RIWAYA:MZIGO MTUNZI:Ahmed Mussa Mniachi SEHEMU YA 7 Mzigo - TopicsExpress



          

RIWAYA:MZIGO MTUNZI:Ahmed Mussa Mniachi SEHEMU YA 7 Mzigo ukaletwa.Lilikuwa begi jeusi la kawaida.Halikuwa tofauti na yale mabegi yanayouzwa pale Karume Dar es salaam kwa wauza mitumba.Nikatabasam kimoyomoyo. Nilianza kuhisi ushindi fulani ndani ya nafsi yangu.Nikakabidhiwa begi na Martin Kisha tukaingia kwenye gari lilelile lililonileta.Wazo likanijia,wakati naingia ndani ya lile gari nikasoma namba zake nikazikariri kichwani. Nilipoingia kwenye gari nikaziandika kwenye note book yangu.Tukaondoka kuelekea ‘guest’.Saa tatu na robo tulikuwa mbele ya jengo lile la kifahari ambalo lilikuwa katika mtaa ambao nilifahamishwa kuwa unaitwa Kirumba. Martin alikuwa amemaliza kazi yake, akaniacha peke yangu pale ‘guest’. Akaondoka baada ya kuhakikisha kuwa amenikabidhi tikiti ya gari ambalo lilikuwa linaondoka kesho.Akili yangu ilikuwa inafanya kazi haraka kuliko uwezo wake wa kawaida. Kwa kiasi fulani hili lilinishangaza.Nikachukua begi langu na kuondoka pale ‘guest’. “Anko vipi mbona unaondoka?” Aliniuliza dada wa mapokezi “Nimepata simu ya msiba hivyo siwezi kulala hapa!” Nilimjibu huku nikiwa nimeshapiga hatua kadhaa kuuendea mlango wa kutokea nje.Bado aliendelea kuongea lakini sikumuelewa,akili yangu yote ilikuwa juu ya mzigo na safari yangu. Teksi chache zilikuwa zimeegeshwa nje ya ‘guest’ hii. Nikaisogelea moja ya teksi zile. “ Sema bosi unaenda?” aliniuliza mmoja wa madereva wa teksi.Nikaitikia kwa kichwa. “Naomba uniwahishe kokote ninakoweza kupata magari yanayokwenda Dar”nilisema huku nikiwa tayari nimeshakaa siti ya nyuma. “Duh! Saa hizi utapata lakini siti za nyuma” “Hakuna shida ninachotaka ni kusafiri leo hata kama itakuwa ni lori la samaki niko tayari!” “ Nahisi Saibaba halijaondoka!” alisema huku akikoleza mwendo wa gari yake.Baada ya dakika kumi na tano tulikuwa Kituo kidogo cha magari yanayoelekea Dar. “ Shilingi ngapi?” “Elfu tano Mkubwa”. Nikachomoa noti ya shilingi elfu tano nikampa. Mungu alisikia maombi yangu.Nilipofika tu,dada mmoja akanifuata. “Kaka samahani kama unasafiri nina tiketi yangu naiuza tena ni D 5 yaani dirishani,mimi nimeahirisha safari mpaka kesho” Alisema yule dada kabla hata ya kusalimiana. “ Unaonje tukibadilishana tiketi,mimi nikupe ya kesho!” “Nitashukuru sana kaka yangu maana kuna mizigo muhimu nimesahau.” Mchezo ulikuwa umekwisha,lengo lilikuwa limetimia.Ni kama Mungu aliamua kunisaidia.Moyo wangu ulitawaliwa na furaha nikajihisi amani zaidi. Tikiti aliyonipa ilikuwa ni ya basi la Mwanza Coach.Safari yetu ikaanza saa sita kamili. Kama ni mawazo basi safari hii nilikuwa na mawazo zaidi kuliko ile ya kwanza.Ule mzigo ulinishughulisha sana. Kuna nini ndani ya ule mzigo. ”Ngoja nifike Dar nitaamua nini cha kufanya” Niliwaza. Lakini upande mwingine nilikuwa nasikia sauti ambayo ilikuwa inanionya,watu wenye vitisho namna ile kweli wataniacha hai nikishafikisha huo mzigo wao,kwanini walimuua yule mwanamke?Maswali hayo yalizidi kunitisha lakini yakiniongezea ujasiri wa kuvunja masharti. ******** Niliwasili Dar es salaam saa tisa na nusu alasiri.Hii ilikuwa ni mapema zaidi kuliko nilivyotarajia.Safari yetu ilichukua siku tatu.Watu walikuwa wametawanyika hovyo pale kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo. Walikuwa kama siafu walioangukiwa na kaa la moto.Miongoni mwao walikuwa nia abiria ambao wanasafiri huku wengine wakiwasili.Pia walikuwepo wapiga debe ambao walileta kero kubwa kwa abiria. Bonge alinionya kuwa nisipitie sehemu nyingine kabla ya kumfikishia mzigo wake.Pia alinionya kuwa iwapo sitatekeleza maagizo yake,basi asingenipa malipo yangu kwa kazi ya kusafirisha mzigo ule.Vile vile alinikumbusha kuhusu ile picha ya hatari.Ni picha yangu ambayo ilikuwa inaniweka katika wakati mgumu.Ni picha ambayo leo inanifanya niwe mtumwa. Kwa sababu ambazo mpaka leo sijazielewa nikaamua kuvunja maagizo yake kwa kupitia nyumbani kwangu Yombo Buza.Sifahamu kama kuna nguvu ya ziada kutoka nje ya nafsi yangu ilinituma kufanya uamuzi huo wa aina yake. Kuvunja maagizo ya mtu kama Bonge halikuwa jambo la kwaida. Ilikuwa ni siku ya tatu toka nikabidhiwe begi lile.Sikujua kilichomo ndani yake ingawa hisia zilinituma kuwa huenda ni almasi.Kidogo nikaanza kuingiwa na mashaka kwani nilionywa kuwa iwapo nitathubutu kufungua tu,basi adhabu yangu itakuwa ni kifo! “Hivi kweli nikiufikisha huu mzigo nitaweza kuepukana na hicho kifo?” Lilikuwa ni swali gumu ambalo nilijiuliza bila kupata majibu. Lazima nifungue kwani Martin na Bonge watajuaje kuwa mzigo umefunguliwa? Nilipofika chumbani nikalitua begi lile kitandani.Moyo ulikuwa unaenda mbio kama mtoto aliyemuona daktari akiwa na sindano mkononi. Nilimfikiria sana Martin.Huyu ndiye aliyenitisha zaidi,jinsi alivyo!Ana umbo kubwa lenye misuli iliyojengeka kama mnyanyua vitu vizito,macho yake ni makubwa kama kurunzi huku uso wake ukipambwa na kovu kubwa lililopita katikati ya uso wake. Kwa jinsi alivyo alitosha kabisa kumnyamazisha mtoto anaelia kwa neno moja, huyo Martin anakuja! Pale alipokuwa ananitizama nilikuwa sijamkosea chochote lakini alikuwa anatisha kama nyoka anayetaka kumrukia mtu.Macho yake yalionesha wazi dalili zote za mtu mwovu kama si muuaji kamili. Atanifanya nini akigundua kuwa nimefungua ule mzigo? Iwapo alikuwa ananitazama kwa sura ambayo kwake ilikuwa ya upole lakini nilibanwa na haja ndogo,vipi nikutane naye siku ambayo amekasirika?Ndo ajue sasa maagizo waliyonipa nimeyavunja, atanifanya nini? Bila shaka atanifanya kama alivyofanyiwa yule mwanamke kule guest. Sijawahi kuona mtu aliyeuwawa.Maiti ambazo nimewahi kuziona kwa macho yangu ni za ajali ya gari. Taswira yake ilinijia kichwani mara kwa mara.Mwili ulisisimka na kufanya vipele vidogovidogo kama mtu anayehisi baridi kali. Maskini Merina,Mungu amlaze mahali pema peponi. Amin. Shauku yangu ya kutaka kujua kuhusu mzigo ule ilisababishwa na vitisho vya Martin na Bonge.Adhabu ya kifo kwa kufungua mzigo tu! Balaa Laiti wasingenionya kiasi kile basi nisingekuwa na wazo lolote juu ya mzigo ule. Ningeufikisha kama walivyotarajia bila hata kuwa na chembe ya wazo juu ya mzigo wao. Nikalikazia macho begi lile jeusi.Lilikuwa kama refarii katika maisha yangu. Nifungue niishi kwa mashaka au niache niishi kwa amani. Kitu kimoja ambacho kilinikosesha raha ni kuwa iwapo sitafungua basi nitakuwa na fumbo moyoni,fumbo ambalo sitaweza kulifumbua maisha yangu yote.Nakumbuka hata nilipokuwa mwanafunzi niliumiza sana kichwa kwenye mafumbo.Nilikuwa sikubali kushindwa.Kwa mara ya kwanza leo nakabiliana na fumbo,fumbo ambalo kufumbua kwake ni kifo. Nikubali kushindwa? Kweli nilikuwa naelekea kushindwa. Lakini kwa nini nishindwe!? Nikiwa mtaalamu wa mafumbo nilikuwa na kazi mbili,kwanza mzigo halafu uhai wangu.Lengo lilikuwa ni kujua kuhusu ule mzigo bila kupata matatizo. Nikatabasamu huku nikiwa nalitazama vizuri begi lile ambalo niliahidiwa pesa nyingi kwa kulifikisha kwa muhusika bila kuvunja masharti.Fedha nilizo ahidiwa sijawahi kufikiria hata siku moja kuwa nitakuja nizitie mikononi. Kwanini kulisafirisha lile begi kutoka Mwanza nilipwe pesa zote hizo?Kutatua fumbo lile kwangu lilikuwa jambo kubwa kuliko zawadi ambayo ningepewa na bonge huku fumbo likiendelea kubaki kama maisha ya kaburini ambayo maiti tu ndiye anayejua yalivyo. Haiwezekani!Lazima begi lifunguliwe. Kabla sijafungua nikapata wazo.Nikatabasamu. Lilikuwa wazo kabambe. Nilitaka niue ndege wawili kwa jiwe moja. Nilidhamiria kulifumbua fumbo lile bila kuniletea matatizo. Nilianza kujihisi kuwa mshindi ingawa bado niliendelea kujionya. ********* Kama nilivyoeleza lile begi halikuwa na tofauti na yale Mabegi yanayouzwa pale Karume.Kwa akili ya Bonge ningewasili Dar Jioni ya siku iliyofuata.Hivyo nilikuwa huru kutekeleza malengo yangu mapema zaidi. Nyumba niliyokuwa naishi haikuwa mbali sana na Kituo cha magari Buza Kanisani. Ilinichukua dakika takribani kumi kutoka nyumbani hadi kituoni.Nilipofika nikapanda bajaji ambalo lilikuwa linaenda kituo maarufu ambacho kinajulikana kama mwisho wa lami.Siku za nyuma hapo ndio ulikuwa mwisho wa lami kama unatokea Lumo,lakini sasa lami ilikuwa imevuka hapo. Jina halijabadilika. Nikiwa ndani ya bajaji nilikuwa nafikiria jinsi nitakavyotumia fedha za mauzo ya almasi ambazo zipo kwenye begi. ”Ni matanuzi tu si kingine!” niliwaza. Ukweli ni kwamba sikuwa na uhakika ni mzigo gani ambao ulikuwa kwenye lile begi lakini sikuwa na shaka kuwa thamani yake ilikuwa kubwa sana.Dola elfu hamsini kwa kufuata mzigo tu, unafikiri mzigo kama huo utakuwa na thamani gani? Tena mtu anakupa milioni moja zisizo na maelezo wala masharti. Bajaji lilikuwa limefika eneo maarufu la mwisho wa lami. Nikamlipa dereva wa bajaji hela yake.Nikapanda daladala kutoka Mwisho wa lami hadi Lumo.Mpaka hapo naomba uelewe wazi kuwa nilikuwa na fedha za kutosha ambazo sijawahi kuzishika maishani mwangu.Fedha hizo ni zile nilizopewa na Bonge.Kwani nilipozihesabu zilikuwa shilingi milioni moja. Nilikuwa sijawahi kushika kiasi kikubwa cha fedha kama hicho katika maisha yangu. Lakini thamani ya zile fedha niliiona kuwa ndogo sana kila nilipoufikiria ule mzigo. Nilijua kuwa miezi mitatu ijayo nitakuwa tajiri mkubwa sana.Ajabu!Nilikuwa nawaza mtaa ambao utanifaa baada ya kupata fedha zangu. Nilikuwa nimeshaamua akilini mwangu kuutorosha ule mzigo,tatizo lilikuwa ni mbinu gani salama ya kuutorosha mzigo ule. Nilitaka kutafuta mbinu ambayo haitamshtua Bonge mapema.Labda agundue wakati nitakapofika sokoni Nairobi,maana nasikia huko ndiko waliko wanunuzi wakubwa wa madini. Nilifika kituo cha teksi Lumo. Moyo ulikuwa unaenda mbio sana,nilikuwa nimeshavunja sharti la kwanza.Nilikuwa nakaribia kuvunja sharti la pili tena kwa staili mbaya zaidi kuliko alivyotarajia muonyaji. Potelea mbali! “Vipi boss! tunaenda wapi?” Dereva teksi aliniuliza baada ya kuona nimeingia kimya kimya kwenye gari lake bila kumueleza lolote.Hapa nilianza kuona hali ya hatari niliyokuwa nakabiliana nayo,akili yangu haikuwa katika hali ya kawaida kwani nilikuwa nimeingia kwenye gari bila kujijua.Nilikuwa nimezidiwa na mawazo kiasi ambacho mwili ulikosa mawasiliano mazuri na akili. “ Nipeleke Karume tafadhali” “Vipi boss unapenda muziki?” aliniuliza huku akikata kona kona kutoka kituo cha teksi na kuingia barabara inayoelekea kariakoo. “Poa tu!” Nilimjibu kwa mkatao lakini kimsingi sikuhitaji aina yoyote ya burudani kwa wakati huo. Muziki mzuri uliokuwa unatoka kwenye gari lile haukuweza kuniliwaza hata kidogo.Ulikuwa muziki wa siku nyingi ambao uliimbwa na Washirika Tanzania stars watunjatanjata. Tulipofika maeneo ya Tazara tukaiacha Bara bara ya Pugu ambayo sasa inajulikana kama barabara ya Mwalimu Nyerere tukaingia barabara ya Mandela.Sikuipenda sana tabia hii ya kupachika karibu kila kitu jina la Mwalimu Nyerere.Ingekuwa bora kama mambo mengi yangefanywa kwa kuiga tabia zake na aina ya uongozi wake.Mimi sio mwanasiasa lakini kitu kimoja kinanifanya nimheshimu na kumthamini Mwalimu,Mwalimu alithamini rasilimali zetu. Mwalimu hakupenda tabia ya kujilimbikizia mali hovyo,Wakati wa mwalimu hakukuwa na misamiati ya ajabu kama; Mafisadi papa,mafisadi nyangumi na mafisadi nini sijui……. Wakati bado naendelea kuwaza dereva akasimamisha gari kwenye kituo cha mafuta cha Buguruni.Akajaza mafuta,kisha akaiondoa teksi kwa kasi.Akafuata barabara ya uhuru. Tulifika Karume Saa 11.47. Nikachagua saizi ya begi nililolitaka.Dereva wa teksi nilishamwambia anisubiri,hivyo nilipolipata lile begi nikaingia kwenye teksi tukarudi Lumo.Tulipofika Lumo nikamwamrisha dereva anipeleke Buza kanisani. “Shilingi ngapi?” nilimuuliza baada ya kufika. “Elfu ishirini bosi!” Alijibu huku akitikisatikisa funguo za gari lake kama mtu anayesubiri upinzani kutoka kwangu tuanze mabishano. “Poa nisubiri!” Nilimjibu huku nikilipeleka begi lile ndani. Nilipofika ndani nikaliacha lile begi ambalo nimetoka nalo Karume kisha nikachukua lile ambalo nilitakiwa kumfikishia Bonge. Hapo nilishaamua kufanya ujanja wa kubadilisha mzigo. Nilipotoka nilikuwa na begi lingine kama lile tulilotoka nalo Karume.Tofauti na madereva teksi walio wengi huyu hakuwa mwongeaji. Muda mwingi alikuwa kimya na alionesha kuwa mtu makini.Tabia yake hii ilinivutia na kunifanya niwe na hamu ya kuongozana nae kila nilikokwenda.Lakini kitu kimoja hakikufichika kwenye sura yake,alikuwa mtu mwenye dalili za huzuni hakuwa na furaha.Hata ule uchangamfu mdogo aliouonesha kwangu ulikuwa wa kulazimisha. “Tuna safari nyingine bosi?” Aliniuliza baada ya kuona nikiingia na begi kwenye gari. Niliitikia kwa kichwa. “wapi?” aliuliza tena kwa mkato. “Mbagala charambe!” nilimjibu kwa mkato. Nilichomoa noti mbili za shilingi elfu kumi nikampa. Hayo yalikuwa ni malipo ya mizunguko ambayo tulikwishaifanya. #kajuna anataka kumzidi akili bonge atafanikiwa au atanunua kifo chake? itaendelea kesho NB;USISOME BILA KU-LIKE NA KU-COMMENT LA SIVYO RIWAYA HII HITASITISHWA
Posted on: Thu, 24 Oct 2013 18:54:56 +0000

Recently Viewed Topics




© 2015