KWA VIWAWA JIMBO KUU LA DAR ES SALAAM Leo nimewiwa kuandika na - TopicsExpress



          

KWA VIWAWA JIMBO KUU LA DAR ES SALAAM Leo nimewiwa kuandika na sina uhakika kama ni ujumbe au waraka huu kwa vijana wenzangu waamini ambao mmekua mstari wa mbele katika utume wa kanisa, hususani VIWAWA. Inawezekana kabisa ujumbe huu haupo katika mpangilio mzuri au maudhui yake hayatawafurahisha baadhi ya watu, lakini naomba niwasilishe ili nipate kutua mzigo nilio nao. Na nitajikita zaidi kwa wapendwa wangu VIWAWA wa jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam, jimbo langu, lakini pia jimbo nililotumikia kama mwanachama na pia kiongozi kwa nafasi mbalimbali za Walei, na vyama vingine vya kitume ikiwemo Vijana/VIWAWA. Baadhi tu ya nafasi za uongozi nilizowahi kushika ni: 1. Katibu wa jumuiya ya Mt. Mikaeli, Kanda ya K/ndoni Soko, Parokia ya Hananasif.(Jumuiya yangu) 2. Makamu M/Kiti jumuiya ya Mt. Mikaeli. 3. Katibu Msaidizi – Kanda ya k/ndoni soko. 4. M/Hazina wa Umoja wa vijana Parokia ya Hananasif (al maarufu Parokia ya Mhe. Pinda) 5. Mwenyekiti wa Kwaya ya Mt. Maria Goreth, Parokia ya Hananasif. 6. Katibu wa kipindi cha mpito wa shirikisho la kwaya Parokia. 7. Mwenyekiti wa Vijana Parokia. 8. Makamu Mwenyekiti wa VIWAWA jimbo kuu la DSM. (kwa muda na baadae nilijiudhuru nafasi hii-nitaeleza baadae ni kwa nini). 9. Mjumbe wa kamati ya haki na amani ya parokia, Hananasif.(nafasi niliyonayo kwa sasa) 10. Mjumbe wa kamati mbalimbali maalum kwa kufanikisha malengo mbalimbali yanayopangwa ktk mipango ya maendeleo ya kanisa. Na nyinginezo ambazo hata sizikumbuki. Lengo langu la kuwakumbusha kidogo kuhusiana na nafasi zangu nilizowahi kushika katika utume wa kanisa si kuwatisha au kutafuta ujiko, la hasha, ni kuweka kumbukumbu sawa, kwamba niliwahi kutumika kwa ajili ya kukuza malezi ya kiroho, kijamii, na pia kama sehemu ya uchaji kama katekesi inavyofundisha. Nafasi hizo ni ndogo sana wala huwezi kuitwa mheshimiwa, au kunyenyekewa, lakini pia kwa kila mtu aliyewahi kufanya utume anajua kabisa hakuna ujira au malipo yoyote ambayo mtu anaweza kulipwa kwa kutumikia kanisa, isipokua kwa imani tunaamini ujira huo siku moja tutaukuta huko mbele za haki. Kimsingi, hoja yangu hapa ni kwamba ukiona mtu amekua kiongozi wa kanisa au taasisi hasa kwa kanisa katoliki ambalo mimi ni muumini wake, basi elewa wazi kwamba mtu huyo anafanya kazi ya kujitolea (volunteerism) ni vigumu sana kupata ujira wowote ukitilia maanani ukosefu wa vyanzo imara vya mapato kwa taasisi za namna hii, sanasana utakuta huyo kiongozi mwenyewe anaingia mfukoni kwake na kutoa hata vijisenti vyake ili kufanikisha mambo mbalimbali katika majukumu yake ya uongozi. Nisiwachoshe kwa simulizi zangu ndefu, nilichokusudia kusema hapa ni: Mosi: Nachukua fursa hii kuwapongeza safu nzima ya uongozi wa VIWAWA Jimbo kuu la DSM mliochaguliwa na mkutano mkuu hivi majuzi. Binafsi nina imani kubwa na nyinyi, ninafahamu uwezo na kujitoa kwenu katika kufanikisha kazi za utume wa vijana. Daima dira yenu iwe upendo, mshikamano na unyenyekevu, kwa kuzingatia hayo, hakika mtafika mnapokwenda. Pili: Jaribuni kuwashirikisha vijana/wanachama katika mipango na maazimio mbalimbali, wala msiwapuuze. Badilisheni sura ya VIWAWA toka ile ya zamani ambayo ilikosa mvuto na vijana wengi kukata tamaa ya kushiriki, kutokana tu na maamuzi ya kibabe na jeuri ya aliyekua Mwenyekiti. Mimi pia nilikua mhanga wa mfumo huo wa uongozi. Tatu: Nilichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa VIWAWA jimbo kuu la DSM kwa kura nyingi sana, nadhani kila mwanachama ni shahidi wa hilo. Na kwa faida tu ya wasomaji wengine, ktk chaguzi zote za kanisa katoliki, huwa hakuna kufanya wala kujihusisha na kampeni ya aina yoyote, kwani kwa imani yetu ni kwamba kiongozi huchaguliwa na roho mtakatifu. Hivyo vijana walikua na matumaini makubwa wakiamini nitakuwa chachu ya mabadiliko. Lakini niwe wazi tu kwamba nilipofika pale ndani nilikutana na ugumu flani kiutendaji, kwani Mwenyekiti alikua akitumia veto kumua kila kitu, kiburi, jeuri, mabavu kama vile ile ni NGO yake. Naomba niwe wazi tu kwamba hata kipindi kingine ilikua ikionekana wazi kwamba viongozi wenzangu pia walionekana kumuogopa hata pale walipokwazika na mambo flani flani. Kuna kipindi nilibanwa sana na majukumu ya kikazi, ikawa mara kwa mara nasafiri hivyo ilikua vigumu kwangu kuhudhuria baadhi ya vikao. Ilifika wakati Mwenyekiti akaanza kuongea kwa mafumbo kuhusu kuniazimia ili niondolewe ktk nafasi yangu. Kwa kuitambua dhana ya uwajibikaji, nilisoma alama za nyakati na kuamua kuachia ngazi ili kutoa nafasi kwa mwingine atakayeweza kutumikia kikamilifu. Nimesema leo nimewiwa kuandika haya nikiamini kuwa ujumbe huu utafika kwa mlengwa kupitia namna ya uwazi kabisa. Sikuweza kuwaambia wanachama kupitia mkutano au vikao vya wazi kuhusiana na uamuzi wangu wa kujihudhuru nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa VIWAWA jimbo kuu la DSM, kutokana na utaratibu wa kawaida kabisa kikanuni, na niliandika barua nikiambatanisha nakala zinazohusika, kwa watu wanaohusika nikiwataarifu kuhusiana na uamuzi wangu wa kuachia ngazi kutokana na majukumu yangu ya kikazi yaliyokua yakinipelekea sana kuwa nje ya mkoa kwa kipindi kirefu. Hivyo niliona ni busara tu ya kawaida niachie ngazi ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine atakayeweza kuitendea haki nafasi hiyo, kuliko kuwa mlafi wa madaraka wakati sitimizi wajibu wangu. Lakini kilichonisukuma leo kuandika makala hii ndefu, ni maneno mengi yaliyofuata ususani toka kwa Mwenyekiti baada ya mimi kuchukua uamuzi huo, ambao kwangu mimi ulikua sahii. Toka nimechukua uamuzi huo sasa yapata miaka mitatu, sijawahi kuzungumzia jambo hilo, lakini pia kwa hekima ndogo tu ya kiuongozi isingekua busara kuzungumzia mapungufu ya Mwenyekiti wangu nje ya vikao rasmi vya kamati tendaji, hivyo niliamua kutokulizungumzia hata pale nilipobanwa sana na baadhi ya wanachama waliokua na ajenda ya kumuazimia Mwenyekiti kwa kura ya kutokua na imani nae, kwani historia inaonyesha kuwa kumekua na hali ya Makamu Wenyeviti wanaochaguliwa chini yake kujiudhuru au kuondoka tu kimyakimya kwa kukosa ushirikiano mzuri toka kwake. Nimekua nikipata taarifa nyingi toka vyanzo rasmi na hata visivyo rasmi kwamba Mwenyekiti huyo alikua na tabia ya kuendeleza mijadala mbalimbali yenye chuki au hoja zisizo za kweli kwamba mimi nilikua na matarajio makubwa, lakini nilipoingia pale nikakuta hali sivyo ilivyo hivyo nikaamua kuachia ngazi, pili mimi ni mwanasiasa hivyo nilikua natafuta umaarufu wa kisiasa. Jamani ipo wazi tu kwamba hiyo haikua mara yangu ya kwanza kuwa kiongozi kanisani(ndio maana nilitaja nafasi nilizowahi kushika hapo mwanzo), na nilikua nafahamu kabisa kwamba hakuna maslahi yoyote katika vikundi vya namna hiyo, zaidi ingenigharimu muda na hata rasilimali zangu mwenyewe. Labda kama kuuliza kwangu kuhusiana na namna pesa za umoja zinavyotunzwa, na nikakutana na jibu kwamba umoja haukuwa na akaunti, pesa zilikua zikitunzwa na Padre Mlezi wa jimbo kwa kipindi hicho akishirikiana na Mwenyekiti (yani hata Mtunza hazina alikua ashiki pesa). Nakumbuka nilitoa hoja ya na baadae kikao kikaondoka na maazimio ya kufungua akaunti ya VIWAWA Jimbo. Kama ni umaarufu wa kisiasa, siwezi kuutafuta kanisani maana hapo si mahala pake. Kwa ufahamu wangu mimi taasisi za kidini tena kanisa katoliki na siasa ni vitu tayari viwili tofauti kabisa. Tena kwa kipindi hicho ningetafuta umaarufu wa nini wakati tayari nilikua maarufu ndio maana wakati ule nililala kitandani usiku kucha, nikaamka asubuhi, nikaingia ukumbini, na wajumbe zaidi ya 500 wa mkutano mkuu wa uchaguzi walinipigia kura zile kuwa makamu mwenyekiti bila kampeni ya aina yoyote au kuomba kura kwa mjumbe yeyote. Kuna Mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema “Kwa kipindi ulichonacho ishi kikamilifu, maana kesho inaweza isifike” Mimi pia nimewiwa kusema hili jambo leo maana inawezekana kabisa kesho isifike kwangu. Nimeona leo niliseme jambo hili wazi ili niweke kumbukumbu sawa kwa Mwenyekiti wangu ambaye mpaka sasa nae yupo nje ya uongozi kama mimi lakini bado anaendelea kunishambulia kwa hoja nyepesi, kwa watu mbalimbali, tena mbaya zaidi nikiwa sipo. Kwa sababu ananisemea pembeni lakini kwenye hadhara, na mimi nimeona nimjibie hapa pembeni pia kwenye hadhara hii ya facebook.
Posted on: Thu, 19 Sep 2013 21:51:31 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015