.MTUME MUHAMMAD (swallallahu alaihi - TopicsExpress



          

.MTUME MUHAMMAD (swallallahu alaihi wasallam) ..SUNNA-SIYRAH.....RAHMA KWA WALIMWENGU SEHEMU YA KUMI NA TATU Kisa Cha Asw-Haabul Fiyl (Watu Wa Ndovu)Abraha Mhabashi aliyekuwa gavana wa Al Najashi katika nchi ya Yemen iliyokuwa ikitawaliwa na Ethiopia wakati ule alikuwa akiona wivu sana kila anapowaona waarabu wakienda kuhiji Al-Ka’abah, akaamua kujenga kanisa kubwa katika mji wa Sana-a na akawatak...a waarabu waache kwenda Makkah na badala yake wakahiji penye kanisa lake. Habari zilipomfikia mmoja katika watu wa kabila la bani Kinaanah, alighadhibika akaingia ndani ya kanisa hilo wakati wa usiku na kukipaka mavi kibla cha kanisa, jambo lililomghadhibisha sana Abraha aliyekusanya jeshi kubwa sana idadi yake askari wapatao elfu sitini pamoja na tembo ishirini na mbili yeye mwenyewe akiwa juu ya tembo mkubwa sana, na kuelekea nalo Makkah kwa ajili ya kuibomoa Al-Ka’abah. Alipowasili penye bonde la Muhsir baina ya Makkah na Muzdalifa (baina ya Muzdalifa na Mina), tembo alipiga magoti na kukataa kuendelea na safari ya kuelekea Makkah. Wakawa kila wanapomuelekeza kusini au kaskazini anainuka na kutembea, lakini wanapomuelekeza upande wa Makkah anakataa na kupiga magoti. Wakabaki katika hali hiyo mpaka pale Allaah Alipowapelekea ndege makundi kwa makundi, wakawapiga kwa mawe ya udongo unaounguza. Allaah Anasema: أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ. أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ. وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ. تَرْمِيهِم بِحِجَارَةٍ مِّن سِجِّيلٍ. فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَّأْكُولٍ “Je! Huoni jinsi Mola wako Alivyowafanya watu wenye ndovu? Je! Hakujaalia vitimbi vyao kuharibika. Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi Wakawapiga kwa mawe ya udongo wa kuchoma. Akawafanya kama majani yaliyoliwa (yakatapikwa)?”[25] Suratul Fiyl Ndege walikuwa wakiwajia kwa wingi makundi kwa makundi, mfano wa vijumba mshale au zuwarde, kila mmoja amebeba mawe matatu, moja mdomoni na mawili ameyabana mguuni ukubwa wa dengu, kila anayepigwa na jiwe mwili wake hukatika vipande vipande na kuangamia. Si wote waliopigwa na mawe hayo, walikuwemo walioachwa wakarudi mbio kuelekea makwao huku wakiangukiana. Lakini Abraha, Allaah Alimsalitishia maradhi yaliyosababisha makucha yake kukatika na kupukutika huku akirudi alikotoka, na alifariki alipowasili Sana-a mwili wake ukiwa mfano wa kuku aliyenyonyoka manyoa. Maquraysh walikimbilia sehemu mbali mbali mbondeni na juu ya vilele vya majabali wakihofia maisha yao, na hawakurudi majumbani mwao mpaka baada ya kutokea yaliyowatokea majeshi hayo. Tukio hili lilitokea mwezi wa Muharram karibu siku hamsini au hamsini na tano kabla ya kuzaliwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), muwafaka wa mwisho wa mwezi February au mwanzo wa mwezi wa March mwaka 571 baada ya Nabii ‘Iysa. Katika tafsiri ya Suratul Fiyl anasema Ibn Kathiyr: “Hii ni mojawapo ya neema za Allaah walizopewa Maquraysh baada ya kuwalinda na shari waliokuja nayo watu wa ndovu waliokuja wakiwa na azma ya kuibomoa Al-Ka’abah na kuiondoa isiwepo tena. Lakini Allaah Aliwaangamiza na kuwalazimisha waliobaki warudi wakiwa wameshindwa, juu ya kuwa walikuwa watu wanaofuata Dini ya Manasara na kwa wakati ule wao walikuwa bora kuliko Maquraysh waliokuwa wakiabudu Masanamu, lakini haya yalikuwa ni matayarisho ya kuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kwa sababu kauli nyingi zinasema kuwa katika mwaka ule alizaliwa.” Anaendelea kusema Ibn Kathiyr: “Kama kwamba uhakika wa mambo unasema; ‘Enyi Maquraysh hamkupata nusura hii juu ya Mahabashi kutokana na ubora wenu, bali kwa ajili ya kuilinda nyumba kongwe itakayopata heshima kwa kuzaliwa hivi karibuni kwa Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) mwisho wa Manabii.” Habari za tukio hili zilienea kila pembe ya ulimwengu wa wakati ule, na kwa vile Wahabashi walikuwa na uhusiano mzuri na Warumi, Waajemi waliokuwa wakiisubiri fursa nzuri kama hii wakaingia na kuiteka nchi ya Yemen kwa haraka sana, na dola mbili hizi (Persia na Rome) ndizo zilizokuwa dola kubwa za wakati ule, na wakati huo huo tukio hili la kuangamizwa kwa watu wa ndovu liliujulisha ulimwengu juu ya utukufu wa nyumba ile ya Allaah na kwamba Allaah ndiye aliyeitukuza na kuiadhimisha, na kwa ajili hiyo atakapotokea yeyote katika watu wake akasema kuwa yeye ni Mtume, basi tukio hilo linampa nguvu mtu huyo. Kwa hivyo ndani ya tukio hili mna hekima ya Allaah iliyojificha ya kuwapa ushindi washirikina dhidi ya watu wa imani kwa njia ya kimiujiza. ITAENDELEA....
Posted on: Wed, 18 Sep 2013 19:56:03 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015