono yake mifukoni Walter akaanza kutetemeka alidhani Lilian anatoa silaha. Lilian akaibuka na kitambulisho. Bila kufanya hatua yoyote mbele akamrushia Walter kile kitambulisho. “Soma Walter…” Lilian akatamka kwa shida. Kwa tahadhari kubwa Walter akainama akakichukua na kukitazama. Akakisoa upesiupesi bila kuelewa chochote. “Suzi? Suzi ni nani?” “Nd’o mimi Walter…naitwa Suzi jina la kazi mimi ni daktari, daktari niliyekuwa namtibu shemeji yako Suzan…..ni simulizi ndefu tafadhali Walter mimi si muuaji……sijawahi kuua. Nisikilize…” Lilian akasihi. Walter akajengeka kidogo na kumruhusu Lilian aketi naye akaketi. Lilian akaanza kumueleza kwa ufupi sana juu ya maisha yake. Akamgusia kila kitu kilichopaswa kuyafikia masikio ya Walter. Akalia na hisia zake za maajabu, hisia ambazo zimewahi kwenda sawa na wanaume wawili tu katika ulimwengu huu. Hisia zilizomtuma kumwekea dawa Walter ili waweze kufanya mapenzi na mwisho wakajikuta penzini. Lilian alinena kwa hisia. Walter akaguswa, akalegeza msimamo wake. “Walter.....najutia kukuingilia katika mapenzi yako, nimemkosea sana Naomi. Nimekukosea wewe pia. Ni mapenzi tu Walter yaliyoibeba taaluma yangu na kuitupa mbali, ni mapenzi yamenifanya kama mtoto nimefanya mambo yanayostahili kuitwa na kijinga katika maisha yangu…hisia Walter Hisia…..mwenzio nina jeraha la hisia…uwepo wako ulinitonesha nimejikuta nikiwa mtumwa wa kuitafuta tiba lakini badala yake nimejikuta na kidonda kibichi. Nimekukosa Walter nimekukosa na bado natakiwa kuhukumiwa…..Naomi …..nisamehe …….” “Naomi yupo wapi?” Walter aliuliza swali lile kana kwamba ndo kitu pekee alichosikia katika mazungumzo ya Lilian yaliyoambatana na kilio cha kwikwi. “Naomi yu mikononi mwa polisi kwa kesi ya uchunaji ngozi…..jambo ambalo…” “Si nimekwambia Lili wewe ni muuaji tena mchun…” “Nooooo Walter…” Lilian akatokwa na ukulele ukiambatana na kilio kikubwa. Walter akatulia na kumtazama huku akitetemeka. Lilian hakutaka kumwachia Walter mwanya wa kufanya maamuzi yoyote. Akaamua kuendelea kuzungumza ili Walter aweze kuelewa ni kipi kinaendelea. Mkasa wa kutokea Dar hadi kukutana na Kibwana katika hoteli maarufu mji kasoro bahari Morogoro ukayavuta masikio ya Walter akajiweka katika hali ya utulivu sana na kusikiliza. Lilian alisimulia kwa uchungu kisa chote kile cha kufanya mambo nje ya uwezo ilimradi tu aweze kulitetea penzi lake kwa Walter. Harakati za Lilian zilimshangaza sana Walter lakini hakuingilia maongezi hadi pale aliposhikwa na butwaa kwa kitendo cha kijasiri cha Lilian kupambana na Kibwana hadi kufanikiwa kutoka katika chumba kile akiwa salama. “Kwa hiyo huyo Kibwana ndo amesema Naomi ni muuaji….” “Walter hadi sasa sijui lakini kuna ujumbe nimeutuma huko hospitali nasi tunatakiwa kufanya jambo kuikoa roho ya Naomi…Walter nina hatia kifuani mwangu tafadhali naomba unisamehe tu kwa yote yaliyotokea najua sina muda mrefu wa kukuomba msamaha nawe ukanielewa lakini elewa kuwa Naomi anakupenda sana….tuwe kitu kimoja kwa sasa Walter nitahitaji muda zaidi kukuomba msamaha wewe na Naomi…..Walter pliiiz” Lilian aliangukia katika kifua cha Walter, zile embe bolibo zilizokuwa zikiishi katika kifua kilichochangamka cha Lilian zilimtekenya Walter, machozi yenye uvuguvugu yakatambaa katika mikono yake. Mara zile hisia za huruma zikamtwaa akajihisi yu salama mikononi mwa Lilian tena. Mara akaikutanisha mikono yake na kumkumbatia kwa nguvu Lilian, mara wakajikuta wote kwa pamoja wakilia kwa uchungu mkubwa sana. hakuna aliyetaka kumwachia mwenzake…..miili yao ikabadilika kuwa mwili mmoja usiotaka kuishi katika hali tofauti na ile iliyokuwepo. Hali ya kimapenzi. Walter akasafiri hadi ulimwengu wa hisia kali…Lilian naye akajikita katika safari hiyo pasipokutegemea. Ghafla Lilian akatokwa na yowe kubwa sana lililomuogopesha Walter. Haraka huku akitetemeka Walter akaitoa mikono yake iliyokuwa imeanza kutamaa katika ncha za matiti ya Lilian. Macho yalikuwa yamemtoka Lilian kana kwamba alikuwa anatazamana na yule malaika mtoa roho. Lilian alikuwa anatisha kutazama…… Walter naye alijikuta amekodoa macho huku akiogopa bila kufahamu kwa nini anaogopa. Macho yake yalianza kumsaili Lilian kuanzia usoni, kasha yakashuka chini kwa hatua moja baada ya nyingine. Hatimae macho yakakutana na mfereji mwekundu uliokuwa unazidi kutiririka, wekundu ule ulikuwa wa damu nzito. Lilian alikuwa anatokwa na damu nyingi katika unyayo wa mguu wake. Walter alipotambua hili, Lilian naye alikumbuka kutokwa na kilio kilichotangaza maumivu yake makali. Zile chupa za dawa ambazo Walter alizivunja vunja bila kutambua zilikuwa zimezua madhara. Kipande kimoja kilikuwa kimekanyagwa na Lilian ambaye hakuwa na kiatu mguuni. Badala ya kuendelea kushangaa Walter alichukua kanga na kuwahi kukabiliana na zile damu zilizokuwa zinatiririka. Daktari akawa anatibiwa na mtu asiyekuwa na taaluma. Lilian alitoa maelekezo kadha wa kadha kwa Walter. Walter akageuka daktari, mara aelekezwe dawa hii mara ile, mwisho akatakiwa kumchoma sindano ambayo aliambiwa kuwa inazuia tetenesi. Walter alifuata maelekezo, akaiondoa nguo ya Lilian, kutokana na maelekezo ya mgonjwa Walter alitakiwa kumchoma sindano matakoni. Walter akiwa anahangaika huku na kule, kila alivyompa mgongo Lilian, daktari huyu alitabasamu kwani maumivu yalikuwa yameisha tayari na alichokuwa anafanya pale ni kumchezea Walter. Hali ya Walter kumjali ilimfurahisha alitamani sana idumu hivyo lakini alikumbuka kuwa kuna kivuli cha Naomi kilikuwa kikilia na kusaga meno juu yake. Hisia hizi zikamweka katika simanzi kuu na kujikuta akitokwa machozi. Walter ambaye alikuwa anamchoma ile sindano alimbembeleza akidhani kuwa ni maumivu ya sindano yalikuwa yamemfanya atokwe machozi. Lakini haikuwa hivyo na kamwe asingeweza kujua kuwa Lilian alikuwa katika kilio cha kuyalilia mapenzi. Mapenzi ya dhati. Hisia zilikuwa zinamvuruga kichwa chake. Alfajiri, Walter alikuwa amemshika mkono Lilian ambaye alikuwa bado anachechemea. Walikuwa wanaelekea kituo kikuu cha mabasi mkoani Mbeya. Wote walikuwa kimya. Basi walilopanda kwa pamoja mara ya kwanza nd’o hili likawa bahati yao tena kwa siku hii. Wakati mara ya kwanza walijikuta wamekaa siti moja bila kufahamiana, wakafahamiana kupitia vitabu vya mzee Beka Mfaume. Sasa walikuwa wanapanda wakiwa wanafahamiana, tena labda walikuwa ni zaidi ya marafiki. Wakafanikiwa kupata siti ya watu wawili, Walter akamkokota Lilian wakaingia ndani ya basi. Kwa jicho la upesi ukiwatazama walifanania kuwa wapenzi na kama hawakuwa wapenzi basi lazima ukaribu wao ungekutia mashaka. Baridi ilikuwa kali sana, walipofikia nafasi zao za kukaa Walter alitangulia upande a dirishani. Lilian akafuatia. Hazikupita dakika nyingi, Lilian akaanza kuyumbayumba kasha akamuangukia Walter. Walter akampokea kwa utulivu kichwa chake, akamlaza katika mapaja yake. Lilian alikuwa amesinzia. Walter alibaki katika tafakari ya aina yake. Alimtazama Lilian kama wanamke wa pekee, anayejua kujali na akikosasi mchoyo wa kujishusha na kuomba msamaha. Kitabia alitofautiana sana na Naomi mkewe wa ndoa ambaye kitu kinaitwa kujishusha kwake ilikuwa ni ndoto ya mchana. Hakuwa tayari walau kujishusha na kumbembeleza hata kama amemkosea. Lilian alikuwa na sauti fulani inayoweza kubadili msimamo wa mtu hata kama hakuwa katika mpango huo. Lilian alikuwa na kipaji cha ushawishi. Lilian alikuwa mpiganaji, kimaisha na kimapenzi. Au elimu nayo inachangia? Walter alijiuliza huku akiilinganisha elimu ya Lilian nay a mkewe Naomi. Hakika walikuwa watu wawili tofauti. “Mh lakini nitachanganuaje kuhusu hili wakati mi myewe sijasoma?” alijiuliza kasha akafanya tabasamu huku akichezea shavu la Lilian ambaye alikuwa amesinzia mapajani kwake. Safari ilipoanza Lilian alishtuka kutoka usingizini, labda milio ya honi ama vinginevyo. Kuanzia hapo hakulala tena. Alichangamka na kumchangamsha Walter. Safari ya kuelekea Morogoro katika harakati za kumkomboa Naomi na kumtia hatiani Kibwana kwa kupotosha ukweli na hatimaye kuzitia roho nyingi katika kesi wasizohusika nazo. ***** Chumba kikubwa kilichoruhusu hewa mwanana kuingia ndani kilichokuwa kinalindwa masaa yote kilitawaliwa na vichwa kadhaa vilivyokizunguka kitanda. Baada ya muda kidogo walibaki watu wawili, mmoja akiwa amelala na mwingine akiwa amekaa katika kitanda, baada ya kuwa wamepeana salamu za hapa na pale hatimaye ukajiri ule muda ambao Yule aliyekuwa amekaa aliungoja. Kwake yeye aliamini kuwa ni jambo ambalo litamfariji sana mgonjwa wake. Akampatia simu aweze kuzungumza na mtu. Namba zilikuwa ngeni sana. Na ulikuwa ni usiku wa saa moja. Kibwana akaipokea ile simu na kuandika zile namba kwa shauku kubwa sana. Kisha akapeleka sikioni aweze kusikiliza ni kipi kinasemwa. “Kibwana nazungumza..” alianza kwa kujitambulisha, Akwino alikuwa anatabasamu akingoja kaka yake aweze kufurahia hali ya kuzungumza na yule binti kwani alitambua jinsi kaka huyo alivyokuwa anampenda japo hakupata nafasi ya kuwa naye. Hofu iliyojitokeza usoni mwa Kibwana haikuweza kufichika mbele ya Akwino, na hata Kibwana alivyojaribu kujilazimisha kuwa kama awali haikuwezekana. “Hebu nenda kule nataka kuongea naye vizuri…” Kibwana alimwondoa Akwino naye akatii. Mazungumzo yakaendelea. Lilian alikuwa yu pamoja na Walter wakati simu ile inapigwa. Lilian akamwomba Walter akae kimya ili aweze kusema neno. “Kibwana….neno ni moja tu..nipo Morogoro na ujinga unaonitangazia nimeusikia japo hujanitaja jina. Sasa ni ombi kwa sasa lakini itageuka kuwa amri….nakuheshimu sana na licha ya kujaribu kunivunjia heshima bado nina masalio ya heshima kwako. Na ili heshima hii kidogo iendelee kubaki nakusihi sana, usimtie yeyote matatani kwa kisingizio cha kutaka kuchunwa ngozi jambo ambalo si kweli….naomba tunga uongo wako mwingine ili uwe huru na raia hao wema wawe huru….najua unamtambua Naomi, amepigwa bila kosa kwa ujinga wowote ambao unaweza kuwa umeufanya wa kumlaghai….nampa kipaumbele. Kama ikifika keshokutwa hajatoka hapo alipo nitausema ukweli wote wa ulichotaka kunifanyia. Kumbuka nilirekodi katika simu yangu kila kitu…nina ushahidi wote. Kibwana…..” “Naam dokta Suzi” Kibwana aliitika kwa hofu. “Nitakufunga usipokuwa makini elimu yako haitakuwa na maana tena baada ya siri hii kuvuja. Kumbuka unaidanganya serikali.” Lilian alisema kiujasiri. Walter aliyekuwa ubavuni mwake alishangazwa na ujasiri huu kutoka kwa mwanamke. “Nimekuelewa Dokta tafadhali naomba usifanye upesi nakuahidi nitatekeleza yote.” “Maneno dhidi ya vitendo. Uwe na usiku mwema.” Lilian aliaga na kisha akakata simu. Uso wake ulikuwa umeiva haswa na alikuwa anatetemeka wakati simu yake ilipoita tena. ***KIBWANA matatani……Dr. Suzi amempagawisha na kauli zake tata…… nini kitajiri???/ ITAENDELEA KESHO JIONI!!!!
Posted on: Thu, 17 Oct 2013 15:00:01 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015