A DAY TOO LONG SEHEMU YA 14 Ilipoishia jana.. “Si nyie tu, - TopicsExpress



          

A DAY TOO LONG SEHEMU YA 14 Ilipoishia jana.. “Si nyie tu, hata nchini kwao mtu huyu hatokwenda. Yupo India na ataendelea kuwa India, haondoki kwenda popote pale, hata nchini kwao hatokanyaga” Dokta Patel alimwambia. “Utake usitake. Atafika Marekani tu, tena mwezi huu huu” Dokta Mickey alimwambia Dokta Patel na kisha kuondoka mahali hapo huku Abuu akibaki kuwa na mshangao. Songa nayo sasa Wazamiaji bado walikuwa wameshikilia mapipa ambayo yalikuwa yametupwa ndani ya bahari ile. Mawimbi yalikuwa yakiendelea kupiga zaidi na zaidi lakini hakukuwa na mtu ambaye alikuwa tayari kuyaachia mapipa yale ambayo walikuwa wameyashika. Hali ya hewa ndani ya bahari iile ilionekana kuwatisha kupita kawaida, mawimbi yale ambayo yalikuwa na nguvu kubwa yalikuwa yakiendelea kuwapiga kupita kawaida. Hali ya mahali hapo ilikuwa ni baridi kali, miili yao ilikuwa ikitetemeka kupita kawaida. Mpaka jua linachomoza, bado hali zao hazikuwa nzuri, walikuwa wakiendelea kupigwa na mawimbi yale zaidi na zaidi. Kila walipokuwa wakiangalia huku na kule, hakukuwa na dalili zozote za nchi kavu au kisiwa chochote kile jambo ambalo waliona kwamba huo ungekuwa mwisho wa maisha yao katika bahari hiyo. Katika kipindi hicho, walitamani sana kuona meli au boti yoyote ikiwa inaelekea kule walipokuwa lakini jambo hilo wala halikuweza kutokea kabisa. Hawakujua ni wapi kulikuwa upande wa mashariki, Magharibi, Kaskazini au Kusini, kote kulionekana kutokuwa na kitu chochote kile. Miili yao ilikuwa ikitetemeka kupita kiasi na kutokana na mawimbi yale ambayo yalikuwa yakiwapiga, yakawafanya kuanza kusikia njaa. Hakukuwa na chakula mahali hapo, hakukuwa na msaada wowote ule japokuwa walitamani sana jambo hilo litokee mahali hapo. Saa la kwanza likapita, likaingia saa la pili na mpaka kufikia masaa kumi, bado walikuwa wameendelea kushilia mapipa yale. Katika kipindi hicho hakukuwa na mtu ambaye alikuwa radhi kuyaachia mapipa yale, kila mmoja alikuwa na imani kwamba ni laizima kungekuwa na msaada ambao ungeweza kutokea mahali hapo na hicyo kuokolewa. “Kuna msaada kweli unaweza kutokea?” Chopa alimuuliza Selemani huku akitetemeka kupita kawaida. “Ngoja tuendelee kusubiri, nadhani tutapata msaada” Selemani alimwambia Chopa huku nae akiwa anatetemeka na huku akiwa amelishikilia pipa moja pamoja na Chopa. Masaa yalizidi kukatika mpaka usiku unaingia, bado hakukuonekana msaada wowote ule jambo ambalo lilionekana kuwakatisha tamaa kabisa. Siku nzima wakawa wameitumia ndani ya bahari hiyo ya Hindi. Mpaka usiku unaingia, hakukuwa na msaada wa meli yoyote ambao ulionekana karibu nao. Katika usiku huo, baridi lilikuwa kali zaidi baharini, walikuwa wakitetemeka kupita kawaida kiasi ambacho ngozi za miili yao zikaanza kujikunja kunja. Kila mmoja akaanza kujuta, walijuta sababu ambazo ziliwapelekea kupanga mikakati ya kuzamia na kuelekea nchi za Ulaya au marekani. Siku nzima wakawa wameitumia katika bahari ile huku kila mmoja akionekana kuchoka kupita kawaida. Matumbo yao yakazidi kusikia njaa zaidi na zaidi lakini hakukuwa na chakula chochote ambacho walikuwa wamekipata. Kazi yao kubwa kwa siku nzima ilikuwa ni kunywa maji ya bahari ile ambayo yalikuwa na chumvi kupita kawaida. Siku ya pili ikaingia, hali haikubadilika, bado ilikuwa vile vile. Njaa zilizidi kuwauma kupita kawaida, kila mmoja akaona mwili wake ukiishiwa nguvu. Mikono yao ikaanza kuonekana kuchoka kushikilia mapipa yale jambo ambalo kila mtu alikuwa akitamani kuyaachia na hatimae kuzama baharini na kufa. Hali ilionekana kutisha kupita kawaida, siku ya pili ikaingia na kukatika, bado walikuwa wakiendelea kuwa katika bahari ile. Katika siku ya tatu ya kuwa baharini pale, wakaanza kukata tamaa. Akaanza Dullah, mwili ulikuwa umechoka kupita kawaida, ngozi yake ilikuwa imejikunja kutokana na baridi pamoja na kukaa baharini kwa muda mrefu, akaviona vidole vyake vikikosa nguvu kabisa. “Nimechoka. Siwezi kushikilia zaidi” Dullah alimwambia Ibra huku akionekana kuchoka zaidi. Dullah alitamani kuendelea kulishikilia pipa lile lakini vidole vyake havikutaka kabisa kuleta ushirikiano na akili yake. Vidole vikaanza kuliachia pipa lile na hatimae kuanza kuzama baharini. Kila mtu alikuwa akimumwangalia, mioyo yao ilikuwa na maumivu sana lakini hawakuwa na jinsi, tayari kwa jinsi hali ilivyokuwa ikiendelea kwenda mbele na ndivyo ambavyo walizidi kuchoka zaidi na zaidi. Bado msaada haukuonekana kabisa machoni mwao baharini pale, waliendelea kushikilia mapipa yale zaidi na zaidi. Mtu wa pili kuachia pipa alikuwa Halidi, kijana ambaye alikuwa na ndoto nyingi sana za kufanya katika kipindi ambacho angefika Ulaya. Bado kila mmoja alionekana kuwa na wasiwasi, vidole vyao vilikuwa vimechoka sana kuyashikilia mapipa yale. Miili yao ilikuwa imeanza kuota mabaka ambayo yalisababishwa na kukaa kwa muda mrefu ndani ya maji yenye chumvi nyingi. Mmoja baada ya mwingine akaanza kuchia pipa ambalo alikuwa amelishika na hatimae kuzama. Hali ilionekana kuwa ngumu zaidi, hata Chopa mwenyewe nae akaamua kuachia pipa lile jambo ambalo lilimfanya kuzama na kufa baharini. Safari ya kwenda Ulaya, kulala na wanawake wa kizungu, kutafuta fedha na hatimae kuyabadilisha maisha yao ilikuwa imeishia katika bahari ile. Vijana wote ambao walikuwa wametangulizana nao walikuwa wameyaachia mapipa yale na hatimae kufa na hivyo kubakia watu wawili tu, Selemani na Ibra. Wote walikuwa wameshikana mikono jambo ambalo liliwafanya kudumu kwa muda mrefu baharini pale. Usiku ukaingia. Baridi la siku hiyo lilikuwa kali kuliko siku nyingine zilizopita. Muda wote walikuwa wakitetemeka kupita kawaida. Mioyo yao ilikuwa ikisali ili Mungu aweze kuwaokoa katika pipa hali ambayo walikuwa nayo. “Yaani tunakufa baharini kabla ya kufika Ulaya?” Chopa alimuuliza Selemani huku akionekana kuchoka kuishikilia mikono ya Selemani. “Hatutokufa. Tutapata msaada” Selemani alimwambia Chopa japokuwa alijua fika kwamba huo ndio ulikuwa mwisho wa maisha yao. Mpaka inaingia alfajiri ya siku ya nne, bado walikuwa baharini pale. Miili yao kwa wakati huo ikaonekana kutisha kupita kawaida. Miili ilianza kuota vitu vya kijani kama maji ambayo yalikuwa yamekaa sehemu moja kwa muda mrefu. Macho yao yalikuwa mekundu kupita kawaida kutokana na maji kuwapiga machoni kila wakati. “Nimechoka” Alisema Chopa kwa sauti ya chini ambayo kwa kuisikia tu, ilionyesha dhahiri kwamba alikuwa amechoka. “Jitahidi. Usiniache peke yangu” Selemani alimwambia Chopa huku aking’ang’ania mikono yake. Hali hiyo haikuweza kusaidia kitu chochote kile, Chopa akaonekana kuchoka kupita kawaida, akaanza kuiachia mikono ya Selemani na hivyo kuanza kuzama, alikuwa amechagua kufa kuliko kuendelea kuteseka baharini pale. Selemani akaonekana kuumia kupita kawaida lakini wala hakuwa na jinsi, kile ambacho kilikuwa kimetokea wala hakuwa na uwezo wa kukizuia kabisa. Chopa akawa amezama baharini na kufa. Wazamiaji wote wakawa wamekwishazama na kubakia Selemani peke yake ambaye alikuwa akiendelea kulishikilia pipa lile. Moyo wake uliumia kupita kawaida, alikuwa akitamani kulia lakini wala machozi hayakuweza kumtoka kabisa. Siku hizo zilionekana kuwa siku za mateso kuliko siku zote katika maisha yake, hakuwa na uhakika kama angeweza kunusurika katika bahari ile. Usiku ukaingia, siku hiyo ikaonekana kuwa mbaya kuliko siku zote, bahari ikachafuka. Mawimbi yakaanza kupiga kupita kawaida. Pipa likaanza kupelekwa huku na kule lakini Selemani hakutaka kuliachia japokuwa alikuwa amechoka kupita kawaida. Kuchafuka kwa bahari ile kuliendelea kwa dakika zaidi ya arobaini na ndipo bahari ile ikaanza kuwa katika hali ya kawaida. Selamani alionekana kuchoka zaidi ya siku nyingine, tumbo lake lilikuwa limeingia ndani, asilimia kubwa ya mwili wake ulikuwa umeota vitu vya kijani kuonyesha kwamba alikuwa amekaa sana ndani ya maji yenye chumvi. Siku ya tano ikaingia huku Selemani akiendelea kuwa baharini pale. Mwili wake ukakosa nguvu, japokuwa alikuwa ameshikilia kwa kipindi kirefu lakini kwa wakati huo hakuona kama angeweza kushikilia zaidi. Bila kupenda, akaviona vidole vyake vikianza kuliachia pipa lile. Moyoni aliumia, hakuamini kama safari ya kwenda Ulaya ilikuwa ikiishia mahali hapo. Alitamani kuendelea kulishikilia pipa lile, ila vidole havikuweza kuendelea kulishikilia. “Mungu! Naomba unisamehe kwa kila kibaya nilichokifanya” Selemani alisema huku akiwa amekwishaachia pipa lile na kuanza kuzama ndani ya bahari ile. ***** Mawasiliano yakaanza kufanyika kupitia kati ya Dokta Patel pamoja na Waziri wa Afya nchini India, Bwana Kumir. Mawasiliano hayo kwa njia ya simu yalikuwa ni kutaka kumuelezea kile ambacho Dokta Mickey kutoka nchini Marekani alikuwa amekizungumza katika kipindi ambacho alikuwa amefika nchini hapo na kuonana na Abuu ambaye alikuwa ametengeneza dawa ya magonjwa ya kansa. Wazo ambalo walikuwa nalo madaktari wa India kwamba ilikuwa ni lazima waidhulumu dawa ile na kisha kuanza kuitoa wao tayari lilikuwa limefutika katika vichwa vyao, kwa wakati huo walikuwa wakitaka kukaa na Abuu kwani tayari alionekana kuwa tayari kuliletea sifa taifa hilo ambalo lilikuwa likisifika kuwa na madaktari walio mabingwa duniani. Bwana Kumir akaonekana kushtuka kupita kawaida, tayari alikwishaona kama wasingefanya jambo fulani basi Wamarekani wangeweza kufanya kile ambacho walikuwa wakitaka kukifanya, kumchukua Abuu kinguvu na kisha kumpeleka nchini Marekani, sehemu ambayo angeweza kuliletea sifa taifa hilo. Alichokifanya Bwana Kumir ni kuanza kuwasiliana na rais wa nchi hiyo, Bwana Ranjit ambaye akataka kuonana nae ili apate kumuelezea kwa kina kile ambacho alikuwa ameongea nae simuni. Bwana Kumir akaanza kuelekea Ikulu ambapo baada ya kufika, moja kwa moja akakaribishwa na kuingia ndani. “Umesemaje?” Rais, Bwana Ranjit aliuliza huku akionekana kushtuka. “Kama nilivyokwambia Mheshimiwa. Wamarekani wanaweza kumchukua mtu huyu” Bwana Kumir alimwambia Rais. “Haiwezekani, labda mimi nisiwe rais” Bwana Ranjit alisema huku akijiapiza kwamba kamwe Abuu asingeweza kuchukuliwa na Wamarekani. Rais Ranjit hakutaka kusema kwa maneno tu, akaanza kufanya kwa vitendo. Kitu cha kwanza alichokifanya ni kumgawia Abuu nyumba ambayo alitakiwa kuishi humo, akapewa gari la kifahari ambalo lilitakiwa kujazwa mafuta kila baada ya siku mbili, akafunguliwa akaunti ya benki na kisha kuingiziwa kiasi cha dola milioni mbili kama kianzio cha kumfanya kuvutika kwao zaidi. Hawakuishia hapo, walichokuwa wakikifanya kwa wakati huo ni kuhakikisha kwamba Abuu anabaki kwao. Kitu kingine ambacho kilifanyika ni kumpa ajira katika hospitali ya Taifa ya nchini India, sehemu ambapo angefanya kazi kama Dokta wa kawaida huku akiwa amesaini mkataba utakaomlipa kiasi kikubwa cha fedha, mara mbili ya kile alichokuwa akilipwa Dokta mkuu wa hospitali hiyo, Dokta Patel. Taarifa za uwezo wa Abuu zikaanza kutangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari, nchi ya India ikajitangaza rasmi kwamba mtu wao ambaye alikuwa akisoma katika chuo kilichokuwa nchini kwao alikuwa ameleta neema kwa watu wote waliokuwa wakiishi katika dunia hii mara baada ya kupata dawa ya magonjwa ya kansa. Kila mtu akashtuka, hawakuamini kama duniani kungekuwa na mtu ambaye angeweza kutengeneza dawa ya aina hiyo. Taarifa zile zikaendelea kutangazwa zaidi na zaidi, kwa wakati huo, kila mtu akataka kumuona mtu huyo, na hata pale ambapo picha yake ilipotolewa, hakukuwa na mtu ambaye aliamini kwamba Abuu angeweza kutengeneza dawa hiyo. Watu walikuwa wakifikiria kwamba mtu huyo angekuwa mzee na mwenye umri mkubwa lakini alionekana kuwa tofauti kabisa. Alionekana kuwa kijana mdogo ambaye alikuwa na miaka ishirini na moja tu, mtu mweusi ambaye alikuwa na ulemavu wa mguu mmoja. Serikali ya Tanzania nayo ikaonekana kucharuka hasa mara baada ya kuona kwamba yule mtu ambaye alikuwa ametengeneza dawa ya kansa alikuwa ni Mtanzania ambaye alikuwa amekwenda nchini India kwa ajili ya kusoma tu tena huku akiwa anadhaminiwa na Serikali ya Tanzania. Watanzania wakamtaka mtu wao arudi katika nchi yake, hawakuwa radhi kuona taifa la India likipata sifa kupitia kwa mtu ambaye wala hakuwa wa taifa hilo. Hapo ndipo maneno mbalimbali yalipoanza kusikika kutoka kwa Watanzania, tayari waliona kwamba nchi ya India ilikuwa ikiendelea kujipatia umaarufu duniani kupitia mtu wao jambo ambalo wala hawakulifurahia. Rais akaambiwa kwamba ilitakiwa afanye kitu kimoja, kuhakikisha kwamba Abuu analetwa nchini Tanzania. Rais wa Tanzania, Bwana Baraka Kyomo alipoongea na rais wa India na kumuelezea kile kilichotakiwa kufanywa, nchi ya India ikawatoa madaktari kumi ambao walikuwa na uwezo mkubwa ili kuachiwa nafasi ya kuwa na Abuu ambaye kwa wakati huo alionekana kuwa juu zaidi ya madaktari wote. Hilo halikuonekana kutosha kwa Watanzania, kitu ambacho walikuwa wakikitaka kwa wakati huo ni kumuona Abuu akiletwa nchini tu. Kazi ilionekana kuwa kubwa kwa rais wa Tanzania, kila alipokuwa akiongea na rais wa India, aliulizwa alikuwa akitaka kitu gani zaidi ili awaachie Abuu ambaye tayari dawa zake zilikuwa zimeanza kusambazwa na watu kupona. “Watanzania hawatonielewa kabisa. Wanachotaka ni kumuona Abuu akirudishwa nchini tu” Rais wa Tanzania, Bwana Baraka Kyomo alimwambia rais wa India, Bwana Ranjit. “Jambo hilo gumu sana. Acha sisi tumtangaze halafu tutawapeni mtu wenu” Bwana Ranjit alimwambia Bwana Baraka Kyomo. “Hilo gumu sana pia” “Wale madaktari kumi hawatoshi tuongeze wengine?” “Kwa ajili ya Abuu, hata ukiwaleta madaktari wote wa India bado hawatotosha” Bwana Kyomo alimwambia Ranjit. “Basi tutawajengea hospitali ya kisasa. Unaonaje hapo?” “Dah!” “Usijali. Kila kitu kitakuwa safi” Bwana Ranjit alimwambia rais Kyomo. Kama alivyoongea ndivyo ambavyo ilivyofanyika, baada ya siku tano, ujenzi wa hospitali kubwa ukaanza ndani ya jiji la Dar es salaam. Kutokana na fedha kumwagwa sana, ujenzi wa hospitali ile ukaendelea kwa kasi ya ajabu sana na baada ya miezi mitatu tu, kila kitu kilikuwa tayari. Bado, hali haikuonekana kuvumilika kabisa, Watanzania hawakuonekana kuelewa, walijua fika kwamba Waindi walikuwa wamefanya vile kwa sababu walikuwa wakitaka kubaki na Abuu ambaye kwao alionekana kuwa na faida kubwa kupita kawaida huku wakiingiza fedha kwa njia ya ujanja ujanja. Kila walipokuwa wakipiga kelele, Watanzania wakaonekana kutokueleweka jambo ambalo likawafanya watu kujipanga na kutaka kuuchoma moto ubalozi wa India pamoja na hospitali ile ambayo ilikuwa imejengwa na Serikali ya India. Jambo hilo kidogo likaonekana kuleta hofu moyoni mwa rais Kyomo ambaye akaanza kuwasiliana tena na rais Ranjit na kisha kumwambia kile ambacho Watanzania walitaka kukifanya. Rais Ranjit akaonekana kuhofia, tayari aliona kwamba kulikuwa na matatizo ambayo yangeweza kutokea, hivyo ilikuwa ni lazima ampeleke Abuu nchini Tanzania japokuwa hakutaka jambo hilo litokee kabisa. Alichokifanya ni kuanza kuwasiliana na Waziri wake wa Afya, Bwana Kumar na kisha kumwambia kile ambacho alitakiwa kukifanya, kumsafirisha Abuu kuelekea nchini Tanzania kabla mambo hayajaharibika. Kwa sababu Abuu alikuwa akiendelea kusoma chuoni, Bwana Kumar akawatuma vijana wake na kisha kuelekea katika chuo hicho kwa ajili ya kumchukua Abuu na kumpeleka katika ofisi yake. Vijana wale wakafika katika chuo kile na kisha kuanza kumuulizia Abuu ambaye alikuwa maarufu sana katika kipindi hicho. “Mmmh! Aliondoka leo mchana” Mwanachuo mmoja alijibu. “Kwenda wapi?” Mmoja wa vijana waliotumwa na Bwana Kumir aliuliza. “Kuna gari la wazungu fulani lilikuja chuoni na kisha kumpandisha, walipoelekea, hatujui” Mwanachuo huyo alijibu. Maneno yale yakaonekana kuwashtua vijana wale, walichokifanya ni kuwasiliana na Bwana Kumir na kisha kumwambia kile ambacho kilikuwa kimeendelea kule chuoni. Bwana Kumir akaonekana kuchanganyikiwa, kitendo cha kusikia kwamba kulikuwa na wazungu ambao walikuwa wamefika na kumchukua Abuu kilionekana kumfanya kuhisi jambo. “Wamarekani” Ilisikika sauti ya Bwana Kumir. Bwana Kumir akazidi kuchanganyikiwa, hapo hapo akaanza kuwasiliana na rais Ranjit na kisha kuanza kumwambia kile ambacho kilikuwa kimeendelea, rais Ranjit akaonekana kuchanganyikiwa zaidi, tayari alijua fika kwamba Wamarekani walikuwa wamewachezea mchezo mchafu. Hapo hapo bila kuchelewa akachukua simu yake na kumpigia rais wa Marekani, Barack Obama na kumwambia kuhusu kile kilichofanyika. “Hatujafanya kitu kama hicho” Ilisikika sauti ya Obama simuni. “Una uhakika?” “Asilimia nyingi tu” “Sawa. Nimekuelewa. Msako unaanza, tutakayempata nae, tunawaua na miili yao kuichoma moto kama zawadi kwa mungu wetu, Bhuddha” Rais Ranjit alisema kwa hasirira. “Subiri kwa…..” Obama alisema lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, simu ikakatwa. Kwa haraka bila kupoteza muda rais Ranjit akaanza kutoa taarifa kwa mkuu wa jeshi la polisi ambaye akaitangazia nchi ya India kwamba kuna watu ambao ni wazungu walikuwa wamefika nchini hapo na kumteka Abuu, hivyo, mipaka ya nchi ilitakiwa kufungwa, uchunguzi ufanyike kwa kila mtu ambaye alikuwa akitaka kusafiri kupitia uwanja wa ndege, kila gari ambalo lilikuwa likitaka kutoka nje ya nchi lilitakiwa kupekuliwa. Hapo ndipo msako rasmi ulipoanza. Kila mmoja alikuwa akitaka kumuona Abuu akirudi mikononi mwao kwa wakati huo. Ukiachana na hiyo, Watanzania bado walikuwa wakimtaka mtu wao aweze kurudishwa nchini mwao. “Sikuamini. Sikuamini hata kidogo, huo utakuwa mchezo mchafu mnaotaka kutufanyia” Rais Kyomo alisikika simuni. “Ndio ukweli. Nilimtuma waziri wa Afya kwenda kumchukua chuo ili tumsafirishe lakini akakuta Wamarekani wamemchukua” Rais Ranjit alimwambia . “Huo ni mchezo tu. TUNAMTAKA ABUU WETU” Iliskika sauti ya rais Kyomo na kisha kukata simu. ******************************************** ***** Je nini kitaendelea? *****Je ni kweli Wamarekani wamemchukua Abuu? Na Abuu ataweza kupatikana? ***** Je Selemani atakufa baharini?
Posted on: Mon, 19 Aug 2013 05:22:19 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015