WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema - TopicsExpress



          

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema mkutano wa siri wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EA), uliofanyika nchini Uganda hauna uhusiano na Jumuiya hiyo. Mkutano huo uliofanyika hivi karibuni ulihudhuriwa na Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni, Paul Kagame (Rwanda), pamoja na Uhuru Kenyetta (Kenya). Mkutano huo ulifanyika bila Tanzania kushiriki ambapo ulijadili masuala ya Jumuia hiyo, kitendo kilichotafsiriwa na wachunguzi wa siasa kuwa huenda nchi hizo zinajiandaa kuanzisha shirikisho lao. Katika kikao hicho kulifikiwa makubaliano ya mikataba ya usafirishaji wa mafuta kati ya Uganda na Kenya kuendeleza ujenzi wa bomba la mafuta la Bandari ya Lamu, na Uganda kuacha kutumia Dar es Salaam au Mombasa kwa madai kuwa ni njia ndefu na yenye gharama kubwa zaidi. Kwa mujibu wa viongozi hao, pia walikubaliana kuhamasishana jinsi ya upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya kujenga reli kutoka Kenya kupitia Uganda na Rwanda, lengo ni kusafirisha bidhaa za nchi hizo. Rais Museveni alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini kwake akisema: “Hata kama wangekuwa wawili au watatu, bado wangezungumzia kuhusu masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki”. Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, kuhusu mkutano huo, Sitta alisema Watanzania hawana haja ya kujiuliza maswali kuhusu mkutano huo, kwa sababu haukuwa wa shirikisho, bali uliandaliwa kama kikao cha ujirani mwema kupitia nchi zao, ambapo walijadili masuala mbalimbali ya nchi hizo. “Tanzania hatutishiki, cha muhimu ni kupata taarifa kamili na sahihi, tutazichambua na kusonga mbele,” alisema Sitta. Sitta alisema Tanzania ilikosekana kwenye mkutano huo kwa kuwa haikualikwa. Aliongeza kwamba kutokana na viongozi hao kutowashirikisha viongozi wa nchi nyingine husika, kuna haja ya masuala hayo kujadiliwa upya kupitia sekretarieti wakati itakapokutana tena mjini Arusha. Nchi ambazo zinaunda Jumuiya hiyo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, ambayo nayo haikuwepo kwenye mkutano huo uliofanyika hivi karibuni nchini Uganda. source: Tanzania daima
Posted on: Sun, 30 Jun 2013 07:48:06 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015