TAARABU AMA TAABU?!! Mngaona nina gubu, kwa maswali - TopicsExpress



          

TAARABU AMA TAABU?!! Mngaona nina gubu, kwa maswali kuyarusha, Kamwe sitakuwa bubu, kwa mambo yakutapisha, Naomba kwenu jawabu, ambalo lakinaisha, Hii yenu Taarabu, ama tuite taabu? Nauliza kwa sababu, nina mwingi mshawasha, Nionayo maajabu, sanaa mwatukanisha, Walivyo lea mababu, leo mwaibadisha, Hii yenu taarabu, ama tuite taabu? Nijuavyo taarabu, ni neno la kukopesha, Asiliye Kiarabu, "Twaraba" nabainisha, Maanaye nahutubu, ni kitu kufurahisha, Hii yenu taarabu, ama tuite taabu? Imekosa taratibu, ni yupi msema hasha? Haina tena adabu, na mara nyingi huchosha, Kwa walo ni mahabubu, ya leo hufarikisha, Hii yenu taarabu, ama tuite taabu!! Sanaa mwaiharibu, mungaona mwatingisha, Nyoyo mwazitia tabu, sumumu mwazirambisha, Mmeifanya halibu, imebaki inatisha, Hii yenu taarabu, ama tuite taabu!! Fani hino ni dhahabu, daima huturubisha, Na huzichota Qulubu, na dhara kuliondosha, Vireje mwaisulubu, viumbe mwagonganisha? Hii yenu taarabu, ama tuite taabu!! Tama niloyahutubu, nimenyesha rasharasha, Wingu la mvua Adibu, nahepa kwa kujimwasha, Nasubiri lenu jibu, ugani kuwasilisha, Hii yenu taarabu, ama tuite taabu?!! "al-ustadh wingu la mvua" ((Mpwa wa sumu baridi))
Posted on: Sun, 29 Sep 2013 13:12:05 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015