Sumaye kukimbia ufisadi CCM • ATAKA SERIKALI ITAJE WALIOFICHA - TopicsExpress



          

Sumaye kukimbia ufisadi CCM • ATAKA SERIKALI ITAJE WALIOFICHA MABILIONI NJE na Abdallah Khamis WAZIRI Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, amesema hatakuwa tayari kukaa na viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iwapo watapitishwa kuwania nafasi za uongozi katika chaguzi zijazo. Mbali na tishio hilo, Sumaye pia amemvaa Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete, akimtaka kuacha kigugumizi cha kushindwa kuanika majina ya mafisadi na viongozi wanaodaiwa kuficha mabilioni ya fedha nje ya nchi. Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Sumaye alidai kuwa anakubaliana na kauli ya Rais Kikwete kuwa chama hicho kitaanguka katika chaguzi zijazo endapo viongozi wake wataendekeza rushwa. Alisema ikiwa CCM itashindwa kuwakabili watoa rushwa na kuwapa nafasi ya uongozi, hatakubali wala kuendelea kukaa na watu hao ndani ya chama hicho. “Kama CCM itapitisha majina bila ya kuangalia namna rushwa ilivyotembezwa, nchi itaanguka na chama kitatoweka, na kwa sababu wanalijua hilo, naamini hawatothubutu kuwapitisha watoa rushwa. Lakini wakifanya hivyo, mimi sitaweza kukaa na watoa rushwa na mafisadi ndani ya chama,” alisema. Hata hivyo, alisema kauli yake hiyo ya kwanza na nzito haimaanishi kuwa lazima kukihama chama hicho, bali atajiweka pembeni ili kuwaonyesha kuwa hakubaliani na rushwa na ufisadi, na kwamba hata wananchi wamechoka vitendo hivyo. Alidai kuwa rushwa ndani ya chama chake imekithiri mno na hata katika maeneo mengine ya nchi, na kwamba vita yake itawezekana tu ikiwa wapambanaji wote wataungana na kuunganisha nguvu za pamoja. Alisema rushwa imekithiri katika nyanja zote, na kwamba hatua ya kukabidhi mapambano hayo kwa Makamu Mwenyekiti, Philip Mangula, itasaidia kuikomesha. “Ninamuunga mkono mwenyekiti wangu katika hili, na hasa baada ya kumkabidhi jukumu hili Jemedari Mangula, ambaye nina hakika hatowaonea aibu watu wote wanaojihusisha na rushwa ndani ya chama. Nipo pamoja nae, na atambue mimi ni miongoni mwa askari wake katika mapambano haya,” alisema Sumaye. Alidai kuwa watu wanaotafuta madaraka kwa njia za rushwa, hususan katika ngazi ya urais katika uchaguzi ujao wa 2015, wameanza kutumia mbinu chafu, ikiwemo kuchafua wenzao na kuwaziba midomo, na hata kujaribu kupenyeza ajenda zitakazowafanya waonekane ni miongoni mwa watu wanaowahurumia Watanzania licha ya kuwa na kashfa mbalimbali za ufisadi. Alitolea mfano matukio ya watu hao kuingilia mialiko mbalimbali katika shughuli za kijamii na kuharibu dhamira nzima ya waandaaji wa shughuli hizo katika kupata faida, likiwemo tukio alilofanyiwa hivi karibuni katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam pamoja na wanachama wa kikundi cha kuweka na kukopa cha Vikoba kilichopo Nshamba wilayani Muleba, kuzuiwa kuendelea na mipango yao kwa hofu ya ujumbe ambao angeutoa ungeweza kuwajeruhi baadhi ya watu. “Taasisi, vikundi vya kijamii au madhehebu ya dini hualika viongozi kuwasaidia katika shughuli walizokusudia, atakayezungumzia maadili na kukemea maovu katika jamii, atatafutwa mtu mwenye kifua cha kufanya hivyo, sasa hawa wanaoingilia kwa hofu ya mambo yao kujulikana, kwangu mimi ni waoga na wasiojiamini mbele ya jamii,” alisema Sumaye. Ataka walioficha mabilioni watajwe Kuhusu mabilioni ya fedha yanayodaiwa kuhifadhiwa na Watanzania nchini Uswisi, Sumaye aliitaka serikali kutaja hadharani majina ya wanaotuhumiwa kuzitorosha badala ya kunyamaza. Alisema badala ya serikali kukaa kimya na kuacha tuhuma hizo zikienda kwa ujumla wake, ishirikiane na wadau kuwabaini watu walioficha fedha hizo na ikibidi ijulikane namna walivyozipata. Sumaye ambaye alishawahi kutuhumiwa kuwa na akaunti ya shilingi trilioni 10 nje ya nchi, alisema kinachomsikitisha ni kuona Waziri wa Mambo ya Nje akiwakaripia viongozi wa Uswisi, pale waliposema wapo tayari kushirikiana nao katika kubaini ukweli wa kuwepo kwa fedha hizo. “Haya mambo yanakera, na sasa kila mtu ananyooshewa kidole kuwa anaweza kuhusika, ni vema serikali ijitokeze na kuweka hadharani majina yao,” alisema Sumaye. Aliongeza kuwa wakati alipokuwa Waziri Mkuu, mmoja wa mawaziri wa wakati huo alimfuata na kumuuliza sababu za kutokuwa na akaunti nje ya nchi kwa ajili ya kumsaidia kuendesha maisha iwapo mambo yataharibika nchini. Amvaa Lowassa Katika hatua nyingine, Sumaye amemvaa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kwa kile alichokiita kupotosha ukweli. Sumaye alisema Lowassa anatumia mradi wa maji ya Ziwa Victoria mkoani Shinyanga kama njia ya kupata umaarufu. Alisema katika siku za hivi karibuni, ilitoka taarifa katika moja ya vyombo vya habari kuwa mradi huo ulikataliwa na baraza zima la mawaziri kasoro Kikwete aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, na Mohamed Seif Khatib, aliyekuwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais. Sumaye alisema mradi huo ulikuwepo kabla Lowassa hajawa Waziri wa Maji, na madai kuwa ndiye aliyeusimamia peke yake ni ya uongo na kutafuta uungawji mkono usiostahili. “Najua mwenzetu (Lowassa) anajua anachofanya kwa sasa, lakini niwaambie mradi ulishughulikiwa na Dk. Pius Ng’wandu na ukasainiwa na Mussa Nkangaa akiwa Waziri wa Maji wakati huo. Sasa kama mtu anasema aliwezesha hili mbona alipokuwa Waziri Mkuu hakuweza kufikisha maji maeneo mengine kama Dodoma?” alisema Sumaye. Ajinadi kwa urais Akijibu maswali ya waandishi wa habari kama atagombea nafasi ya urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2015, Sumaye alisema taratibu za chama chake hazimruhusu kuliongelea hilo kwa sasa. Alisema yeyote anayeliongelea hilo ndani ya CCM kabla ya maagizo ya kujitangaza kutolewa, atakuwa anavunja kanuni za chama, na kwa upande wake hataki kuwa sehemu ya wavunjaji kanuni. “Kama ni kugombea, nina haki, sifa na uwezo. Kama ni imani kutoka kwa Watanzania wananiamini kwa kiasi kikubwa, kilichobaki ni mimi kutamka kama nitagombea au sigombei, na ninyi mnajua kanuni za chama chetu kinasemaje. Je, mnataka niadhibiwe?” alihoji Sumaye.
Posted on: Wed, 06 Nov 2013 18:11:53 +0000

Recently Viewed Topics




© 2015