RIWAYA: KIZUIZI MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU YA MWISHO - TopicsExpress



          

RIWAYA: KIZUIZI MTUNZI: George Iron Mosenya SEHEMU YA MWISHO PART 02 Ghafla akavamia na hisia nyingine ambazo ni za kustaajabisha sana. “Inawezekana kuwa hata mimba ni ya jamaa, sio ya kwangu?” alijiuliza kwa sauti ya juu. Hakujali Maalim anasikia ama vipi. “Emmy yupo wapi kwa sasa?” aliuliza hatimaye. “Wallah hatujafanya naye biashara zaidi. Hadi sasa ninamsubiri, hakuweza kufika sijui alipo, tazama meseji katika simu yangu nd’o zitanitetea mimi.” Alijieleza kwa kutetemeka Maalim. James akamuamini baada ya kuzisoma meseji za makubaliano kati yao. James akatoweka bila kuaga. Maalim hakuamini kama amebaki hai kwa usali mkubwa alioufanya kwa James. Wazo la kuukimbia mji pakikucha lilimvamia. Akaamua kuondoka alfajiri sana. **** Wazee wawili walikuwa wanajadiliana jambo kwa kina. Umri wao uliendana sana na walionekana kushibana vilivyo. Mbele yao palikuwa na jagi la maji. Wote walikuwa wamevaa kanzu nyeupe na vibalaghashia huku mmoja akiwa na tasbihi akihesabu wakati mazungumzo yanaendelea. Mzee Ndula alikuwa haamini kama kitendo cha mtoto wake Said kujiingiza katika kufuatilia kesi iliyopita muda mrefu ndiyo ilikuwa tiketi yake ya kwenda akhera. “Mwanajeshi amemuua kijana wetu mzee Sadiki..hili si jambo la kunyamazia. Kesho tunamzika mi sitakubali lipite hivihivi.” Alizungumza kwa sauti ya chini, bwana Sadiki akatikisa kichwa kuashiria kukubaliana naye. Licha ya wazee hawa kulingana kiumri lakini kuna heshima kubwa kati yao. Mzee Ndula ndiye alikuwa mshenga wa Sadiki alipokuwa anataka kumchumbia mkewe wa sasa ambaye amezaa naye watoto wengi. Hivyo palikuwa na udugu kati yao zaidi ya urafiki. Uzuri wote walikuwa katika jeshi. Japo Sadiki alikuwa amestaafu tayari, lakini alitumikia jeshi kimya kimya. Bwana Sadiki aliahidi kushirikiana na Ndula bega kwa bega kuhakikisha huyo muuaji anapatikana na ikiwezekana kuadabishwa. “Nadhani unafahamu golgota ya nyumbani kwangu, labda asipatikane maana atajuta kuzaliwa, hakuna jasiri mbele ya pango lile.” Bwana Sadiki alijisifu, mzee Ndula naye akamuunga mkono. Jioni mzee Sadiki aliaga na kuondoka kwa minajiri ya kurejea tena baadaye. Sauti ngeni zilimpokea, alisikia mazungumzo ya tofauti katika nyumba yake. Akajihakikishia kuwa kuna mtu aidha amekuja kumtembelea ama ni mgeni kutoka kijijini. Bwana Sadiki akajikongoja hadi ndani. Akatabasamu baada ya kumtambua mgeni wake. “Dume la simba...lisilotetereka.” alitoa sifa kemkem. Mgeni akafanya tabasamu hafifu. Akasimama na kumwendea mzee Sadiki akamkumbatia. **** Lameck, baada ya kufanya dhahama ya aina yake kwa kumtengua Mpelelezi Said Ndula, na kumpoteza kifahamu mwanadada Emmy alitokomea kuelekea katika vijiji vilivyopo jirani. Alidumu katika vijiji akizunguka hapa na pale hadi kigiza kilipotanda. Akafanya safari ya kwenda barabarani kisha akarukia gari inayoelekea Morogoro mjini. Majira ya saa tatu usiku alikuwa katika nyumba za kulala wageni. Akalipia chumba. Chumba kilikuwa na luninga. Taarifa ya habari ya saa nne usiku ilimkuta akiwa anatokea bafuni kujisafisha mwili. Taarifa nzito ilikuwa juu ya mauaji katika kijiji cha Mikese. Mwanajeshi aliyeua na kujeruhi. Taarifa hii ilielezewa kwa urefu na ilikuwa na mashiko haswaa. Lameck alijikaza kijeshijeshi asijionyeshe kuwa ameshtuka sana. Lakini aliukosa usingizi. Aliamini kuwa baada ya muda sura yake itazagaa katika pande zote za nchi na huo utakua Mwanzo wa kuikosa amani. Lameck akaamua kufikiri kiume. Akamkumbuka Mwanajeshi mstaafu ambaye ndiye aliyemshawishi hadi kuingia jeshini. Akaamua kumchagua kuwa mshauri wake mkuu. Alimuamini sana tangu mwanzo wa kufahamiana kwao. Anakumbuka hata siku alipokuwa anampa kichapo Jose B alilitumia golgota la mzee Sadiki kumpa dawa yake kijana huyo ambaye alijikuta akisema kila kitu. Mzee Sadiki na golgota yake ni hatari. Alikiri Lameck. Usiku huo ukapita, siku iliyofuata kabla habari hazijatapakaa sana. Lameck akarejea jijini Dar, akaenda moja kwa moja nyumbani kwa mzee Sadiki. Mavazi aliyoyavaa hata wangeitangaza sura yake ilikuwa ngumu sana kumtambua. Alikuwa tofauti sana lakini mzee Sadiki alimtambua alipofika. Lameck akasimama akamkumbatia mzee Sadiki kisha akampigia saluti ya heshima. Lakini tatizo lilikuwa moja tu. Lameck hakuwa na furaha na mzee Sadiki hakuwa na raha. Wakati Lameck anawaza atajinasua vipi kutoka katika kashfa ya mauaji, mzee Sadiki alikuwa anawaza atalipa vipi heshima ya ushenga kwa kumsaidia mzee Ndula kumsaka muuaji wa mtoto wake. Kazi kwelikweli. “Mzee mimi si mkaaji sana....nahitaji tuzungumze kidogo tu...” Lameck alinong’ona. “Umenywea sana leo kani kuna nini?” aliuliza mzee Sadiki. Lameck hakujibu. Mzee Said akaongoza njia hadi katika ukumbi wa kuegesha magari. Palikuwa na viti kadhaa vya plastiki. Wakaketi pale. “Kinywaji gani dogo nikuletee.” “Hapana tuzungumze kwanza.” Alijibu Lameck. Mzee Sadiki akatulia katika kiti. Lameck akachukua nafasi ya kuzungumza. “Mzee wangu, mzee ninayekuheshimu sana, mzee uliyenifanya mimi niitwe mwanajeshi wa kimataifa..nipo mbele yako nina tatizo. Kijana wako uliyenituma kulipigania taifa nimelipigania sana, nimejitoa kwa uwezo wote kulipigania lakini bado leo nina tatizo nahitaji busara zako ili niwe na amani tena. Mzee nadhani unakumbuka kuwa nilienda Sudani na ulifanya sherehe ya kunipongeza, na niliporejea hukujua kwanini nimerejea japo vyombo vya habari vilipotosha umma. Mzee mimi si mwanaume tena....risasi ya mwarabu ilinifanya vibaya na kuondoka na heshima yangu yote. Sasa si mwanaume. Lakini hilo sio tatizo, kabla ya kwenda Sudani kuna mwanamke nilimuacha akiwa na mimba yangu, japo alikuwa mke wa mtu mtarajiwa......”, Lameck akasimulia kila kitu kuhusu yeye na Emmy, uhusiano wao na utata wa ile mimba. Akajieleza jinsi alivyopigania kuipata haki ya damu yake. “Lakini katika mapigano kuna kuua ama kuuliwa, mzee mimi niliua bila kutarajia. Hasira za risasi ya mwarabu zilinifanya niue.” Alisita Lameck kisha akaendelea kujieleza juu ya kifo cha mama yake Emmy na baadaye akasema jambo ambalo laiti kama mzee Sadiki asingekuwa amepitia jeshi basi mshtuko wake ungeonekana waziwazi. “Sijui alipata wapi taarifa za kutoroka kwangu, lakini sikuitaka aibu hii, nilimrukia kichwa kimoja na teke moja maridadi, sikutegemea kama atakufa.” Alimalizia. “Mzee nipo hapa kama nilivyosema nahitaji busara zako....na zangu zilizonijia kichwani ni kwamba namuhitaji Emmy, yule ndiye atakayenifunga mimi ama kuniweka huru. Namuhitaji kwa hali na mali.” Kimya kikatanda baada ya simulizi hiyo ya kustaajabisha, kuhuzunisha na kuchekesha katika baadhi ya vipengele. Mzee Sadiki alijitambua mwenyewe na hofu yake. Hakuamini kuwa yu katika kizuizi cha kutenda kazi. Amtendee yupi? Akimtendea Lameck kuna kizuizi cha mzee Ndula, akimtendea Ndula basi amemuweka katika kitanzi Lameck..... Patashika. ***** HALI ya kiubaridi cha namna ya kipekee na harufu nzuri ya manukato ambayo aliyeyapuliza haonekani ilimfanya atabasamu. Jambo jingine lililompa faraja ni kusimama na wazungu daraja moja. Alifarijika sana na kujiona yu mtu kati ya watu. “Akina Rweyemamu nikiwaambia kwa maneno tupu hawataniamini..” alizungumza sauti ya chini ambayo bado ilikuwa imemezwa na lafudhi tamu ya kabila la wahaya. Kisha akachukua simu yake na kuanza kupiga picha na wakati mwingine kujipiga picha yeye mwenyewe. Alifanya hivyo hadi akaridhika. Akaitazama picha moja, ilimuonyesha vyema, jinsi alivyojawa na madevu. Na sura yake ilivyotangaza chuki na ubaya. Picha nyingine zilionyesha madhari ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam ulivyo wa kipekee. Ilikuwa mara yake ya kwanza kusafiri kwa kutumia ndege na ilikuwa mara yake ya pili kutua katika jiji hilo. Baada ya kujiridhisha na kushangaa kwake. Aliandika namba kadhaa katika simu ya mkononi, kisha akapiga. Sasa hakuwa akitabasamu tena. “Nimewasili tayari. Nimevaa miwani nyeusi, suruali ya jeans na koti kubwa na kofia aina ya mzula.” Alitoa maelekezo kisha akakata simu. Baada ya dakika takribani tatu, aliguswa bega na mwanamke kisha akapitilizwa. Alielewa maana akamfuata yule mwanamke kwa mbali. Baada ya hatua kadhaa walikuwa katika gari moja. “Mussa Mujuni. Mume wangu kipenzi.” Sauti ya kike ilivunja ukimya. Maneno haya yakarejesha lile tabasamu alilokuwanalo uwanja wa ndege. Mwanaume hakujibu kitu. “Karibu jijini...karibu sana.” Mwanamke aliendelea. Akazidi kumfaidisha dereva wa taksi. Mwanaume hakusema neno hadi waliposhuka katika taksi. “Umesema kuwa yu tayari kwa kuchinjwa? Unaamini vipi?” hatimaye mwanaume alizungumza, sasa alikuwa ameondosha kofia yake na miwani yake. Cha kustaajabisha akaziondosha na zile ndevu. Hakika alikuwa kijana mtanashati. Kwa nini anajificha? Hilo likabaki kuwa swali. “Nimemtengeneza tayari hawezi kuchomoka yule, nimekuwahisha wewe kabla polisi hawajaingilia kati.” Alijibu bila wasiwasi. Mengi yalizungumzwa na mipango kufanyika. Kisha wakaingia kulala wakiwa wanaungoja utendaji tu. Baada ya starehe za kimwili, mwanaume alisinzia. Mwanamke akabaki macho, alikuwa na wasiwasi na huruma ilipiga hodi. Japo hakuikaribisha. Kitendo cha Jose B wa ukweli kumtamkia Mamu, siri kadhaa juu ya James na jinsi alivyowaua Bibiana na Deo ilimradi tu wasimuwekee kizuizi katika ndoa yake kilimuumiza sana na kuzidi kumwona James hana huruma hata kidogo. Tena hastahili kuonewa huruma. Mariam akaikumbuka siku aliyopata fahamu baada ya siku nane za kuishi dunia ya giza. Sura ya mwanaume ambaye si malaika ilikuwa mbele yake kumaanisha kuwa bado Mariam yu hai hajafa kama wabaya wake walivyotaka. Akamkumbuka Mussa, kijana mtanashati ambaye alimuokoa. Historia ya Mussa ilikuwa inaogopesha kiasi lakini cha muhimu ulikuwa uhai wake maana bila Mussa angekuwa marehemu tayari. Harakati za Mussa za kufanya ujambazi kisha kutokomea na kujificha porini ndizo zilimuwezesha kukutana na mwili wa Mariam ukiwa unapumua. Mariam akaokolewa na jambazi. Siku ambayo Mussa anamueleza juu ya shughuli yake na kwanini anafanya vile. Alimgusia juu ya umasikini uliokithiri pia ukosefu wa ajira kutokana na kukosa elimu. Mussa alilalamika kuwa hapendi kukaba wala kuua. Lakini bunduki ambayo alirithishwa na marehemu baba yake ambaye alikufa katika harakati za kusaka pesa kwa njia haramu ilimpa nguvu ya kufikiri mara mbilimbili. Hatimaye akauvaa ujambazi. Akawa anafanya uhalifu mjini na kujificha porini. Pori la Kakonko, na ni huku alipokutana na Mariam. “Mariam, mimi nikipata pesa ya kutosha huu ujambazi basi tena nakwambia. Unadhani napenda haya maisha ya kujifichaficha..” Mussa aliwahi kumwambia Mariam siku moja wakiwa katika chumba kimojawapo katika hoteli ya Katuma iliyopo katika mbuga za Katavi. Ni muda mrefu ulikuwa umepita tangu waanze kuishi pamoja japo Mariam hakushiriki sana vitendo vya uharifu. Mariam aliguswa na kauli hiyo. Ni siku hiyo alipomwambia Mussa kuhusu unyama wa Kindo (James). “Kwa hiyo jamaa anaweza kuwa na pesa hadi sasa?” “Lazima atakuwa nazo, yale madini yalikuwa ya thamani sana. Nimeona picha yake gazetini amefunga ndo ya kifahari” Mazungumzo haya hatimaye yakawaingiza katika harakati rasmi za kumsaka James. Sasa Mariam alikuwa amewasiliana na Mussa ambaye aliishia naye kinyumba na kujikuta wakizoea kuitana MAMU. Mussa alihitajika kwa ajili ya shughuli moja tu. Aidha kuua ama kumfilisi James. Sasa yu jijini na mipango tayari imesukwa ikasukika. Ni aidha James afe ama aachie mali zote. ***** Bwana Sadiki alikosa jibu sahihi juu ya wapi pa kuegemea, je ni Lameck ama ni mzee Ndulla ambaye amefiwa na mwanaye, mkewe alishtukia jambo hilo lakini mzee Sadiki hakutaka kumshirikisha kwa kuhofia mambo ya wanawake wasivyojua kutunza siri. Mara amwambie mama Karim, mama Karim naye amshirikishe mama Abdul. Hakuna siri tena hapo. Mzee Sadiki, mjeshi wa zamani tena anayeheshimika sana hakutaka kuzikwa kwa dharau kwa kuficha maovu. Hivyo hakutaka kupaparuka. Alitakiwa kuwa makini sana. Usiku mnene akainuka kitandani, akaenda kukaa sebuleni. Akatoa pombe kali katika jokofu akaanza kuigida kwa utaratibu maalumu. Alipoitua mezani akachukua viganja vyake, akaisugua misuli ya kichwa chake. Kisha akaweka mezani mjadala, maneno yam zee Ndulla na maneno ya Lameck. Alipoyalinganisha akashambuliwa ghafla na jina ambalo halikuwa limetiliwa maanani kabisa. James. Katika maelezo ya mzee Ndula palikuwa na jina hili. Jina hili lilitajwa na Emmy ambaye alidai kuwa huyo ni mumewe ambaye alitaka kumuua yeye pamoja na huyo mwanajeshi ambaye ni Lameck. Hicho nd’o kilikuwa chanzo cha kuamua kutoroka. Hatimaye Sadiki akatabasamu. “Bwege huyu nd’o wa kunyutrolaizi mambo.....” alitokwa na sauti nzito. Akachukua bia yake katika mtindo wa tarumbeta akaipeleka kinywani. Alipoitua ilikuwa chupa tupu, uso umekujwa haswaa. Pombe ilikuwa imemuingia. Sadiki akafikiria kumuuzia kesi James, ili aonekane kuwa ndiye muuaji wa askari polisi na lolote lile baya ambalo litatokea liwe juu yake. Ili haya yatimie, Emmy hatakiwi kuwepo kutoa ushahidi. Kizuizi kingine. Emmy anapotezwa vipi katika ramani? Swali gumu. Kichwa kikaanza kumuuma tena japo si kwa maumivu makali kama mwanzo alipokuwa akifikiria juu ya Ndula na Lameck. Akajiondoa sebuleni na kukiendea chumba, akajitupa kitandani. Akautafuta usingizi huku kichwani akiwa na jina la Emmy. Palipambazuka mapema kutokana na kelele zilizopigwa na si yake. Alipoitazama alikuwa ni mzee Ndula. “Salama mkuu.” Alisalimia. “Salama, pole kwa kukutoa usingizini. Yule Emmy anapelekwa leo kwa ajili ya ukaguzi nyumbani kwake. Nilionelea kuwa akitoka huko tumchukue tukazungumze naye chemba moja.” Mzee Ndula alitetemesha katika simu. Mzee Sadiki hakupingana naye. Akakubali, kisha simu ikakatwa. Akatafuta namna ya kumshawishi mzee Sadiki waweze kumfanyia mipango Emmy ya kuwa huru ili mpango wao uende sawa. Akaendelea kuumiza kichwa. **** Baada ya kufanikisha kumuadabisha Maalim Shaban, na bado akiwa hajapata majibu ya wapi mkewe atakuwa amekimbilia. James akiwa amechanganyikiwa na uchovu ukiwa unaendesha akili yake aliamua kurejea nyumbani ili aweze kupumzika na kuangalia ni jinsi gani anaweza kuanza kumsaka Emmy. Kitoto katika tumbo la Emmy alikitilia mashaka, na sasa alimuhitaji Emmy kwa ajili ya mambo mawili, aidha kuitoa ile mimba na mahusiano yaendelee ama kutalikiana. James alifika nyumbani kwake, Grace na Gloria wakiwa bado wamelala. Naye akaingia chumbani kwake kulala. Usingizi ukampitia. Mara akajikuta kama yu ndotoni. Akawaona watu kadhaa wakiwa wanamchekea huku wakiwa na visu. Walikuwa wengi na vicheko vyao vilikuwa vya bandia. Walikuwa na hasira sana na yeye. James alijaribu kupiga kelele lakini haikutoka sauti. Akajikaza mara akayafumbua macho. Haikuwa ndoto tena. Chumbani kwake palikuwa na ugeni. Ugeni usiokuwa na heri. Bunduki mbili zilikitazama kichwa chake. Waliokuwa ndani walikuwa wamezificha nyuso zao. Hawakusema neno lolote. Kifo kilikuwa kinanukia. Na James hakujiandaa kukabiliana na tukio kama hili. Mara mmoja kati ya wageni hao akakifunua kitambaa chake. Uso kwa uso na James. “Kindo...” akaita yule mwanamke ambaye sasa alikuwa yu wazi. James akakodoa macho. Ana kwa ana na marehemu Maria. Msichana waliyemuua ili wapate mali. Mali wakaipata lakini sasa inamtokea puani. Maria alikuwa ameshika kisu kikali. Hakuwa mzimu alikuwa mzima kabisa. James hakupata nafasi ya kujitetea. Mwanaume mwenye ndevu nyingi naye akajifunua. “Kadi ya benki, kadi ya magari na hati ya nyumba hii tafadhali.” Alizun gumza bila hata chembe ya utani, alikuwa na macho mepesi na mkono imara ulikuwa umeikamata bunduki kiustadi. James akiwa bado anatetemeka, ghafla alipigwa na kitako cha bunduki katika kiuno chake. Yowe la uchungu likamtoka. Alikuwa katika mtihani mkubwa sana hakutegemea kama itatokea siku akutane na maajabu kama haya, mwanamke ambaye anaamini kuwa alikufa sasa amemtokea chumbani mwake. Akiwa ameimarika kimapambano. James alifanya alivyoambiwa. Vilivyokuwepo akavitoa bila kusita. Wakati James akiwa katika kitimoto chumbani huku, Emmy alikuwa katika taksi na askari watatu waliovaa kiraia, jukumu kubwa walilopewa ni kufanya upelelezi katika chumba cha Emmy iwapo watakutana na takwimu zozote zitakazowawezesha kumtambua huyo mwanajeshi ambaye amemuua mpelelezi Said Ndula. Walilifikia geti lililokuwa wazi. Gari ikaegeshwa mbali kidogo. Askari wakiwa makini kabisa na mitutu yao walimtanguliza Emmy pale ndani katika nyumba ile iliyokuwa kimya sana. Emmy alikuwa amejitabiria tayari kuwa maisha yake lazima yaishie jela. Anaishia jela kwa sababu ya madhaifu yake kimwili yaliyomsababisha afanye mapenzi na baba yake mdogo. Sasa hakuna kesi ya kufanya mapenzi na baba mdogo bali kuua. Emmy katika hatia. USIKOSE TENA SAA KUMI NA MBILI JIONI NGWE YA MWISHO!!!!
Posted on: Sat, 16 Nov 2013 09:00:00 +0000

Recently Viewed Topics




© 2015