TAARIFA YA TUHUMA ZA KUPANGA NJAMA ZA KUBAMBIKIZA KESI MAKADA WA - TopicsExpress



          

TAARIFA YA TUHUMA ZA KUPANGA NJAMA ZA KUBAMBIKIZA KESI MAKADA WA CHADEMA ZILIZOELEKEZWA DHIDI YANGU NA KUCHAPISHWA KWENYE MAGAZETI YA “TANZANIA DAIMA” NA “MAWIO” MIMI CHAGULANI ADAMS DIWANI KATA YA IGOMA JIJI LA MWANZA. “Uhuru wa vyombo vya habari ni lazima uendane na usalama wa raia”. Kauli hii imebeba ujumbe adhimu kwa muhimili usio rasmi wa serikali nikimaanisha tasnia ya vyombo vya habari. Agosti 9,2013 gazeti la Tanzania Daima liliandika habari yenye kichwa cha habari “ Makada wa CHADEMA watoka gerezani” katika habari hiyo ambayo ninadiriki kusema haikuzingatia maadili ya uandishi wa habari na taaluma ya uandishi kwa ujumla. Habari hiyo inaeleza sakata zima la makada wa CHADEMA wanaokabiliwa na kesi ya kumwagia tindikali Musa Tesha, usiku wa Septemba 9, 2011 katika msitu wa Hanihani, Igunga. Katika habari hiyo nimebebeshwa tuhuma nzito za kutisha zinazotweza na kuchafua hadhi na heshima yangu mbele ya umma ninaouongoza, ndugu na jamaa na watanzania kwa ujumla. Katika toleo la 3173 la Jumapili liliendelea kushadadia uhusika wangu katika kupanga njama za kuwabambika kesi ya ugaidi makada hao jambo ambalo si kweli hata kidogo. Kwenye gazeti la Mawio la Alhamis Agosti 15 hadi 21 2013 sura ya 10-11 liliandika habari hiyo pia yenye kichwa cha habari “Ugaidi wa CHADEMA waibua makubwa” ikieleza pia mimi ushiriki wangu kupanga mkakati wa kuwabambika kesi makada wenzangu wa CHADEMA. Katika gazeti la Tanzania Daima la Agosti9, 2013 mmoja wa makada Seif Magesa wa Mwanza anasema “alikamatiwa Mwanza na Mabaunsa wa Meya wa manispaa ya Ilemela Henry Matata akiwa na mimi Chagulani Adams na maafisa usalama wa taifa”. Binafsi sajawahi kushirikiana na Henry Matata, maaafisa wa usalama wa Taifa kupanga njama za kumkamata Seif Magesa (Majige) aliyejinasibu kutambua uwepo wangu wakati wa kukamatwa kwake, binafsi simfahamu Seif Magesa sijawahi kukutana naye au kushiriki kwa namna yeyote ile katika kupanga njama za kumkamata maana sina ugomvi naye na sioni faida ya kumtendea yeye mambo kama hayo. Madai ya Seif Magesa (Majige) na Tanzania Daima ni uzushi mtupu, uchonganishi, uchochezi, uzandiki na umbea wa mtaani wenye lengo la kuchafua jina langu mbele ya umma wa watanzania maana maelezo yake na Tanzania Daima na maelezo ya Seif aliyoyatoa kwenye gazeti la Mawio yanapishana, sijui malengo yake yeye na Tanzania Daima kunihusisha mimi ni yapi na kwa faida ya nani? Madai ya ndugu Rajab almaarufu kama (Y-dash), huyu ni mmoja kati ya wanaodai mimi kuhusika na kupanga mkakati na njama za kuwabambika kesi, Binafsi ninakiri kumfahamu Rajab Daniel Kihawa, nimemfahamu tangu mwishoni mwa mwaka 2011alipokuwa akiishi kwa Henry Matata (Mstahiki meya wa manispaa ya ilemela) ndipo nilipomjua na kubahatika kujua habari zake kiundani. Ameishi kwa Henry Matata akifanya kazi za u DJ, mlinzi na msaidizi wa shughuli za nyumbani pamoja na ukuli kwenye meli ya Mv Matata iliyozama kwenye kisiwa cha Gozi, baada meli hiyo kuzama alikuwa akifanya kazi ya u DJ kwenye hotel Magnum na wakati mwingine kwenye mikutano ya CHADEMA Kabla ya mimi na Matata kuvuliwa uanachama wa CHADEMA. Hapo ndipo nilipo mjua Rajab Kihawa na kujenga naye ukaribu kila nilipokuwa nikienda kuonana na Matata au katika vikao vya chama au madiwani wa chadema vilivyokuwa vikifanyika kwa Matata nae kama kijana mwenzangu, amekua akinishirikisha masahibu au changamoto zilizokuwa zinamkabiri kwa kuniomba ushauri au msaada alipokuwa akikwama katika kazi zake kwa muajiri wake. Kutokana na sintofahamu kati ya muajiri wake Henry Matata kuvuliwa uanachama, Rajab aliondoka kwa Henry Matata bila kumuaga bosi wake Matata, binafsi kutokana na ukaribu tuliokuwa nao mimi na yeye aliniaga kuwa anaenda Morogoro kutafuta kazi za vibarua kwenye mashamba ya mpunga, hii ni kutokana na mgogoro kati ya mwajiri wake (Matata) aliniambia hawezi tena kuendelea kuishi hapo, tangu hapo tumekuwa tukiwasiliana, kusalimiana na hata mimi kumsaidia kifedha nilipopata wasaa au yeye kupata wasaa huo na mara ya mwisho alinipigia simu kwa namba ya rafiki yake na kuniambia yuko Mpwapwa Dodoma akijishughulisha na kilimo cha alizeti. Nilipata habari za kukamatwa kwake kupitia vyombo vya habari wakati wa mchakato wa kesi inayowakabiri sasa lakini cha kunishangaza Rajab Kihawa kwenye maelezo yake katika gazeti la Tanzania Daima na gazeti la Mawio ananitaja kuwa mimi nilikuwepo wakati anakamatwa na pia nilishiriki kumsihi akubali kitita cha pesa shilingi milioni 30 ili awataje viongozi wakuu wa chama kuwa wahusika wakuu wa mpango wa utesaji, utekaji na umwagaji wa tindikali unaoendelea sehemu mbalimbali kwa ahadi ya pesa kutoka kwa viongozi wa serikali pamoja na CCM ili awataje viogozi wakuu wa chama. Madai ya ndugu Rajab Kihawa ni uongo mtamu na ukweli bandia na kauli kifuniko zenye kuleta hitilafu na mitikisiko yenye kujenga chuki, uchochezi, fitina na majungu dhidi yangu kwa umma ili kubinua fikra na mawazo ya wananchi wenye imani na dhamira njema dhidi yangu ili kujenga taswira na kuhalalisha usaliti na hujuma ambazo wanadai mimi nazifanya dhidi ya chama changu CHADEMA. Katika toleo la 3171 la Ijumaa Agosti 9,2013 anasema Shibuda alimuonesha simu anawasiliana na Rais Kikwete lakini kwenye toleo no.3173 maelezo ya Rajab anadai Shibuda alikuwa anaongea na Sophia Simba huku akiwa ameweka loud speaker kumuomba Mhe. Sophia Simba amuunganishe na Rais Kikwete. Inaonesha kuwa maelezo ya Rajab katika gazeti la Tanzania Daima toleo namba 3171 na 3173 yanapingana, hii ni kuonesha kuwa ndugu Rajab anazungumza uongo mtamu ili kujihalalishia huruma kwa jamii na kwa waliomtuma kunipakazia tuhuma za uongo dhidi yangu ili kunijengea chuki katika jamii. Binafsi sijawahi kushirikiana na viongozi aliowataja Ndugu Rajab kuhujumu chama eti kwa sababu nina mgogoro na chama changu, mimi bado ni mwana CHADEMA kindakindaki na ninaipenda CHADEMA siwezi kushiriki kuihujuma kwa maslahi yangu binafsi, hata kama nina ugomvi na baadhi ya viongozi, Kutofautiana katika familia hakukwepeki ila siwezi kubomoa nyumba ya familia eti kwa sababu sielewani na kaka au dada, kufanya hivyo utakua ni upogo na ushenzi wa hali ya juu. Nimekuwa nikifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi, rafiki na wanachama wenzangu wenye nia njema na mimi na kutambua uwezo wangu na umuhimu wangu katika chama ili kumaliza tofauti zetu na tuweze kusonga mbele, lakini kuna watu kila uchao wanajenga tabia na hulka za kutanua mgogoro kwa maslahi yao binafsi na kunijengea taswira ya ubaya, chuki na hujuma jambo ambalo si jema hata kidogo a si tabia yangu. Waungwana hunena “kugombana na askofu /shehe hakuondoi uislam / ukristo wa mtu” Chagulani Adams nitaendelea kuwa mpinzani (mwana CHADEMA) wa kupandwa na kuota (Kindakindaki), mapito ya tuhuma,fitina na chuki dhidi yangu ni tanuru linalonipika kuelekea ukamilifu wa kweli kwa maana ili dhahabu iwe safi ni lazima ipitishwe kwenye Kalibuni (Tanuru la moto mkali) kisha hutoka ikiwa safi hivyo ni lazma niyapitie magumu haya ili nitakapo kabidhiwa dhamana kuu niwatendee watu wetu haki maana asili ya uongozi na haki na watu. “Mwalim Nyerere katika kitabu cha “Tujisahishe” alisema “Ukweli una tabia moja nzuri sana, haujalishi mkubwa wala mdogo, haujalishi adui wala rafiki, kwake watu wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kulipiza kisasi kama ukipuuzwa. Ukiona nataka kulipiga jiwe teke kwa kuwa nafikiri ni mpira, natumai utanionya, lakini nikilipuuza onyo lako eti kwa sababu wee ni mdogo ama kwa sababu sikupendi nikalipiga teke basi nitavunjika japo ningekua nani, ukweli haupendi kupuuzwa puuzwa” Imani yangu mimi Chagulani siasa si vita, kutofaautiana ki mtazamo isiwe chanzo cha kutupiana tuhuma nzito za kutisha zisizo na ukweli wowote ule kufanya hivyo ni kutumia vibaya uhuru wa vyombo vya habari na kuhatarisha usalama wangu. Kwa kulijua hilo wakenya wameweka kwenye katiba yao kuwa ni marufuku kuchapa habari yoyote inayomtuhumu mtu mwingine bila kumhoji au kusikia maoni ya mtu huyo. Lakini cha kushangaza gazeti la Tanzania daima katika toleo la 3171 lilichapisha habari likinihusisha mimi kushiriki kupanga mkakati wa kuwabambikizia kesi makada wenzangu bila kunihoji kuhusiana na ukweli wa jambo hilo kwa lengo laa kujenga chuku dhidi yangu. Ndugu Josephat Isango alinipigia simu kupitia namba 0786426414 akiniuliza ushiriki wangu katika kupanga mkakati wa kuwabambikizia kesi, mwandishi huyu tayari alikua na upande na akiamini kuwa mimi nimehusika katika kupanga njama chafu za kuhujumu CHADEMA na viongozi wake. Ndugu Isango aliamini maelezo ya ndugu Rajab na Seif Magesa kuwa ndiyo ya kweli bila kuuliza upande wa pili unaotuhumiwa na kuchapisha habari zile katika toleo la 3171 la Tanzania Daima kwa kivuli cha mwandishi wetu kwa lengo la kunijengea chuki bila kusikiliza maelezo yangu. Katika majibu yangu kwa ndugu Isango baada ya kunipigia simu akiniuliza ushiriki wangu pamoja na uwepo wangu Dodoma mwezi wa 4 na kukamatwa kwa Rajab Kihawa na Seif Magesa, nilimjibu ndg Isangu lakini hakuandika kama nilivyomjibu katika toleo la 3173 la siku ya Jumapili 11,Agosti 2013, kwa maslahi yake na gazeti aliamua kupotosha ukweli na kutoandika maelezo yangu ya kina ili kunijengea taswira mbaya kwenye chama na umma wa watanzania na ni kuonesha mimi ni mtu hatari sana katika siasa za CHADEMA. Uwepo wangu Dodoma hauhusiani na kupanga njama za kukamatwa kwa Rajab wala Seif Magesa. Nilienda Dodoma (Kondoa) mara mbili mwezi wa pili na mwezi wa nne nikifuatilia uhamisho wa mke wangu Editha Gabriel Issaya aliyehama kutoka Kondoa kuja Mwanza jiji katika hatua za awali na baadaye kupeleka viambatanisho TAMISEMI mwezi wa nne. Ili kuthibitisha hilo nilimtaka aangalie orodha ya watumishi waliopata uhamisho mwezi Juni mwaka huu jina la Editha Issaya anahama kutoka Kondoa kwenda Mwanza jiji. Hivyo uandishi wake ulilenga kutumia vibaya uhuru wa vyombo vya habari kuandika mambo na tuhuma bila kuhoji kwa malengo anayoyajua yeye na gazeti la Tanzania Daima katika toleo la 3171pia kuhatarisha usalama wangu mbele ya jamii na umma kwa ujumla, kuwa mimi ni msaliti wa mageuzi ya kuondoa chama cha mapinduzi madarakani, hii imekuwa ni tabia ya gazeti la Tanzania Daima maana hata katika toleo la Septemba 11,2012 toleo la 2838 waliandika “CHADEMA watimua madiwani wao wawili kwa usaliti Mwanza” jambo ambalo ni tofauti na barua yangu ya kuvuliwa uanachama yenye kumb. Na. C/HQ/M/MZA/14/56 iliyoandikwa na katibu mkuu Dr. Slaa inayotaja kuvuliwa kwangu uanachama ni “utovu wa nidhamu” na sio usaliti kama ambavyo Tanzania Daima imekua ikiandika na kluaminisha umma wa watanzania wakiwa na lengo la kujenga chuki, fitna na uhasama dhidi yangu. Ni lazma watambue kuwa uhuru wa vyombo vya habari ni lazma uendane na usalama wa raia na sio kuandika habari zenye tuhuma juu yangu bila kuniuliza au kusikia maoni yangu maana kufanya hivyo ni kuhatarisha usalama wangu mimi familia yangu na ukoo wa Chagulani Adams Ibrahim dhida ya wapenzi wa mageuzi na wanachama wa CHADEMA. Niaminivyo mimi uongozi ni mchakato wa kujifunza kila siku, kosa nililo litenda jana likijirudia leo nitakuwa na uelewa na maarifa ya jinsi ya kulitatua na kuliepuka maana tunajifunza kutokana na makosa. Watu makini na wenye uelewa mpana hujikita kutafuta suluhu palipo na mvutano baina ya pande mbili ili kufikia malengo, ni wapuuzi na washenzi hujikita katika kutanua na kukuza mgogoro kwa malengo yao binafsi. Ninaipenda sana CHADEMA na kamwe siwezi kushiriki kukihujumu chama wala viongozi wake eti kwa sababu nina mgogoro na chama ndio maana ninatafuta suluhu ili tusonge mbele kwa pamoja, banadamu tunamadhaifu yetu, tukijifunza kusameheana, kushirikiana , kuchukuliana na kuvumiliana tutafikia ukombozi wa kweli tunaoutarajia. Hakuna kulala mpaka kieleweke, CHADEMA tumaini jipya la watanzania, haya nayo yatapita. Mungu nibariki Chagulani Adams , Mungu ibariki Igoma, Mungu ibariki CHADEMA, Mungu ibariki Mwanza, Mungu ibariki Tanzania. Niandikie kupitia chagulaniadams@ymail (0783/0717/0767-137831)
Posted on: Sun, 25 Aug 2013 16:14:34 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015