SURA YA KUMI NA MOJA UTUMISHI WA JAMHURI YA MUUNGANO 176.-(1) - TopicsExpress



          

SURA YA KUMI NA MOJA UTUMISHI WA JAMHURI YA MUUNGANO 176.-(1) Utumishi wa umma katika Jamhuri ya Muungano utazingatia misingi na kanuni zifuatazo: (a) utumishi wa umma ni dhamana kutoka kwa wananchi na hivyo mtumishi anatakiwa kutumikia wananchi kwa uadilifu,uaminifu na unyenyekevu; (b)kudumisha na kukuza viwango vya juu vya maadili ya kitaaluma; (c) kuhamasisha matumizi bora na yenye tija ya raslimali; (d) kutoa huduma kwa umma kwa njia ya haki, usawa na bila upendeleo; (e) kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye maandalizi ya sera mbalimbali za nchi; (f) kuitikia matakwa na mahitaji ya watu kwa haraka na kwa wakati unaofaa; (g) kujitolea katika utekelezaji wa sera na mipango ya kitaifa; (h) uwajibikaji wa viongozi kwa makosa yanayofanyika chini yao; (i) kuhamasisha sera ya uwazi katika kutoa habari za kweli kwa umma na kwa wakati ufaao; na (j) kuhakikisha kwamba watu watateuliwa katika nafasi mbalimbali kwa kuzingatia uwezo wa kitaaluma, weledi, maarifa, ujuzi na uzoefu wao katika eneo husika. (2) Misingi na Kanuni za Utumishi wa Umma zilizoainishwa katika Ibara hii zitazingatiwa na kutumika katika uteuzi wa kushika nafasi za madaraka ya uongozi katika: (a) mamlaka katika mihimili yote ya Dola; (b) taasisi na idara zote za Serikali; na (c) mashirika yote ya Serikali. (3) Bunge litatunga sheria kuweka masharti ya utekelezaji wa misingi ya utumishi iliyoainishwa katika Ibara ndogo ya (1). 177. Bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii, utumishi wa umma na uongozi katika Jamhuri ya Muungano utazingatia misingi kwamba utoaji wa ajira na uteuzi wa viongozi utakuwa kwa uwiano baina ya Washirika wa Muungano, kwa kuzingatia weledi na taaluma katika eneo au nyanja husika. 178.-(1) Kutakuwa na Tume ya Utumishi wa Umma itakayokuwa na Mwenyekiti na wajumbe wengine sita watakaoteuliwa na Rais na kuidhinishwa na Bunge. (2) Katika kuteua wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma, Rais atazingatia Kanuni za Utumishi wa Umma zilizoainishwa katika Katiba hii. (3) Kutakuwa na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma ambaye atakuwa ndiye Mtendaji Mkuu na mtekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Tume. (4) Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma atateuliwa na Rais baada ya kuidhinishwa na Bunge kutoka miongoni mwa watumishi waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. 179.-(1) Tume ya Utumishi wa Umma itakuwa ni chombo cha juu katika Utumishi wa Umma chenye mamlaka ya kusimamia na kuratibu mambo yote kuhusu Utumishi wa Umma. (2) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1), majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma yatakuwa ni: (a) kumshauri Rais juu ya uteuzi wa viongozi katika nafasi mbalimbali kwa mujibu wa Katiba hii; (b) kutoa miongozo mbalimbali na kusimamia mchakato wa ajira katika utumishi wa umma kwa kuzingatia vigezo stahiki; (c) bila kuathiri masharti ya Katiba hii, kuteua watu kuhudumu au kushikilia ofisi kwa muda katika idara ya utumishi wa umma, kuidhinisha uteuzi na kudhibiti nidhamu na kuwaondoa watumishi wanaohudumu au kushikilia ofisi hizo; (d) kusimamia na kuhamasisha utekelezaji wa misingi na kanuni za utumishi katika sekta zote za utumishi wa umma; (e) kushughulikia rufani zinazowasilishwa na watumishi wa umma dhidi ya uamuzi wa mamlaka mbalimbali za nidhamu katika utumishi wa umma; (f) kutekeleza majukumu mengine yoyote kama yatakavyoainishwa katika sheria itakayotungwa na Bunge juu masuala ya utumishi wa umma na sheria nyingine za nchi; (g) kuunda na kudurusu mishahara na marupurupu ya watumishi wa umma, ikiwemo viongozi wa juu wa nchi, viongozi wa kisiasa, watumishi waliopo chini ya utumishi wa Mahakama, Bunge na Serikali; na (h) kusawazisha mishahara na marupurupu ya maafisa wote wa Serikali, Bunge, Mahakama na maofisa wa umma pamoja na maofisa wa majeshi ya ulinzi na usalama....
Posted on: Fri, 30 Aug 2013 09:46:55 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015