RIWAYA: HATIA MTUNZI: GEORGE IRON SEHEMU YA THELATHINI NA - TopicsExpress



          

RIWAYA: HATIA MTUNZI: GEORGE IRON SEHEMU YA THELATHINI NA SABA Jibu lilipokuwa gumu huku akiwa bado kaduwaa, jibu la uhakika lilitolewa. Mmoja kati ya wanaume waliokuwa hapo chumbani akachomoa kitu mfano wa mti uliochongwa vyema. Lakini mbele kilikuwa ni kijicho cha aina yake. Bunduki!!!. Monica akaanza kutetemeka, jicho likafunguka hadi hatua ya mwisho. Sura zote zilikuwa katika hali ya ukatili. Dalili ya urafiki haikuwepo kabisa. “Yupo wapi hawara yako??” sauti kali ya kiume ilimuuliza mwanamama huyu. “Si…si..siju..i” alijiumauma wakati akijibu swali hilo. Kiganja kilichotua kwa nguvu katika uso wake mweupe kiliacha alama za vidole vitano katika paji la uso wake na kisha kufuatiwa na kilio kikali. “Shhhh!!!!!!!” Kidole cha shahada katikati ya mdomo wa John mapulu kilimnyamazisha Monica akabaki kulia kwa kwikwi. “Yupo wapi Adrian…..” safari hii John aliuliza kwa utulivu. Monica naye akajaribu kuulazimisha utulivu, lakini bado alikuwa anatetemeka. “Sijui alipo…ila alisema kuwa atakuja” alijaribu kuzungumza japo kwa kutetemeka. “Hujui eeh!!” alizungumza kwa sanifu John. Kisha akawaamuru Michael na Bruno kumchukua Monica. Kama walivyoambiwa palepale wakamtwaa mzegamzega na kuanza kutoka naye nje. “Michael mwache Bruno amchunge huyo we njoo huku” aliamuru John, Michael akatii. Monica akabaki katika mikono ya Bruno. Michael na John wakaanza kuikagua vyema nyumba kama kuna uwezekano wa mabaki yoyote yanayoweza kuwasaidia kujua wapi Adrian yupo. Hapakuwa na chochote cha ziada wakatoweka Kishindo kilichosikika kwa nje kikawaweka katika tahadhari kila mmoja akatoka akiwa ameiweka sawa silaha yake. Kitu kama furushi kilichomoza gizani, Michael akiwa ameitanguliza bunduki yake mbele alikimulika kwa tochi yenye mwangaza hafifu huku akikisogelea. John alikuwa anaelekea upande mwingine. “John!!” Michael aliita kwa sauti ya chini lakini iliyomfikia John. John hakuitika bali akarejea katika namna ya tahadhari kuu. Alipomfikia Michael alilitazama lile furushi, lilikuwa linapanda juu na kushuka chini. Halikuwa furushi bali alikuwa ni Monica mchumba wa Adrian akiwa amefungwa kamba vyema mikononi. “Bruno yuko wapi??” John aliuliza swali hilo, lakini aliamini kuwa hatapata jibu lolote kutoka kwa Michael kwani wote walikuwa wametokea ndani na walikuwa wamemwacha Bruno nje. Monica aliachwa hivyo hivyo akiwa amefungwa kamba. Michael na John wakaanza kumtafuta Bruno. “John!!!” Michael aliita, safari hii sauti ilikuwa ya juu mno. John akakurupuka kutoka alipokuwa akakimbilia sauti ilipotokea. Sasa kilikuwa ni kifurushi kingine lakini hiki cha sasa hakikuwa kikipanda na kushuka. Kilikuwa kimetulia tuli, huku kikiwa kina rangirangi nyekundu zisizokuwa rasmi. Kifurushi hiki kilifanana na jamaa yao na John , aliyeitwa Bruno. Walipokiita kwa jina hilo hakikuitika wala kutetemeka. Bruno alikuwa maiti!!!Kifua chake kilikuwa kimeruhusu risasi kupita katikati yake. Hofu ikatawala!!! John akapandwa na hasira. Akakitazama kifurushi kilichokwenda kwa jina la Monica. Akaiweka bunduki yake katika kiwambo cha kuzuia sauti. Akafyatua!!! Monica akaungana na Bruno katika safari hiyo!!!!! Michael na John wakatoweka. Huku wakiamini kuwa vita ndiyo imeanza. Kwa miungu yote aliyoiamini Michael alikuwa akiomba Joyce aendelee kuwa salama. John Mapulu yeye alikuwa akimlaani Adrian kwa kuianzisha vita hiyo. **** Adrian alikuwa kama anayekaribia kuchanganyikiwa, suala la Stallone kupoteza uhai akiwa katika kutekeleza alichomuagiza kulimtia katika hofu kuu. Aliamini alikuwa katika kuwindwa na muuaji, muuaji aliyeihalalisha roho ya Stallone kuingia peponi. Hata ule mpango wake wa kumvisha pete Monica aliuona kuwa ni batili sasa. Upesi upesi Adrian aliichukua simu yake na kuandika ujumbe mfupi wa kuhairisha shughuli hiyo kisha akautuma kwa wahusika wote. Baada ya zoezi hilo akaamua kuizima simu yake huku akiweka namba ambayo ni Monica na watu wengine wachache muhimu waliokuwa wanaitambua. Baada ya hapo aliingia katika mgahawa mmoja akaagiza kinywaji chenye kilevi. Alifanya hivyo kwa kurudia chupa hadi zikafike nne, alikuwa anakunywa kwa mfumo wa kupiga tarumbeta, hakutumia glasi iliyowekwa mbele yake. Mfululizo huu uliendelea hadi alipoanza kuona glasi iliyokuwa mezani ikizaa nyingine na kuwa mbili. Mara miujiza mingine na meza zikawa mbili na hata wahudumu wakaanza kuja wawili wawili kumuhudumia. Adrian akatabasamu!!! “We malaya..kuna vyumba hapo.” Aliuliza kwa sauti ya kilevi. “Vipo shilingi elfu kumi na tano!.” Alijibu yule mwanamke bila kujali alikuwa ametukanwa kabla ya kuulizwa. Hata kama angekataa kutoa huduma, angekuja mwingine angeitwa jina hilo hilo na angetoa huduma kama kawaida bila kinyongo. Akili ya Adrian bado ilikuwa na uwezo wa kufanya kazi. Akampatia yule msichana shilingi elfu ishirini kwa ajili ya chumba. Chumba kikalipiwa, chenchi haikurudishwa.Ningeitoa wapi kama ningekataa kuitwa malaya??? Alijiuliza yule muhudumu huku akiitia vyema katika pochi yake. Adrian alikuwa amejiweza kwa dozi ya pombe aliyojipatia kwani alipoingia tu alipitiwa na usingizi murua. Hakukumbuka hata kuvua viatu. Adrian alipoteza kumbukumbu majira ya saa tano asubuhi na sasa ilikuwa imetimu saa nne usiku, kumbukumbu zikarejea. Masaa kumi na mbili ya kuwa mbali na dunia. **** Suala la kumshirikisha kila jambo Michael Matha alianza kuliona kuwa ni la kipumbavu. Baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu akifikia maamuzi yake ya kimya kimya si Michael wala John aliyepatwa na wasiwasi baada ya Matha kuwaeleza kuwa hataweza kuandama nao kwenda kumuadabisha Adrian. Michael alisikitika sana kwani alijua ni kipi kinamsumbua Matha. Michael alidhani Matha anasumbuliwa na utata wa mimba yake, lakini haikuwa hivyo wakati huu. Matha alikuwa katika mgongano wa nafsi yake akijifikiria jinsi ya kumwokoa Adrian katika kifo kisichomuhusu hata kidogo. Baada ya kuhakikisha kuwa John na timu yake wametoweka, harakaharaka Matha alimpigia simu Adrian. Simu iliita mara ya kwanza haikupokelewa, mara ya pili ikapokelewa. Sauti ya Adrian ilisikika ikiwa imetawalia na uoga. Matha aliligundua hilo lakini hakumuuliza. “Adrian mambo vipi mpenzi wangu?” Matha alizungumza kwa utulivu huku akiwa amezibana pumzi zake asiweze kusikika kama anahema kwa kasi. “Matha...hebu ngoja kidogo nitakupigia baadaye.” Alijibu Adrian kisha akakata simu. Matha alitaka kuongezea neno lakini tayari simu ilikuwa imekatwa. Haraka haraka Matha akabonyeza tena kitufe ili ampigie Adrian. Hakuwa anapatikana tena na tayari ilikuwa saa tatu usiku!!!! Matha alichaganyikiwa, alijiuliza ni kipi kinamsibu Adrian huko alipo Wasiwasi wake ukawa kwamba Adrian anaweza akawa ameingia katika mikono hatari ya John Mapulu. Mwanaharakati huyu wa kike akaamua kucheza pata potea. Upesiupesi akavaa bukta ngumu na viatu vya michezo. Akabeba pochi yake ambayo kwa wanawake wa kawaida ungeweza kukuta wameweka vipodozi, kanga ya dharula, na simu zao. Lakini Matha hakuwa mwanamke wa kawaida sasa!!! Yeye alikuwa amehifadhi, visu viwili vyenye sumu kali katika ncha ya mbele. Bastola ndogo kabisa na unga unga mweupe usiokuwa kwa matumizi ya kawaida kwa watu wa kawaida. Kama mwanajeshi kamili aliyefuzu mafunzo kambini, Matha alilifunga geti akatoka nje. Giza lilikuwa nene lakini halikumtisha hata kidogo, ni yeye aliyelitisha giza hilo. Hatua kwa hatua, akakutana na dereva wa pikipiki. Akamsimamisha akapanda. Alivyokaa kwenye kiti, ile pensi yake ikapanda juu zaidi mapaja yakawa nje akafanana na wale machangudoa ambao huo ndio ulikuwa muda wao wa kutoka. “Wapi hiyo dada!!.” “Isamilo fasta.” Alijibu Matha. “Buku saba ipo hiyo.” Matha hakujibu kitu, pikipiki ikawashwa na kuanza kukata upepo kuitafuta Isamilo. “Niache hapahapa.” Matha walipoikaribia nyumba ya Adrian alimsihi mwendesha pikipiki. Naye akatii. Matha akatoa shilingi elfu kumi. “Nenda tu usijali.” Matha alimweleza yule mwenye pikipiki baada ya kumuona akihangaika kusaka chenchi. Dereva akashukuru akapanda pikipiki akatoweka kwa mwendo wa kawaida. Matha hakupiga hatua yoyote mbele badala yake alitulia tuli na kufanana na mti mkavu usio na matawi. Kuna jambo alikuwa analingojea. Tano...nne....tatu....mbili....puuu!! kilisikika kishindo kidogo, Matha akageuka na kutimua mbio kuelekea kishindo kilipotokea. Alijuakilichokuwa kinaendelea!!! Alimkuta yule mwendesha pikipiki akiugombania uhai wake, alikuwa amejikita kumkabili israeli ili asiweze kuondoka na roho yake. Lakini Israeli alikuwa yupo katika kushinda na aliyejua hayo alikuwa ni Matha mtoto wa Mwakipesile. Dereva hakujua kama alitoa shukurani yake ya mwisho duniani. Matha alikuwa ameandaa ile noti ya shilingi elfu kumi kwa ajili ya kuondoa uhai wa dereva huyu. Matha alikuwa na shida na pikipiki. Hakuwa na njia zaidi ya kuua. Mwendesha pikipiki akaiaga dunia na kuiacha pikipiki yake ikiwa hai. Matha akatoa ‘glovus’ akavaa mikononi. Akainyanyua pikipiki akaufunga mkoba wake kwa nyuma akakaa juu yake. Akaipiga stata ikaitika, akapepea nayo. Akafunga breki katika baa moja ambayo hadi wakati huo ilikwa haijafungwa bado. “Samahani babu..aah!! shkamoo.” Matha alitoa salamu zake. Mzee aliyekuwa na mvi lakini akionekana kuupenda bado ujana alijibu kinyonge. Huenda hakupenda kusalimiwa. Matha alimnyenyekea yule mzee ambaye alikuwa ni mlinzi katika baa ile. Akamsihi amlindie pikipiki yake kwa ujira maalumu. Yule mzee akachangamka. Akakubali biashara, Matha akapaki pikipiki yake ya wizi. Akampatia shilingi elfu tano kama kianzio cha biashara. Kisha akatoweka kwa mwendo wa kawaida kama asiyekuwa na haraka, alipofika katika uchochoro akaanza kutimua mbio. Aliupita ule mwili wa mwendesha pikipiki kwa kuuruka kama vile gogo. Bunduki mkononi, Matha akawa ananyata sasa. Macho yake makali yaliweza kung’amua baadhi ya vitu gizani. Alisubiri kwa muda na sasa alichokingojea alikiona. Alishuhudia, viwiliwili viwili vikiwa katika hali tofauti. Kimoja kilikuwa cha kiume kikiwa wima na kingine cha kike kikiwa katika mateso makali, kilikuwa kimefungwa kamba. Baadaye kidogo kiwiliwili cha kiume kikaanza kunyata kuelekea gizani, Matha naye alianza kunyata kwa kutembelea vidole. Hakuweza kusikika. Alipoweza kukiona kiwiliwili kile tena sasa kilikuwa kimemkaba koo mwanaume. Huyu alikuwa ni Adrian na kiwiliwili kiliitwa Bruno. Mwanga hafifu ulimuwezesha kutambua hilo. Matha alishukuru kwa kumkuta Adrian akiwa hai, sakata la kukabwa na Bruno hata halikumshtua. Aliiweka bastola yake sawasawa, huku akihakikisha kuwa ipo katika kiwambo cha kuzuia sauti. Matha alitabasamu baada ya kumwona Adrian akiwa ametulia tuli kwahofu. Ni hivyo alitaka iwe, ili aweze kuipata shabaha yake vyema. Bastola ilinyanyuliwa, kisha ikakohoa kimyakimya, kama vile gunia Bruno akatua chini. Akiwa hana taarifa yoyote Adrian, katika taharuki kubwa alipitiwa kwa kasi kama vile mwewe anavyonyakua kifaranga, alikuwa amezibwa mdomo huku akilazimishwa kukimbia. Hakuamini kwa yule ni Matha!!! Haukuwa muda wa kuulizana maswali wala kutoa majibu. Adrian alilazimika kufuata amri. Matha alimsihi Adrian amsubiri mahali kwa dakika mbili. Adrian akaulia Matha akatoweka. Mzee alikuwa ameanza kusinzia Matha alipofika pale. Matha alimshtua naye akashtuka huku akizuga kuwa alikuwa hajalala. Matha alitaka kumtokomeza naye duniani lakini huruma ikamshika. Akamsamehe. Akamwongeza elfu tano nyingine,biashara ikaishia hapo!!! Pikipiki ikafunga breki miguuni mwa Adrian. Akatoa ukelele wa hofu. “Panda!!!.” Sauti ya kike iliamrisha. Ady akapanda. Kwa kasi kubwa mwanadada akaindoa ile pikipiki kutoka eneo lile. Walipoufikia mji, Matha akasimamisha ile pikipiki eneo ambalo halikuwa na watu wengi. Adrian akashuka, wakaanza kuelekea mahali alipopajua Matha na halmashauri ya kichwa chake. Wakaitelekeza pikipiki. Wakaenda nyumba ya kulala wageni. Kila aliyewatazama alijua kuwa Adrian alikuwa ameopoa changudoa mshamba anayekubali kuingizwa gesti hovyo. Haikuwa kama walivyodhani.!!! **** ITAENDELEA KESHO
Posted on: Sat, 07 Sep 2013 09:08:50 +0000

Recently Viewed Topics




© 2015