pata mda upitie hitimisho la Prof Shifji katika kitabu chake - TopicsExpress



          

pata mda upitie hitimisho la Prof Shifji katika kitabu chake katika mhadhara alio ufanya wakati anamaliza mda wake katika kigoda cha mwalimu pale UDSM kuhusu Rasim ya katiba na serikali 3 Katika kuhitimisha mhadhara wangu nitarejea kwenye udhani au hypothesis yangu. Nilisema kwamba ninavyodhani mimi, masharti mengi ya Rasimu yalikuwa maamuzi ya maelewano kwa maana ya compromise na sio mwafaka kwa maana ya consensus. Baada ya uchambuzi wangu, ninadiriki kusema kwamba muundo wenyewe wa serikali tatu uliopendekezwa ni compromise kati ya wale waliosimamia serikali mbili na wale waliopigania muungano wa mkataba, kwa maneno sahihi, kuuvunja muungano. Wanaserikali mbili waliona afadhali kuwa na Muungano, hata kama ni wa serikali tatu, badala ya kuuachia uvunjike; wakajifariji kwa matumaini ya dhamira ya wananchi na nia ya viongozi. Wana-mkataba wakaona kuwa kwa wakati huu wakubali serikali tatu wakijua fika kwamba muundo wa serikali tatu hautadumu na vyovyote vile utavunjika. Nilisema pia kwamba compromise inazaa uamuzi legelege. Compromise juu ya muundo, kwa maoni yangu, imezaa muundo wa muungano legelege. Kuna maeneo mengi nimechambua na kudhihirisha kwamba yatazaa migogoro ambayo hatimaye inaweza kuuvunja Muungano. Kero za Muungano zitaendelea, safari hii kutoka pande zote mbili. 38 Muungano ukivunjika hakuna mwananchi atakayenusurika, awe wa Tanganyika au wa Zanzibar. Tuna mifano mingi ya hivi karibuni. Shirikisho la Sovieti liliposambaratika, likazaa migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe – mgogoro wa mpaka kati ya Uzbekistan na Krygistan; mgogoro kuhusu maji kati ya Uzbekistan na Tajikistan; vita vya Chechnya visivyoisha; vita kati ya Azerbaijan na Armenia, n.k. Waliofaidika ni mashirika ya kibeberu ambayo walitua kama tai kupora rasilimali za Urusi. Shirikisho la Yugoslavia lilipogawanyika likazaa vita katika eneo lile kiasi kwamba mpaka leo halijatulia. Wanasiasa wenye uchu wa madaraka wakisukumwa na nchi za Magharibi, wakatumia uhasama wa jadi kati ya makabila na dini kushawishi mgawanyiko. Makabila na dini zilizofanya kazi kwa pamoja, kwa kiasi fulani, chini ya uongozi wa Rais Tito, na mfumo wa Shirikisho, yakagawanyika. Leo hii nchi ambayo ilikuwa na amani kwa zaidi ya miongo mitatu imegawanyika katika nchi kama saba (Croatia, Serbia, Bosnia, Macedonia, Montenigro, Kosovo na Slovenia). Na vita bado vinaendelea. Waliofaidika ni nchi za Magharibi kupitia NATO yao. Mwandishi mmoja anaweka wazi maslahi ya nchi za Magharibi katika kusambaratisha Yugoslavia. Nimnukuu kwa sababu mfano huu una mengi ya kutufundisha: Beginning in 1990 Germany and the United States sought and achieved the breakup of Yugoslavia in two stages—1992-1995 and 1998-1999. The German government aimed at this division because it wanted to include as territory of its “vital interest” Slovenia and Croatia, the most economically developed states of the Yugoslavian confederation. … Through them Germany would achieve access to the Adriatic Sea. 39 The United States was interested in the more recently established states (Bosnia, Serbia, the former Socialist Republic of Macedonia), which controlled the only route from east to west and from north to south through the Balkan mountains. The Balkan area, along with Romania, Bulgaria, Turkey and the Arab nations, forms a European-Middle East bloc, which the United States wants to control (including the former states of the Soviet Union—Kazakhstan, Azerbaijan, Turkmenistan, Tajikistan) for the complete exploitation of the great oil resources of the Caspian Sea.10 Na hapa, karibu na nyumbani, Sudan ya Kusini ilipojitenga kumekuwa na migogoro juu ya mafuta, ambayo bado inaendelea. Nimewahi kusema na ninarudia. Suala la Muungano sio letu tu. Kuna nchi za kibeberu zina maslahi makubwa ya rasilimali pamoja na ya kijeshi katika eneo letu, hasa Bahari ya Hindi. Tukibeza mambo haya nyeti kwa sababu tu ya uchu wa madaraka ya viongozi wachache, tutawapeleka watu wetu kwenye hali mbaya. *** Tume imesema, ingawa hatujaiona taarifa yao rasmi bado, kwamba wananchi wengi walitaka serikali tatu. Lakini, kwa heshima, ningependa kuhoji msimamo huu. Jukumu la Tume halikuwa tu kukusanya maoni na kuhesabu nani amesema nini. Jukumu la Tume lilikuwa ni kupokea maoni, kuyaainisha na kuyachambua ili kupata kiini chake na sababu zake. Wajumbe walipoambiwa na wananchi wa eneo moja kwamba wajengewe india ndogondogo, haikumaanishwa hivyo, bali wananchi walikuwa wanadai hospitali; kwa kuwa viongozi wanapelekwa India kupata huduma za kiafya, basi wao pia wakataka wajengewe hospitali bora katika maneneo yao na wote, viongozi na wananchi, watibiwe humohumo nchini. 40 Hatimaye, ukiangalia kwa undani kero za Muungano, kwa mfano, suala lenyewe sio idadi ya serikali bali ni la demokrasia. Wazanzibari kwa muda mrefu tu wamedai haki yao ya kujiamulia mambo yao wenyewe; kushirikishwa katika maamuzi muhimu; kutokudhalilishwa, na kupewa heshima ya mshirika huru. Madai haya ni halali. Hoja yangu kwa muda mrefu ni kwamba tusiangalie suala la Muungano kwa jicho la idadi ya serikali bali kwa mtazamo wa demokrasia. Na tukifanya hivyo tunaweza kubuni muundo wa kipekee kutokana na historia yetu na hali halisi ya Washirika kutokuwa na uwiano wa uchumi, eneo au idadi ya watu. Muundo wa serikali tatu, au shirikisho kama unaoainishwa, unajikita kwenye usawa wa kisiasa (political equality). Kwa msingi huu, uwakilishi, hususan katika vyombo vya kuchaguliwa, hauna budi uwe sawa bila kujali idadi ya watu. Lakini katika hali yetu ya uchumi, mchango wa Washirika katika gharama za shirikisho hauwezi ukawa sawa, wala sio haki, kwa sababu hatuna usawa wa kiuchumi. Kwa vyovyote vile, Tanzania Bara itachangia asilimia kubwa ya gharama za Shirikisho. Hatimaye, anayelipa mpiga zumari ndiye anayechagua wimbo. Kwa maoni yangu, kama tungekuwa na mtazamo wa kidemokrasia tungeweza kubuni muundo ambao unakidhi matakwa ya pande zote mbili bila hatari ya kuuvunja Muungano. Mimi binafsi nimewahi kutoa pendekezo la muundo mbadala. Mara ya kwanza niliwasilisha pendekezo langu kwa Baraza la Wawakilishi kama miezi michache iliyopita. Kwa muhtasari, nilipendekeza dola kamili mbili, la Zanzibar na la Muungano. Bunge la Muungano litakuwa na mabaraza mawili, Baraza la Wananchi na Baraza la Nchi. Wajumbe wa Baraza la Wananchi watachaguliwa moja kwa moja na wananchi wa pande zote mbili kutoka majimboni. Baraza la Nchi litakuwa dogo lenye, tuseme kama wajumbe 30, 15 kutoka Bara na 15 kutoka Zanzibar wakichaguliwa na Bunge 41 la Zanzibar na wabunge kutoka Bara katika Baraza la Wananchi ilimradi wasiwe wajumbe wa bunge lolote lile. Na nilipendekeza orodha tatu – moja ya mambo ya muungano, nyingine ya mambo ya kushirikiana (concurrent matters) na orodha ya tatu ni juu ya mambo ya pamoja (joint interest). Kutokana na muda siwezi kufafanua; nia yangu ni kudhihirisha kwamba muundo mbadala unawezekana. Rasimu imezinduliwa. Imeanza kujadiliwa. Tuchukue nafasi hii kuijadili kwa makini ili hatimaye malengo na matumaini ya walio wengi yatimizike. Makamu Mkuu wa Chuo, wanakigoda wenzangu, rafiki zangu na wageni waalikwa. Mhadhara huu ulikuwa ni mchango wangu wa mwisho katika wadhifa wangu wa Nyagoda wa Mwalimu Nyerere lakini, nikiwa na uzima wa afya, hautakuwa mchango wangu wa mwisho katika mijadala ya kitaifa. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza. Ahsanteni na kila la heri.
Posted on: Tue, 25 Jun 2013 15:48:03 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015