RIWAYA;MTAFITI. MTUNZI;HUSSEIN TUWA. SEHEMU YA KUMI Akauma - TopicsExpress



          

RIWAYA;MTAFITI. MTUNZI;HUSSEIN TUWA. SEHEMU YA KUMI Akauma midomo yake kama mtu anayejitahidi kuiziba kumbukumbu mbaya kutoka kwenye akili yake, na hata akafanikiwa kupata mlengo-lengo wa machozi machoni mwake. “Ni hali ya kusikitisha kwa kweli…” “Ndio tuelezee hiyo hali sasa!”Inspekta alimjia juu. Luis alijikohoza kidogo, halafu akamtazama mwanasheria wake kama anayemtaka ushauri iwapo aeleze juu ya swala lile au la. Mwanasheria akamtikisia kichwa kuashiria kuwa aendelee tu kutoa maelezo aliyotakiwa. Na ndipo Luis Kambesera alipomchafua vibaya sana hayati Grayson Mochiwa mbele ya yule Inspekta… “Kama nilivyokwambia, Grayson alitoweka hapa ofisini kwa siku tatu bila taarifa zozote baada ya mimi kumkatalia ombi lake la mkopo. Kazi zikalala. Sheria za kazi zinasema wazi kuwa mfanyakazi asipoonekana kazini kwa siku tatu mfululizo bila taarifa zozote kwa mwajiri basi huwa amejifukuzisha kazi mwenyewe…” “Hata kama ni Mkurugenzi?”Inspekta alidakia. “Hata kama ni Mkurugenzi…naye si mwajiriwa tu?Yeye angeweza kunipigia simu tu na kunitarifu kuwa ana tatizo au udhuru hiyo ingetosha…hakufanya hivyo!”Luis alizidi kumfitini marehemu. “Kwa hiyo?” “Kwa hiyo tulichukua jukumu la kumfukuza kazi…tukamuandikia barua iliyotangazania yetu hiyo kwake na kumpa nafasi yayeye kujieleza kwa nini hatua hiyo isichukuliwe dhidi yake. Nakala za barua hiyo zipo kama mkizihitaji...” “Kwa hiyo nd’o akakutolea bastola baada ya kupata barua hiyo? Mbona inaniwia vigumu kuamini, hasa ukizingatia uchunguzi wangu umeonesha kuwa jamaa alikuwa msomi mwenye PhD, jambo linaloniambia kuwa uwezo wake wa kufikiri na kuchanganua mambo ni mkubwa tu?” Inspekta alisaili. Luis akasita kidogo. “Afande, nadhani we’ umetaka maelezo. Mteja wangu anakupa maelezo. Kama una mashaka na maelezo yake unaweza kuchukua hatua zozote utakazoona zinafaa ndani ya misingi ya sheria, lakini sio kumbishia anayokueleza!” Mwanasheria wa Luis aliingilia kati, na Inspekta akamkata jicho kali. “Haya ni mahojiano wewe…sio maelezo ya upande mmoja!” Alimkoromea, kisha akamgeukia Luis, “ Jibu swali hilo bwana!” Alimshurutisha. Ilikuwa zamu ya Luis kumkata jicho yule Inspekta. “Okay…yeye hakutushikia ile bastola pale kwa ajili ya ile barua...” Luis alianza kujieleza, na Inspekta akamkatisha tena. “Nilichoona mimi wakati naingia mle ndani ni kwamba alikuwa amekuwekea wewe bastola, sio wewe na wale wengine mle ndani. La hasha…ni wewe peke yako nd’o ulikuwa umewekewa mtutu wa bastola kichwani!” Luis alitetereka kidogo. “Ah, ndio hivyo bastola ilikukwa kichwani kwangu, na wote wengine walizuiwa wasitoke mle ndani ama si hivyo angenilipua. Sa’ mi’ naona hiyo ilimaanisha kwamba sote tulikuwa tumetaitiwa pale!” Jamaa hakukosa jibu la kujitetea. “Endelea!” “Sawa. Kile kilikuwa ni kikao cha kumjadili yeye na hatima yake, na ndio maana hakuitwa kushiriki kikao kile. Matokeo yake akavamia kikao kile na kushurutisha apewe hela akalipe deni…akisema kuwa amekuwa akijificha kwa siku tatu mfululizo kuhofia maisha yake…na kudai kuwa watu wamekuwa wakimfuata nyuma kila aendapo na amefanikiwa kuwatoroka ndio akaingia mle ofisini…Mi’ nikwambia hatumuelewi, na kwamba kuanzia muda ule yeye hakuwa mfanyakazi wetu tena, ya kwamba kile kikao kilikuwa kinapitisha maamuzi kuhusu barua aliyoandikiwa ambayo hakuijibu. Hapo ndipo alipotoa bastola na kunitishia…tena akasema mbele ya kila mtu mle ndani kuwa amepewa muda mpaka saa nne asubuhi ile alipe hizo hela ama si hivyo anauwa!” “Mnh!” Inspekta akaguna. “Ndiyo! Kwa hiyo akasema kama sisi tunaidhinisha kifo chake kwa kukataa kumpa hizo hela atakazo, basi bora yeye aanze kutuua sisi…akianzia na mimi!”Luis aliongopa akiwa macho makavu, na Inspekta akabaki mdomo wazi. “Na…unataka kuniambia kuwa wote wale waliokuwemo mle ndani walisikia hayo maneno?” “Si ulisema utahitaji kuwahoji na wao? Well…be my guest…nenda kawahoji na wao usikie watakalokuambia, lakini hivyo ndivyo ilivyokuwa. Jamaa alinitolea bastola akisema kuwa hayuko tayari kufa wakati anajua thamani yake kwenye kampuni hii ni zaidi ya hizo milioni nane azitakazo…” Luis alimjibu, na kubetua mabega. “Well…inaonekana jamaa waliokuwa wanamsaka walikuwa karibu naye kuliko alivyodhani…wakamuua!” Alimalizia na kubaki akimtazama Inspekta kwa macho ya kusubiri swali jingine. Inspekta alishusha pumzi ndefu na kumgeukia yule askari wa kike aliyekuwa anaandika yale maelezo. “Umeyapata maelezo yote hayo mpaka hapo?” Alimuuliza, na yule askari akakiri kuwa ameyapata maelezo yote yale kwenye maandishi. “Okay…kwa hiyo unataka kuniambia kuwa hao watu waliokuwa wanamdai Grayson milioni nane, ambao hata hawajulikani waliko wala iwapo wapo kweli, ndio waliomuua kwa kumdungua kwa risasi asubuhi hii?” Alimuuliza, na Luis akatoa sauti ya kukereka na swali lile. “Akh! Mi nakueleza kile kilichojiri asubuhi hii kama jinsi ninavyojua…wewe ndiye Inspekta hapa, sio? Fanya upelelezi wako basi kujua iwapo hao waliomuua ndio hao waliokuwa wakimdai au vingnevyo!” Inspekta alimtazama kwa muda mrefu bila ya kusema neno. Kisha bila kuondoa macho yake usoni kwa Luis alimwambia yule askari aliyekuwa akirekodi yale maelezo yake kwa maandishi. “Mpe bwana Luis Kambesera hayo maelezo ayasome kuona kama yako sahihi kama alivyoyaeleza, koplo!” Koplo alimpa Luis yale maelezo aliyoyaandika. Badala ya kuyapokea, Luis akamuashiria kuwa ampe mwanasheria wake, ambaye aliyapokea na kutumia muda mrefu kuyasoma. Muda wote wakati mwanasheria anasoma maelezo yale, Inspekta na Luis walikuwa wanatazamana bila ya kuambiana lolote kwa midomo yao, ingawa macho yao yaliambiana mengi - yale ya Inspekta yakimwambia Luis kuwa yule Inspekta alikuwa hamuamini kwa asilimia mia, na yale ya Luis yakimwambia Inspekta kuwa alikuwa hajali iwapo atamuamini au la, ila maelezo yake ndio hayo. Fukuto lilikuwa linaelea baina ya watu wale wawili waliokuwa pande mbili tofauti za sheria. “Maelezo yako sawa…unawesa kusaini!” Mwanasheria alisema, na ndipo Luis alipobandua macho yake kutoka kwa yule Inspekta na kusaini maelezo yake. Kisha akamsukumia yule Inspekta yake maelezo pale mezani, naye badala ya kuyapokea, akamwamuru yule koplo ayapokee huku bado akimtazama Luis machoni. “So, twaweza kwenda sasa Inspekta?” Luis alimuuliza. Kwa kama nusu dakika zaidi, Inspekta alizidi kumtazama machoni bila ya kufanya bidii yoyote ya kuficha hisia alizokuwa nazo dhidi ya yule kiongozi wa ile kampuni kubwa ya tafiti za nishati nchini, kabla ya kumjibu. “Muwe makini tu msijigonge mlangoni wakati mnatoka!” Luis na Mwanasheria wake walitoka nje ya kile chumba cha mahojiano huku wakitikisa vichwa. ____________ Alipotoka msalani Zay alijihisi utulivu kiasi ukimwingia. Alijifuta machozi na kujaribu kufikiri kwa kituo juu ya hatua muafaka ya kuchukua. Jambo la kwanza alilofikiri lilikuwa ni kwenda kutoa ripoti polisi. Halafu akalifuta wazo hilo kwa muda. Alijua kuwa polisi huwa hawachukui hatua ya kumsaka mtu aliyepotea mpaka baada ya saa ishirini na nne tangu asemekane kuwa amepotea. Sasa Mwamtumu hakupotea. Mwamtumu alikuwa hapokei simu tu, na hilo sio la kuripoti polisi. Lakini pia ule ujumbe kuwa alikuwa amekimbizwa na jibaba lenye bastola kutoka kule ofisini ulitosha kumfanya akatoe ripoti polisi, akihofia usalama wa rafikiye. Lakini polisi watamuelewa? Watajua wenyewe, yeye atapeleka ripoti tu. Lakini kwanza aliamua kujihakikishia kwa mara ya mwisho. Akaipiga tena namba ya rafikiye na hali ikawa ile ile. Alikuwa anataka kuiweka simu mfukoni ile aende polisi kutoa maelezo wakati wazo jipya lilipomuingia. Haraka alienda kwenye ile sehemu ya ujumbe wa sauti wa “whatsapp” aliotumiwa na Mwamtumu na kutazama kama Mwamtumu aliacha wazi ile programu iliyopo kwenye “whatsapp” ambayo iliwezesha kuonesha mahala alipo mwenye simu husika. Ilikuwa wazi! “E bwana we!” Alimaka kwa kiherehere huku akibofya kile kijimshale kilichowezesha kutafuta mahala mwenye simu iliyomtumia ujumbe alipo, na mara moja ramani ya mitaa ya Dar ikajitokeza na kimshale kikaonesha mahala simu ya Mwamtumu ilipokuwa muda ule. Kilionesha kuwa ile simu, na kwa maana hiyo Mwamtumu, yuko Changombe mtaa wa Mkamba. “Nyumbani kwake?” Alimaka kwa mshangao. Bila kujishauri zaidi, alikwapua mkoba wake na kutoka mbio nje ya nyumba yake huku akipekua ndani ya mkoba ule kutoa ufunguo wa gari lake. Huko nje, alijitosa ndani ya gari lake dogo aina ya Toyota Vitz na kuondoka kwa kasi kuelekea Chang’ombe, moyo ukimwenda mbio huku akijiuliza ni lipi litakuwa limemkuta Mwamtumu kule nyumbani kwake hata akashindwa kupokea simu mara zote zile alizokuwa akimpigia. Alizidisha kasi kuwahi kule nyumbani kwa rafiki yake kipenzi… ____________ Dakika kumi na tano baada ya kutoka kule kituo cha polisi kusema uongo, Luis aliingia ofisini kwa afisa usalama wa kampuni, na kumkuta Chabbi Cheka akiwa ameketi nyuma ya meza yake ilhali miguu ameipandisha juu ya meza ile. “Okay, nimeshamalizana na yule askari mpuuzi…sasa niambie hali ikoje!” Alimwambia. “Funga mlango uketi bosi…” Chabbi alimwambia. Luis alifanya alivyoshauriwa, na Chabbi akamuelezea kila kitu alichofanya tangu pale aliposikia ile kengele ya tahadhari iliyobonyezwa na Luis ikiunguruma mle ofisini kwake, hadi pale alipomuondoa Grayson duniani. Kimya kilitanda kwa muda. “Yah! Umefanya lililotakiwa Chabbi…hali ilikuwa tete.” Luis alisema, na Chabbi akaguna tu. Kuua mtu kwake halikuwa jambo kubwa sana. “Unajua kama Grayson angeangukia mikononi mwa polisi, hatujui angeropoka maneno gani huko… lakini nakuhakikishia kuwa yasingekuwa ya kutupamba na kutusifia. Jamaa angetuharibia kila kitu!” Luis alisema. “Yeah…hilo tulishalijadili mbona bosi?. Ila kiutaratibu ingeleta mashaka sana kama pamoja na tafrani yote ile aliyoanzisha, bado tungeacha kupiga simu polisi …” “Kweli!” Luis alikubaliana naye. “Anyway, mi’ nilitaraji wale polisi wakimzonga angeweza kuhamanika na kuanzisha mashambulizi, na kuwalazimisha polisi wamuue. Hiyo ingekuwa poa sana kwetu…lakini ndo haikuwa. So nilipoona ameamua kujisalimisha nikajua hamna jinsi…nikamaliza mchezo!” Chabbi alimwambia. “Ilikuwa ni hatua muafaka sana! William alishafanikiwa kufuta kila kitu kwenye kompyuta zake. Grayson angeweza kutufanyia taabu kama angeanza kuropoka hovyo juu ya hili swala, lakini kwa kuwa sasa kikwazo pekee kilichobaki kimeshaondoka, shukrani za dhati zije kwako kwa kufanya litakiwalo kwa wakati utakiwao, tunaweza kusema kuwa tuko salama kuendelea na mpango wetu kama tulivyopanga…” Luis alisema, na akaona Chabbi akitikisa kichwa. “Siwezi kusema hivyo kwa asilimia mia moja Luis…” “What…kuna nini? Au ndio hicho kimeo ulichoniambia kwenye simu?” Luis aliuliza, sasa akiwa na mashaka kidogo. *** Haya Luis ndio keshamchafua marehemu Grayson mbele ya vyombo vya dola. Lakini bado Chabbi hamhakikishii usalama wa siri yao kwa asilimia zote. Itakuwaje? *** Zay naye anaenda nyumbani kwa rafikiye ambaye hayupo. Atachukua hatua gani? TUKUTANE KESHO SAA MOJA ASUBIHI!
Posted on: Wed, 04 Sep 2013 03:32:13 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015