A DAY TOO LONG SEHEMU YA 29 Ilipoishia jana.. Alichokifanya - TopicsExpress



          

A DAY TOO LONG SEHEMU YA 29 Ilipoishia jana.. Alichokifanya Pokwane asubuhi iliyofuata ni kwenda katika sehemu ya kituo kikubwa cha mabasi yaliyokuwa yakielekea nje ya nchi hasa Afrika Mashariki kwa ajili ya kuambiwa ratiba ya masabi yaliyoondoka juzi asubuhi na kuambiwa ni basi moja tu la scandinavia ambalo lilikuwa limeondoka kuelekea katika nchi za Afrika Mashariki siku hiyo aliyoiulizia. Songa nayo sasa... Asubuhi ya siku hiyo hiyo Pokwane pamoja na vijana wake wakaanza safari ya kuelekea Mozambique kwa kutumia ndege ya shirika la Gulf Air ambalo lilikuwa likifanya safari zake katika nchi mbalimbali za Afrika na Asia. Kwa sababu mipango ya kufanya safari zake huku mizigo ya madawa ya kulevya ikiwa ndani ya ndege kuwa ndio kawaida yake tena akisafirisha bila kukatwa wala mizigo yake kupekuliwa kwa sababu alikuwa akiipitisha kiwizi, uwanjani pale aliweza kupita nayo salama kabisa. Ndani ya ndege, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Tandi ambaye alikuwa amelisaliti penzi lake kwa kijana wa KiTanzania ambaye aliamini kwamba alikuwa amefika nchini pale kwa ajili ya kutafuta maisha tu. Hasira zake zilikuwa zimemkaba kooni, hakutaka kuyahisi mapenzi ambayo alikuwa nayo juu ya Tandi, katika kipindi hicho, mapenzi yale yakaanza kubadilika na kuwa maumivu makali. Wakati mwingine Pokwane alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa, hakuamini kama Tandi, msichana ambaye alikuwa akimuamini sana ndiye ambaye alikuwa amefanya jambo lile katika siku ile. Kila wakati alikuwa akijipiga ngumi pajani kuonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa na hasira. Mara baada ya kufika Mozambique, kama kawaida yake mizigo yake ikapitishwa katika upande mwingine kabisa kutokana na kufanya madili ya kuuza madawa yale pamoja na baadhi ya viongozi katika nchi ile ambao walikuwa wakimuonyeshea ushirikiano mkubwa na kumlinda. Mara baada ya mizigo yake kufikishwa salama nje ya jengo la uwanja wa ndege kwa kupitia milango ya dharura, hapo ndipo walipokodi teksi moja ambayo waliomba iwapeleke katika moja ya hoteli kubwa hapo Mozambique. Hilo halikuwa tatizo, dereva akapiga gia na baada ya dakika kadhaa akapaki teksi yake nje ya hoteli moja kubwa na ya kifahari ambayo nje iliandikwa Georgia na kisha kuteremka na kuanza kuelekea katika sehemu ya mapokezi ambapo wakalipia na kupelekwa vyumbani. “Nataka leo hii hii uondoke mahali hapa Tseseko” Pokwane alimwambia mmoja wa vijana wake. “Kwenda wapi?” Tseseko aliuliza. “Nataka uende mpaka Lichinga, sehemu ambayo ninaamini basi lile litapita kuelekea nchini Tanzania” Pokwane alimwambia Tseseko. “Baada ya hapo?” “Utatakiwa kupanda ndani ya basi hilo” Pokwane alimwambia. “Basi gani sasa?” “Scandinavia” “Hayo si yapo mengi mkuu? Nitajuaje kama hili ndilo?” “Utajua tu. Hakuna basi lililoondoka nchini Afrika Kusini kuelekea Afrika Masharini zaidi ya basi hilo tu” Pokwane alimwambia. “Sawa” Tseseko aliitikia. “Nitakachotaka ufanye ni kitu kimoja” “Kitu gani bosi?” “Nataka ukishaingia ndani ya basi hilo, ingia nalo nchini Tanzania huku ukimfuatilia Tandi na huyo masikini wake mpaka watakapofikia na kisha njoo unipe taarifa” Pokwane alimwambia Tseseko. “Na kama watafikia hotelini?” “Hilo usijali. Nawe fikia humo hotelini. Asubuhi wakiwa wanaondoka kama kuhama, utatakiwa kuwafuata” Pokwane alimwambia Tseseko. “Mmmh! Nitaweza kweli bosi?” “Kwa nini usiweze? Kama tunaweza kuipitisha mizigo ya dawa za kulevya katika viwanja mbalimbali vya ndege utashindwa kuwafuatilia hao?” Pokwane aliuliza. “Sawa bosi. Nitafanya hivyo. Ila niwaue moja kwa moja au?” “Hiyo si kazi yako. Wewe utawaonea huruma. Niachie mimi. Ukishapajua wanapokaa, niachie mimi kila kitu” Pokwane alimwambia Tseseko. Mipango ikapangwa na kupangika vilivyo. Tseseko alikuwa na uhakika wa kukamilisha kazi ambayo alikuwa ameambiwa aifanye katika kipindi hicho. Alichokifanya ni kuondoka ndani ya hoteli ile kwa lengo la kuelekea Lichinga ambapo kabla ya kitu chochote kile akaelekea katika moja ya maduka ya kubadilishia fedha na kuzibadilisha fedha zake. Kutoka jiji la Beira mpaka Lichinga haukuwa umbali mdogo, kulikuwa na umbali wa zaidi ya kilometa elfu moja na mia tano jambo ambalo lilimchukua siku mbili tu njiani tena kwa sababu barabara haikuwa nzima kama barabara nyingine. Mpaka wanaingia Lichinga, Tseseko alikuwa amechoka kupita kawaida. Hakutaka kwenda kulala hotelini kwa kuhofia kwamba basi lile lingeweza kupita mahali hapo bila kufahamu, alichokifanya ni kulala hapo hapo kituoni pamoja na abiria kadhaa ambao walikuwa wakisubiri mabasi ya kwenda mikoani na nje ya nchi. Saa nne kamili basi la Scandinavia likaanza kuingia ndani ya kituo cha Lichinga ambapo abiria wakateremka kwa ajili ya kwenda uani. Tseseko alikuwa makini akiwaangalia abiria wote ambao walikuwa wakiteremka katika basi lile. Hakuonekana kuridhika ila baada ya kumuona Tandi akiwa pamoja na Selemani, kwake ikaonekana kuwa amani kabisa. Akaanza kuwafuata mpaka katika kipindi ambacho wakaingia katika moja ya hoteli ndogo zilizokuwa mahali hapo na kisha yeye kuanza kuelekea kule kulipokuwa na basi lile. Kitu cha kwanza ambacho alikifanya ni kuanza kuongea na utingo kwamba uhitaji wake mkubwa ni kuvuka mpaka na kuingia nchini Tanzania. Hata utingo alipohitaji fedha, Tseseko akamgawia kiasi hicho cha fedha ambacho kilihitajika na kuruhusiwa kuingia ndani ya gari na kulala. Vibali vyote vya kizushi alikuwa navyo mifukoni mwake na vibali hivyo ndivyo ambavyo vingemfanya kuuvuka mpaka wa hapo Lichinga na kisha kuingia nchini Tanzania. Alfajiri ilipofika, abiria wote wakarudi ndani ya basi lile na kisha safari kuendelea zaidi na katika kipindi hicho walikuwa wakiutafuta mpaka wenyewe hasa kuanza huku katika kila kilichokuwa kikifanyika kwa Selemani na Tandi ndani ya basi lile, Tseseko alikuwa akifuatilia kwa makini. **** Pokwane alikuwa ametulia chumbani mule pamoja na kijana wake ambaye alikuwa amebakia nae, Tolxosa. Muda wote walikuwa wakipiga stori za hapa na pale japokuwa kwa Pokwane hakuonekana kuwa na furaha yoyote ile. Akili yake katika kipindi hicho bado haikuwa imetulia, alikuwa akifikiria mara nyingi kwamba Tandi alikuwa amekosa nini katika maisha yake kutoka kwake lakini hakupata jibu lolote lile. Walicheza karata, wakacheza kamari mpaka kuchoka na kuamua kulala huku wakiwa wamejiachia kwa kuuacha mzigo wa madawa ya kulevya chini ya meza. Saa kumi alfajiri mlango ukaanza kugonhwa, kivivu, Pokwane akaamka na kwenda kuufungua mlango, alichokutana nacho, ilikuwa ni midomo mitano ya bunduki ikimuangalia. Polisi wale wakamtaka watulie na wao kuingia ndani na kumuweka Tolxosa chini ya ulinzi na kisha kuanza kufanya upekuzi. Kitu ambacho walikuwa wakikitafuta mahali hapo wala hakikuwa kimefichwa, kilikuwa chini ya meza tu. Pokwane na Tolxosa wakafungwa pingu na kisha kutolewa ndani ya chumba kile huku polisi wale wakiwa wameshika mzigo ule uliokuwa na madawa ya kulevya. Pokwane hakutaka kujiuliza juu ya mtu ambaye alikuwa amehusika katika lile, akili yake ilimwambia kwamba kuna watu ambao alikuwa akifanya nao kazi walikuwa wamemgeuka katika kipindi hico. Maumivu ya kukimbiwa na Tandi pamoja na kuchomwa kwa polisi kwamba alikuwa na mzigo wa madawa ya kulevya vikaonekana kumchanganya akili kabisa. Baada ya siku kadhaa, Pokwane na Tolxosa wakapelekwa mahakamani ambapo baada ya kesi kusikilizwa vya kutosha, wakahukumiwa kwenda jela miaka kumi kila mmoja. Hapo ndipo machungu yalivyozidi kumkamata moyoni mwake, alijua kwamba bila Tandi kumfanyia ule mchezo mchafu basi katika kipindi hicho asingekuwa nchini Mozambique na kuhukumiwa kifungo cha miaka kumi. Chuki yake juu ya Tandi na Selemani ikaongezeka zaidi, alikuwa tayari kulipiza kisasi hata katika kipindi ambacho angetoka jela lakini ili mladi tu awaue Tandi na Selemani au hata kuwawekea vidonda ambavyo visingekuja kupona katika maisha yao yote. “Nitaua. Ni lazima niue nitakapotoka. Niombe Mungu Tseseko apafahamu watakapokuwa wanaishi” Pokwane alijisemea katika kipindi ambacho alikuwa akiingia katika mlango wa gereza kubwa ambalo lilijengwa karibu na mpaka wa Palma, sehemu ya kuingia nchini Tanzania na kufikia Mtwara. ***** Maisha ya gerezani hayakuwa ya kawaida kabisa kwa watu wengine lakini kwa Pokwane yalikuwa ni ya kawaida sana ila kitu ambacho alikuwa akinyimwa ni uhuru tu. Viongozi mbalimbali wa nchi walikuwa nae kwa sababu yeye ndiye alikuwa mzizi wa uuzwaji wa madawa ya kulevya ambayo yalikuwa yakifanyika sana katika nchi za Kusini mwa Afrika. Kila siku alikuwa akiletewa magazeti, alikuwa akiangalia televisheni pamoja na kupata vitu vingine katika maisha yake ya gerezani. Jina lake lilikuwa kubwa, wafungwa wengi walikuwa wakimuogopa kwani walijua fika kwamba mtu huyo alikuwa na nguvu nyingi. Kila siku mawazo ya Pokwane yalikuwa ni kumfikiria Tandi ambaye alikuwa amemuacha katika kipindi kibaya sana, kipindi ambacho wangeweza kuoana na hatimae kuwa mume na mke. Bado moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, alijua fika kwamba Tandi ndiye ambaye alikuwa amesababisha yale yote mpaka kuwa ndani ya gereza hilo siku hiyo. Katika kipindi chake cha miezi mitatu ndani ya gereza lile ndipo ambapo alipokea ugeni wa Tseseko ambaye alifika mahali hapo na kumwambia kwamba alikuwa amekwishapafahamu mahali ambapo Tandi na Selemani walipokuwa wamehamia nchini Tanzania. Kwa Pokwane ikawa kama faraja kwa kuona kwamba jambo ambalo alitakiwa kulifanya mbele ya safari yake wala halikuwa kubwa, alichokuwa akimuomba Mungu ni amlinde mpaka katika kipindi ambacho angetoka gerezani. Mwaka wa kwanza ukakatika, wa pili ukaingia, mwaka wa tatu mpaka miaka mitano ikakatika, bado Pokwane alikuwa gerezani akikitumikia kifungo chake cha miaka kumi. Miaka iliendelea kukatika mpaka katika kipindi ambacho miaka kumi ilipotimia na ndipo alipotolewa gerezani. Mazingira mengi ya nchi ya Afrika kusini yalikuwa yamebadilika jambo ambalo lilikuwa likimshangaza sana. Muda mwingi alikuwa akiyaangalia majengo makubwa ambayo yalikuwa yamejengwa huku barabara zikiwa ni za kisasa tofauti na kipindi kile. Katika sehemu hiyo, Pokwane alikuwa amefuatwa na mwanaume mmoja aliyekuwa na ndevu nyingi ambaye alikuwa katika gari la kifahari. Mara baada ya macho yake kutua usoni mwa Pokwane, mwanaume yule akateremka kutoka garini na kisha kumfuata na kumkumbatia. Walipomaliza kusalimiana kwa furaha, wakaelekea katika gari lile la kifahari na kisha kuanza safari ya kuelekea nchini Afrika Kusini kutoka hapo nchini Mozambique. Ndani ya gari, kila mtu alikuwa muongeaji kupita kawaida huku Pokwane akiuliza maswali kadhaa kuhusiana hali ambayo ilikuwa ikiendelea nchini Afrika kusini. Walichukua muda wa siku moja na ndipo wakaingia katika nchi ya Afrika Kusini. Pokwane akabaki na mshangao mkubwa, hakuamini kama nchi ya Afrika Kusini ilikuwa imejengeka namna ile ndani ya kipindi cha miaka kumi kukaa gerezani. “Jamaa amechukua fomu bwana nae anataka kugombea urais” Mwanaume yule aliyakuwa akijiita Nebu alimwambia Pokwane. “Jamaa gani?” “Zuma” “Acha utani bwana” “Ndio hivyo. Na sisi tunataka tumsimamishe mtu wetu ashindane nae” Nebu alimwambia Pokwane. “Tutashinda kweli?” “Kwa nini tusishinde? Tutatumia kila aina ya wizi wa kura mpaka tunashinda” Nebu alimwambia Pokwane. Japokuwa walikuwa wakiongea mambo mbaliimbali lakini Pokwane hakuacha kuyaangalia majengo makubwa na marefu ambayo yalikuwa yamejengwa katika kipindi alichokuwa gerezani. Mambo mengi yalionekana kubadilika, nchi ya Afrika kusini ilikuwa na muonekano mwingine kabisa. Nebu na wazee wenzake ndio ambao wakaamua kuwa pamoja na Pokwane katika kila kitu ambacho alikuwa akikihitaji. Alichokifanya Pokwane mara baada ya wiki kadhaa ni kuwasiliana na Tseseko na kisha kumwambia juu ya mpango wake ambao alikuwa akitaka kuufanya, mpango ambao ulikuwa umedumu katika moyo wake kwa muda wa miaka kumi. “Inatupasa twende. Bado nina hasira na wale watu” Pokwane alimwambia Tseseko. Baada ya wiki kupita, wakaanza safari ya kuelekea nchini Tanzania. Katika kipindi hicho walikuwa wakitumia ndege ambayo baada ya kutua katika uwanja wa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere wakaanza kutoka katika ndege ile na kisha kuingia ndani ya jengo la uwanja huo ambapo mizigo yao ikachunguzwa na kisha kuruhusiwa. Katika kipindi hicho mawazo ya Pokwane yalikuwa juu ya Tandi, mwanamke ambaye alikuwa amemuachia jeraha kubwa la mapenzi ndani ya mwili wake. Wakachukua teksi ambayo iliwapeleka mpaka katika hoteli ya New Africa na kisha kuchukua chumba. “Unapajua wanapoishi?” Pokwane alimuuliza Tsetseko. “Nadhani naweza kupakumbuka. Hatuwezi kupata huduma ya internet sehemu?” Tseseko alimuuliza Pokwane. “Nadhani hapa kuna uhitaji wa kompyuta ya mapajani. Kuna huduma ya internet ambayo haitumii waya” Pokwane alijibu. “Sawa. Ngoja nikaongee na wahudumu kama tunaweza kupata kompyuta hiyo” Tseseko alimwambia Pokwane na kisha kuinuka na kuanza kwenda nje. “Unaelekea wapi?” “Kwa mhudumu” “Achana nae. Tutatumia hata simu yangu” Pokwane alisema. Alichokifanya Pokwane ni kuionganisha simu ile na huduma ya internet bila kutumia waya (wireless) na kisha kumgawia Tseseko simu ile ambayo akaanza kufungua katika akaunti yake ya Yahoo. “Kuna nini humo” “Niliyahifadhi majina katika akaunti yangu ya Yahoo” Tsese alijibu. “Majina ya nini?” “Ya sehemu wanapoishi” Pokwane akabaki kimya na kumwangalia Tseseko ambaye alikuwa akiendelea kufanya kile ambacho alikuwa akitaka kukifanya katika simu ile. Alikaa nayo huku akiendelea na kazi yake kwa muda wa dakika kumi na ndipo uso wake ukaanza kuonyesha tabasamu. Akasimama na kuelekea katika meza ndogo ambayo ilikuwa ndani ya chumba kile na kisha kuchukua kalamu na karatasi na kurudi kitandani. “Hapa. Ni sehemu hii inayoitwa Magomeni Mapipa nyumba namba 788” Tseseko alimwambia Pokwane huku akiwa ameandika sehemu ile katika karatasi yake. Siku iliyofuata, wakampigia simu dereva ambaye alikuwa amewaleta hotelini hapo na kisha kuja kuwachukua na kumtaka kuwapeleka Magomeni Mapipa. Tofauti na kipindi kile cha nyuma, katika kipindi hiki nyumba zilikuwa nyingi kupita kawaida, ila kwa sababu walikuwa na namba ya nyumba hiyo, dereva akawasaidia kuitafuta mpaka pale walipoipata na kisha dereva kwenda kuanza kuongea na wanawake waliokuwa kibarazani huku wao wakiwa garini. “Samahanini” Dereva aliwaambia wanawake waliokuwa kibarazani mara baada ya kuwasalimia. “Bila samahani” “Kuna mtu namtafuta anaitwa Tandi, sijui mnamfahamu?” Dereva yule aliwauliza. “Tandi! Ndiye nani?” Mwanamke mmoja aliuliza. “Mwanamke mmoja aliishi mahali hapa miaka kumi iliyopita na mwanaume wake” Dereva yule, Salum alisema. “Mmmh! Sisi unaotuona hapa wote ni wa juzi juzi tu, labda uongee na mwenye nyumba” Mwanamke mmoja alimwambia Salumu. “Mwenye nyumba yupo?” “Amejaa tele. Pita ndani kwenye chumba cha nne mkono wa kushoto” Mwanamke huyo alimwambia Salumu ambaye akapita ndani mpaka kwenye mlango wa chumba kile na kisha kuanza kugonga. Wala hazikupita sekunde nyingi, mwanaume mmoja mwenye ndevu nyingi nyeupe akatokea mlangoni hapo na kisha kuannza kumwangalia Salumu ambaye alikuwa akionekana kutokuwa na wasiwasi kabisa. “Nikusaidie nini?” Mzee huyo aliuliza mara baada ya salamu. “Namuulizia dada yangu” “Dada yako! Nani?” “Anaitwa Tandi. Aliwahi kuishi ndani ya nyumba hii miaka kumi iliyopita” Salum alimwambia mzee yule ambaye akainamisha kichwa chake chini. “Alikuwa akiishi na nani?” “Na mwanaume wake” “Anaitwa nani?” “Wala simfahamu” “Itakuwaje haumjui mwanaume aliyekuwa akiishi na dada yako?” “Alitoroka nyumbani kwetu” “Nyumbani kwenu wapi?” “Musoma” “Sawa. Miaka kumi iliyopita ndani ya nyumba hii kulikuwa na mpangaji mmoja tu, aliitwa Selemani na mke wake, Siwema. Huyo Tandi wala simfahamu” Mwanaume yule alimwambia Salumu. “Hapana. Yeye anaitwa Tandi” “Huyo simfahamu” “Na huyo Siwema ndiye nani? Yule mke wa tajiri Selemani?” Dereva yule aliuliza. “Ndiye huyo huyo” “Nashukuru. Asante sana” Salumu alisema na kisha kuanza kutoka ndani ya nyumba ile. Alipofika nje, akawaaga wale wanawake ambao walikuwa wamekaa kibarazani na kisha kuingia garini. “Kumbe mlikuwa mnamuulizia Siwema?” Salumu aliuliza huku akionekana kutabasamu. “Hapana. Hatukusema Siwema. Tulikwambia Tandi” Pokwane alimwambia Salumu. “Sikilizeni. Huyo Tandi mnayemuulizia ni mwanamke ambaye ana asili ya Afrika Kusini, ana kidoti hapa juu ya pua yake. Si ndio?” Salumu aliuliza. “Ndiye huyo huyo” “Huyo ni Siwema na si Tandi kama mlivyosema” Salumu aliwaambia. “Mmmh!” Tseseko aliguna. “Inawezekana akawa amebadilisha jina. Kama unamjua naomba utupeleke anapoishi” Pokwane alimwambia Salumu. “Huwezi kuonana nae. Mwanaume wake ana pesa hatari. Nyumba yake haisogelewi hata mara moja” “Sawa. Ila unaweza kutupeleka?” “Hakuna noma” “Anaishi wapi? “Mbezi Beach” Salumu alisema na kisha kuwasha gari na safari ya kuelekea Mbezi Beach kuanza. ****************************************** *** Nini kitaendelea hapo..??
Posted on: Sat, 24 Aug 2013 08:11:44 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015