Simulizi za Kalibonge Barua ya Halima (14) Ilipoishia - TopicsExpress



          

Simulizi za Kalibonge Barua ya Halima (14) Ilipoishia jana... Tukaingia Morogoro majira ya saa saba unusu adhuhuri. Nikateremka lakini sikwenda kula, badala yake nikanunua maji chupa kubwa, nikanawa usoni kisha nikarudi tena garini kusubiri safari. *********** Endelea... Saa saba na dakika arubaini, tukaanza safari ya kuitafuta Dodoma. Muda huu sikuwa na wasiwasi kuwa huwenda nikawa nafuatiliwa kwani hadi waje wamkute pale alipolala ni saa kumi na moja jioni, atakuwa ameshaoza zamani. Pia wale wafanyakazi wengine wa nje hawakuruhusiwa kuingia ndani tena wakati huu walijua hamna mtu mule ndani kwani hawakuniona wakati natoka hivyo hapo hadi atakaporudi mama Egla saa kumi na moja. Wakati huo nitakuwa Dodoma tayari na ikiwezekana nitakuwa miguuni mwa mama na baba nikiwaeleza mkasa huu huku nimezungukwa na kaka zangu Sufiani na Jemedari. Kama ni mechi basi kusimama kwetu pale Msamvu, ilikuwa kama mapumziko na sasa kipindi cha pili kikaanza. Tulipoanza tu safari, hali ikawa kama awali, ukimya. Basi lilitawaliwa na ukimya huku zikisikika kwa mbali sauti za meno ya baadhi ya abiria waliokuwa wanakula garini. Meno hayo yakasikika yakishindana na mifupa ama yakisaga viazi. Mbali na kelele hizo za meno kushindana na mifupa, gari lilitawaliwa na utulivu mkubwa. Nikaegemea kiti na kujikuta narudi tena kijijini. Wakati huu nikakumbuka siku aliyokuja mama Egla na vile nilivyomkatalia kuondoka naye. Nikajiona kama mtu ninayekwenda kuwasuta wazazi wangu kutokana na kilichotokea. Nilikataa katakata kuondoka na mama Egla, lakini wazazi wakanilazimisha. Siwalaumu ila najua kwa nini walifanya vile; umasikini na kushindwa kumudu gharama za maisha. Sidhani kama walikusudia kunufaika nami, yaani nitaabike namna hii ili wao waishi vema. Sikuwahukumu na sitofanya hivyo kamwe. Hakuna hata mzazi mmoja ambaye angaliendelea kumkumbatia mwanawe hata kama ametokea mhisani eti kwa sababu anahofia jambo kama lililonikuta mimi. Mama Egla hakunikosea hata kidogo ila mumewe. Mumewe amenikosea mimi, mkewe, wanawe na zaidi amewakosea wazazi na kaka zangu kwa kitendo alichonifanyia. Amemkosea mkewe kwa sababu ameshindwa kuwa mwaminifu katika ndoa yake, pia amemkosea kwa kumdhalilisha kwa wazazi wangu na kaka zangu. Amewakosea wanawe kwa kuwaonesha kuwa hakuwa baba mwema na aliyekuwa na tabia mbaya hata kwa wasichana wa watoto wake. Kutokana na kitendo alichotukuta tunakifanya mimi na Joshua, ilimpasa akubali matokeo kuwa mimi na mwanawe tulikuwa watu wa namna gani. Kwa hivi, adhabu ile ilimstahili sana. Bado basi n mulikuwa kimya sana. Sasa tulishapita Gairo na tukasimama kituo hiki ama kile na kushusha abiria halafu safari ikaendelea kuitafuta Dodoma. Maisha ya kuwa na Joshua ndiyo ambayo yatabaki katika kumbukumbu za milele. Nilimpenda sana mvulana huyu hata ikawa najiachia kwake kila aliponihitaji na kufanya kila alichonitaka kufanya. Nilimkabidhi moyo wangu licha ya kuwa nilijua wazi hawezi kuwa mume wangu kutokana na kisomo chake. Nilifahamu alinipenda sana na huenda huko aliko anataabika kila anikumbukapo, lakini sikujipa asilimia zote za kuwa naye katika maisha ya kuanzisha familia. nikajivunia kukutana na mvulana wa namna yake ambaye aliuchukua moyo wangu wote akakaa nao. Pia kitendo cha baba yake kikaweka doa kubwa, jeusi katika moyo wangu-doa ambalo halitofutika hata nifanye nini zaidi ya kuongezeka na kuuchafua moyo wangu kila nikikumbukapo kitendo hicho. Nikamlaani, nikamlaani na nitaendelea kumlaani mwanaharamu yule. Tukaingia Dodoma majira ya saa kumi na moja jioni. Muda huu nikajua tu kuwa huko nitokako, mayowe yameanza na tayari watu wamejaa na polisi na madaktari na kila namna ya upuuzi. Nikajua hivyo kwa sababu ndiyo muda wa mama Egla kurudi nyumbani. Tukafika kituo kikuu cha mabasi na tukaanza kuteremka huku kila mmoja akishika njia yake. Mimi nikateremka na kuangaza huku na huko kana kwamba namtafuta mwenyeji wangu. Ghafla nikiwa bado katika hali hii ya kushangaa, likaja taxi na kusimama jirani yangu. “Wapi dada nikuwahishe?” Akaniuliza yule dereva wa taxi. Sikumjibu ila nikafungua mlango na kuingia ndani. “Ntyuka!” Nikamwambia dereva taxi. “Elfu thalathini.” Akasema dereva taxi bila kuniangalia usoni. “Wewe wasiwasi wako nini? Washa gari twende.” Dereva hakuwa mkaidi, akalitia gari mafuta na kuanza kuondoka, lakini wakati injini ikianza kuchanganya nikahisi kujawa na usingizi mzito ajabu. Usinginzi ambao uliambatana na giza nene machoni, kizunguzungu hata nikajikuta nalala kwenye ile siti. Sikumbuki kitu gani kilifuatia ila nakumbuka badala ya kuwa nyumbani Ntyuka kama nilivyotarajia, nikajikuta niko hospitalini huku pembeni yangu kukiwa na kijana mmoja ambaye baada ya kurudisha kumbukumbu zangu, nikamtambua, alikuwa ni yule dereva taxi. ********** Halima amefanikiwa kufika Dodoma, lakini anazimia ndani ya taxi. Anazindukana na kujikuta yuko pembeni ya kijana. Je, ni wapi hapo? Kilimkuta nini hata akazimia? Andika ubashiri wako hapo chini na usikose sehemu ya 15 hapo kesho. Tunawatakia siku njema____
Posted on: Thu, 08 Aug 2013 02:20:39 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015