Jaji Franscis Mutungi Hatakuwa na Tofauti Sana na John Tendwa - TopicsExpress



          

Jaji Franscis Mutungi Hatakuwa na Tofauti Sana na John Tendwa Kiutendaji..!! Pamoja na kwamba watanzania wengi wameshabikia uteuzi wa Jaji Franscis Mutungi kuchukuwa nafasi iliyoachwa wazi na John Tendwa ya msajili wa vyama vya siasa, lakini mimi naamini kwamba Mutungi hatatofautiana sana na Tendwa kiutendaji pamoja na kwamba ni jaji! Nasema hivyo kwa kujiamini kwa vile nafahamu ni jinsi gani na hasa ni akina nani wanaoteuwa wafanyikazi mbalimbali hapa nchini; na pia nafahamu ni akina nani wanaokwamisha watu kupandishwa vyeo na hata kufukuzwa kazi hapa nchini! Ukiyajua yote hayo kwa undani na kuyafanyia uchambuzi wa kina utakubaliana na mimi kwamba Jaji Franscis Mutungi hatakuwa na jipya zaidi ya kuipendelea CCM! Nikilithibitisha hili ni kwamba kwanza tukumbuke ni akina nani wana dhamana ya kuchagua viongozi hapa nchi au ni akina nani ambao wanachaguliwa viongozi hapa nchini? Nikilijibu maswali haya ni kwamba kulingana na utaratibu uliowekwa na mwasisi wa taifa hili ambaye ni Mwalimu Nyerere viongozi wote wa Serikali na mashirika, makampuni na taasisi zote za Serikali ni lazima watoke aidha kwenye kitengo cha usalama wa taifa (TISS) au waidhinishwe na kitengo hicho kwamba wanakidhi matakwa ya kitengo cha usalama wa taifa (TISS)! Hivyo basi kulingana na ukweli huo ni kwamba Jaji Mutungi aidha ni mwanakitengo wa TISS au ni jaji mtiifu wa kitengo cha TISS! Haiwezekani upate upendeleo wa rais (Presidential appointment) halafu uwe siyo aidha mwanakitengo au mtiifu wa kitengo hicho. Tanzania ni nchi ya kikomunist na kama ilivyo kote duniani nchi za kikomunist ni nchi zinaongozwa na kitengo cha usalama wa taifa hakuna idara imbayo ipo huru mbele ya usalama wa taifa haya mateso wananchi wanayoyapata toka jeshi la polisi na JWTZ hayatokei kwa bahati mbaya hapana, ni mambo yanayopangwa na kitengo cha usalama wa taifa ila watekelezaji ni wengine na hawawezi kukataa kwa vile kitengo hiki kipo ndani ya ofisi ya rais na wanapotoa amri hutoa kwa niaba ya rais! Ndiyo maana mnaona matukio mengi ya kutisha yametokea dhidi ya raia wasiokuwa na hatia, lakini pamoja na wananchi kulalamika kwamba wahusika ni vyombo vya ulinzi na usalama, hakuna kilichobadilika kwa vile hizi ni amri toka kwa mwenye nchi na mnayemlalamikia ni mwenye nchi, hivyo hawezi kwenda kinyume na kauli zake! Nikirudi kwenye uteuzi wa Jaji Mutungi ni kwamba kama alivyokuwa John Tendwa ndivyo atakavyokuwa Jaji Mutungi kwa vile watoaji amri ni wale wale TISS bado hawajabadilika; kilichobadilika tu ni mtekelezaji wa amri za TISS lakini amri ni zile zile za kuibeba CCM isiondoke madarakani kwa vile ndicho chama kinachopendelea watawala na wale waliokuwa karibu nao! Kwanza tukichunguze kitengo hiki cha usalama wa taifa (TISS) ambacho ndicho kilichompelekea jina rais Kikwete kwamba Jaji Mtungi anafaa kuwa msajili wa vyama vya siasa! Je, TISS wapo kwa ajili ya watanzania au wapo kwa ajili yao na watawala wa CCM? Je, ni matukio mangapi ya kutisha ambayo kitengo hiki cha TISS wamehusishwa moja kwa moja na rais ameshindwa kuwachukulia hatua za kisheria? Je, si mnakumbuka hivi majuzi waziri Mark Mwandosya aliwakingia kifua TISS wasijadiliwe bungeni kwa vile ni majasusi? Je, kuwateka raia na kuwatesa huo ndiyo ujasusi? Pia kitengo hiki kimekuwa kikishutumiwa mara nyingi kwamba kimekuwa kikichakachua matokeo ya viongozi wa umma kwa kuipendelea CCM! Kitengo hiki kimekuwa hakivipendi na wala hakivitambui kabisa vyama vya upinzani, hasa vile ambavyo vinaonekana kukataa kutumiwa aidha na CCM au na TISS yenyewe kwa manufaa ya CCM! Na hali hiyo imesababisha vyama vya upinzani kupelekewa wanachama wengi ambao wote ni wanakitengo kwa makusudi ya kuvidhoofisha vyama hivi kwa manufaa ya CCM! Na wanakitengo hawa wanaanzia ngazi za shina hadi ngazi ya taifa na wengi wamejipendekeza mpaka wamefanikiwa kuwa viongozi wa vyama hivi; na wengine wamefanikiwa mpaka kupata udiwani, ubunge wa kuchaguliwa na wengine ubunge wa viti maalumu! Kuna wengine wanaandaliwa na TISS kuwa marais wa Tanzania lakini hata umri wao bado hivyo mikakati inawekwa ili katiba ipunguze muda wa kugombea urais ili mradi mamluku wao waweze kuvihujumu vyama vya upinzani kwa manufaa ya CCM! Wengine hata baba zao wamejitokeza kwenye magazeti wakidai kwamba wakati wa watoto wao kuwa marais umefika! Je, ni mzazi gani asiyependa mwanawe awe rais wa nchi!? Je, kuwa rais wa nchi ni uamuzi wa baba yako au ni uamuzi wa watanzania!? Je, uwezo wa mtu kuliongoza taifa unasababishwa na mbunge kufukuzwa bungeni na baadae kurubuniwa na TISS na kuitumikia CCM ndani ya kambi ya upinzani? Je, uwezo wa kuongoza nchi unatokana na kushabikiwa na vyombo vya habari ambavyo vinadhibitiwa na hata vingine kumilikiwa na kitengo cha usalama wa taifa (TISS)!? Kuwa mbunge haina maana kwamba unaweza kuwa rais, tena mbunge mwenyewe wa kufundishwa cha kuongea na TISS! Mnamkumbuka vizuri kwamba Kikwete yule wa mwaka 2005 siyo Kikwete huyu wa 2013! Hawa ni watu wawili tofauti hasa tukizingatia umaarufu wao; Kikwete yule wa 2005 alitengenezewa sifa za kupaa kwa Roketi ya Apolo 11 ya kwenda mwezini na sifa hizo alitengezewa na kile kitengo kinachochagua viongozi ambacho ni TISS! Walimpamba Kikwete kwa kila sifa iliyowezekana kwa makusudi makubwa ya kuwafikisha watanzania hapa walipofika, hasa kwa vile walikuwa wanamjua Kikwete kwa undani na upana zaidi! Umaarufu wa Kikwete wa sasa hivi una mwendo sawa na ile baiskeli ya Kihindi ya miguu mitatu kwa jina maarufu GUTTA ambayo hata mwendo wake unategemea injini kiuno! Ni kitengo hicho hicho cha TISS ambacho sasa hivi ndani ya CCM kimemchagua mbunge wa Monduli Edward Lowasa na kimekuwa kikimjengea sifa za kila aina kuwa Lowasa ni mchapa kazi; Lowasa ni dikteta na nchi hii hapa ilipofikia inahitaji eti rais Dikteta! Je, Lowasa ni mchapa kazi wa wapi? Je, ni mchapa kazi wa hapa Tanzania au ni mchapa kazi wa huko nchi za nje? Kama ni hapa Tanzania amefanya nini kizuri kwa watanzania? Kama ni shule za kata mbona zimeshindwa! Huwezi kuwa kiongozi wa kitaifa kwa miaka 40 halafu tukudhamini kwa mradi mmoja mdogo na ambao umeshindwa! Kama ni tatizo la ajira kwa vijana alishapiga makelele sana na mwishowe akatuambia anajivunia Boda-Boda ni ubunifu wa sera za CCM! Je, udikteta wa Lowasa unalenga nini? Unalenga maslahi ya binafsi au unalenga maslahi ya umma? Kama Lowasa ana hulka za akina Hugo Chaves au Thomas Sankara basi udikteta wake utakuwa wa manufaa kwa watanzania! Ikumbukwe kwamba Captain Thomas Sankara aliuwawa kwa kuwapigania wanyonge wa Burkina Faso na wakati anakufa licha ya kwamba alikuwa rais wa nchi hiyo lakini kwenye akauni yake ya benk alikuwa kiasi cha US $ 1,000 sawa na shilingi za kitanzania milioni moja na laki sita (Tsh. 1,600,000), na alikuwa na sare za kijeshi pair mbili na buti za kijeshi pair mbili basi! Pia ningependa kukikumbusha kitengo cha usalama wa taifa (TISS) kwamba hapa nchi ilipofikia wao ndiyo waliochangia kwa asilimia tisini na nane (98%) na hiyo asilimia mbili (2%) iliyobakia imechangiwa na wananchi wenyewe, hivyo kwa matokeo hayo wanatakiwa waelewe kwamba uongozi wao kwa taifa hauna manufaa yoyote au kwa maneno mengine twaweza kusema TISS kimegeuka madhara na janga kubwa kwa taifa (Menace for society) hili! Hivi karibuni makamu wa mwenyekiti wa CCM Mzee Philip Mangula amekaririwa akisema kwamba kujadili mambo ya TISS hadharani ni makosa! Mangula anawafanya watanzania kwamba ni wajinga wasioona na kujua kazi na malengo makubwa ya TISS! Watanzania wameshaamka usingizini na wanafahamu fika kwamba TISS haipo kwa ajili ya umma, bali ipo kwa ajili ya kuilinda CCM na wale wote wanaoshabikia chama hicho, hivyo kwa sababu hizo kuijadili TISS hadharani ni kitendo cha kizalendo kwa manufaa ya umma. Vitengo vya usalama wa taifa kama vile CIA, M16 na Mossad kazi zake hazijadiliwi hadharani kwa vile wanafanya kazi za KIJASUSI kwa manufaa ya mataifa yao, lakini vitengo hivi haviteki watu nyara na kuwatesa, havishabikii siasa za chama chochote wala kuchakachua matokeo ya uchaguzi, pia havilindi maslahi ya watawala na kushirikiana na watawala katika zoezi zima la kuangamiza na kuhamisha rasimali za nchi kinyume cha sheria kama ilivyo hapa kwetu Tanzania! Philip Mangula ana siri kubwa moyoni mwake tena anajua kwamba TISS ndiyo roho, kichwa, miguu, mikono na kiwiliwili cha CCM, na CCM yenyewe imebakia na mdomo mrefu wa kupiga Tararira za kuzungumza tu yale yote yanayobuniwa na kitengo hiki! Watanzania msimshangae Nchemba Mwingula kwa vile hayo anayoyasema si akili yake, bali hiyo ndiyo akili ya kitengo chenu cha TISS! Nimekuwa nikiandika mara kwa mara kwamba bila ya kukiondoa kitengo cha usalama wa taifa (TISS) katika ofisi ya rais hakuna idara yoyote itakayokuwa huru katika nchi hii hata kama tukawa na katiba nzuri kiasi gani! Idara zote za Serikali na mashirika ya umma yataendelea kuwa watumwa wa TISS na watakuwa wanatekeleza yale yote yanabuniwa na kuamriwa na TISS bila ya kujali kwamba hayo yanayomuriwa kutendeka yana maslahi ya umma au binafsi! Jambo muhimu ni kutekeleza yale yanayoagizwa na kitengo hiki cha TISS bila ya kuhoji wala kupinga! Na kitengo hiki kinajua kwamba chama cha siasa hapa nchini ni kimoja tu nacho ni CCM! Na yeyote anaipinga au anayesababisha CCM kushindwa kuendelea kuongoza nchi hii ni adui wa taifa na anastahili kutendewa lolote liwezekanalo ili mradi kuinusuru CCM! Kulingana na ukweli huo hapo juu msitegemee lolote la maana kutoka kwa Jaji Mutungi zaidi ya kuipendelea CCM kama alivyokuwa anafanya John Tendwa; isipokuwa Jaji Mutungi atakuja kwa staili tofauti kidogo na ile ya mtangulizi wake; Mtungi anaweza kuja na kutoa tamko kwamba vyama vya siasda visiwe na vikosi vya ulinzi (Green guard; Red Brigade; Blue Guard n.k. ), lakini ni lazima tufahamu kwamba akisema hivyo atakuwa anawadanganya wapinzani (danganya toto) kwa vile CCM miaka yote imekuwa ikilindwa na kupendelewa na vyombo vya ulinzi na usalama (TISS, JWTZ, Polisi) majeshi yote haya ya dola bila aibu na bila kujali yamekuwa yakilinda na kupigania haki na dhuluma za CCM kwa gharama zozote zile, hivyo Jaji Mutungi akija na sera ya kuwakataza Chadema wasiendelee na mpango wao wa kuimarisha kikosi chao cha Red Brigade atakuwa anawadanyanya kwa kuwahadaa kwamba vyombo vya dola vya ulinzi na usalama vitalinda maslahi ya vyama vyote, kitu ambacho hakitawezekana hata siku moja! Jaji Mutungi akae akijua kwamba akiendeleza sera za Tendwa itabidi kampuni zote za ulinzi hapa nchini zifutwe na kazi walizokuwa wanazifanya kampuni hizo zichukuliwe na jeshi la polisi; kwa vile haiwezekani mtu binafsi au kampuni iwe na vikosi vya ulinzi lakini chama cha wananchi kikatazwe kuwa na vikosi vya ulinzi! Je, jeshi la polisi litakuwa na askari wa kutosha kulinda hadi majumbani mwa watu!? Hivyo nawatahadharisha watanzania wenzangu mnaopenda kutetea haki katika nchi hii, mkae mkisubiri kauli atakayokuja nayo Jaji Mutungi, akija na kauli ya kuvifuta vikosi vya ulinzi vya vyama vya siasa, lazima mjue kwamba utendaji wake ni ule ule wa kupangiwa aseme nini kama alivyokuwa John Tendwa ila tu amekuja kwa sura nyingine! Na kulingana na hali ilivyo ni kwamba John Tendwa amestaafishwa ili aje msajili mwingine atakayetoa kauli ambayo alitakiwa aitoe John Tendwa lakini hakufanya hivyo kwa wenye nchi waliona haina haja! Waliona haina haja si kwa vile kweli ilikuwa haina haja, bali walifanya hivyo kwa vile walijua watanzania ni watu wa kufuata amri na siyo watu wabishi wa kuhoji kwanini; kumbe watanzania wamebadilika hawataki tena kuburuzwa! Mwisho kabisa nawataarifu kwamba Jaji Mutungi hawezi kuacha kuipendelea CCM kwa vile waliomchagua wanaamini kwamba chama pekee cha siasa hapa nchini ni CCM, na Mutungi hawezi kwenda kinyume na imani hiyo kwa vile naye ni sehemu ya hao waliomchagua! Na kama atakuja na sera za kuvifuta vikundi vyote vya ulinzi vya vyama vya upinzani atakuwa hajawatendea haki wapinzani kwa vile pamoja na CCM kuwa na green guard lakini pia siku zote wamekuwa wakipendelewa na vyombo vya dola vya ulinzi na usalama (TISS, JWTZ na Polisi), hivyo hata kama green guard ikivunjwa kinyemela bado CCM wapo wa kuwapigania kwa hali na mali ambao ni vyombo vya ulizi na usalama vya dola, lakini je, wapinzania watapiganiwa na nani!? Hivyo namuomba Jaji Mutungi akae akijua kwamba watanzania wengi wameshaona nini anakusudia kukifanya, na hatushangaa akija na sera za kuendelea kuwabana wapinzani, kwa vile waliomustaafisha John Tendwa ndiyo hao hao walimteua yeye; na bila shaka John Tendwa na Jaji Mutungi wote wanatoka idara moja. Hivyo basi Mutungi anamrithi Tendwa kwa kuwa msemaji na mwakilishi wa TISS kwenye taasisi hiyo ya umma ya msajili wa vyama vya siasa. noordinjella.livejournal
Posted on: Fri, 16 Aug 2013 11:50:43 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015