ULINIUA GLORIA 6 Bwana Stewart bado alikuwa mkimya, alijua - TopicsExpress



          

ULINIUA GLORIA 6 Bwana Stewart bado alikuwa mkimya, alijua kabisa kwamba alifanya makosa kumwambia Gloria kwamba kitu ambacho alikuwa akikitaka ni kumuua Kaposhoo lakini katika kipindi hicho akaona bora liwe la kutokea lakini si kumuacha Kaposhoo aendelee kuwa ndani ya dunia hii na wakati yeye mwenyewe alikuwa akitaka kuendelea kutanua na msichana huyo ambaye mpaka katika kipindi hicho alionekana kuufanya ukahaba bila mwenyewe kufahamu. Fedha zikaonekana kumlevya, fedha zikayapoteza mapenzi ambayo alikuwa nayo moyoni mwake, fedha ambazo kwake alionekana kama kuziabudu tayari zilikuwa zimebadilisha kila kitu katika maisha yake. Mapenzi hayakukoma, bado Bwana Stewart alikuwa akiendelea kutanua na Gloria kisiri. Chumba chao kilikuwa chumba namba mia na tano ndani ya hoteli ile, chumba ambacho kilionekana kama kuwa staff ndani ya hoteli hiyo. Wafanyakazi wote wakajua ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea lakini hakukuwa na mtu ambaye alithubutu kuufungua mdomo wake na kuongea kitu chochote kile kibaya. Katika kipindi hicho bado Bwana Stewart alikuwa akisikiliza mchogo ambao alikuwa ameupanga pamoja na wauaji wa kundi la Kunta Kinte. Bwana Stewart alikuwa akisikilizia kujua ni kitu gani ambacho kingetokea katika kila kitu ambacho alikuwa amekipanga, hakutaka kuona Kaposhoo akiendelea kuishi na wakati moyoni mwake alikuwa na uhitaji wa kuendelea kuishi na Gloria ambaye alionekana kuwa radhi kwa kila kitu. Bwana Stewart hakujali kuhusiana na ukaribu ambao alikuwa nao na Bwana Mbwana, baba yake kaposhoo, kitu ambacho alikuwa akikitaka kwa wakati huo ni kuona kwamba anaendelea kuishi na Gloria tu. Mapenzi yakamteka, uzuri wa Gloria ukazidi kumchanganya kupita kawaida, hakuamini kama fedha ambazo alikuwa nazo zingeweza kumpa msichana mrembo kama Gloria. “Fedha ndio kila kitu” bwana Stewart alikuwa akimwambia tajiri mwenzake, Bwana Andrew katika kipindi ambacho walikuwa katika mkutano wa matajiri ndani ya ukumbi mkubwa ambao ulikuwa katika hoteli ya Paradise 5 huku lengo la mkutano huo likiwa ni kuisaidia nchi ya Zambia ambayo kwa kiasi fulani uchumi ulionekana kuyumba. “”Kuna jipya lililotokea?” Bwana Andrew alimuuliza huku akinyanyua kinywaji chake na kupiga fundo moja. “Unapokuwa na fedha unaweza kupata msichana yeyote mzuri” Bwana Stewart alimwambia. “Hilo naamini” “Na unaweza kumpata msichana mzuri zaidi ya wazuri katika dunia hii. Unaamini hilo” Bwana Stewart alimwambia na kuuliza. “Inategemea” “Inategemea na nini?” “Wakati mwingine hawa watoto wa kike wanapenda watu maarufu” “Hilo si tatizo. Kwanza unapokuwa na fedha, moja kwa moja unakuwa maarufu. Unakubaliana na mimi?” Bwana Stewart alimwambia Bwana Andrew na kumuuliza. “Kivipi?” “Tafuta fedha ili uwe maarufu. Na kama ikitokea umekuwa maarufu, basi fedha zitakufuata zenyewe” Bwana Stewart alimwambia. “Hapo kidogo nimekuelewa. Ila kuna kitu gani kipo nyuma ya haya yote unayoniambia?” Bwana Andrew alimuuliza. “Ngoja kikao kiishe tutaongea zaidi” Bwana Stewart alimwambia Bwana Andrew. Kikao kikaendelea zaidi, matajiri zaidi ya kumi na mbili wa nchini Zambia walikuwa wamekusanyika katika ukumbi wa hoteli hiyo. Muda wote Bwana Stewart alionekana kwa na furaha kupita kawaida, bado hali ya kuwa na Gloria ilikuwa ikimpa furaha kupita kawaida. Muda mwingi mahali hapo alikuwa akimfikiria msichana huyo, kwake, kikao kikaonekana kuwa kirefu mno, alitamani kimalizike haraka na kisha kumuona tena Gloria. Moyo wake ulikuwa umetawaliwa sana na Gloria, hakuambiwa kitu chochote kile, kwake, Gloria alikuwa namba moja moyoni mwake. Alijua fika kwamba alikuwa na mke pamoja na watoto lakini kwake hilo halikuweza kuonekana kuwa kizuizi cha yeye kuwa na msichana huyo. Mapenzi yake yakawa zaidi kwa Gloria kuliko kwa mke wake ambaye aliahidi kanisani kwamba angempenda kwa moyo mmoja. Kila kitu ambacho alikuwa amekiahidi kanisani juu ya mke wake siku ya harusi kikaonekana kusahaulika moyoni mwake, wanawake walionekana kuuyumbisha moyo wake kutoka kwa mke wake lakini ujio wa Gloria, ule moyo ambao ulikuwa ukiyumbishwa ukaanguka kabisa. Japokuwa mkutano ulikuwa ukichukua muda mchache sana huku waziri mkuu, Bwana Mbwani akiwepo ndani ya mkutano huo lakini kwa Bwana Stewart ulionekana kuchukua muda mrefu sana. Kila wakati alikuwa akijisikia kuwa karibu na Gloria, kila alipokuwa mbali na msichana huyo, moyo wake ulikuwa ukimwambia kwamba alikuwa akichukuliwa na mwanaume mwingine jambo ambalo lilikuwa likimuumiza sana moyoni mwake. Japokuwa mkutano ulikuwa ukiendelea, Bwana Stewart akashindwa kuvumilia, alichokifanya ni kuanza kuwasiliana na Gloria kwa kutumia meseji jambo ambalo lilimfanya kuwa bize na simu yake. Mkutano huo mfupi wala haukuwa mrefu sana, ukamalizika. “Vipi?” Bwana Andrew alimuuliza Bwana Stewart ambaye alimfuata huku akiwa na tabasamu kubwa usoni mwake. “Angalia hiyo picha” Bwana Stewart alimwambia huku akimgawia simu ambayo alikuwa ameiweka picha ya Gloria. “Mmmmh!” Bwana Andrew alibaki akiguna tu mara baada ya kuiona picha ile. “Vipi?” “Nani huyu” “Ndio maana nilikwambia kwamba fedha ndio kila kitu, msichana yeyote mzuri unaweza kutembea nae” Bwana Stewart alimwambia Bwana Andrew ambaye alibaki akiwa ameduwaa huku akiiangalia picha ya Gloria. “Ila haujaniambia, nani huyu?” “Subiri kwanza. Unamuonaje?” “Kabla sijasema namuonaje, nani huyu” “Malaika wangu” “Umemtoa wapi?” “Kwani yupo vipi?” “Mzuri mno. Halafu anaonekana kama sio Mzambia” “Hahaha! Huyo msichana katoka mbali sana” “Wapi?” “Tanzania” “Kweli kuna wasichana wameumbika, huyu kapewa kila kitu, kuanzia sura mpaka umbo. Anakaa wapi?” Bwana Andrew alisema na kuuliza. “Usijali. Nilitaka kukudhihirishia kile nilichokwambia kabla” Bwana Stewart alimwambia huku akiichukua simu yake. Mipango bado ilikuwa ikiendelea kusukwa huku Kaposhoo akitakiwa kuuawa ndani ya siku mbili tu kwa ajili ya kuwapa uhuru Gloria na Bwana Stewart ambaye alitaka kuwa huru pamoja na Kaposhoo. Kila wakati alikuwa akisikilizia simu yake, muda mwingi alikuwa akitarajia kupokea simu kutoka kwa vijana wa kundi la Kunta Kinte ambao alikuwa amewapa kazi ya kumuua Kaposhoo tu. Masaa yaliendelea kukatika lakini hali bado ilikuwa kimya, hakupokea simu yoyte kutoka kwa vijana hao ambao tayari alikuwa amewalipa kiasi kikubwa cha fedha kwa kufanya kazi ile tu. Bwana Stewart alikuwa na presha kubwa, kila wakati alikuwa akiangalia saa yake kama mtu ambaye alikuwa akitaka kuwahi jambo fulani ambalo lilikuwa likitarajiwa kutokea mahali fulani. Saa nne usiku, simu yake ya mkononi ikaanza kuita, kwa haraka sana, akaichukua na kisha kuipeleka sikioni. “Vipi?” Bwana Stewart aliuliza mara baada ya kupokea simu ile na kugundua kwamba mpigaji alikuwa mmoja wa vijana wa kundi la Kunta Kinte. “Kila kitu tayari” “Unasemaje?” “Kazi imefanyika” “Mmemuua?” “Kama kawaida” “Asante Mungu! Mmemuua kwa kifo gani?” “Risasi tatu mwilini mwake. Kashatangulia kabla yetu” Sauti ya kijana yule ilisikika simuni. Bwana Stewart hakutaka kuendelea kuongea, katika kipindi hicho furaha ilikuwa imemshika kupita kawaida, alichokifanya huku akiendelea kuwa katika hali hiyo ni kuanza kumpigia simu Gloria kwa kuona kwamba Kaposhoo hakuwepo nyumbani. Mara baada ya kuona kwamba simu inaita, akaanza kusikilizia. Simu ile iliita zaidi na zaidi lakini wala haikupokelewa kabisa. Bwana Stewart hakuonekana kuwa na wasiwasi kwa kuamini kwamba simu ile ingepokelewa tu. Simu iliita, iliita na kuita lakini wala haikupokelewa hadi ikajikata. Bwana Stewart hakuonekana kukata tamaa, alichokifanya ni kuanza kupiga tena, alipiga zaidi na zaidi mpaka katika kipindi ambacho simu ile ikapokelewa. Tofauti na mategemeo yake, Gloria aliipokea simu ile huku akilia na sauti ya mwanaume ikisikika kwa mbali huku ikilalamika. Bwana Stewart akaonekana kushtuka, hakujua ni mwanaume gani ambaye alikuwa na Gloria katika usiku huo na wakati Kaposhoo alikuwa ameuawa kama alivyoambiwa simuni. “Hallow....!!” Sauti ya Gloria iliita huku akilia. “Kuna nini tena mpenzi? Huyo nani?” Yalikuwa ni maswali mawili yaliyotoka mfululizo mdomoni mwake. “Ni Peter” “Peter! Anafanya nini hapo usiku huu” Bwana Stewart aliuliza huku akionekana kushtuka. “Ame......” Gloria alijibu lakini hata kabla hajamalizia jibu lake, simu ikakatika. Bwana Stewart akaonekana kuchanganyikiwa , hakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea. Kitendo cha Gloria kulia huku Peter akisikika akiropoka kilionekana kumchanganya kupita kawaida. Kitu ambacho alikuwa akikijua ni kwamba Gloria alikuwa msichana wa Kaposhoo na Peter alikuwa ni rafiki wa kawaida tu ambaye wala hakuwa akiishi katika nyumba hiyo, ilikuwaje katika usiku huo Peter alikuwa ndani ya nyuba hiyo? Kila alichokuwa akijiuliza akakosa jibu. “Hebu subiri” Bwana Kaposhoo alijisemea na kisha kuanza kupiga tena simu. Simu ikaanza kuita, iliita zaidi na zaidi mpaka ikakata. Bwana Stewart akaonekana kukasirika kupita kawaida, kichwa chake kikazidi kuchanganyikiwa zaidi juu ya kile kilichokuwa kikiendelea. Bwana Stewart hakuishia hapo, akarudia tena kuipiga simu ile lakini hali ikawa ile ile, simu haikupokelewa zaidi ya kukatwa. Hapo ndipo ambapo kichwa chake kilipoanza kuhisi kitu, akajua kabisa kwamba kulikuwa na kitu ambacho kiliendelea nyumbani hapo, alichokifanya ni kutoka nje na kisha kuchukua gari lake na kisha kuanza kuelekea Maluba, mtaa ambao Kaposhoo alipokuwa akiishi. Bwana Stewart akaliingiza gari lake katika barabara ya Chilimbulu na kisha kuanza kueleka upande wa Kaskazini Magharibi. Bwana Stewart alikuwa akiendesha gari huku akionekana kuchanganyikiwa . Katika usiku huo, hakukuwa na magari mengi barabarani kitu ambacho kilimfanya kuendesha kwa kasi. Hakuchukua muda mrefu, akawa amekwishafika katika Makumbusho ya Taifa ya Lusaka ambapo baada ya kuyavuka tu akachukua barabara ya Burma ambapo akaonganisha nayo mpaka kufika katika barabara ya Kanisa ambayo ilikuwa ikionganisha mpaka katika jengo la makao makuu ya Aitel nchini Zambia. Bwana Stewart hakutaka kwenda na barabara ile moja kwa moja kwani baada ya sekunde chache akaingia katika barabara nyingine ndogo ya Belt ambayo ilimpeleka moja kwa moja mpaka katika mtaa wa Maluba, mtaa ambao ulikuwa na nyumba nyingi zilizoonekana kuwa za kifahari. Aliendelea mbele zaidi na zaidi mpaka kufika katika eneo ambalo kulikuwa na nyumba aliyokuwa akiishi Kaposhoo, akateremka na kisha kuanza kulifuata geti ambapo kulikuwa na mlinzi nje. “Gloria nimemkuta?” Lilikuwa swali la kwanza ambalo aliliuliza Bwana Stewart kwa mlinzi ambaye alikuwa getini pale. Hata kabla mlinzi hajajibu swali lile, wote wakashtuka mara baada ya kumuona Gloria akitoka nje huku akikimbia, alikuwa akilia kwa sauti kubwa, miguuni hakuwa na viatu, walipoona hivyo, wote wakaanza kumfuata na kisha kumzuia. “Kuna nini?” Bwana Stewart alimuuliza Gloria huku kila mmoja akionekana kushangaa. “Anataka kuniua” “Nani?” “Peter” “Anataka kukuua! Kwa nini?” “Huyo hapo anakuja” Gloria alisema huku akilia. Peter akatokea mahali hapo, alionekana kuwa na hasira kupita kawaida, mkononi mwake alikuwa ameshika kisu hali ambayo ilionekana kumshtua kila mmoja. Peter hakuonekana kuwa katika hali ya kawaida hata mara moja, alionekana kuwa radhi kumuua Gloria kwa kumchoma kisu kile, hakuona kama msichana huyo alistahili kuwa hai katika kipindi hicho. “Kuna nini?” Bwana Stewart alimuuliza Peter ambaye alionekana kuwa na hasira huku akiwa hatua kumi kutoka kwake aliposimama na Gloria. “Nataka kumuua huyo malaya” Peter alijibu na kisha kuanza kumsogelea Gloria huku akionekana kuwa na hasira kupita kawaida, hasira ambazo ziliwaonyeshea kwamba endapo wasingemzuia basi angeweza kumchoma Gloria na kisu kile. Je nini kitaendelea? Je Peter ataweza kumuua Gloria?
Posted on: Wed, 24 Jul 2013 04:10:50 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015