Intelejensia ya Tanzania Inaitafuta Vita ya Rwanda Kwa Wudi na - TopicsExpress



          

Intelejensia ya Tanzania Inaitafuta Vita ya Rwanda Kwa Wudi na Uvumba Ilimradi Kuinusuru CCM..!! Mwaka 1978 rais Julius Nyerere alitangaza vita dhidi ya Uganda na vita hiyo ilidumu kwa takribani mwaka mmoja. Kijeshi tulishinda vita hiyo kwa kufanikiwa kumng’oa madarakani kiongozi wa nchi hiyo Field Marshal Idd Amin Dadaa, lakini kiuchumi tulishindwa vita hiyo na badala yake tuliimarisha uchumi wa Uganda na hali ya kisiasa ya nchi hiyo hadi hivi sasa! Hali hii ilisababishwa na kutokuwa na wataalam makini wa idara ya intelejensia wenye uwezo wa kupima na kuona faida na hasara ya vita hata kabla haijafanyika. Nchi za jumuiya ya kujihami za NATO huwa zinapenda sana vita, lakini wao hawaendi vitani hata kwa kuchokozwa kama wanaona kwamba vita hiyo haina maslahi ya kiuchumi na kisiasa. Kwa mfano, Marekani ililazimisha vita ya Iraq kwa kisingizio kwamba Sadam Hussein ana silaha za maangamizi; nia ya Marekani ilikuwa siyo kumnyang’anya Saadam Hussein silaha hizo bali walikuwa wanayatamani mafuta ya Iraq kwa miaka mingi, na kilichofanyika katika nchi hiyo ni kuhakikisha wanaharibu miundombinu yote kwa kuipiga mabomu mazito na baada ya vita kumalizika Amerika ndiyo ikachukuwa tenda zote za kuijenga miundombinu ya nchi hiyo upya kwa gharama za mafuta ya Iraq! Wakati Nyerere anatangaza vita dhidi ya Uganda alisingizia kwamba majeshi ya Uganda yameingia ndani ya Tanzania na yanadai kwamba kipande cha ardhi ya Tanzania ni mali yao, hivyo hatuna budi kwenda vitani kuikomboa nchi yetu! Baada ya hapo zikaanza propaganda za kuwahamasisha wanajeshi na watanzania kwa ujumla kama vile: Nia ya kumpiga Idd Amin tunayo! Sababu za kumpiga tunazo! Uwezo wa kumpiga tunao! Wakati Nyerere anaifagilia vita ya Uganda upande mwingine wa vyanzo vya habari ukawa unasema Idd Amin hakuivamia Tanzania bali wanajeshi wetu ndiyo waliotumwa waingie ndani ya ardhi ya Uganda kwa madhumuni ya kumchokoza Idd Amin ambaye alikuwa mtu wa vitendo na asiyependa mizaha, hivyo wanajeshi wetu walipoingia Uganda wanajeshi wa Idd Amin wakawashambulia na kuwafukuza ndani ya nchi yao hadi ndani ya ardhi ya Tanzania; wanajeshi wa Uganda walipokanyaga tu ardhi ya Tanzania tayari intelejensia yetu ikapata sababu ya kuitengeneza vita ya Uganda tukaanza kupiga mayowe ndani na nje ya nchi kwamba Idd Amin ametuvamia na anataka kumega kipande cha ardhi yetu! Ikumbukwe kwamba Idd Amin alikuwa mkuu wa majeshi ya Uganda kabla ya kumpindua rais wa nchi hiyo Dr. Milton Obote ambaye alipinduliwa akiwa safarini kuhudhuria mkutano wa nchi zisizofungamana na upande wowote kule Jakarta – Indonesia; safari ya Jakarta Obote aliikataa kwa vile alikuwa na ugomvi na Idd Amin na alijua fika kwamba akiondoka nchini lazima atapinduliwa, lakini Nyerere alimshawishi waende pamoja na kama akipinduliwa basi atamsaidia kumrudisha madarakani. Siku ambayo Nyerere na Obote wanawasili mjini Jakarta Idd Amin anatangaza kumpindua rais Obote na kuchukua madaraka! Obote alihudhuria mkutano kama msikilizaji tu kwa vile alikuwa siyo kiongozi wa Uganda! Baada ya mkutano walirudi na Nyerere na kupewa hifadhi ya ukimbizi wa siasa hapa nchini, na baada ya hapo ikaanza mikakati ya chini kwa chini ya kutekeleza ahadi ya Julius Nyerere aliyokuwa amemuahidi rafiki yake mkubwa Dr. Milton Obote ya kumrudisha madarakani! Ilipofika mwaka 1978 ndipo mikakati ikawa imekamilika na vita ya Uganda ikaanza ambayo iliung’oa utawala wa Idd Amin na hatimaye kumrudisha rais Milton Obote madarakani baada ya marais wa mpito wasiopungua watatu ambao waliwekwa makusudi ili kuupotosha umma kwamba madhumuni ya vita na Uganda ilikuwa siyo kumrudisha Obote madarakani, hapana, bali ilikuwa ni vita ya kuikomboa nchi yetu! Tangu rais Jakaya Kikwete atoe ushauri kwa rais Kagame wa Rwanda kule Addis Ababa – Ethiopia, ushauri ambao ulichukuliwa na Serikali ya Rwanda kama kebehi na kuingilia mambo ya ndani ya Rwanda. Tangu ushauri huo utolewe na kupingwa vikali na rais Kagame uhusiano wa Kikwete na Kagame umekuwa siyo mzuri, na kumekuwa na kupigana vijembe vya hapa na pale kwa sehemu zote mbili! Na kwenye vijembe hasa vya watu wakubwa kama marais wa nchi mapaparazi huwa hawakosekani kuchombeza huku na kule. Nimechukua fursa hii ya kuandika makala hii kutokana na habari zilizoandikwa kwenye gazeti la kila siku la Mwananchi la Jumatano August 21, 2013 gazeti hili liliandika habari nyingi kuhusu mvutano wa Kikwete na Kagame. Kwenye sherehe za mashujaa zilizofanyika kule mkoani Kagera Kikwete alikaririwa akisema “mtu yeyote atakayeivamia au atakayedhubutu kuimega ardhi yetu tutamchapa” na baada hapo alielezea kwa ufupi jinsi Idd Amin wa Uganda alivyochapwa baada ya kuivamia na kutaka kuimega ardhi ya Tanzania. Katika sherehe hizo pia Kikwete aliamuru wahamiaji haramu waondoke mara moja nchini ambapo raia wa nchi jirani za Uganda, Burundi, Rwanda na DRC wametii amri hiyo. Rwanda pekee ilikuwa na wahamiaji haramu wasiopungua 7,000 ambayo ilikuwa ndiyo idadi kubwa kuliko jumla ya idadi ya nchi zingine tatu zilizobakia. Waandishi wa gazeti hili la Mwananchi wanadai kwamba mzozo wa Kikwete na Kagame umeingia hatua mpya baada ya Rwanda kudai kwamba Mama Salma Kikwete ni binamu yake rais wa zamani wa nchi hiyo Juvenal Habyarimana; pia waandishi wanadai kwamba Rwanda wanataka ugomvi kwa vile mbona wanalalamika kuhusu kufukuzwa kwa raia wao Tanzania wakati hata nchi za Uganda, Burundi na DRC watu wao wamefukuzwa lakini wao hawalalamiki; mhariri anaendelea kusema kwamba “Kagame, Kujenga nchi miaka kuibomoa dakika.” Mimi ningependa kuzijibu makala hizi kama ifuatavyo: Kwanza turudi nyuma tukumbuke uhusiano wa Rwanda na Tanzania miaka hiyo ya utawala wa Nyerere na Habyarimana; kulikuwa na makubaliano ya kuwaruhusu raia wa Rwanda laki nane (800,000) wapewe uraia wa Tanzania kwa vile Rwanda ina watu wengi na ardhi ni ndogo sana, makubaliano ambayo Nyerere hakuyakataa moja kwa moja na wala hakuyakubali moja kwa moja, hivyo kulingana na hali hiyo ndiyo maana Wanyaruanda wengi waliweza kuingia na kuhamia nchini kwa vile mazungumzo ya wao kuhamia Tanzania yalikuwa yanaendelea na mazungumzo haya yalififia baada ya rais Habyarimana kuuwawa na ajali ya ndege mwaka 1994, na mazungumzo haya yakafa moja kwa moja baada ya Nyerere kufariki dunia mwaka 1999. Rwanda ni lazima walalamike kwa vile raia wao hawakuingia tu kienyeji, bali kulikuwa na mazungumzo ambayo yalikuwa yanaendelea ya kuhalalisha kuwepo kwao hapa nchini; hata hivyo wanayo haki ya kulalamika kwa vile idadi ya wahamiaji hao haramu ni kubwa sana ukilinganisha na idadi ya nchi zingine! Watu 7,000 ambao wahapo kwenye budget ya nchi wanaporudi nchini kwa wakati mmoja ni mzigo kwa taifa kwa vile watu hao wanahitaji ardhi jambo ambalo ni tatizo kubwa kwa nchi ya Rwanda ambayo ina eneo dogo na watu wengi kupita kiasi; watu hao wanahitaji miundombinu kama vile barabara, mashule, mahospitali, maji, umeme na simu; vyote hivi ni mzigo kwa taifa! Tukumbuke kwamba miaka 15 iliyopita Serikali ya Tanzania iliwakataa raia wake wa kabila la Wazigua waliokimbia vita na ubaguzi huko nchini Somalia; nchini Somalia kulikuwa na raia wa Tanzania ambao ni kabila la Wazigua waliohamia miaka mingi kwenye nchi hiyo na wakawa raia wa nchi hiyo ya Somalia, lakini hawakutupa lugha na mila zao za Kizigua, hivyo vita ya wenyewe kwa wenyewe ilipoanza wakawa wanauwawa na kubaguliwa na Wasomali na walipoamua kurudi nyumbani Tanzania Serikali ya CCM iliwakataa kwamba haiwatambui! Walipoenda Kenya napo wakakataliwa kwa vile Kenya hakuna kabila la Wazigua! Serikali ya Marekani chini ya utawala wa rais Bill Clinton aliwaonea huruma na kuwapa uraia wa Marekani na hivi sasa wote wanaishi kwenye jimbo la Arizona nchini Marekani na ni raia kamili wa nchi hiyo licha ya kwamba walikuwa Wazigua wa Tanzania waliolowea Somalia! Je, mbona sisi hatujishangai kwamba tumewakataa Wazigua wetu wa hapo Handeni ambao walilowea Somalia kutafuta maisha!? Sisi tuliwakataa Wazigua na hivi sasa wamekuwa Wamarekani! Kagame yeye hakuwakataa Wanyaruwanda wenzie licha ya kwamba ana matatizo makubwa ya ardhi, lakini amewapokea ili wabanane hapo hapo kwa vile ni nchi yao wote! Je, bado tu hatujatambua ni Serikali ipi isiyowajali wananchi wake!? Kuhusu Mama Salma Kikwete kuwa binamu yake rais Habyarimana kuna tatizo gani hapo!? Hata kama rais Kikwete ndiye angekuwa mdogo wake rais Habyarimana bado kusingekuwa na tatizo kwa vile bara la Afrika lilikuwa nchi moja kabla ya wakoloni kuligawagawa vipande kwa madhumuni ya kututawala, hivyo mgawanyo huu umeweza kuwagawa ndugu wengine wakawa nchi moja na wengine nchi nyingine; ni mgawanyo huu huu ambao umeweza kuligawa kabila moja likawa katika nchi mbili tofauti; ni mgawanyo huu huu ndiyo ulioweza kuzigawa koo mbalimbali na kuziweka katika nchi mbili na hata wakati mwingine zaidi ya nchi mbili! Mbona Nyerere alikuwa rais wa Tanzania kwa miaka 23 lakini ana asili ya Kitusi toka Burundi na jina lake halisi ni Lunyerere!? Kule nchini Burundi ukoo wa akina Lunyerere ni ukoo mkubwa sana. Mbona rais wa kwanza wa Zanzibar Abeid Karume alikuwa raia wa Malawi lakini aliweza kutawala Zanzibar na ameacha watoto, wajuu na vilembwe ambao ni Wazanzibar!? Mbona rais wa pili wa Zambia Fredrick Chiluba alikuwa na asili ya DRC lakini aliweza kuitawala Zambia kwa miaka kumi!? Mbona rais wa kwanza wa Zambia Kenneth Kaunda alikuwa na asili ya Malawi lakini aliweza kuitawala Zambia kwa zaidi ya miaka 20 na hadi leo ni raia wa nchi hiyo!? Mimi simuelewi mhariri anaposema kwamba “Kagame, Kujenga nchi miaka kuibomoa dakika.” Kwanini mhariri anakimbilia vita haraka haraka kiasi hicho!? Tusiifanyie vita mzaha! Vita inagharimu maisha ya watu wengi hasa watoto wadogo na wazee ambao hawawezi kukimbia! Malumbano siyo vita! Au ubinamu wa Mama Salima Kikwete na rais Habyarimana ambaye alikuwa Muhutu ndiyo unatumika kama chanzo cha ugomvi kati ya Kikwete na Kagame hasa kwa vile Kagame ni Mtutsi na Wahutu ni mahasimu wao wakubwa wa jadi!? Kwani Kikwete na Kagame wameingia madarakani lini!? In maana kwamba miaka yote hiyo walikuwa hawajui kwamba Mama Salima Kikwete ni binamu yake Habyarimana!? Je, Kagame ana ugomvi na watu wote wenye undugu wa damu na rais Habyarimana au ana ugomvi na Wahutu wote!? Kwani ndugu zake Habyarimana wako wangapi na wametapakaa nchi ngapi za Afrika na hata duniani kote!? Je, ina maana Kagame yupo tayari kwenda vitani na nchi zote ambazo ndugu zake Habyarimana wanaishi!? Rais Obama wa Marekani bado hajamtambua rais Uhuru Kenyatta, lakini ikumbukwe kwamba ndugu zake rais Obama wanaishi kwenye kijiji cha Lugelo kule Kisumu na rais Kenyatta hana mpango wa kugombana na ukoo wa kina Obama kwa vile ndugu yao hajaitambua Serikali yake! Kulingana na utafiti wangu nimegundua kwamba tangu rais Kikwete ahutubie maadhimisho ya sikukuu ya mashujaa kule mkoani Kagera mwaka huu, kumekuwa na mikakati ya chini kwa chini ya kiintelejensia ya kutengeneza mazingira ya kivita kati ya Tanzania na Rwanda! Magazeti yetu yanavyoripoti siyo sawa na hali halisi ya mahusiano kati ya marais Kagame na Kikwete yalivyo, bali kumekuwa na hali fulani ya kuongeza chumvi kwa maana ya kujenga mvutano kati ya viongozi hawa wawili wa nchi jirani. Kutofautiana kwa maneno kati ya Kikwete na Kagame hakuwezi kuzipileka nchi hizi vitani! Itakuwa ni fikra za kijinga na wananchi wa pande zote mbili hawatakubali wapelekwe vitani kwa mambo ya kipuuzi na yenye mwelekeo wa ubinafsi usiolenga maslahi ya umma! Tukumbuke mwaka 1978 wakati Nyerere anaipeleka nchi hii vitani uchumi wa Tanzania ulikuwa mzuri dollar moja ya Kimarekani ilikuwa inabadilishwa kwa Shillingi tano (5/=) za Kitanzania! Leo hii dollar moja ya Kimarekani inabadilishwa kwa Shillingi 1700 za Kitanzania! Hii yote ni matunda ya vita ya Uganda na Tanzania, vita ambayo ilikuwa haina sababu zozote za kimsingi kufanyika! Majeraha mengi ya vita hii bado hayajapona: wananchi wengi wa mkoa wa Kagera wameachwa masikini, wameachwa wakiwa, wameachwa wajane na bado Serikali haijawafidia kwa kutumia ardhi yao kama uwanja wa mapambano! Kabla Serikali haijatatua matatizo yaliyosababishwa na vita iliyopiganwa miaka 35 iliyopita, leo hii Serikali hiyo hiyo inatafuta vita nyingine, tena vita ya kijinga ambayo haina mbele wala nyuma! Ukienda vitani lazima uende vitani kwa madhumuni ya kufaidika kiuchumi hasa kwa vile tunatafuta vita ya nchi jirani; sasa tujiulize tukipigana na Rwanda tutapata faida gani za kiuchumi katika nchi hiyo? Rwanda ni nchi masikini kuliko Tanzania licha ya kwamba wana gesi asilia nyingi kuliko sisi, lakini je, tunafuata gesi asilia huko Rwanda au tunataka kuitumia vita ya Rwanda kama kisingizio cha kukwepa shindikizo la kisiasa linalotukabili hapa nchini!? Kama tunataka kwenda vitani kwa kisingizio cha Gorilla wa Rwanda hata hapa nchini tuna mbuga ya hifadhi ya Gombe ambayo ina Gorilla wengi na imetushinda kuimudu kiasi kwamba Gorilla wanauwawa ovyo na majangili! Pia tusijiandae kwenda vitani na Rwanda kwa kisingizio cha kwa kwamba eti Serikali ya Rwanda imekasirika kwa vile Tanzania imepeleka majeshi yake nchini DRC kupambana na waasi wa M23! Mpango wa kupeleka majeshi DRC siyo mpango wa Serikali ya Tanzania, hapana, huu ni mpango wa umoja wa mataifa (UN) ambao unaungwa mkono na mataifa yote makubwa duniani, na siyo Tanzania peke yake iliyopeleka majeshi yake huko DRC, hapana, ni nchi nyingi ambazo zimepeleka majeshi yao huko DRC ikiwemo South Africa. Rwanda hawawezi kuwa na chuki na Tanzania kuwa na majeshi yake huko wakati kuna nchi nyingi za Kiafrika ambazo nazo zina majeshi yao huko DRC! Kama ni chuki basi Rwanda ilitakiwa iichukie UN na Marekani ambao hasa ndiyo wabunifu wa mpango huo! Chama cha mapinduzi (CCM) kimepoteza umaarufu wake kwa kiasi kikubwa mbele ya jamii ya Watanzania, na kulingana na hali hiyo chama hiki hakiwezi kushinda uchaguzi wowote wa ukweli na uhuru wa kupiga kura katika jimbo lolote la uchaguzi hapa nchini; matumaini makubwa ya chama hiki yanabakia kwa vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo siku zote vimekuwa vikikiuka taratibu na sheria za nchi kwa kukipendelea chama cha CCM kwenye chaguzi mbalimbali kwa kukisaidia kuchakachua matokeo ya uchaguzi ili kiweze kuendelea kuwapo madarakani! Kulingana na mwamko wa kisiasa hapa nchini kuanzia mijini hadi kule vijijini, mbinu zote zinazotumiwa na vyombo vya ulinzi na usalama katika mikakati ya kuchakachua matokeo ya uchaguzi zimeshajulikana kwa wananchi wengi wenye mwamko na mambo ya siasa za hapa nyumbani. Kulingana na hali hiyo Serikali ya CCM imekuwa haitaki mabadiliko ya katiba mpya, katiba ambayo imekuwa ikikipendelea chama hicho kwa miaka yote tangu tuanzishe mfumo wa vyama vingi hapa nchini mwaka 1992. Marekebisho ya katiba hii mpya yanatarajiwa kutumika katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015; uchaguzi ambao pia chama cha mapinduzi (CCM) hakiutaki kabisa uchaguzi huo na kama ingelikuwa ni amri yao wangeliufuta uchaguzi huo usifanyike kabisa; CCM hawautaki uchaguzi huo kwa vile wanafahamu fika uchaguzi huo ukifanyika ndiyo mwisho wa chama hicho; mwisho wa chama hicho kwa vile hakitashinda uchaguzi mkuu ujao na kitashindwa vibaya na vyama vya upinzani ambavyo vitajinyakulia majimbo malimbali yaliyokuwa yakimilikiwa na madiwani na wabunge wa CCM na pia wapinzani watakinyakua kiti cha urais tena kiulaini kabisa! CCM inapotafakari hali hali ya kisiasa hapa nchi inapata kiwewe na ndiyo maana imekuwa ikiwatafutia viongozi wa kitaifa wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) kesi mbalimbali zikiwemo za ugaidi, uchochezi na zinginezo ili mradi tu waangalie ni namna gani wanaweza kuwadhibiti viongozi hawa ambao wanaonekana kukubalika sana mbele ya jamii ya Kitanzania hivi sasa! Visingizio vyote vya kesi za kupangwa za ugaidi, uchochezi na zile za kumaliza mikutano muda usiopangwa zimeonekana hazitainusuru CCM kupoteza kiti chake hicho cha enzi ambacho imekikalia kwa zaidi ya miaka 52 sasa, hivyo nafasi pekee inayoweza kuinusuru CCM isiondolewe madarakani ni VITA ya RWANDA na TANZANIA kama nchi hizi zikienda vitani, basi uchaguzi hautakuwepo tena hapo 2015 na rais Kikwete ataendelea kuwa madarakani mpaka hapo hali itakapokuwa nzuri!! Mnakumbuka wabunge wawili wanaowania nafasi ya urais kupitia chama cha mapinduzi (CCM) mbunge wa Monduli Edward Ngoyai Lowasa na Mbunge wa Mtama Bernard Kamillius Membe waliwahi kutangaza kwamba wapo tayari kupigana na Malawi na wakijisifu kwamba tuna majeshi imara na tumejiandaa vya kutosha! Pamoja na kwamba maneno haya yalitamkwa na wabunge hawa wawili lakini maneno haya yalikuwa siyo maneno yao, bali yalikuwa ni maneno ya Kiintelejesia ambayo ipo nyuma ya wabunge hawa wawili kama washauri wao wakuu! Na baada ya hapo tumesikia taarifa mbalimbali za uongo zikidai kwamba majeshi ya Malawi yamerusha mabomu kwenye ardhi yetu! Mara tukasikia mbunge mmoja ambaye ni shabiki mkubwa wa Lowasa akisema ameziona manowari za Malawi zikiwa ndani ya maji yetu! Kwanza mbunge huyu ni mbumbumbu kwa vile ziwa hilo ni mali ya Malawi, hata wananchi wa Tanzania wanaochota maji na kuvua samaki kwenye ziwa hilo wanaonewa huruma tu na Serikali ya Malawi! Sasa iweje mbunge mzima atoe kauli tata kwamba eti meli za Malawi zimeonekana upande wa Tanzania!? Yote hii ni mikakati ya kuinusuru CCM isishindwe kwa vile haijawahi na wala haikuzoea kushindwa, hivyo kilichokuwa kinatafutwa au kinachoendelea kutafutwa ni kuvuruga hali ya kisiasa na kiuchumi kwa muda usiojulikana hasa kwa kipindi hiki tunapojiandaa na uchaguzi mkuu wa 2015 kwa makusudi ya kuinusuru CCM! Wakati Nyerere anaipeleka nchi hii vitani alitumia strategy ya kuivamia Uganda kwa muda mfupi na kutoka, na Idd Amin alipoingia ndani ya ardhi yetu kwa makusudi ya kuwafukuza wavamizi Nyerere akaanza kupiga makelele kwamba amevamiwa! Sasa sitashangaa kabisa hasa kwa vile Intelejensia ya Nyerere ndiyo hii hii ya Kikwete kama itakuja na sababu kwamba majeshi ya Rwanda yamevamia nchi yetu! Majeshi yetu yanaweza kufanya kama vile tulivyofanya kule nchini Uganda mwaka 1978 na majeshi ya Rwanda yatakapofanya kama alivyofanya Idd Amin basi tunaweza kuanza kupiga makelele kwamba tumevamiwa!!! Kikwete amebakiza miaka miwili tu akamilishe muda wake wa miaka mitano ya kipindi chake cha pili na miaka kumi ya kukaa Ikulu; katika kipindi chake cha pili Kikwete aliahidi ahadi nyingi mno na hadi hivi sasa bado hajatekeleza hata 5% ya ahadi zake kwa wananchi! Sasa jambo la kushangaza muda uliobakia ni mdogo sana, badala ya kujitahidi kukamilisha ahadi zake kwa wananchi Serikali yake ipo mbioni kutafuta chokochoko na nchi ya jirani ya Rwanda! Serikali imefilisika haina pesa ya kuwaongeza walimu mishahara, haina pesa ya kuwaongeza madaktari mishahara, Serikali haina pesa za kuwakopesha wanafunzi wasome vyuo vikuu, Serikali haina pesa za kuajiri wafanyikazi wapya! Lakini Serikali ina uwezo na ipo tayari kupigana na Rwanda na Malawi!!!! Kikwete mwaka 2005 aliwaahidi Watanzania kwamba ataleta maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini cha kushangaza hakuna chochote wala lolote linalofanana na maisha bora, bali wananchi wamezidi kuwa masikini na huku watawala wetu wameweza kujilimbikizia utajiri wa kutisha ndani na nje ya nchi!!! Je, vita na Rwanda ndiyo itakayotatua matatizo ya uchumi wa Watanzania au ndiyo itazidi kuwaongezea umasikini..!!!!!???? Mwishi kabisa nasema ugomvi wa Kagame na Kikwete tuwaachie wao wenyewe wakikutana huko Addis Ababa – Ethiopia wataamua wenyewe kama wanakaa meza moja na kumaliza tofauti zao au wanaendelea kununiana! Sisi wasituhishe kabisa na ugomvi wao, na tena wasivihusishe vyombo vyetu vya umma vya ulinzi na usalama! Pia napenda kuijulisha CCM kwamba ukizaliwa lazima utakufa, hivyo muda wa kuishi wa CCM umekwisha na lazima ife ipende isipenda! Hata Nyerere alikufa kwa vile umri wake wa kuishi ulishafika! Ni jambo la kijinga na ni upumbavu mkubwa kama unataka tu kuishi, lakini hutaki kufa! Haiwezekani! Mungu ameumba uhai na kifo kwa wakati mmoja hivyo binadamu kufurahia uhai bila kifo ni ujinga mtupu! Nawaombeni wana CCM wote na vyombo venu vya ulinzi na usalama kwa pamoja mkae mkijua kwamba kila chenye uhai kina siku yake ya kufa, hivyo siku ya kifo cha CCM inakaribia, isitake ife na kila mtu hata na watoto wadogo kama akina CHADEMA ambao wamezaliwa majuzi tu! CCM kufanya hivyo si uungwana na haikubaliki hata kwa mungu, kwamba siku zako zikifika za kufa hutaki kufa peke yako bali unataka ufe na watu wote wanaokuzunguka! Hata hivyo CCM kina umri mkubwa usiopungua miaka 60 tukizingatia kwamba hata TANU ni CCM. Ndiyo maana nasema kwamba Intelejensia ya Tanzania inaitafuta vita ya Rwanda na Tanzania kwa Ubani na Uvumba ili nradi tu wainusuru CCM iendelee kutawala, potelea mbali hata wananchi wengi wakipoteza maisha yao au uchumi ukiporomoja jambo muhimu CCM iwepo madarakani na wao waendelee kutesa..!! noordinjella.livejournal
Posted on: Thu, 29 Aug 2013 19:00:28 +0000

Trending Topics



they put in the Pass
Insta News Cabinet nod for Kota nuclear fuel
I went to had an eye test just this morning . My eyes was almost

Recently Viewed Topics




© 2015