MIRATHI YA KAKA sehemu ya 10 ILIPOISHIA........ Kichwa changu - TopicsExpress



          

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 10 ILIPOISHIA........ Kichwa changu sasa nilianza kukiona ki chepesi, uzito kiliokuwa nao mara baada ya kugutuka kutoka ndotoni nikawa siuhisi tena. Niliamua kuanza kurudi nyumbani kwani machweo nayo yalikuwa yamewadia. ******************************* SASA ENDELEA....... Ilikuwa ni asubuhi, kwa muda huo nilikuwa nipo kwenye meza ya chakula nikipata kifungua kinywa; supu ya kuku na mikate ya boflo. Mara nilisikia kengele ya getini ikinijuza kuwa kuna mgeni pale getini. Nilimuomba Kishoka aende kumsikiliza mgeni aliyekuwa anapiga hodi kule getini kwani mimi nilikuwa ninakula wakati yeye alikuwa hali. Naye bila ubishi aliondoka na kwenda getini. Punde si punde alirudi, akaja na taarifa iliyosema kwamba mgeni aliyekupo pale nje kakataa kuingia ndani hivyo ananitaka niende tukaongee palepale nje. Nilipomuuliza Kishoka mwonekano wa mgeni huyo upoje, alinieleza jinsi alivyokuwa. Mwonekano wa mgeni huyo kwa mujibu wa maelezo ya Kishoka ulionekana kuendana na mwonekano wa msichana niliyekuwa nimemuona jana yake kule ufukweni. “Umemuuliza jina?” Nilimuuliza tena Kishoka. “Ndiyo nimemuuliza.” “Akakwambia anaitwa nani?” “Alichonijibu ni kwamba nije nikuambie kuwa mlionana naye jana kule ufukweni na mkapeana miadi ya kuonana leo asubuhi.” Nilifurahi sana kusikia kuwa mrembo wa jana aliyejifanya kudengua kaingia kwenye anga zangu mwenyewe. Niliinuka na kuachana na supu yangu haraka kisha nikaenda moja kwa moja mpaka getini kumwangalia mgeni huyo. Nikiwa naelekea huko getini nilijaribu kujifutafuta midomo yangu ili kuondoa mabaki ya boflo na mchuzi wa supu ya kuku. Nilifika mpaka getini, nikafungua geti na kuangalia pale nje, cha ajabu sikuona mtu yeyote. Nikaanza kujiuliza mgeni aliyekuwepo hapo kaenda wapi? Kusema kakaa sana mpaka akachoka kusubiria huo ni uongo kwani ulikuwa haujapita muda mrefu sana tangu Kishoka aingie ndani kuniita, sikujua alikokuwa kaelekea. Hata kama angekuwa kaghairi kunisubiri akaondoka, haiwezekane nisimuone wakati njia ya kutoka kwangu kuingia kwenye barabara ni ndefu kiasi, ni kama mita mia moja kutoka kwenye geti la nyumba yangu mpaka kufika kwenye barabara kuu. Nilijaribu kuangaza kwenye njia lakini sikuona mtu. Nikaamua kurudi ndani kuendelea kushambulia boflo zangu na supu yangu ya kuku. DUH! KIJANA KAZI ANAYO, HUYO MWANADADA NI NANI NA KAPOTELEA WAPI? USIKOSE SEHEMU YA 11.
Posted on: Wed, 11 Sep 2013 13:45:09 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015