Rebecca (13) Ilipoishia jana... Alipofika hapa John akaacha - TopicsExpress



          

Rebecca (13) Ilipoishia jana... Alipofika hapa John akaacha kuisoma barua na kuichukua ile bahasha alimozitoa picha na barua ile, akaitazama ndani yake-hakuona kitu. Akainyanyua juu na kuigeuza chini juu-juu chini, hakuna kilichotoka kadhalika. Akadhani kuwa fedha zilizotajwa katika barua zimo katika bahasha ile kubwa, lakini kabla hajaichukua, akakumbuka kuwa kuna bahasha nyingine ndogo ya khaki hajaifungua. Akaangaza macho hapo kitandani, asiione! Akataharuki. Endelea... Katika pekua ya hapa na pale, akaiona bahasha hiyo mwishoni mwa kitanda upande wa kulia, akaichukua na kuifungua haraka haraka. Alipoifungua, macho yakamtoka pima kama mtu anayeishangaa maiti ya ndugu yake. Ndani ya ile bahasha mlikuwa na noti nyekundu tupu, akazitoa na kuzihesabu. Zilikuwa ni noti thelathini zenye thamani ya shilingi Elfu kumi kila moja. Hivyo kwa noti thelathini, zilifanya jumla ya shilingi laki tatu. John hakuamini kile alichokiona, alijiona kama mtu aliyekuwa anaota. Akazigeuza mara kadhaa na kuzihesabu mara tatu tatu. Aliporidhika kuwa hakuwa ndotoni, akazirejesha zile fedha katika ila bahasha na kuendelea kusoma barua. …picha na hizo fedha, ni zawadi yako. Tafadhali naomba tuwasiliane utakapokuwa shuleni ili moyo wangu upate faraja. Sina la zaidi, ila tambua kuwa NAKUPENDA SANA JOHN. Nakutakia safari njema na masomo mema. Mungu akipenda tutaonana. Akupendaye kwa dhati, Rebecca Kimaro. Alipomaliza kusoma na kuridhika na kile alichokisoma, aliirudisha barua katika ile bahasha yake. Akazichukua tena zile picha na kuanza kuziangalia kwa makini. Picha ya kwanza, Rebecca alipiga ufukweni ambapo alikuwa amevalia mavazi ya ufukweni-bilauzi iliyombana sana na kuishia juu ya kitovu na sketi fupi iliyoishia juu ya mapaja. Alipiga picha hii akiwa amesimama ndani ya maji yaliyoishia katikati ya miguu. Picha ya pili, Rebecca alipiga katika uwanja wa mpira wa mikono. Alikuwa amevalia fulana ya kijani iliyokuwa pana kiasi na kupanguliwa mikono yake bila utaratibu, lakini kwa namna ya kumpendeza mvaaji. Kupitia mikono hiyo iliyopanguliwa, ilionekana nguo fulani hivi ya rangi nyeupe kwa ndani mfano wa sidiria iliyositiri maungo mengine ya ndani kutoonekana. Chini alivaa kaptura ya dengrizi ya rangi nyeusi na miguuni kabisa alivaa raba nzuri nyeupe huku kichwani akijifunga kitambaa cheupe kilichofungwa vizuri. Picha ya tatu na mwisho, Rebecca aliipiga akiwa shuleni na sare zake. Baada ya kumaliza kuziangalia picha hizo, alizirudisha mahala pake pamoja na zile fedha. Vyote kwa pamoja akavirejesha katika ile bahasha kubwa na kuviweka katika begi lake la nguo, kisha akatoka nje. Ilishatimu saa moja unusu usiku. *************** Alipoingia ndani ya gari, Rebecca alijawa na haya, alidhani kuwa dereva ameshuhudia kila kitu, hivyo alipoingia tu garidi kichwa alikiinamisha chini na hakutaka kumwangalia dereva wala kuongea naye kama ambavyo hufanya kila siku. Dereva naye wala hakujishughulisha naye. Hii haikumaanisha kuwa hakuushuhudia mchezo, la! Ameushuhudia, mwanzo-mwisho. Kwanza tangu ile jana pale bosi wake alipoondoka mapema bila kuingia darasani huku wenzake wakiingia. Pia leo ameshuhudia kila kitu tangu pale walipokuwa wamekaa hadi wakainuka na kulifuata gari, kisha kwenda nyuma ya gari na hata kilichofuatia alikishuhudia kupitia kioo cha kuangalia nyuma kilichopo ndani ya gari. Kiasi fulani alimhurumia sana bosi wake kwa vile alivyoteseka na mapenzi na kubaini kuwa alimpenda sana huyu kijana kiasi kwamba anashindwa kujizuia na kumuonesha hisia zake wazi wazi. Ila yeye alipiga kimya kwa kuwa hakushirikishwa. Walipofika nyumbani, Rebecca alipitiliza kama kawaida yake hadi chumbani kwake ambako hakutaka kupoteza muda, akaingia bafuni huko huko chumbani kwake kujifanyia usafi. Alipomaliza kuoga, alirudi chumbani na kujitupa kitandani akiwa na taulo tu na kukirihusu kichwa chake kifanye kazi. Kweli kikafanya kazi kama aliyoitaka, akarudisha fikra nyuma na kulikumbuka tukio lililotokea saa chache zilizopita-tukio la kumalizia picha. Yaani ilikuwa kama filamu ambayo nyota wa mchezo anakutana na adui kuu wa mchezo huo na kupambana naye hadi anamshinda, hivyo kulipiza kisasi. Rebecca akajihesabu mshindi tena aliyeshinda kwa kishindo kikubwa. Lakini ghafla akajiona kuwa ni mshindi aliyeshinda ila asiyeufaidi ushindi wake. Kama vile ameshinda kikombe walichokigombea na kukitamani kukimiliki na aliposhinda kikombe hicho akakinyanyua juu kufurahia ushindi huo. Punde kikombe hicho cha thamani kubwa kinamtoka mikononi mwake na kudondoka chini alipokuwa amekiinua juu na kinapofika chini sakafuni kinavunjika vipande vipande visivyofaa kuungwa na kuwa kikombe tena. Akabaki kuviangalia asiweze kuamua jambo la kufanya. Pia alijikuta akijawa na fikra za pengine ataeleweka tofauti na John kutokana na kitendo chake cha kumtongoza. Huenda John akamdhania kuwa ni Malaya mwenye kutumia hila za fedha na vitu vya gharama kuwanasa wavulana. Japo John alionesha kuvutiwa naye na kumfanyia yale yote, lakini bado hakujipa asilimia zote kuwa ndiyo tayari amemkubalia ombi lake. Akaingia katika mgogoro wa nafsi akijilaumu kwa kujirahisisha kwa John, huku upande mwingine akijipa matumaini. Pamoja na hayo, bado alifarijika kila alipolikumbuka tukio lile lililotokea kwa mara ya kwanza katika maisha yake. Tukio lililompatia joto la John baada ya kukumbatiwa na kuibua vugu vugu la huba lililofichama mbali katika mwili wake. Huba hilo lilipofichuliwa, mhusika akaliacha linaelea angani tu kisha mwenyewe akaondoka. *************** Siku, wiki, mwezi hatimaye mwaka ukawadia bila mawasiliano kati ya John na Rebecca. Haikufahamika kuwa ni kutingwa na masomo ama vipi. Rebecca aliendelea kumuwaza John ukweli wa kumuwaza na kujitahidi kuulizia anuani ya shule yao, lakini bahati haikuwa upande wake. Aliishi maisha ya shida sana hata kuathiri mfumo wake wa maisha. Hakuwa tena Rebecca yule aliyekuwa na afya tele. Rebecca huyu alidhoofu kila leo. Nyumbani alipoulizwa kwa nini anazidi kupukutika, aliwajibu kuwa masomo yamekuwa magumu mno naye hataki yamzidi nguvu, hivyo anafanya kila linalowezekana kupigana nayo hata yawe magumu namna gani. *********** John ameingia moja kwa moja katika moyo wa Rebeccca. Kukosekana kwa mawasiliano baina yao, ni pigo kubwa sana kwa Rebecca anayeandamwa na mawazo kumuwaza John. Je, nini hatma ya mambo haya upande wa Rebecca? Je, ndiyo kusema kuwa John hampendi Rebecca, hivyo amemsahau? Unafikiria nini katika muendelezo huu? Unaruhusiwa kuandika ubashiri wako hapo chini. Usikose kuifuatilia hapo kesho!. Tunawatakia siku njema__
Posted on: Wed, 04 Sep 2013 02:18:21 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015